Janga la Covid-19 Lilivyowakatisha Tamaa Wakulima Wakutegemea Unyunyiziaji Maji Nchini Kenya na Uganda

Janga la Covid-19 Lilivyowakatisha Tamaa Wakulima Wakutegemea Unyunyiziaji Maji Nchini Kenya na Uganda

Dicta Asiimwe na Ruth Keah

Tabitha Kisinga ni mkulima ambaye alikua akitegemea sana mvua kutekeleza shughuli zake za kilimo. Ni mama wa watoto kumi. 

Hadi mwaka wa 2017, alikuwa akitegemea msimu wa mvua ya vuli na mwaka ili kutekeleza kilimo katika shamba lake eneo la Kinango-Kaunti ya Kwale nchini Kenya.

Lakini kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi  yanayoshuhudiwa ulimwengu mzima, ukulima wa kutegemea mvua umekuwa tatizo kubwa hivyo kuwa vigumu kwa Tabitha na mume wake kutegemea mvua kufanya kilimo,kupata mazao ili waweze kuuza na kujikimu kimaisha. 

Mwaka wa 2016, Tabitha alisema walishuhudia msimu mrefu wa kiangazi kiasi cha kwamba bidhaa zote alizopanda shambani zilikauka. Hapo ndio akajua kwamba endapo yeye na mume wake hawatabadilisha mfumo wa kutekeleza kilimo basi huenda familia yao ikaangamia kutokana na makali ya njaa,kwani hawakuwa na njia nyengine ya kujipatia mapato.

image 1
Mama Tabitha Kisinga

Akiwa na mume wake na wakulima wengine 21 kutoka eneo hilo la Kinango, walishirikiana na kuchanga shilingi Ksh 70,000 ($615) wakanunua kipande cha ekari 3 za ardhi karibu na bwawa la Ngangani eneo hilo la Kinango ili waanzishe kilimo cha unyunyiziaji maji. 

Zaidi kila mwanachama alitoa shilingi Ksh 22,000 ($193) ili kununua mapipa ya kuwekea maji na mtambo wa generate ili kusaidia kupiga na kufikisha maji shambani. Baadaye kikundi hicho kilijisajili kwa serikali  kwa kima cha shilingi Ksh 1,100 ($10) ili kuanzisha mradi wao huo.

“Tulianzisha mradi huu mwaka wa 2017 ili kutusaidia kufanya ukulima ili tuweze kumaliza hali ya umaskini na ukosefu wa chakula katika jamii yetu,” Alisema Tabitha ambaye ni mwenyekiti wa mradi huo- Ngangani irrigation scheme. 

irrigation in Kwale
Unyunyuziaji maji Kwale

Baadhi ya bidhaa ambazo wanachama hao wanapanda ni pamoja na Tomato, Sukuma wiki, Vitunguu, mchicha, Mnavu na Tikiti – Maji.

Licha ya kikundi hicho kufanya vyema kiasi cha wanachama kujiendeleza kwa kujenga nyumba za kudumu, kujinunulia mifugo kutokana na pesa walizopata baada ya kuuza mazao yao na kujisimamia kichakula, ujio wa virusi vya Corona humu nchini Kenya ulibadilisha mfumo wao wa ukulima. Hii ni kutokana na sheria zilizowekwa na serikali ikiwemo kutosafiri kutoka eneo moja hadi jengine na masaa ya kutotoka nje usiku maarufu Kafyu.

Kulingana na Tabitha, ilikua vigumu kwao kusafiri maeneo mbalimbali kuuza bidhaa zao. Huku wateja wao pia wakikosa kufika shambani mwao kununua bidhaa zao. Hivyo basi kusababisha kuoza kwa takriban nusu ekari ya tomato zilizokuwa zimenawiri sana.

Usemi ulioungwa mkono na baadhi ya wakulima ambao ni wanachama wa mradi huo.

Zaidi ya hayo, bei ya mafuta pia ilipanda. Ikawa vigumu zaidi kwa wakulima hao kupata bidhaa hiyo kutokana na pesa za mazao yao. 

Timothy Mwaniki ambaye ni katibu mkuu wa kikundi hicho, alisema ilikuwa vigumu kwao kukimu bei hiyo ya juu ya mafuta kutokana na pesa za mapato yao.Alisema ilimlazimu kila mwanachama kutoa pesa zake mfukoni kujalizia ili wapate bidhaa hiyo muhimu.

Halmashauri ya uthibiti wa kawi na mafuta ya petroli nchini Kenya-(EPRA), iliongezeka lita moja ya petroli kwa asilimia 9.27 , kutoka shilingi 44 hadi shilingi 491.5.

Kenya ni mojawapo ya nchi ambazo zinaendelea kukabiliana na tatizo la njaa. Kufikia Julai mwaka wa 2019, zaidi ya Wakenya 2 milioni walikuwa wanakabiliwa na ukosefu wa chakula.Hii ni licha ya Kenya kutegemea ukulima kwa njia kubwa zaidi kujikimu kiuchumi.

