Wavuvi na viwanda vya ndani viko hatarini kufilisika huku uvuvi haramu ukiendelea kushika kasi katika maji ya Ziwa Victoria, Tanzania
Na Sylivester Domasa
Taarifa hii imeandaliwa Kwa ushirikiano Na InfoNile, na kwa usaidizi wa kituo cha Pulitzer (Pulitzer Center).
Kuzunguka ndani ya maji ya Ziwa Victoria kwaajili ya kufanya shughuli za uvuvi wa samaki unazidi kuwa kam mchezo wa mieleka miongoni mwa wavuvi wa Tanzania.
Viwanda sita kati ya 12 vya kusindika samaki vilivyosajiliwa vimelala (Havifanyi kazi). Vingine Sita- Nile Perch, Vick Fish, TFP, VICTORIA, MZAWA na Mwanza Fish – pia vinafanya kazi chini ya asilimia 30 ya uwezo wao, kulingana na chama cha wavuvi na wasindikaji.
Wavuvi waliokuwa wamezoea kuvua kilo 500 kwa siku sasa wanahangaika kupata hata kilo tano, mara nyingi wanarudi mikono mitupu.
Wavuvi wengi huvua Sangara, Sato, Furu) na Dagaa, lakini Sangara wanaongoza katika mauzo na mapato.
Sasa maisha yao na ya wenyeji wanaotegemea shughuli za uvuvi jijini Mwanza, jiji la bandari kwenye mwambao wa Ziwa Victoria kaskazini mwa Tanzania, yamegeuka kuwa kilio, huku umaskini ukiwaandama, kama siyo tayari umeshameza uwepo wao.
Simulizi hii ya kusisimua inatokea katika eneo ambalo asilimia 3.3 ya uchumi unategemea uvuvi – ambao umepungua kwa kiwango kikubwa kutoka asilimia 7 mwaka 2011. Wenyeji na wataalamu wamehusisha kwa haraka ukweli huo na kupungua kwa hifadhi ya samaki katika ziwa hilo.
“Mwanza hakuna kiwanda ambacho kwa sasa kinafanya zanu mbili. Viwanda vya ndani sasa vinapata malighafi angalau baada ya siku mbili au tatu kila wiki,” alisema Katibu Mtendaji wa Chama cha Wavuvi na Wasindikaji Tanzania (TIFPA), Onesmo Sulle.
Hii yote ni matokeo ya shughuli za uvuvi haramu, zisizodhibitiwa na zisizoripotiwa (IUU) ambazo zimepunguza wastani wa samaki wanaovuliwa kwa siku hadi kufikia chini ya kilo tano katika kipindi cha miaka 10 tu.
Utafiti wa papo hapo kwenye viwanda hivi kati ya Desemba 2023 na Januari 2024 ulibaini shughuli chache zisizo na dalili za uendeshaji wa kawaida wa kiwanda. Baadhi ya viwanda vikiwemo Vick Fish na Tan Perch vilifungwa, na maafisa wa usalama walikataa kulizungumzia.
Viwanda hivi vilitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa makumi ya mamia ya watu wanaoishi karibu na Ziwa.
Katibu Mtendaji wa TIFPA, Onesmo Sulle, hakuweza kutoa maelezo ya kina kuhusu orodha ya viwanda vilivyoacha kufanya kazi, lakini alieleza kuwa vinavyofanya kazi havipati faida tena.
“Viwanda vinafanya kazi chini ya kiwango. Vipo kwa sababu tu lazima walipe mkopo na hisa,” alisema.
Jijini Mwanza na maeneno mengine yaliyo karibu na Ziwa Victoria, sekta ya uvuvi inategemea sana uhusiano wake mahususi kati ya viwanda vya ndani na mabenki.
Viwanda hupata mikopo ya kuendesha shughuli zao, ambayo, kwa upande wake, hutolewa ili kusaidia wavuvi wa ndani kwa kuwapatia zana za uvuvi, mafuta, chakula, na gharama zingine muhimu. Kwahiyo, wavuvi wanatakiwa kusambaza Samaki kiwandani sawa na thamani ya fedha walizosaidiwa.
