Habari ya ardhi inayozama inaangazia tamu na chungu ya uhusiano uliopo kati binadamu na maji kwa wakazi waishio eneo la Ripon eneo ambalo lipo karibu kabisa na chanzo cha mto Nile kwenye Ziwa Viktoria upande wa Uganda.
Ni mwendo wa kati ya dakika tano na kumi kwa usafiri wa boti kutoka eneo hili hadi Ziwa Viktoria sehemu ambayo maporomoko ya zamani ya Ripon, Mto Nile na ziwa Victoria yanakutana. Eneo hili ndio linafahamika kuwa mto Nile unapoanzia nchini Uganda na kumwaga maji yake hadi Nchini Misri.
Eneo hili lina wakazi wapatao 574 kwa mujibu wa daftari la wapiga kura la mwaka 2021 na linaendelea kukumbwa na upungufu wa ardhi na kupungua idadi ya wakazi wake kutokana na ongezeko la kina cha maji kwenye Ziwa Viktoria.
Awali eneo hili lilikuwa takriban mita 100 kutoka ufukwe wa ziwa na sasa zaidi ya mita hamsini zimemezwa na maji kwa mujibu wa Bwana Abdu Nantabya ambaye ni Mwenyekiti Halmashauri ya Kijiji ambaye ameishi mahali hapa kwa muda wa miaka 34.
Ongezeko la sasa la kina cha maji lilianza mwezi wa Octoba 2019 na kufikia kina cha juu cha mita 13.32 mnamo tarehe 30 Aprili 2020 kwa mujibu wa taarifa ya iliyotolewa na Wizara ya maji na mazingira.
Kina hiki kilidumu kwa muda wa miezi sitana ni kina cha chini cha mita 13.42 kilichorekodiwa mwaka 1964 kukiwa na tofauti ya mita 0.8 ambapo wakazi wa waliokuwa wakiishi eneo hilo walikumbwa na mafuriko na mamia kukosa makazi.
Habari hii inachunguza jinsi watu wanaoshi, kufanyakazi na kutembalea eneo hili wanavyoweza kukabiliana na mabadiliko ya kina cha maji na jinsi maisha yao yavyoathrika kutokana na kadhia hii.
Agnes Naigaga mwenye umri wa miaka 53 akiwa kwenye boti ziwani Viktoria amesimama kwenye eneo ambalo hapo awali kulikuwa na kliniki aliyokuwa akifanya kazi. Anakumbuka kliniki ilikuwa hapo mnamo Agosti mwaka 2020 kyeye akiwa ni mkunga na tabibu wa kwenye eneo hili kwa miaka 20.
Alihamia eneo hili mwaka 1997 na tangu wakati huo kiliniki yake imezungukwa na maji karibu mara tatu hali iliyomlazimu kuhama.
Eneo ambalo kiliniki ilipo hivi sasa ni jipya lililofadhiliwa na mamlaka inayosimamia eneo hili baada ya eneo la awali kuzamishwa na mji. Wakazi wa eneo hili hawakuwa tayari kumpoteza tabibu wao pekee na kuwalazimu kumpatia jengo hili ambalo lipo mita 200 kutoka ufukweni, eneo ambalo bado n hatari iwapo mafuro yatatokea siku za usoni.
Bi Naigaga alihamia hapa miezi minane iliyopita baada ya mafuriko kuzamisha kliniki yake na makazi yake ya sasa madogo na ya muda ambayo yamejengwa kwa kutumia mbao na mabati kama kuta.
“Naweka akiba ya fedha ninazopata kutokana na kazi yangu ili niweze kumaliza kujenga nyumba yangu kijijini kwani mafuriko yanaweza kutokea wakati wowote na kufika hapa pia. Maji yanaongezekea kwa kasi kwa miaka yote ambayo nimeishi hapa na sina uhakika itachukua muda gani mpaka maji yatafikia eneo hili jipya ninaloishi kama eneo hili litazama nitarudi kijijini kwetu Butalajja. Nimeishi hapa miaka mingi.”Anasema
Kwa mujibu wa bwana Abdu Nantabya ambaye ni mjumbe wa Halmashari ya kijiji, idadi ya wakazi hapa Ripon imepungua kutoka wakazi 700 hadi 500 mpaka kufikia mwezi Machi 2021
Sababu zinasababisha ongezeko la kina maji ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo yameathiri misimu na mzunguko wa unyeshaji wa mvua na pia uwepo hafifu au kutokuwepo kabisa kwa jitihada za kila siku za utunzaji wa mazingira kwenye maisha ya kila siku ya wakazi wanaoishi kwenye mabonde ya ziwa.
Mmomonyoko wa ardhi pia umeongezeka kutokana na mvua kubwa zinazonyesha ikiwa ni pamoja na ongezeko la makazi na shughuli za kilimo kwani watu wanageuza maeneo ya misitu na maeneo oevu ambayo kwa kawaida yanadhibiti maji kuwa miji na mashamba.
Taarifa za umoja wa mataifa zinazohusu maporomoko ya udongo kwenye tovuti yao ya mafuriko na ukame zinaonyesha maporomoko kwenye maeneo yanayopakana na ziwa Viktoria yameongezeka kwa asilimia 575 kwa miezi minne iliyopita mwaka 2019 ukilinganisha kipindi kama hicho mwaka 2018.
Pia inakisiwa kuwa maji yanaweza kuongeka mwaka wote wa 2021 kutokana na ongezeko la mvua na kusababisha maporomoko ya ardhi kuingia kwenye mito na vijito vinavyoingiza maji kwenye ziwa.
Ziwa Viktoria ni kusanyiko la maji linalomilkiwa kwa pamoja na nchi za Uganda, Tanzania na Kenya, ziwa hilo linajumuisha mito inayomwaga maji yake ziwani humo vikianzia nchi za Rwanda na Burundi hata hivyo, ziwa hili lina sehemu moja tu ya kutoa maji yake kupitia Mto Nile uliopo Jinja nchini Uganda na maji yapoingia kutoka kwenye mito yanaliathiri ziwa lenyewe pia.
“Kila kitu kilitokea kwa ghafla sana.“
Daku Musa mwenye umri wa miaka 43 ni mfanyabiashara na pia mwenyekiti wa kitongoji cha Ripon anaonekana akiwa kwenye boti kwenye eneo ambalo hapo awali yalikuwepo makazi yake. Ongezeko la kina cha maji kwenye ziwa Viktoria kulimlazimu kuiondoa familia yake kwenye eneo hili mnamo Agosti ya mwaka 2020 na kuhamia eneo lingine la jirani na hapo.
Ilimbidi bwana Daku kuondoa familia yake na kuhamia eneo jirani ambako kwa sasa analipa kodi ya pango ya kila mwezi ili hali akiwa kwenye makazi yake mwenye alikuwa akilipa kodi ndogo ya kiasi cha shilingi za Uganda 300 ambazo ni sawa dolari za marekani 0.09 kila siku kwa halmashari ya wilaya Jinja.
“Kila kitu kilitokea kwa ghafla sana. Mimi na familia yangu tulikuwa na muda mfupi sana wa kuhama “ Anasema Bwana Daku Musa.
Anasema awali ilionekana kama mawimbi ya kawaida ya maji ambayo walitazamia yatatulia baada ya siku chache kwa kuamini hivyo familia yake ilifunga mlango unaoelekea ziwani na kuhifadhi vifaa vyao vya muhimu kwenye dari za nyumba.
Hata hivyo katika kipindi kisichozidi wiki moja maji yalianza kupanda kwenye vitanda na kuwalazimu kuondoka haraka sana huku wakiokoa vifaa vya matumizi ya nyumbani kama vile vijiko, sahani , vyakula, vitanda, nguo na vitabu vya shule vya watoto.
“ Hatukuwa na fedha za kukodisha gari, ilitubidi tuhamishe vitu kwa awamu ilikuokoa kile tunachoweza kukiokoa kabla giza halijaingia” Anasema
Eneo ambalo Daku alikuwa akiishi sasa hivi ni sehemu ambayo maboti yanatia nanga kwenye eneo hili.
‘Siwezi tu kukata tamaa na kuondoka’
Bi Kitonto Hussein(20) mmiliki wa mgahawa kwenye eneo la Ripon anasema:
“ mgahawa wetu umehamishwa mara kadhaa kutokana na maji yanayoendelea kutujia”
Mgahawa waBi Kitonto unatoa huduma nafuu kwa wakazi na wageni wanaotembelea mahali hapa na upande wa nyuma ya mgahawa huu unapakana kabisa na maji ya ziwa na hakuna ardhi yoyote inayotenganisha ziwa na mgahawa na hii inaamanisha kuwa iwapo kutatokea ongezeko la maji biashara yake itabidi ihamishwe.
Hata hivyo Bi Kitonto analazimika kuendelea kuwapo mahali hapa kwani ndipo mahali panapompatia kipato chake cha kila siku cha kujikimu kimaisha.
Mgahawa huu ni maarufu kwa chapatti na mayai au kama kinavyojulikana na wakazi wa hapo, chakula hicho ni maarufu nchini Uganda na inasemekana asili yake ni Jinja ambako bi Kitonto anafanya kazi.
Wale waliokaa
Biashara ya usafirishaji kwa kutumia maboti inafanyika kwenye eneo la Ripon. Kabla ya kina cha maji kupanda, biashara ya kusafirisha watu na mizigo ilikuwa imeshamiri hapa ikiwa ni pamoja na kuwasafirisha watalii wanaokuja kuangalia chanzo cha mto Nile na wafanya biashara wanaofanya kazi zao kwenye visiwa mbali mbali vilivyopo ziwani.
Awali kabla ya kina cha maji kupanda na baadhi watu kulazimika kuondoka, kulikuwa na wamiliki 15 wa maboti hata hivyo zaidi ya nusu waliondoka na kwa hivi sasa ni mboti 23 tu ndio yanayofanya kazi na wamiliki wapatao sita.
