Kupungua kwa Idadi ya Samaki Kwasababisha Migogoro katika eneo la Uvuvi huko Homa Bay, Kenya

Kupungua kwa Idadi ya Samaki Kwasababisha Migogoro katika eneo la Uvuvi huko Homa Bay, Kenya

Na Sharon Atieno

Taarifa hii imeandaliwa kwa ushirikiano na InfoNile, na kwa usaidizi wa kituo cha Pulitzer (Pulitzer Center).

Mnamo Desemba 2023 Asha Okoth Jaoko, mmiliki wa boti kutoka Ufukwe wa Kiumba, Kisiwa cha Rusinga, alipata taarifa kwamba jumla ya vipande 18 vya nyavu zake za sangara vimeibiwa. Taarifa hii ilikuja ikiwa ni wiki moja tu tangu apoteze vipande 30 vya nyavu katika kisa kama hicho.

Kama ilivyo desturi ya uvuvi wa Sangara, Wavuvi huacha Nyavu zao majini wakati wa mchana na kuzifuata asubuhi ya siku inayofuata. Matukio haya hutokea nyakati za usiku.

 “Ili mtu aweze kufanya vizuri uvuvi wa Sangara, unahitaji takriban vipande 40 vya nyavu ambavyo hutengeneza Mtego mmoja mkubwa wa samaki,” Jaoko anayeonekana kuchanganyikiwa anasema huku akiongeza kuwa alikuwa na mashua mbili za uvuvi kabla ya matukio hayo mawili ya wizi kutokea, ambayo yamemrudisha nyuma kabisa katika shughuli hiyo. 

“Wakati ambao vipande 30 vya kwanza vinaibiwa sehemu nilipokuwa nimeweka Nyavu zangu, nilikuwa nikitumia mashua moja nyingine ilikuwa ikifanyiwa ukarabati. Kwa hivyo, nilijua nilikuwa na mashua hii nyingine ambayo niliitumia kama mbadala kwa sababu bado ulikuwa na nyavu 40,” alisema. “Sasa kwa vile nyavu za huu pia zimeibiwa, siwezi kurudi tena ziwani vinginevyo labda nipate msaada.”

Asha Okoth Jaoko a boat owner in Kiumba beach whose fishing nets have gotten lost in the lake 1
Asha Okoth Jaoko, mmiliki wa boti katika ufukwe wa Kiumba ambaye nyavu zake zimepotea ziwani

Kipande kimoja cha Nyavu kinachotumika kuvua samaki aina ya Sangara kinagharimu takriban KShs. 3,200 (USD $21), kulingana na bei za soko zilizopo. Mvuvi anahitaji takriban vipande 40 vya nyavu kama hizo, na hivyo kumgharimu karibu takriban KShs. 128,000 (USD $835).

Jaoko hayuko peke yake. Haya yamekuwa masaibu ya wavuvi wengi wa Sangara katika ufukwe wa Kiumba na maeneo jirani kama vile Wayando, Lwanda Rombo na Ngodhe. 

Matukio hayo pia yamelalamikiwa na wavuvi wa Dagaa, ambao huenda kuvua usiku. Migogoro kama hii miongoni mwa jamii za wavuvi imekuwa ikikithiri kutokana na kupungua kwa Samaki katika ziwa hilo kunakotokana na uvuvi wa kupita kiasi na uvuvi haramu, kwa mujibu wa Mamlaka ya Huduma ya Uvuvi ya Kenya (KeFS).

Sekta ya uvuvi ni mojawapo ya shughuli muhimu zaidi nchini Kenya, huku zaidi ya watu 700,000 wakitegemea Uvuvi kama chanzo cha maisha. Ziwa Viktoria – linalohudumia nchi za Tanzania na Uganda – ndilo eneo la uvuvi mkubwa zaidi wa ndani nchini.

Kati ya jumla ya uzalishaji wa Samaki kwa mwaka wa 2022, takriban Megatoni 173,741 wenye thamani ya KShs.37.6 bilioni (USD $286 milioni), uvuvi wa nchi kavu ulichangia asilimia 67 ya uzalishaji, huku sehemu kubwa ikitoka Ziwa Victoria (Megatoni 86,394).

Ziwa linahusisha uvuvi wa spishi nyingi na nyingi zinajulikana, lakini Dagaa (Omena), Sangara na Sato ndizo zenye umuhimu mkubwa kiuchumi. Licha ya hili, kumekuwa na mwelekeo wa kupungua katika uvuaji wa samaki hawa watatu kwa miaka.