Makubaliano hayo yenye manufaa kwa pande zote yanategemea utendaji kazi wenye tija kwa pande zote mbili. Kiukweli, kiwanda kikifungwa, fedha wanazopewa wavuvi hawazipati tena, lakini pia wavuvi wanaposhindwa kufikia lengo la kusambaza malighafi, kiwanda kiko hatarini kushindwa kurejesha mikopo yake na hivyo kusababisha kufilisika.
Masumbuko Polla, Anold Mashimba, na Magesa Jackson, waliowahi kujiita wavuvi wakubwa wa Ziwa Victoria, ambao kila mmoja aliendesha boti na kambi za uvuvi zaidi ya 50 huko Musoma (mkoani Mara), Sengerema, Ukerewe, na Magu (zote za mkoa wa Mwanza) na Kalebe mkoani Kagera, wote wametangaza kufilisika. Kuna mamia ya wavuvi wengine ambao pia wametoka kwenye ramani ya uvuvi.
Polla ametumia miaka 25 ya maisha yake yote katika shughuli za uvuvi lakini alisema alilazimika kuachana nao kutokana na Operesheni Sangara. Wizara ya Uvuvi na Mifugo nchini Tanzania ilianzisha Operesheni hiyo mwaka 2017, ambayo iliboresha kwa kiasi kikubwa hifadhi ya samaki katika Ziwa Victoria kwa kukamata zana haramu za uvuvi, kukamata zaidi ya watu 1,000, na kupunguza shughuli za uvuvi haramu kutoka asilimia 60 hadi 25.
Kulingana na mvuvi huyo, operesheni hiyo iliharibu sehemu kubwa ya mali zake. “Madhara yalikuwa makubwa …” Polla alisema.
Leo, Polla anasema alikuwa akitumia karibu lita 40 za petroli kuvua kilo saba tu za Samaki, wakati mwingine anatoka patupu.
“Hiyo inakuwa changamoto kubwa sana kwangu na isiyo endelevu wala matumaini ya kuihuisha. Ilinibidi kufanya uamuzi mgumu wa kuhamia katika kilimo,” alisema.
Kukithiri kwa uvuvi haramu katika ziwa hilo kumemfanya Polla na wavuvi wengine wengi kukata tamaa kuhusu matarajio ya kurejea ziwani.
Mashimba alirejea kauli sawa na Polla, akisisitiza kwamba hakuna uwiano sawa wa gharama na faida katika mazingira ya sasa ya uvuvi.
Sera ya Taifa ya Uvuvi Tanzania ya mwaka 2015 imekiri uvuvi haramu kuwa ni changamoto ya pili katika kusimamia sekta ya uvuvi nchini. Kupitia sera hii, serikali iliapa kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti ili kukabiliana na uvunjaji sheria ndani ya sekta hiyo pamoja na mamlaka ya kushughulikia uhifadhi na ulinzi wa rasilimali na mazingira ya uvuvi katika maeneo ya bahari na maji baridi.
Pia, serikali iliahidi kushirikiana na wadau ili kuondoa zana haramu na vitendo haribifu vya uvuvi.
Hii, hata hivyo, sivyo ilivyo kwa Ziwa Viktoria, ambako uvuvi unachukua zaidi ya asilimia 60 ya samaki wote wanaovuliwa nchini.
Wavuvi hapa wanazidi kupeleka Makokoro,” nyavu za Timba, Trela, na Nyavu za Sangara zenye ukubwa wa chini ya milimita 17 – zote zikiwa ni zana haramu za uvuvi, kulingana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI).
Hakujaanzishwa Mamlaka ya kushughulikia uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi kwenye maji yasiyo na chumvi. Wavuvi pia wanasema ufuatiliaji na udhibiti katika ziwa ni wa msimu, kwa kawaida wakati wa shughuli maalum.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alithibitisha kuwa chini ya asilimia 40 ya doria 8,400 zilizopangwa zilifanyika katika mwaka wa fedha 2023/24.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa wizara inapanga kupeleka ndege 85 zisizo na rubani kufanya doria kwenye vyanzo vya maji nchini.
Takwimu rasmi za serikali za Wizara ya Fedha zinaonyesha kuwa mauzo ya Sangara nje ya nchi kati ya mwaka 2019 na 2022 yalipungua.
Kutoka takriban tani 25,000 za Sangara zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 128 zilizouzwa nje mwaka 2011, mauzo haya ya samaki yaliongezeka maradufu mwaka 2015, lakini yakapungua kutokana na kuongezeka kwa matukio ya uvuvi haramu ambao ulimaliza samaki.
Jitihada za kurekebisha, ikiwa ni pamoja na Operesheni Sangara I, II, na III, zilikuza mapato hadi kufikia Tsh bilioni 17.6 (USD $6.9 milioni) ilipofika mwaka 2019, na uchumi wa samaki nchini uliongezeka.
Lakini kutoka 2019, mauzo ya nje yalianza kupungua taratibu. Ripoti ya hivi karibuni ya utafiti wa serikali inaonyesha kuwa kufikia mwaka 2022, mapato kutokana na mauzo ya Sangara nje ya yalipungua hadi Tsh bilioni 8.9 (USD $3.5 milioni).
Kushuka huko kwa mapato pia kumesababisha familia na jamii zinazotegemea shughuli za uvuvi kuelemewa.
“Hakuna samaki,” alisema Paulina Misalaba mwenye umri wa miaka 65, anayeishi kitongoji cha Kigoto wilayani Sengerema, karibu kilomita 56 kutoka Mwanza.
“Maisha yangu yote nimekuwa nikitegemea ziwa hili. Uvuvi na kufanya baadhi ya shughuli zinazohusiana na uvuvi. Lakini sasa hakuna samaki na watu wamekata tamaa,” Misalaba alisema.
Wakazi katika jamii hii ya wavuvi walisema walikuwa wakitumia muda mfupi kupata Sangara na Sato wengi kwa siku.
Lakini sasa, wanakabiliana na hali ya sintofahamu, bila kuwa na uhakika iwapo ukosefu wa samaki unahusiana na mabadiliko ya hali ya hewa, uvuvi haramu, uzembe wa serikali katika kutekeleza afua za udhibiti mkali, au kutowajali wenzao ambao wanashindwa kufikiria madhara ya kesho yao.
Alexander Onesmo, ambaye amekuwa akitengeneza nyavu haramu kwa miaka sita iliyopita katika eneo hili, alisema kupungua kwa samaki ni matokeo ya hatua zao za pamoja.
Onesmo alisema wavuvi wadogo kama yeye wana uchaguzi mdogo sana wanapokuwa ziwani, wavuvi wakubwa na wa kati wananyonya kila sehemu ya ziwa.
“Serikali inaonekana kutojali… Sijui kama kutojali kama hivyo kunatokana na kujali mifuko yao au malipo yao ya kodi,” alisema Onesmo, ambaye alikuwa akitengeneza nyavu yake mpya (haramu) ya uvuvi. “Hata tunapopeleka mabeberu hawa kwa polisi, safari nzima inageuka kuwa hali ya sintofahamu.”
Onesmo na wavuvi wengine kadhaa hulinda ipasavyo Makokoro yao, ambayo hayaruhusiwi.
Uvuvi wa Furu (Neke) watumika ili kukamata Sangara
“Uvuvi ni mchezo wa kuwinda,” Philemon Nsinda, mwanabiolojia wa uvuvi na mtafiti mkuu katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ya Mwanza, aliiambia Daily News/InfoNile. Ujio wa teknolojia umewezesha kutoka kwenye uvuvi wa nyavu za vikapu na nyavu za uzio hadi kwenye utumiaji wa nyavu kubwa zinazovutwa na boti zenye Machine imeruhusu wavuvi kuwinda katika maji ya kina na aina yoyote. Hata hivyo, kupungua kwa akiba ya samaki kumesababisha mapigano ya mara kwa mara kati ya wavuvi wa Dagaa na wenzao wa Sangara.
Nsida analaumu wavuvi wa Sangara kwa tatizo hilo.
“Wavuvi hawa (Sangara) ndio wabunifu wa uvuvi haramu. Wote wanajihusisha na uvuvi haramu,” alidai.
Alisema wavuvi hao wanazidi kutumia mbinu mpya za uvuvi wa viwandani, wanashusha nyavu zao katika ziwa hilo dogo na wanapunguza ukubwa wa matundu ya nyavu zao na kuwa kama ya wavuvi wa dagaa.
“Mara tu unapomfikia mvuvi wa dagaa, [Hizo Nyavu] hukatwa na kutupwa ziwani au samaki waliokuwa wamenaswa wanachukuliwa na wavuvi haowa dagaa.”
Uvuvi wa Uvutaji- Ni njia ya uvuvi inayohusisha kuvuta nyavu zenye umbo la koni kwenye maji kwa kutumia mitumbwi/boti, ulianza mwaka 1998. Inaaminika kuwa wavuvi wanaotumia njia hiyo huwasaidia wavuvi kuwa na nafasi nzuri ya kuongeza samaki wao kila siku kuliko wale ambao huweka tu nyavu zao za uvuvi.
Kanuni za uvuvi wa maji safi ya Tanzania ziko kimya juu ya matumizi ya aina hii ya nyavu, ambayo imesababisha kuongezeka kwa migogoro kati ya wavuvi.
Dagaa ni chanzo muhimu cha lishe kwa familia nyingi za hali ya chini na hata za kipato cha kati nchini Tanzania. Wavuvi walio wengi katika Ziwa Victoria leo wanajihusisha na uvuvi wa dagaa, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Muungano wa Wavuvi (FUO) jijini Mwanza, Juvenary Matagiri.
Hata hivyo, Uvuvi wa Furu wa maji baridi pia unazidi kutumika kama njia ya kuhalalisha shughuli za uvuvi hatari. Idadi kubwa ya wavuvi wa Sangara kwa sasa wanachagua kufanya uvuvi wa dagaa kwa nia mbaya ya kulenga Sangara.
Serikali ya Tanzania imeidhinisha rasmi matumizi ya nyavu zilizotengwa kwa ajili ya uvunaji wa dagaa. Wakati nyavu za milimita 10 zikiwa ni halali, nyazu za milimita tano zinazotumiwa na wavuvi wengi ni kinyume cha sheria.
Leo, baadhi ya wavuvi wa Sangara wanatumia nyavu za dagaa kuvulia Sangara, badala ya nyavu zake halali, ambazo unapaswa kuwa na ukubwa wa matundu unaozidi inchi 7 (milimita 177.8). Lakini nyavu ndogo hukamata Sangara, ambayo huathiri uwezo wa spishi kuzaliana.
Utafiti wa hivi karibuni wa Mfumo wa Uvuvi wa Ziwa Victoria, uliochapishwa kwa pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania na Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria (LVFO) mwezi Aprili 2023, unaonyesha kuwa asilimia 98 ya nyavu zinazotumiwa na wavuvi wa dagaa waliosajiliwa ni nyavu ndogo.
Na karibu nyavu zote hizi ndogo zina ukubwa wa matundu ya milimita tano au chini.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilikubaliana kwamba kiwango cha chini cha Sangara wanaovuliwa wawe ni sentimeta 50. Lakini “wengi wanadai kuhusika katika uvuvi wa dagaa, ndiyo maana hilo kwao ni kama Ilani tu.
Wanavua samaki wadogo kama Sangara chini ya sentimeta 20 kwa jina la dagaa … na samaki hao wako kila mahali sokoni na sehemu za chakula,” Matagiri alisema.
Uvuvi wa dagaa hapa ni biashara inayostawi kila wakati. Sekta inayostawi ya uvuvi wa dagaa kwenye ziwa hilo hutengeneza mandhari nzuri ya kuvutia nyakati za usiku.
Ukiingia Mwanza, utaona taa nyingi kwenye maji zinazotumika kwajili ya shughuli za uvuvi zinafanana na anga la jiji la New York. Kutoka Kemondo mjini Bukoba hadi Mwanza kupitia Musoma mkoani Mara, taa hizi zinamulika njia- Asante kwa wavuvi wa dagaa wenye shughuli nyingi.
Kutoka kwenye matumizi ya taa za mafuta ya taa na betri za asidi- hadi sasa taa zinazotumia nishati ya jua, wavuvi hutumia mbinu za kuwasha taa ili kuvutia samaki na kunasa dagaa wakati wa usiku. Lakini matumizi ya taa zinazotumia miale ya jua na betri za asidi ya risasi zimesababisha mkanganyiko kati ya wavuvi, huku wavuvi wengi wa dagaa kwa sasa wakichagua njia ya pili kutokana na imani potofu na kutaka mwanga zaidi.
Taasisi ya Uvuvi na Utafiti Tanzania imeonyesha wasiwasi wake katika mazingira juu ya matumizi ya betri zinazoweza kusababisha uchafuzi wa mazingira na kuathiri vibaya ufugaji wa samaki na mazingira ya ziwa.
“Kama hatua za haraka hazitochukuliwa haraka, idadi ya Sangara itapotea kabisa katika miaka ijayo,” Matagiri alionya.
Kulingana na TAFIRI, karibu nusu ya spishi 500 tofauti za Furu katika Ziwa Victoria zimetoweka, pamoja na samaki wengine kadhaa kama vile aina fulani za Sato, kutokana na kuletwa Sangara katika ziwa Victoria miaka ya 1950-1960.
Lakini taasisi hii inafichua kuwa kupungua kwa idadi ya Sangara leo katika ziwa kumeruhusu kuibuka tena spishi zingine kadhaa za samaki zikiwemo Sato na Furu.
Leo, viwanda vya kusindika Sangara ambavyo awali vilikuwa vikifanya kazi zake angalau mara mbili vinashindwa kupata hata kilo tano za samaki. Ingawa vinakosa usambazaji wa samaki, soko la ndani linashuhudia ugavi mkubwa wa samaki, wengi wao wakiwa ni samaki walio chini ya kiwango.
Sangara mkubwa zaidi aliyewahi kuvuliwa alikuwa na uzito wa kilo 133.6 na alikuwa na urefu wa sentimita 167 karibu miongo miwili iliyopita. Uvuvi unaoendelea hivi karibuni ni chini ya kilo 50.
Mwanaikolojia wa Uvuvi Enock Mlaponi alieleza kwa kina kwamba Sangara wanaweza kukua hadi kufikia urefu wa karibu sentimita 200, wakiwa na uzito wa kilo 160 au pauni 360. Samaki hao hutaga mayai madogo kati ya milioni 1.5-19, ambapo asilimia moja tu ndiyo yanarutubishwa na kuishi.
Samaki wanaweza kuishi hadi miaka 16 na wanaweza kuanza kuvunwa wakiwa na umri wa miezi 18.
Kuongezeka kwa uvuvi haramu, usiodhibitiwa na usioripotiwa (IUU), Magonjwa, Uharibifu wa mazingira, Mabadiliko ya hali ya hewa na Ukosefu wa malisho huamua hatima ya kila samaki katika ziwa.
Kuongezeka mahitaji ya Mabondo kwa Wa-Asia kunaongeza ugumu na uvuvi wa kupitiliza
Wadau wa sekta hiyo walisema kuwa kupungua kwa ukubwa wa Sangara katika ziwa pia kunatokana na kuongezeka kwa mahitaji ya Mabondo katika masoko ya Asia.
Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe ili kulinda usalama wake, alisema kumekuwa na uhitaji mkubwa wa Mabondo ya Samaki hasa katika nchi za India na China, jambo ambalo linawasukuma wavuvi kuwinda Sangara wa aina yoyote.
Jesca Adams, mtaalamu wa Samaki (Ichthyologist) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alionya kuwa uvunaji wa Sangara kabla ya wakati unapunguza uwezo wa uzazi wa samaki.
“Inavuruga umri wa Samaki na kuchangia kupungua kwa ukubwa wa samaki kwa ujumla, na kusababisha uhaba wa Sangara waliokomaa katika mfumo wa ikolojia,” alisema.
Mabondo ya Samaki hutolewa katika Sangara. Jijini Mwanza, kuna watu wachache wanaojihusisha na usindikaji na usafirishaji Mabondo kwenda Asia. Watu hawa wameweka kambi karibu na maeneo ya uvuvi na masoko, ambapo wavuvi wadogo na wauzaji wa samaki hukusanya na kuwauzia.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, sheria na kanuni za Tanzania zinatambua Mabondo kama mazao makuu ya samaki, na sheria inasalia kwa ujumla katika kuwasaidia wafanyabiashara ili wanufaike na biashara hii mpya yenye faida kubwa.
Jijini Mwanza, kilo moja ya Bondo la Samaki inauzwa kati ya Tsh.750,000 na 900,000 (karibu USD $350). Kilo moja ya samaki, kwa kulinganisha, inauzwa kati ya Tsh.4,000 na 8,000 tu.
Nchini China, kulingana na Business Insider, kilo inaweza kuleta kati ya USD $450-1,000. Mabondo ya samaki nchini China inaonekana ni matamu na inachukuliwa kuwa ishara ya utajiri na ustawi.
Wakati wavuvi wa Tanzania wakidai mabondo hayo hutumika kama malighafi kuzalisha nyuzi za Operesheni (Sutures) nchini China – baada ya kufanyika kwa upasuaji, nchini China mara nyingi hutolewa kama zawadi kwenye matukio muhimu, zinazotumiwa katika matriki ya ziada ya seli inayopatikana katika tishu mbalimbali za mwili na pia huhifadhiwa kama uwekezaji.
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, Machi mwaka jana alisema kuwa, Tanzania ilikuwa katika majadiliano na Alibaba– jukwaa la China la biashara ya jumla ya kimataifa, ili kuwezesha wafanyabiashara wa mabondo ya samaki nchini Tanzania kupata soko la China moja kwa moja.
Bondo la Samaki ni bidhaa ya samaki yenye thamani kubwa katika soko la kimataifa. Usafirishaji wa mabondo ya samaki katika mwaka wa 2019 ulichangia dola za Kimarekani milioni 77.9 nchini Tanzania; Dola milioni 76.3 nchini Uganda na dola milioni 3.7 nchini Kenya. Nchi hizo tatu ziliuza nje jumla inayokadiriwa ya tani 1,640.19 za Sangara mnamo 2019.
Kutokana na mahitaji haya yanayoongezeka, wavuvi nchini Tanzania wanawinda kwa nguvu Mabondo ya Sangara.
Haja ya ufuatiliaji na udhibiti zaidi
Meneja Operesheni katika Kiwanda cha Usindikaji wa Sangara jijini Mwanza, Renatus Elius, moja ya viwanda vilivyoathiriwa na vitendo vya uvuvi haramu, alisema serikali inatakiwa kuongeza kasi katika udhibiti na ufuatiliaji.
Alipendekeza haja ya kuiga mtindo wa ufuatiliaji unaotumiwa nchini Uganda kwa kupeleka jeshi katika ziwa.
“Kwa bahati mbaya, inaonekana kama kazi nzito kupambana na kuibuka kwa kasi kwa uvuvi haramu katika maji yetu. Ninaiomba sana serikali yetu kufuata nyayo za Uganda na kuchukua hatua madhubuti,” alisema, na kuongeza: “Inakatisha tamaa … Sina shaka kwamba kama wanajeshi wangechukua udhibiti, utulivu ungerejeshwa haraka katika sekta ya uvuvi. Lakini kwa sasa tunahangaika tu.”
Kuanzia mwaka 2014 hadi 2022, Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Mwanza iliendesha kesi mfululizo zinazohusu uvuvi haramu katika wilaya mbalimbali zikiwemo Mwanza, Nyamagana, Magu, Sengerema, Misungwi, Chato, na Geita. Geita mara kwa mara walirekodi kesi nyingi.Licha ya kuendelea kuwepo kwa uvuvi haramu, takwimu zinaonyesha kuwa wasiwasi juu ya tatizo hilo ulishika hatamu mwaka 2014-2015, ambapo jumla ya kesi 205 na 211 zilifunguliwa mahakamani. Idadi hii ilipungua haswa kutoka 2016-2021, ingawa iliongezeka kidogo tena hadi kufikia kesi 145 mwaka 2022.
Shirika la Uvuvi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria (LVFO), linakiri kwamba hatua za usimamizi ilizopendekeza – kama vile kupunguza uwezo wa uvuvi na kufunga msimu wa uvuvi kwa angalau miezi miwili kila mwaka- hazijapitishwa.
Mkakati huu ulikubaliwa katika ngazi ya kikanda (Tanzania, Kenya na Uganda) mwaka 2021 ili kupunguza juhudi za jumla za uvuvi na kulinda mazalia au samaki kabla ya kuzaa.
Je, uongozi mpya utatoa matumaini kwenye sekta ya uvuvi?
Mkurugenzi wa Huduma ya Uvuvi katika Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mohamed Sheikh, alikiri kuhusiana na kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria.
Kulingana na utafiti wa hivi punde uliofanywa na serikali mwaka 2023, kulikuwa na upungufu mkubwa wa asilimia 33 wa idadi ya Sangara tangu 2014.
Sheikh aliteuliwa Novemba mwaka jana kufuatia uamuzi wa Waziri wa kumfuta kazi mtangulizi wake Stephen Lukanga kutokana na utendaji duni na kushindwa kutekeleza mifumo kabambe ya kukomesha uvuvi haramu.
Sheikh alisisitiza kuwa ulinzi wa rasilimali za samaki ni jukumu letu sote na wala si la Wizara. Alisema wananchi wanaendelea kufahamu madhara yatokanayo na uvuvi haramu.
“Wizara inaandaa njia bora ya kushughulikia suala hili kwa kina, ikilenga uboreshaji mkubwa katika sekta… hii itachukua pengine miezi sita,” alisema.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, wizara imewashirikisha wakurugenzi watendaji wa wilaya zinazozunguka Ziwa Victoria ili kuimarisha juhudi za mashirikiano. Mipango inaendelea ya kuanzisha vituo 16 vya ufuatiliaji na utoaji taarifa ili kukomesha shughuli za uvuvi haramu, kwa mujibu wa Sheikh.
Wizara pia imetenga takriban Tsh. 1 bilioni (karibu dola 400,000) kulinda maeneo hatarishi, muhimu kwa kudumisha hifadhi endelevu ya samaki.
“Kuna mengi tunataka kufanya ili kuhakikisha sekta hiyo inarejesha utukufu wake uliopotea,” Sheikh alisema, akikiri kwamba kuna haja ya kupitia upya kanuni za uvuvi ili kupambana na uvuvi haramu katika bahari na maji baridi.
Serikali ilisema kumekuwa na ugumu wa kulinda ziwa hilo, hasa kwa kutumia boti za mwendo kasi ambazo ni gharama kubwa, na inapanga kupitisha matumizi ya ndege zisizo na rubani (UAV) ili kuimarisha ufuatiliaji.
Pia inajadiliana na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (the Nelson Mandela African Institute of Science and Technology) ili kutengeneza teknolojia ya hali ya juu ya kuweka kanuni na kufuatilia shughuli zote za uvuvi katika ziwa hilo. Hii ni pamoja na kusakinisha chip (installing chips ) kwenye boti zilizosajiliwa ili kufuatilia na kufuatilia mienendo yao, hatimaye kuimarisha hatua madhubuti za uhifadhi.
“Tunachukua hatua kadhaa, lakini sasa tunalenga kuongeza uelewa, hasa kwa kushirikisha wadau wengine kama vile Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), ili watambue kuwa uvuvi haramu utawakosesha mapato.
“Kupambana na uvuvi haramu pekee haitoshi; lengo letu ni kulinda mazalia ya samaki na hili litatunufaisha sana,” alisema na kusisitiza kuwa serikali itarekebisha kanuni za uvuvi haraka iwezekanavyo.