Kwa mujibu wa Bwana Abdu Nantabya mmoja wa viongozi wa eneo hili ni ukosefu wa maeneo ya kuegesha maboti changamoto ambayo imeletwa na mafuriko haya. Yeye akiwa mmoja wa wamiliki wa maboti anasema changamoto kubwa iliyoletwa na mafuriko haya ni ukosefu wa sehemu ya kuegesha maboti, kwani awali kulikuwa na sehemu ya kutosha kuegesha maboti mbali na makazi ya watu .
Hivi sasa inawabidi kugombania sehemu za kuegesha kwenye makazi ya watu na maduka.
Kwa mujibu wa bwana Nantabya, zuio la kutotoka kutokana na janga la Korona nalo pia limesababisha hali kuwa mbaya sana kwenye biashara ya usafirishaji majini. Hata hivyo, pamoja na changamoto hiyo bwana Ntabya anasema hawezi kuondoka Ripon.
“Nimewasomesha wanangu kutokana na fedha nilizokuwa napata kutokana kusafirisha watalii ziwani kupitia maboti yangu na ni mwendo wa dakika kumi na tano tu kwenda kilipo chanzo cha mto Nile” Anasema bwana Ntatabya.
Waundaji wa maboti haya ni wakazi wa Ripon. Bwana Muganga Hussein ni mmiliki wa karakana kubwa ya kuunda maboti yeye anasema wateja wake wakubwa ni wanawake kwa sababu wanawake hawa ndio wamiliki wakubwa wa biashara mbalimbali hapa Ripon.
Ifikapo saa 12 asubuhuhi wavuvi wanakuwa na kazi ya kuzichambua nyavu zao na kuondoa samaki walionasa pamoja viumbe vingine vya majini vilivyobakia kwenye nyavu.
Kupanda kwa kina cha maji kumesababisha baadhi ya viumbe vya ufukweni kama kaa na wengineo kunasa kwenye nyavu za wavuvi pamoja na samaki. Hivyo kazi ya kutenganisha samaki na viumbe wengine inafanyika na samaki wanapelkwa kwenye soko la mjini Jinja soko ambalo lipo mwendo wa dakika ishirini tu kwa kutembea.
Kati ya wakazi 574 wa eneo hili kiasi cha watu 80 mpaka 100 ni wavuvi. Ukiwajumuisha na wachuuzi wa samaki jumla yao inafikia 130.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya hapa bwana Abdu Nantabya, kabla ya mafuriko hayajatokea kulikuwa na wavuvi na wachuuzi wa samaki wapatao 250.
Mafuriko yalipozidi idadi yao ilipungua na hii inatokana na kwamba maji yakiwa kwenye kwenye kina cha kawaida, samaki wanakuwa karibu na ufukwe lakini kina cha maji kikizidi samaki wanakimbilia kwenye kina kirefu cha maji ambako inakuwa ni vigumu kuvuliwa.
Wavuvi hao wanafungua kapu lililojaa samaki wanaojulikana kwa jina la ‘Empuuta; kwa lugha ya Luganda.
Aina nyingine ya samaki wanaopatikana ziwani humo ni pampja na helikopta(bukolongo), (Mukene) na wengine wengi.
Kadhalika wavuvi hao wanaonyesha kaa aliyenasa katika neti za wavuvi hao kutokana na ongezeko la maji na inaelezwa kuwa kaa hao wanasababisha nyavu kuchanika.
Mwanaume mmoja analitoa begi la mkaa katika eneo ambalo ardhi inazama, eneo la kijiji cha Old Boma, wilaya ya Jinja, nchini humo.
Biashara ya mkaa ni kubwa jijini Jinja, mkaa unavushwa kutoka kisiwa cha Buvuma kwa kutumia boti hadi upande wa nchi kavu, ambapo pia husafirishwa kwenda katika vijiji nba miji mikubwa kwa kutumia magari makubwa na wakati mwingine bodaboda, ambazo zinatumiwa zaidi katika usafiri eneo hilo.
Tabasamu, kwa sasa
Wakati huo, bendi ya muziki ifahamikayo kama ‘Mata ga baana’ inaendelea kutumbuiza eneo hilo na wakazi wakitoa kiasi kidogo cha pesa. Eneo la nchi kavu, ni miongoni mwa maeneo ambapo bendi husimama zikitokea upande mwingine wa vijiji.
Wakati bendi ikiendelea kutumbuiza wakazi wa Ripon, kwa muda wanasahau hatari yao ya ardhi kumezwa na maji, hatari ya maji kubeba eneo na makazi yao.
Haijalishi kesho itakuwaje, kwa sasa, angalau, kuna muziki, kucheza na tabasamu kwa wote.
Hadithi hii ya #EverydayNile iliungwa mkono na InfoNile kwa ufadhili wa IHE-Delft Global Partnership for Water and Development.