Takwimu kutoka Mamlaka ya Huduma ya Uvuvi ya Kenya zinaonyesha kuwa uzalishaji wa samaki katika kaunti zote zinazopakana na Ziwa Victoria isipokuwa Kaunti ya Siaya umepungua ikilinganishwa na viwango vya 2013. Kaunti ya Homa Bay, ambayo ni sehemu kubwa zaidi ya ziwa, haijahifadhiwa. Kati ya 2013 na 2022, uzalishaji wa kaunti ulipungua kutoka tani 80,150 hadi 50,053.

Katika Kisiwa cha Rusinga hasa, mzozo kati ya wavuvi wa Sangara na Dagaa ulikaribia kuisha kwa kunyukana ngumi kama isingekuwa kuingilia kati kwa wakati.

Naye makamu Mwenyekiti wa kitengo cha usimamizi wa fukwe za Kiumba (BMU) Peter Okong’o Magunda anasema baada ya kuweka nyavu zao mchana, wavuvi hao wa Dagaa ambao huvua usiku hutoka kwenye fukwe nyingine bada ya kutafuta eneo jingineambalo unakuta mtu hajaweka mtego wake, huenda kuweka mitego yao mahali pale pale ambapo wavuvi wa Sangara wameweka yakwao.

“Wanapofanya hivyo, wanachukua Samaki wanaowapata kwenye nyavu zetu na pia kuharibu nyavu zetu,” analaumu, akiongeza kuwa wanaporejea siku inayofuata alfajiri, wanakuta hasara tu.

RUSINGA ISLAND translated 01

Magunda anasema kwamba ingawa ziwa halina mipaka, sheria za BMU huongoza jinsi wavuvi wanavyofanya kazi. Sheria zinasema wazi kwamba ikiwa mtu ameweka mtego wake, mtu mwingine anahitaji kwenda mbali mita chache kutoka kwao kwa manufaa ya kila mmoja.

Anabainisha kuwa wavuvi hao wa Sangara wanatumia boti zisizo za mashine ambazo zinategemea upepo hivyo ni vigumu kwao kuhamia fukwe nyingine. Zaidi ya hayo, ikiwa watasonga mbele zaidi kutoka hapo walipo, wakati mwingine wanaingia matatani na mamlaka ya Uganda ambao huwakamata wavuvi, huzuia boti na kuwanyang’anya samaki. Wanaachilia tu mashua na wavuvi kwa faini ya karibu KShs. 30,000 (USD $196).

Kulingana na Wasunga Okeyo, msaidizi wa mwenyekiti wa doria wa BMU ya Kiumba, wavuvi hao wa Dagaa ambao wamekuwa wakizozana nao wanatoka katika fukwe za karibu na za mbali, zikiwemo Litare, Koguna, Kisui Nyachebe, Sindo, Wadiang’a, Misori na Gwasi.

RUSINGA ISLAND translated 02 2

Anabainisha kuwa licha ya eneo dogo la uvuvi, mtu anaweza kupata angalau boti 15 za kuvulia Dagaa, mali ya mtu mmoja katika eneo moja. Katika eneo linalokaliwa na mvuvi mmoja wa Sangara, kunaweza kuwa na hadi wavuvi 40 wa Dagaa katika sehemu moja.

Zaidi ya hayo, aina ya nyavu zinazotumika kuvua Dagaa huleta changamoto kubwa kwa wavuvi wa Sangara, kwa sababu ukubwa wa matundu kwenye nyavu huruhusu kuvuliwa kwa Sangara ambao hawajakomaa, na kusababisha uhaba wa spishi katika ziwa hilo.

Tofauti na nyavu zinazotumiwa na wavuvi wa Dagaa, Okeyo asema: “Nyavu za gill (kwa ajili ya uvuvi wa Sangara) zina matundu makubwa sana kuanzia inchi nne hadi nane, ambazo huruhusu hata Dagaa kupita.”

Wasungu Okeyo, Assistant Chairman patrol, Kiumba beach BMU displaying net used for fishing dagaa
Wasungu Okeyo, Mwenyekiti Msaidizi wa doria, Kiumba beach BMU akionyesha nyavu zinazotumika kuvulia Dagaa.

Katika ufukwe wa Litare, Karibu kilomita 10 kutoka Kiumba, mtu anaweza kusema kwamba biashara ya Dagaa inastawi kwani mazulia juu ya mazulia ya samaki hawa yanawekwa kwa ajili ya kukaushwa na jua kando ya ufukwe.

Katika mwezi mmoja, ufukwe huzalisha wastani wa tani 10 za Dagaa, na kuifanya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa samaki hawa katika Kaunti ya Homa Bay, Peter Odhiambo, katibu msaidizi, Litare BMU, anasema.