Ukulima huchangia katika uchumi wa nchi kwa kiwango cha asilimia 24.Hii ni kulingana na ripoti ya mwaka 2019 ya Taasisi ya Masomo ya Usalama – Institute for Security Studies.Ili kufikia hatua ya kuwa na hakikisho la chakula cha kutosha kufikia mwaka 2030, itahitajika kuongezea mapato na mavuno ya chakula kwa asilimia 75.

image 3
Wakulima wa Ngangani shambani

Laureen Achieng ni afisaa mkuu wa mipango katika shirika la Kenya National Farmers Coperation. Alisema kama shirika ujio wa virusi vya Corona nchini Kenya ulisababisha wao kuanzisha mpango wa kusaidia wakulima, ambapo wao wenyewe wanatambua shida walizo nazo kisha wapendekeze mradi wanaouna utawasaidia kutatua shida hiyo ili waweze kuzalisha chakula bila ugumu hata wakati wa majanga.

‘Tunataka miradi itoke kwa wakulima wenyewe, waandike mapendekezo rahisi waseme hivi ndio tunataka kufanya ili tujenge uthabiti wa ukulima hata wakati wa majanga kama vile Covid-19 na mabadiliko ya tabia nchi,’Alisema Laureen.

Nchini Uganda, hali haikuwa tofauti kwa wakulima wanaotegemea unyunyiziaji maji mashamba yao wakati wa ujio wa virusi vya Corona katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Kufungwa kwa masoko ilikuwa shida kubwa kwa Noeline Nakanwajji – mkulima wa bidhaa tofauti tofauti kutoka eneo la kati ya nchi hiyo ya Uganda la Ankole-Masaka. Mwaka wa 2019, Nakanwajji alibahatika kupata pipa la kuhifadhia maji linalotumia  nguvu za miale ya jua linaloweza kuhifadhi maji lita 10,000 kutoka kwa Huduma ya kitaifa ya ushauri wa kilimo Uganda – Uganda’s National Agricultural Advisory Services (NAADS). 

Ufadhili huo ulimuwezesha Nakanwajji kutekeleza unyunyiziaji maji mazao yake ikiwemo tomato na miche ya matunda. 

image 4
Noeline Nakawanji

Lakini Nakanwajji alisema juhudi zake hazikuzaa matunda, kwani bei ya matunda ilishuka sana kutokana na sheria ya kufungwa kwa maeneo Fulani ili kuzuia msambao wa virusi vya Corona. 

 “Tulikuwa tukipanda tomato kwa ajili ya kuzisafirisha taifa la Sudan Kusini na Kenya, lakini soko likapungua sana wakati wa Covid-19,” Alisema Nakanwajji.  

Kulingana na Nakanwajji, sanduku moja la tomato lilikuwa likiuza pesa za Uganda Ush 400, 000 ($112.6) lakini wakati wa Covid-19 ikapungua hadi pesa za Uganda Ush 100,000 ($28.2). Hatua iliyosababisha yeye kushindwa kuwekeza zaidi katika kilimo chake.

Margaret Tabaruka pia ni mkulima, alifaidika na msaada huo wa mapipa yakusaidia kunyunyizia maji kutoka kwa NAADS. Anapanda mahindi,viazi na pia anaweka mifugo.  

Alisema kipindi cha Covid-19 kilishuhudia wao kupunguza bei za bidhaa zao hivyo basi kutoweza kufanya kilimo kikamilifu, huku wakulima wengine wakichukua mapumziko kabisa.

NOELINE AKIWA SHAMBANI 2 scaled
Noeline akiwa shambani

Kulingana na ripoti ya pamoja  mwaka 2005 kutoka kwa shirika la chakula duniani FAO na benki ya Afrika ya maendeleo -African Development Bank (AfDB) ukulima wa unyinyizaji maji nchini Uganda hupanda kwa asilimia 0.05 kila mwaka,mabadiliko ya tabia nchi yakisukuma wakulima wengi kuwacha ukulima  wa kutegema mvua.

Afisaa wa mipango kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kutoka shirika la FAO Daktari Kennedy Ignokwe alisema, wakulima wengi walikumbatia ukulima wa unyunyizaji maji nchini Uganda kabla ya janga la Virusi vya Corona. Hii ni  kwasababu ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoshuhudiwa ulimwenguni. Kwani wakulima hawakuweza kutegemea mvua pekee.

Hata hivyo alikriri kuwa ujio wa janga la virusi vya Corona ulisimamisha kasi hiyo kwa wakulima.

Jonathan Bukenya ni mhandisi kutoka shirika la  Davis& & Shirtliff, shirika linalouza vifaa vya kusaidia unyunyiziaji maji shambani. Alikubali kuwa ujio wa virusi vya Corona uliathiri shughuli zao vibaya sana.

‘Kabla ya ujio wa virusi vya Corona tulikuwa tukiuza vifaa kwa wingi kwa wakulima nchini Uganda, lakini kwa sasa wakulima wengi wamekosa ari ya kununua vifaa hivyo,’ Alisema Bukenya.

Bukenya alisema ununuzi huo umepungua kwa asilimia 60 kwa sasa ikilinganishwa na wakati kabla virusi vya Corona vilipoingia nchini Uganda.

Makala haya yametayarishwa na Ruth Keah kutoka Kenya pamoja na Dicta Asiimwe kutoka nchini Uganda. Yamefanikishwa na InfoNile na kufadhiliwa na IHE-Delft Water and Development Partnership Programme.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts