Na Fredrick Mugira

Punde Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alipoongeza muda wa amri ya kutotoka nje nchi nzima ili kukomesha ueneaji ya virusi vya corona kwa siku 21 zaidi mwezi wa Aprili, Birungi Joyce ambaye ni mama wa nyumbani katika eneo la Kacerere, Bisya, ndani ya wilaya ya milima ya Buhweju, alihisi wasiwasi.

Tembe za kuzuia ushikaji mimba, ambazo yeye humeza kila siku, zilikuwa zimekwisha. Birungi alidhania kwamba baada ya amri ya kutotoka nje ya muda wa awali wa siku 14, yeye angesafiri; muendo wa takriban kilomita 30 kutoka kwake nyumbani, akitumia texi ya pikipiki, ili kununua tembe kutoka duka lake la dawa, lakini alipigwa na butwaa, kwa vile amri hii iliongezwa kwa siku 21 zaidi.

Hakuwa na budi, ila kujinyima. Hata hivyo, mumewe hakuwa tayari.

“Wakati mwingine, alinipiga kwa kukataa kushirikiana ngono,” aeleza Birungi huku akiongezea kusema, “hata hivyo, nilivumilia. Ilikuwa bora hivi, kuliko kupachikwa mimba na kujifungua mtoto wetu wa sita.”

Birungi, aliye na umri wa miaka 35, asema kwamba wametaabika kulisha wana wao watano na kwamba hawawezani na gharama ya mtoto mwingine zaidi.

Pasipo kujua afanye nini lingine, Birungi alitafuta ushauri kutoka kwa wanawake kadhaa kijijini, ambao walimshauri kutafuata usaidizi kutoka kwa maafisa wa EPHWOR, shirika lisilo la kiserikali na ambalo linaongozwa na wanawake.

Hapo awali, wanawake hawa waliwatazama maafisa wa shirika hili wakizungumza katika runinga. Walinakili nambari zao za simu.

Kisha baadaye, Birungi akapigia simu shirika hili. Siku moja baadaye, maafisa wa shirika hili walizuru kijiji chake na kumpa tembe za kuzuia upachikaji mimba zitakazodumu miezi miwili.

IMG 8545

Milioni saba za mimba ambazo hazikupangwa

Asingelikuwa amepokea msaada huu, basi pengine Birungi angelikuwa anabeba mimba ambayo hakuipangia, hivyo kuwa miongoni mwa “mimba milioni saba ambayo haikupangwa,” na ambazo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu, UNFPA “linatarajia kutokea,” ikiwa hali ilioko sasa, “ya amri ya kutotoka nje itaendelea kwa miezi sita hivyo kutatiza huduma muhimu kutokana na Covid-19.”

Lakini sasa, yuko miongoni mwa wanawake 300 kutoka wilaya nane zilizoko eneo la kusini magharibi nchini Uganda, ambaye EPHWOR, lijulikanalo pia kama shirika la kudumisha haki za wagonjwa na wauuguzi nchini Uganda, limenusuru kutokana na mimba ambazo hazikupangiwa wakati huu wa amri ya kutotoka nje iliyotokana na Covid-19.

Wanawake hawa wanatoka wilaya za Mbarara, Ibanda, Buhweju, Sheema, Isingiro, Rwampara, Kiruhura na Kazo.

Shirika la EPHWOR lilianzishwa mnamo mwaka wa 2017. Limekuwa likiendesha shughuli zinazolenga kutetea na kudumisha haki za wanawake, haki zao za kimapenzi na afya ya uzazi pamoja na haki za wagonjwa walioko mashambani pamoja na maeneo ya majiji nchini Uganda.

Dkt. Aruho Amon Kategaya, Mshauri wa Tiba na Maswala ya Afya ya Uzazi katika EPHWOR asema, juhudi hii, “itazuia wanawake kupachikwa mimba kiholela huku nchi ya Uganda ikipiga hatua muhimu katika viwango vya ugavi wa mbinu tofauti za upangaji uzazi.”

Kiwango cha uwezo wa kuzaa nchini Uganda mwaka wa 2020 ni 4.78 kwa kila mwanamke.

Rindima la watoto

Imekuwa vigumu kwa wanawake na wasichana waliobalehe ambao walijisajilisha katika mpango wa uzazi nchini Uganda na nchi zingine zinazoendelea, kupata uzazi wa mpango, kufuatia amri yja kutotoka nje iliyosababishwa na Covid-19. Hali hii ilizorota zaidi baada usafiri kupigwa marafuku, kuwawacha wengi wao bila namna ila kutembea muendo wa kilomita nyingi hadi katika vituo vya afya, zahanati na katika maduka ya madawa ili kupata njia za mpango wa uzazi.

Hali hii ilizoroteka nchi nzima kufuatia kufungwa kwa vituo vya huduma vya upangaji uzazi ambayo imekuwa ikitolewa na shirika la afya ya uzazi Uganda (RHU), punde mkurupuko wa COVID-19 ulipotokea.

Dkt. Kenneth Buyinza, ambaye ni msimamizi wa zahanati ya RHU hivi juzi aliliambia gazeti la New Vision kwamba walilazimika kuhairisha huduma zao, kwa vile hawangeliweza “kuzingatia ushauri wa kutenga nafasi ya mita nne kati yao kwa vile wao huwa na idadi kubwa ya wateja,” alisema.

Dkt. Therestine Barigye, ambaye ni mkurugenzi katika hosipitali ya rufaa ya Mbarara, asema kwamba, ingawaje baadhi ya kina mama hutembelea hospitali kupata huduma ya upangaji uzazi, ukosefu wa usafiri inamaanisha kuwa, ugumu wa kufikia vituo vya afya na hosipitali huenda ikaathiri “wanawake na wasichana wengi,” hivyo kuwaweka hatarini mwa kupata “watoto zaidi.”

“Waweza kulitaja kama rindima la watoto,” aeleza Dkt. Barigye, huku akidokeza kwamba, “kwa sababu sasa watu (wachumba) wamebakia manyumbani mwao. Waweza kufikiria nini hutendeka wanapoishi pamoja.”

Dkt. Barigye anabashiri kuongezeka kwa idadi ya watoto katika eneo la kusini magharibi katika muda wa miezi tisa kutoka sasa kufuatia amri ya kutotoka nje iliyosababishwa na COVID-19.

Mwezi jana, askofu mkuu wa kanisa la Uganda, Stephen Kazimba Mugalu, aliwatahadharisha wanawake kwamba huenda wakashika mimba huku akiwashauri wasisahau kutumia mipango ya uzazi.

“Wanaume hawa wamo humu humu; wao wanala na kutenda mambo. Tahadhari,” alidokeza Askofu Mkuu, Dkt. Kazimba alipohubiri kupitia runinga ya kitaifa kutoka nyumbani kwake jijini Kampala.

Idadi nchini Uganda ya watu milioni 45.7 inatarajiwa kufika milioni 103.5 itimiapo mwaka wa 2060 katika nchi yenye eneo la kilomita mraba 241,037 pekee.

IMG 20161208 104722

Mzigo kwa jamii zisizo na uwezo mkubwa

Kuongeza mtoto mwingine zaidi katika familia, hasa mtoto yule hakupangiwa, huwa ni mzigo kwa hali ya kifedha ya jamii hii, kama tu vile ambavyo ongezeko la watu hupelekea kuathirika kwa raslimali za kitaifa.

Wilson Twamuhabwa, mshauri wa kiuchumi wa waziri wa fedha, mipango na maendeleo ya kiuchumi asema, ongezeko la watu wasio na faida ni “mzigo kwa raslimali chache za serikali na jamii.

“Ongezeko la watu huwa ni mzigo kwa raslimali, kwa vile serikali ama jamii hulazimika kuipangia wale watu ambao wameongezwa kwa idadi ya watu iliyoko,” alinena.

Hali hii ni mbaya zaidi katika maeneo ya mashambani nchini Uganda, ambako wanawake wengi hutegemea mpango wa uzazi kuepukana na mathara ya umaskini wanapokabiliana na jamii kubwa.

Kuwawezesha wanawake wanoishi na virusi vya HIV kupokea madawa

Shirika la EPHWOR haliwapatii wanawake huduma ya mpango wa uzazi bila malipo tu. Kwa mujibu wa Dkt. Aruho, linashughulika pia katika, “ugavi wa kila mwezi wa madawa ya ARV, saratani pamoja na kutoa matibabu kwa wanawake na wasichana walio hatarini katika wilaya hizi nane.”

Ikishirikiana na vituo vya afya vya serikali, kama vile Hosipitali ya Mbarara, kituo cha afya manispaa ya Mbarara, kituo cha afya cha nne cha Ruhooko na kituo cha nne cha afya cha Nsika miongoni mwa vituo vingine, EPHWOR imeweza kupata madawa bila malipo pamoja na nyaraka za wagonjwa kwa madhumuni ya ufuatiliaji na utoaji wa madawa.

Inapohusu madawa yanayopatikana kwa ugumu katika vituo vya umma vya afya na hospitali, EPHWOR  hununua madawa haya ikitumia fedha zake binafsi huku ikihakikisha zinawafikia wanawake wanozihitaji kwa wakati ufaao.

Dkt. Aruho analalamika kwamba watu wanouguza magonjwa hatari ikiwemo saratani, UKIMWI, kisukari na magonjwa mengine yanohitaji ujazo wa madawa wa muda kwa muda, wametengwa nchini wakati huu wa COVID-19.

Katika miezi hii miwili ya amri ya kutotoka nje, shirika hili limewasaidia wanawake 40 kupata madawa ya UKIMWI bila malipo. Wanawake 100 zaidi, wamesaidiwa kupata madawa ya kisukari na ya shinikizo la juu la damu. Halia kadhalika, limegawia wanawake wasio na chakula zaidi ya kilo 1,500 ya unga wa mahindi. Zaidi ya shilingi milioni 10 (USD 2,700) tayari imeshatumika na shirika hili katika juhudi hizi.

Dkt. Aruho anasema kwamba hakuna wakati bora wa kutoa msaada kwa wanawake walioko mashambani kama wakati huu.

Mradi huu wa kuripoti linalosimamiwa na shirika la InfoNile, limewezekana kupitia kwa usaidizi mkubwa wa Pulitzer Center on Crisis Reporting na National Geographic Society.