Carpets of silver cyprinid (dagaa) and fulu being sundried in Litare beach
Mazulia ya Dagaa na fulu yakiwa yamekaushwa na jua katika ufukwe wa Litare

Anabainisha kuwa wavuvi wa Dagaa wanaendelea kusogea kulingana na upatikanaji wake, akiongeza kuwa hawatulii kama wenzao wa Sangara.

“Kuna wakati Dagaa hupatikana katika maeneo yanayoendeshwa na wavuvi wa nyavu za Sangara. Hivyo, wakati wao pia wanaenda kuvua samaki katika maeneo kama hayo, nanga ya Nyavu za Dagaa hunasa kwenye Nyavu za Sangara, na inapovutwa juu, huja na samaki, ambao mara kwa mara huwachukua,” anakiri.

“Pili, nanga inaweza kukwama na wanapoivuta, hatimaye kuharibu nyavu za Sangara ambazo ziliwekwa. Hiki ndicho kinacholeta mzozo.”

Odhiambo anaona kuwa ingawa kuna taratibu za kutatua migogoro kati ya BMUs na wavuvi, BMU ya Kiumba hujibu uvamizi wa wavuvi hao wa Dagaa kwa kufanya doria wakati wa usiku ili kuwanasa wahusika wote, kuharibu nyavu zao na kuiba samaki wao. Hata hivyo, kwa maelezo yake anasema, kwa kawaida hawakufuata utaratibu unaofaa wa kuwaripoti wahalifu kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

Anasema katika harakati hizo timu ya doria ingeweka kizuizini mashua na wavuvi na kuharibu hata vifaa vyao. Kwa wamiliki wa mashua, ili kurejesha mashua na wafanyakazi wao, wangetozwa pesa kubwa.

Engine boats lined up along Litare beach waiting for silver cyprinid (dagaa) fishing expedition at night
Boti za Mashine zikiwa zimejipanga kando ya ufukwe wa Litare zikisubiri msafara wa uvuvi wa Dagaa usiku

Maureen Akinyi Odila, mmiliki wa boti huko Litare Beach, anasema amepata hasara kubwa kutokana na mgogoro huo. Kwa zaidi ya tukio moja amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa wafanyakazi wake kwamba aidha taa zinazotumika katika uvuvi wa Dagaa zimeharibiwa au kwamba wafanyakazi wake wamekamatwa na boti kuzuiliwa na watu kutoka katika ufukwe wa Kiumba.

Odila anabainisha kuwa malipo yanahitajika hadi KShs. 8,000 (USD $60) ili kuachilia boti na wafanyikazi. “Kando na hayo, wakati mwingine unakuta baadhi ya vifaa pia vimeharibiwa au kuibiwa, kumaanisha kwamba bado unapaswa kuingia gharama ya kubadilisha na kurekebisha vifaa hivi,” amesema, akiongeza kuwa ukarabati unaweza kugharimu hadi KShs. 20,000 (kama dola za Kimarekani 131).

Odhiambo anasema kesi za kuzuiliwa zilikithiri kiasi kwamba hata wavuvi wa Dagaa na wamiliki wa boti walikuwa wakipanga njia ya kujipanga upya kulipiza kisasi. Bila kuingilia kati kwa wakati, mambo yangeweza kubadilika kutoka kuwa mabaya hadi kuwa mabaya zaidi.

Kulingana na takwimu zilizopakuliwa kutoka kwenye Mradi wa Data ya Mahali kwenye Migogoro na Matukio, ambayo hufuatilia takwimu kuhusu migogoro duniani kote, migogoro inayohusiana na samaki kwa ujumla imeongezeka nchini Kenya kutoka 2010 hadi 2023, na kufikia kiwango cha juu cha migogoro tisa iliyorekodiwa mwaka wa 2023 ikilinganishwa na wastani wa migogoro mitatu kwa mwaka kuanzia 2010-2015. Jumla Migogoro 50 ilirekodiwa katika kipindi cha miaka 14, huku 23 kati ya hii ikilenga raia. 

Angalau migogoro 19 ilifuatiliwa kwenye fukwe au visiwa vya sehemu ya Ziwa Victoria nchini Kenya, mingi ikihusiana na mapigano ya kuvuka mpaka kati ya wavuvi wa Uganda na Kenya na Kisiwa cha Migingo kinachozozaniwa. Migogoro miwili ilirekodiwa mwaka 2023 kati ya vikundi vya wavuvi wa Kenya kuhusu maeneo ya pamoja ya uvuvi na kupungua kwa samaki. 

Kulingana na afisa wa uvuvi katika kaunti ndogo ya Suba Kaskazini na Suba ya Kati Michael Ogemba Akoko, anasema ukosefu wa ajira umesababisha utegemezi mkubwa katika ziwa hilo, na kusababisha kuongezeka kwa juhudi za uvuvi, lakini eneo la uvuvi ni dogo. Ushindani wa samaki wachache unasababisha migogoro kati ya wavuvi.

Akisimamia fukwe 61 katika kaunti ndogo mbili zikiwemo Litare na Kiumba, Akoko anabainisha kuwa katika eneo la Remba na sehemu za visiwa vya Mfangano, wavuvi hao wa Dagaa huiba Samaki kwenye nyavu hizo nyakati za usiku, huku katika fukwe za Kibuogi, Sindo na Remba, wavuvi wa Dagaa waliojificha huiba nyavu za gill (Nyavu za Sangara) na kuziuza kwa bei chee (Ndogo) ya takriban KShs.500 (kama USD $3).

Wasungu Okeyo, Assistant Chairman patrol, Kiumba BMU displaying nets used for Nile perch fishing
Wasungu Okeyo, Mwenyekiti Msaidizi wa doria, Kiumba BMU akionyesha nyavu zinazotumika kuvulia samaki aina ya Sangara

Pia kuna mzozo kati ya mstari mrefu na wavuvi wa nyavu kati ya mpaka wa Suba Kaskazini na Suba ya Kati. Pia, katika baadhi ya fukwe, Soko la biashara haramu huchochea mvutano kati ya wafanyabiashara wa samaki na wamiliki wa boti.

Soko la biashara haramu linahusisha baadhi ya wafanyabiashara haramu wa samaki- ambao hawajasajiliwa na BMUs yoyote- hushirikiana na wavuvi kununua samaki moja kwa moja kabla ya kupeleka samaki kwenye maeneo yaliyotengwa kama inavyotakiwa na sheria ndogo za BMU. Baadhi ya samaki hawa wameibiwa kutoka kwenye nyavu zingine.

Pia, baadhi ya wavuvi hao wanapotoka kwenye msafara wao wa uvuvi kwa sababu tayari wameshapata pesa kinyume cha sheria, wanarudi wakidai hakuna samaki waliovuliwa.

Akoko anasisitiza kwamba sababu kuu ya migogoro ya mara kwa mara miongoni mwa wavuvi ni upungufu wa usambazaji. “Fukwe hazizalishi samaki wengi kama ilivyokuwa hapo awali. Kwa hivyo, kila mtu anajaribu kupata kitu kidogo, hata ikimaanisha kutumia njia zisizo halali, “anasema.

Baadhi ya vitendo vya uvuvi haramu vilivyotajwa katika ripoti ya 2021 ya Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi ya Kenya (KMFRI) ni pamoja na matumizi ya nyavu chini ya inchi tano (<5″); Nyavu zenye matundu madogo zaidi za namba 10 au ndogo zaidi, uwekaji wa saizi zote za Timba, matumizi ya Kokoro, Matumizi ya magugu hatari, baruti (Vilipuzi) na Nyavu za kutupwa.

LEGAL ILLEGAL NETS translated 03

Uvuvi wa kupita kiasi na utumiaji wa haramu hizi husababisha uharibifu na uvuvi wa samaki wachanga na akina mama ambao wangeweza kutaga mayai, anasema Dk. Christopher Aura, Mkurugenzi wa Utafiti wa Mifumo ya Maji Safi KMFRI.

Vile vile, KeFS inabainisha kuwa uvuvi wa kupindukia umekuwa suala linaloendelea katika ziwa hilo kwa miaka mingi huku ongezeko la watu na mambo ya kiuchumi yakisababisha kuongezeka kwa shughuli za uvuvi, na kuweka shinikizo kubwa katika akiba ya samaki.

Kwa mujibu wa ripoti ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya Shirika la Uvuvi katika Ziwa Victoria, inasema kati ya mwaka 2000 hadi 2016, idadi ya wavuvi wanaoendesha shughuli zao katika Ziwa Victoria iliongezeka kutoka 129,305 hadi 219,919. Kati ya hao, asilimia 50 walikuwa kutoka Tanzania, asilimia 30 Uganda na asilimia 20 nchini Kenya. 

Katika kipindi hicho, idadi ya shughuli za ufundi wa uvuvi zinazofanywa kwenye Ziwa hilo iliongezeka kutoka 42,519 hadi 74,257,  42% nchini Tanzania, 39% Uganda na 19% nchini Kenya. 

Nile perch fishing boats parked at Kiumba beach
Boti za uvuvi za Sangara zimeegeshwa katika ufukwe wa Kiumba

Sababu nyingine ya kupungua kwa Samaki, Dk Aura anasema, ni kuongezeka kwa virutubisho kutokana na shughuli zinazofanywa kwenye maeno ya mito inayotiririsha maji ziwani, ikiwa ni pamoja na kilimo na viwanda. Hii imeathiri ubora wa maji, na samaki wanajitahidi kuishi.

Kando na hilo, anabainisha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha kupungua kwa mazalia. “Samaki wanakwama kuzaliana kutokana na kiwango kidogo cha oksijeni na ongezeko la joto linalotokana na mabadiliko ya hali ya hewa,” anasema.

Ili kuzuia migogoro kati ya wavuvi wa Dadaa na Sangara isiendelee katika fukwe zilizoathiriwa katika Kisiwa cha Rusinga, BMUs ziliitisha mikutano kadhaa ya wadau katika robo ya mwisho ya 2023 iliyohusisha watu kutoka sekta ya uvuvi, ambayo ilisababisha uamuzi wa kuja na njia ya “kugawa maeneo”.

Njia ya kugawa maeneo inajumuisha kuzunguka kwenye maeneo ya uvuvi baada ya siku 15. Kila kikundi kinaruhusiwa kuvua katika sehemu fulani ya ufukwe katika kipindi hiki, na kisha wanabadilishana kwa muda fulani.

A fisherman holding nile perch after a fishing expedition
Mvuvi akiwa ameshika Sangara baada ya msafara wa uvuvi

“Katika siku tatu za kwanza, yaani, 16, 17 na 18, lazima tufanye doria kwenye maji ili kuhakikisha wavuvi wanabadilishana. Baadhi yao walikuwa wakikataa, lakini baada ya muda, wameuzoea utaratibu huo,” Rimba, ambaye anasimamia BMUs 18 kote Rusinga, anasema.

BMUs ziliongoza uamuzi huu kama moja ya majukumu yao chini ya Kanuni za Uvuvi (Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe), 2007 ili kuzuia au kupunguza migogoro katika sekta ya uvuvi.

Kwa mujibu wa Nick Rimba, Mwenyekiti wa Kaswanga BMU na Rusinga BMU Network, njia hiyo inatekelezwa mita 200 kwenda ndani kutoka kwenye fukwe ambako kulikuwa na ushindani kati ya vikundi viwili vya wavuvi. Hizi ni pamoja na fukwe za Litare, Kaswanga, Kiumba, Wayando, na Lwanda Rombo.

Rimba, iliyopewa jukumu la kuhakikisha kuwa utaratibu huo unafanya kazi kwa utulivu, inaongoza doria za kila siku pamoja na wawakilishi wa fukwe tano ili kuhakikisha kuwa wavuvi wanaishi kwa amani wakati wa shughuli zao za uvuvi.

Anasema tangu zoezi hilo lianze Novemba 2023, migogoro imepungua hadi kufikia asilimia 80, huku kesi za wizi zikipungua na kufikia takriban asilimia 30. Hata hivyo, anaona kuwa kufanya doria karibu usiku ni gharama sana kwani boti hutumia mafuta na gharama ya mafuta ni kubwa sana. Zaidi ya hayo, kwa kuwa kazi ya doria ni ya hiari, baadhi ya wanachama wanaowakilisha BMUs wakati mwingine hushindwa kujitokeza.

Fish being weighed in Kaswanga beach
Samaki wakipimwa uzito katika ufukwe wa Kaswanga

Wavuvi hao hasa kutoka fukwe za Litare na Kiumba ambazo zimekuwa zikizozana mara kwa mara, wanakubali kwamba amani na utulivu vimerejeshwa tangu utaratibu huo ulipoanza kutekelezwa. Hata hivyo, wanatafuta suluhu ya muda mrefu kuhusu kupungua kwa idadi ya Samaki ili kila mtu aweze kufaidika sawa sawa na ziwa hilo.

Dk. Aura anabainisha kuwa serikali inafanya kazi Ili kuja na Mpango kazi mahususi unaoweza kusaidia kupunguza tatizo la kupungua kwa idadi ya Samaki katika Ziwa Victoria. Tayari Mpango wa kuwajaza tena Sato katika vyanzo vidogo vya maji, hasa mabwawa katika maeneo ya magharibi na kati ya nchi, unaendelea ili kuongeza usalama wa chakula na lishe huku wakihamasisha ufugaji wa samaki.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts