Ziwa katika kitanda chake cha mauti; Nani Nani Anaweza kuliokoa Ziwa Victoria?

Ziwa katika kitanda chake cha mauti; Nani Nani Anaweza kuliokoa Ziwa Victoria?

By Sarah Biryomumaisho, Nabaasa Innocent, Sarah Natoolo and Nalweyiso Barbra

Mamilioni ya Waganda hasa mjini Kampala na maeneo ya jirani wanaendelea kutumia maji yasiyochujwa kutoka Ziwa Victoria, licha ya kuwepo kwa Bakteria watokanao na kinyesi ambao wanayafanya maji hayo yasiwe salama kwaajili ya matumizi.

Pia likifahamika kama Nalubaale, Ziwa Victoria ni ziwa kubwa zaidi la maji baridi barani Afrika linalohusishwa na nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni nchi za Uganda, Kenya na Tanzania. Ikiwa na eneo la kilomita 68,800, pia ni ziwa la pili la maji safi duniani.

Ziwa hili linasaidia moja kati ya uvuvi wenye tija zaidi duniani ambapo makadirio ya jumla ya samaki waliovuliwa kutoka ziwani kwa kipindi cha 2011 hadi 2014 ni takribani tani milioni 1 huku thamani ya ufukwe ikiongezeka kutoka takriban dola za Kimarekani milioni 550 mwaka 2011 hadi takriban dola milioni 840 mwaka 2014. 

Nyakandito
Nyakandito, mfanyabiashara wa samaki katika Kisiwa cha Rusinga, Kenya, akibeba samaki wabichi kutoka Ziwa Victoria ili kukaushwa kabla ya kuwapeleka sokoni. Picha na Anthony Ochieng.

Hata hivyo, kwa Waganda, ziwa hilo huzalisha zaidi ya samaki. Hutoa maji kwa ajili ya kunywa, kupikia, kuosha na matumizi mengine kwa mamilioni ya Waganda wanaoishi Kampala na maeneo jirani. Lakini wanasayansi wanasema ziwa hilo linatishiwa na uchafuzi wa mazingira, na kufanya maji kutokuwa salama kwa viumbe hai wa majini na binadamu.

Uchafuzi wa maji unatokana na kuingizwa ziwani kwa vitu kama kemikali na  vijidudu kwenye vyanzo vya maji kwa viwango vinavyoyafanya maji kutofaa kwa matumizi tofauti kama matumizi ya binadamu,  burudani au hata ikolojia.

Kulingana na Dk. David Were, mhadhiri na mtafiti katika idara ya usimamizi wa mazingira katika Chuo Kikuu cha Makerere, uchafuzi wa mazingira katika Ziwa Victoria umejikita zaidi karibu na maeneo ya mijini ambayo kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira.

Dk. Were anasema suala la uchafuzi wa mazingira katika Ziwa Viktoria ni changamoto ya siku hizi, zaidi katika mwambao wa mijini kama vile katika Ghuba ya Murchison huko Portbell, Kampala.

“Suala la uchafuzi wa mazingira ndani ya ziwa linazidi kukua siku hadi siku. Linajikita katika uchafuzi wa jadi, haswa matumizi ya virutubisho. Ukitembelea ziwa kwenye Ghuba ya Murchison, kuna supu ya kijani kibichi ziwani na hii ni kawaida kiashirio cha uchafuzi wa virutubishi, mara nyingi ule wa nitrojeni na fosforasi. Kukiwa na viingizi vingi au utiririshwaji wa virutubishi ziwani, huchochea ukuaji wa mwani,” anasema Dk Were.

Timu yetu ya waandishi wa habari ilitembelea maeneo tofauti ya Ziwa Victoria na tuliona watu wakifua nguo, magari na kuoga ziwani, lakini kulingana na wanasayansi, kuosha au kuoga ndani ya ziwa huchangia uchafuzi wa virutubishi, kwani sabuni ina viwango vya juu vya fosforasi.

algae bloom
Mwani kwenye maji huko Murchison Bay, Luzira

Dk Were anabainisha kuwa uchafuzi wa virutubishi hufanya maji kutofaa kwa matumizi yake hasa matumizi ya binadamu na viumbe vya majini ikiwemo ikolojia. Anaeleza kuwa samaki hao huwa na hali nzuri ya kuishi ndani ya maji; Kuna halijoto ifaayo, Ph (kipimo cha maji ya asidi au maji yasiyo na asidi) na mahitaji ya oksijeni. Vichafuzi vinapoingizwa ziwani, hubadilisha oksijeni na kufanya iwe vigumu kwa samaki kuishi.

“Uingizaji mwingi wa virutubisho katika ziwa huchochea ukuaji wa mwani ambao husababisha maua ya mwani kutumia oksijeni nyingi kwenye maji, na oksijeni huendelea kupungua kadri maua yanavyoongezeka,” anasema Dk Were.

Akiongeza kuwa “hii hukata kabisa oksijeni na kusababisha mazingira ambayo si rafiki kwa samaki. Hapo ndipo tunapoona samaki wanakufa.”

Dk. Were anaelezea kuwa mnamo Desemba 2020 na mapema 2021, Uganda ilirekodi vifo vingi vya samaki hasa Sangara. Wanafajamika zaidi kama samaki  wanaohitaji sana oksijeni, na mabadiliko yoyote au kupungua kwa oksijeni wanaweweseka kwa kiasi cha kuua samaki.

Serikali ya Uganda kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za Uvuvi katika Wizara ya Kilimo, Wanyama na Uvuvi, Bi Joyce Ikwaput Nyeko, ilitangaza kuwa nchi hiyo imepoteza zaidi ya tani 100 za sangara na takribani dola 400,000 za mapato.

Wanasayansi wanasema kwamba ingawa suala la uchafuzi wa asili bado halijashughulikiwa vizuri, sasa tunahama kutoka kwenye uchafuzi wa jadi kwenda kwenye uchafuzi unaoibukia, kama vile uchafuzi kupitia chembechembe za plastiki (microplastics), vichafuzi vya dawa(pharmaceutical pollutants), taka za vifaa vya kielektroniki (umeme) kama vile kompyuta, TV, frijim simu na vifaa vingine vya umeme.

 “Tuna ziwa lenye mchanganyiko wa uchafuzi wa mazingira kutoka katika uchafuzi wa asili ambao hatujaushughulikia, hadi uchafuzi unaoibukia. Hivi sasa ukiangalia eneo kubwa la Kampala, nyumba nyingi hazijaunganishwa na mfumo wa maji taka. Takriban 6% tu ya nyumba zimeunganishwa kwenye mfumo wa matibabu ya maji taka. Nyumba nyingi hutupa uchafu wao kupitia vyanzo visivyo vya uhakika ambavyo huishia ziwani moja kwa moja. Hiki ni chanzo kikuu cha uingizaji wa vichafuzi vya mazingira, “anasema Dk Were.

Kwa kuwa uchafuzi huu ni mpya, haujajumuishwa katika mfumo wa mitambo iliyopo ya kutibu maji. Mfumo wa sasa hauwezi kutibu aina hiyo ya taka kama vile kuondoa uchafuzi wa plastiki kutoka kwenye maji machafu.

Mtu anapolitembelea ziwa, hasa siku ya mvua, ni nadra kutokuona plastiki kando ya ziwa na kwenye mifereji ya maji na madimbwi ndani ya ziwa. Pia, uvamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji kama vile misitu na madimbwi unaofanywa na binadamu umefanya iwe rahisi kwa plastiki kupata njia ya kuingia ziwani.

“Jambo linalosumbua zaidi ni uchafuzi wa vyanzo vya maji ambapo kuna rasilimali zinazotoka kwenye vyanzo vya maji na hivyo kubadilisha mazingira wanamoishi samaki,” anasema Dk Anthony Tabu Munyaho, naibu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria.

water hyacinth at Luzira
Magugu maji na chupa za maji za plastiki hufanya iwe vigumu kwa boti kuhamia Ggaba Landing Site.

Kwa bahati mbaya, vichafuzi hivi vinapoingia katika maji, hupungua taratibu na kuvunjika katika chembe ndogo ndogo ambazo hubakia ndani ya maji. Vichafuzi hivi huchukua miongo kadhaa kuvunjika kwa njia ya asili. Vinaweza kumezwa na samaki, na kupitia mfumo wa chakula, samaki pia hutumiwa na binadamu.

Utafiti wa mwaka 2015 wa Jarida la Utafiti wa Maziwa Makuu, uliofanyika katika mkoa wa Mwanza nchini Tanzania, ulioko mwambao wa kusini mwa Ziwa Victoria, ulichunguza samaki Sangara na Sato wanaovuliwa kienyeji na kuthibitisha kuwepo kwa chembechembe za plastiki kwa asilimia 20  katikakila aina ya samaki.

Ziwa Viktoria kwa muda mrefu limekuwa likikabiliwa na upungufu wa samaki unaochangiwa na uvuvi kupita kiasi pamoja na kuibuka kwa mimea vamizi, kama vile magugu maji, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini zaidi, uchafuzi wake na kuenea kwa chembechembe za plastiki kunasogeza ziwa na kuzima injini hii ya kiuchumi kwa nchi tatu.

Kulingana na utafiti uliofanywa na Robert Egesa, mwanasayansi kutokaTaasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Rasilimali za Uvuvi (NaFIRRI) mwaka 2020, Uwepo, Uwingi, usambazaji, kemikali na chembechembe za plastiki za ukubwa wa 0.3-4.9mm, vilitathminiwa katika upeo wa maji kaskazini mwa Ziwa Victoria. Sehemu za juu ya ziwa zilichukuliwa sampuli kwa kutumia wavu wa manta na kuchambuliwa kwa ajili ya plastiki ndogo.

Plastiki zote zilikuwa za upili kwa asili zikitokana na vitu vya plastiki vinavyotumiwa na jamii,” anasema Dk Winnie Nkalubo, ambaye alizungumza kwa niaba ya timu ya utafiti.

Kulingana na utafiti huo, sehemu kubwa zaidi (asilimia 36) ya hesabu za chembechembe za Plastiki zilikuwa za ukubwa wa 1mm, ambayo inaleta tishio katika ubora wa maji na uvuvi wa ziwa. Uchambuzi wa kemikali za chembechembe za plastiki ulionyesha kutawala kwa kiwango kidogo cha polima; polyethilini na polypropen katika aina za chembechembe za plastiki. Hizi huzalishwa na bidhaa za plastiki ambazo zinayeyuka na zingine ambazo ni ngumu (zisizo yeyuka). Hizi ni pamoja na; chupa za plastiki, mifuko miongoni mwa nyingine.

Wakati huo huo, Dk. Were anasema kutokea kwa chembechembe za plastiki zinazotokana na uchafu mkubwa wa plastiki ina maana kwamba hatua sahihi za usimamizi wa taka za plastiki lazima zitekelezwe katika jamii zinazofanya kazi kwenye ziwa na jirani zake ili kulinda manufaa ya mfumo wa ikolojia unaotokana na ziwa.

woman washing at Jinja
Mwanamke akifua nguo katika eneo la kutua Masese huko Jinja.

Kama vile binadamu yeyote anavyohitaji makazi safi, Dk. Anthony Tabu Munyaho, Naibu Katibu Mtendaji wa Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria, anasema hata samaki wanahitaji maji safi ili kuwa salama. 

“Sisi pamoja na mashirika yetu dada ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi ya Kenya, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania na NaFIRRI ya Uganda tumefanya tathimini ya pamoja ya pamoja ili kuhesabu samaki halisi katika ziwa, na tumeona mabadiliko makubwa hasa katika maeneo ya maji machafu,” alisema. anasema.

Dkt. Munyaho anaongeza kuwa kuna msongamano wa samaki katika maeneo yaliyowekwa alama kuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira na haya ni karibu na miji mikuu katika nchi hizo tatu. Anataja Ghuba ya Murchison nchini Uganda, ghuba ya Nyanza ya Kisumu, na Emin Pasha katika eneo la Kyoto, Tanzania, akiongeza kuwa sasa kuna tatizo kubwa la uchafuzi wa mazingira linalotokana na kilimo kinachozunguka ziwa hilo.

“Tumeona idadi ya samaki ikipungua kutoka kwenye utafiti wa kwanza ambao ulifanyika mwaka 1999, ambapo tulikuwa na zaidi ya tani bilioni 1.9 za sangara pekee. Hii imepungua huku tafiti za hivi punde zikionyesha kuwa tunakaribia kufikia chini ya tani 600,000,” anasimulia.

Uchimbaji mchanga ni sababu nyingine ya uchafuzi wa mazingira katika Ziwa Victoria unaochangia uhaba wa samaki, hasa sangara, Dk Munyaho anafichua.

“Sangara hutaga mayai kwenye viota kwenye mchanga ulio chini ya vyanzo vya maji. Haya ni maeneo ya kuzaliana. Mchanga unapotolewa, huenda na viota na mayai – kuhatarisha mchakato wa kuzaliana kwa samaki,” anaongeza.

Timu yetu ilitembelea eneo la Ggaba huko Kampala ambapo baadhi ya mchanga kutoka Ziwa Victoria huuzwa. Tuliambiwa kwamba mchanga unachimbwa. Tulipoomba kutembelea maeneo hayo tulikabiliwa na upinzani kutoka kwa wauzaji, ambao walishuku kuwa tunatoka kwa vyombo vya sheria.

Kulingana na utafiti wa Taasisi ya Uchunguzi wa Usalama, uchimbaji usiodhibitiwa, haswa karibu na Ziwa Victoria unadhoofisha ikolojia ya eneo hilo.

“Pia kuna ushahidi kwamba inatishia maisha ya watu wa vijijini, ikiwa ni pamoja na uvuvi na kilimo,” unasema utafiti huo.

trucks ferrying sand
Trucks ferry sand from Ggaba landing site after it is delivered by boat. 

Nchini Uganda, Shirika la taifa la Maji na Maji Taka (NWSC) ndilo shirika la serikali lililopewa mamlaka ya kusambaza maji safi na salama ya bomba. Maji mengi yanayosambazwa katika Jiji la Kampala na maeneo ya jirani yanachukuliwa na kutibiwa kutoka katika eneo la Ggaba, kwenye mwambao wa Ziwa Victoria.

Mhandisi Andrew Muhwezi, meneja mkuu wa uzalishaji katika Kiwanda cha Maji cha NWSC Ggaba, anasema inawachukua saa 24 za kazi kutibu maji kutoka ziwani na kuyafanya yawe yanayofaa kwa matumizi ya binadamu. Hata hivyo anabainisha kuwa kutokana na uchafuzi wa mazingira, matibabu ya maji yana gharama kubwa.

“Tuna pointi mbili zinazounganisha Ggaba na Katosi. Leo, mazingira yanayozunguka Ggaba yamejengwa kwa kiasi kikubwa na karibu na Jiji la Kampala. Kutoka ndani ya Ghuba ya Murchison tulibaini kiwango fulani cha uchafuzi wa mazingira na ilibidi tuhamishe eneo letu la kuingia mwaka wa 2009 hadi takriban mita 500 kutoka ufukweni,” anasema.

Anaongeza kuwa kuhama kwa sehemu ya kuchotea maji ni kwa sababu imekuwa ngumu kutibu maji katika sehemu ambayo walikuwa wakiyapata kutokana na uchafuzi mkubwa wa mwani na uchafuzi mwingine kama plastiki na metali nzito.

“Tuna maabara ya kisasa sana na tuna uwezo wa kupima asilimia 100 ya vipimo ambavyo tunatakiwa kufanya. Pia, kama sehemu ya uhakikisho wa ubora, tunapeleka majaribio yetu kwenye maabara za nje ili kuboresha uhalali wa matokeo. Baadhi ya matokeo si ya kutisha kama yale ya metali nzito, kwani nyingi ziko chini ya viwango vya utambuzi,” anasimulia.

“Tunatumia takriban dola za Kimarekani 3,480,263 (UGX bilioni 13) hadi dola 4,817,581 (UGX bilioni 18) kununua kemikali na karibu dola 9,634,691 (UGX bilioni 36) kununua umeme. Na, kutokana na kwamba viwango vya uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya uondoaji vinatofautiana, gharama ya mtambo wa kutibu eneo la Ggaba ni ghali zaidi kuliko ile ya mtambo wa Katosi na kama isingekuwa uchafuzi wa mazingira, tungetumia gharama ndogo,” Muhwezi anadai.

Tulifanya ziara kamili ya kuangalia mtambo wa kutibu maji ulioko Ggaba na tukagundua kuwa maji yanachujwa na kutibiwa kabla ya kupelekwa kwa mtumiaji wa mwisho. Kulingana na Eng Malambala ambaye alitutembelea katika kituo hicho, maji yote hutiwa kemikali kama klorini ili kuyafanya kuwa salama kwa matumizi ya binadamu. Anaeleza kuwa maji hayo yanapotoka kwenye mimea yao husafishwa kwaajili ya  matumizi ya binadamu. Hata hivyo, kuna uwezekano wa kuchafuka wakati wa kupita kutokana na mabomba na uchafu wa matanki ambayo watu hutumia majumbani mwao. Ndiyo maana watu wanashauriwa kila mara kuchemsha maji kabla ya kunywa.

Maji huchukuliwa sampuli mara 3 kwa siku, saa 9:00 asubuhi, 3:00 alasiri na 3:00 usiku. Sampuli hukusanywa moja kwa moja kutoka ziwa Victoria na klorini huongezwa ili kuua bakteria kwenye maji.

Ili kuthibitisha kuwa maji yanayotumiwa na Waganda ni salama, tulifanya uchambuzi huru wa sampuli ya maji na Les Rams Consult, maabara huru yenye makao yake makuu mjini Bwaise, Kampala, ili kubaini usalama wa maji kutoka ziwani kwa matumizi ya binadamu. Tulichukua sampuli za maji kutoka juu, katikati na chini ya chaneli ya Nakivubo, ambayo hutiririsha maji yake ya ndani ya Ghuba ya Murchison, chanzo kikuu cha maji ya kunywa kwa jiji la Kampala. Sampuli tisa za maji zilikusanywa kutoka Kanyogoga Borehole, Kitintale Stream, na Portbell Murchison Bay kwenye Ziwa Victoria (Sampuli tatu kila moja kwa siku tatu tofauti).

Lita moja ya maji ilichukuliwa kutoka kwa kila sehemu ya sampuli na kusafirishwa hadi kwenye maabara hii kwa uchunguzi. Vigezo vya uchanganuzi vilijumuisha mahitaji ya oksijeni ya kibayolojia (BOD), mahitaji ya oksijeni ya kemikali (COD), pH, conductivity ya kielektroniki (EC), mafuta na grisi, tope, jumla ya fosforasi, naitrojeni, metali nzito (risasi, cadmium na zebaki) na kolifi ya kinyesi. 

Matokeo ya uchanganuzi kwa ujumla yanaonyesha kuwa maji si salama kwa sababu ya kuwepo kwa kolifu za Kinyesi. Hii ilithibitishwa katika sampuli zote. Kiwango cha kinyesi, ambacho ni pamoja na bakteria unaotokana na uchafu wa binadamu na wanyama, hutoa dalili ya jumla ya hali ya usafi ya usambazaji wa maji.

Akichanganua matokeo hayo, Dk. Were alibainisha kuwa hakuna hatari yoyote iliyoonekana kutokana na Kolifi hizo za vinyeshi kwa binadamu au wanyama. Hata hivyo, pindi zinapogundulika huonyesha kuwepo kwa bakteria wengine wanaosababisha magonjwa kama vile wanaosababisha Typhoid, Kuhara damu,, Hepatitis A na Kipindupindu.

Matokeo yetu yanafanana na yale ya utafiti wa Wizara ya Maji na Mazingira uliofanyika mwaka 2005 ulioitwa ubora wa maji na hali ya afya katika eneo la Ziwa Victoria, Uganda.

Lengo la utafiti lilikuwa kuchunguza mwelekeo wa magonjwa na hatari za afya katika jamii za pwani na kupendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

“Hesabu za coliform ya kinyesi katika sampuli za maji zilichanganuliwa ili kuashiria uchafuzi wa kinyesi. Kolifomu kwa ujumla zilikuwa nyingi sana katika sehemu nyingi za sampuli, ikionyesha kuwa maji yalikuwa na uchafu mwingi, “unasema utafiti.

Utafiti mwingine uliofanywa na Taasisi ya Kitropiki na Afya ya Umma ya Uswizi na Baraza la Kitaifa la Sayansi na Teknolojia la Uganda, pamoja na sampuli zilizokusanywa mwaka wa 2013, pia ulionesha “uchafuzi wa vijidudu zaidi kuliko ilivyoripotiwa hapo awali Kampala.”

“[Hii] inaweza kusisitiza kupungua kwa kazi ya matibabu ya asili ya ardhi oevu ya Nakivubo… Matukio ya mafuriko katika mkondo wa Nakivubo na ardhioevu yanaweza pia kuchangia uchafuzi wa chemchemi zilizohifadhiwa,” utafiti uliripoti.

Ingawa viwango vya coliform vilipungua katika Ghuba ya Murchison, kuwepo kwa bakteria hizo hata kidogo kunaonyesha kwamba “chanzo cha maji ya kunywa huko Kampala kinaweza kuchafuliwa na bakteria, virusi na viumbe vya protozoa, ambavyo visivyokufa katika mchakato wa matibabu.”

Watafiti wa 2005 waliongeza kuwa jamii za mwambao huchukua maji yao kwaajili matumizi ya nyumbani hasa kutoka kwa ziwani. “Misimu ya mvua ilikuwa na viwango vya juu zaidi vya coliform kuliko misimu ya kiangazi kwa maeneo yote ya ufukwe wa ziwa. Tofauti hii ya msimu katika hesabu za coliform inahusiana vyema na matukio ya magonjwa yanayoenezwa na maji ambayo ni ya juu katika msimu wa mvua. Magonjwa yaliyoenea zaidi ni pamoja na malaria, kuhara damu, kuhara na kichocho. Kesi za kipindupindu, maambukizo yanayohusiana na ngozi na mafua, pia zilizionekana.”

Utafiti huu pia uligundua kuwa kuna uhusiano wa kibinadamu na maji machafu kwenye mwambao wa Ziwa Victoria unatokana na ukweli kwamba kimsingi kuna vyanzo viwili muhimu vya maji vinavyoathiri afya za wakazi wa mwambao wa ziwa: Maji ya ziwa yenyewe na maji ya kunywa ya mwambao. (mito/vijito, visima na chemchemi, ambavyo vipo).

Kulingana na watafiti, vyanzo vingine vya maji vinavyoathiri afya ya binadamu, Ni kama vile maji ya mafuriko ndani na karibu na jamii wakati wa msimu wa mvua, pia hutumika kwa matumizi ya nyumbani ni muhimu lakini ni ya muda mfupi. Mwingiliano vyanzo vya maji na wanadamu umeonekana kuwa na madhara makubwa kiafya , Muingiliano huo hasa ni: kuogelea/kuoga, kunywa na kula (samaki wenye sumu au waliochafuliwa).

Licha ya idadi ndogo ya tafiti zilizofanywa kuhusu magonjwa ya vimelea yanayoenezwa na maji Afrika Mashariki katika kipindi cha miongo saba iliyopita, taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba, maambukizi ya magonjwa muhimu ya vimelea bado ni makubwa katika miaka ya hivi karibuni. Katika ukanda wa Afrika mashariki, idadi ya watu wanaotumia vyanzo vya maji ya kunywa ni asilimia 50 hadi 75 huku asilimia 50 ya watu wameboresha huduma za vyoo (WHO, 2015). Hii inaweza kuwa sababu ya kuu ya kuenea kwa magonjwa ya vimelea ya maji. Hivyo kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kungepunguza mzigo wa magonjwa haya.

Kulingana na Uchunguzi wa sampuli za maji wa 2022 uliofanywa na InfoNile, thamani za Mahitaji ya Kemikali ya Oksijeni (COD) pia yalikuwa juu ya viwango vya kitaifa na Viwango vya Utiririshaji wa Effluent Afrika Mashariki.

Mahitaji ya Oksijeni ya Kemikali (COD) ni kiasi cha oksijeni kinachohitajika ili kuoksidisha mabaki ya kikaboni yaliyopo kwenye maji. Kadiri thamani ya COD inavyoongezeka, ndivyo uchafuzi wa maji unavyozidi kuwa mbaya.

 

Kulingana na sampuli za maji ya InfoNile, vigezo vingine vingi vya ubora wa maji viko ndani ya viwango vinavyokubalika.

Baadhi ya vigezo, kama vile Mahitaji ya Oksijeni ya Kibiolojia, Fosforasi, Risasi na Cadmium, vilionekana kuwa karibu na thamani sawa au vilikuwa vimeongezeka kidogo kutoka katika sampuli zaa 2013.

Nitrojeni, hata hivyo, iliongezeka kidogo. Nitrojeni, ambayo huchochea ukuaji wa mwani ambao hupunguza oksijeni, inaweza kutoka kwa mbolea za kilimo, maji machafu, na uchafu wa wanyama.

Pamoja na ongezeko la watu hasa katika miji na maeneo ya mijini karibu na ziwa, tatizo la uchafuzi wa mazingira linatarajiwa kuendelea kwa miaka mingi zaidi.

Hii kwa sehemu kubwa inaongezeka kutokana na uvamizi wa binadamu katika misitu na ardhi oevu ili kukaa na kufanya makazi yao. Utafiti wa 2015 uliochapishwa katika Jarida la Maji na Afya ulichambua ubora wa maji katika hifadhi nne za misitu ndani ya kilometa 50 za Kampala ambazo hufanya kazi kama kizuizi cha maji yanayotiririka katika Ziwa Victoria.

“Katika utafiti wa sasa, takwimu zinaonyesha kuwa kila hifadhi ya msitu ina angalau eneo moja lenye ubora wa maji hasa uliopungua. Katika hifadhi ndogo za misitu ya Zika na Kitubulu hii inatisha hasa kwa vile eneo la ardhi limeunganishwa na chemichemi za maji ya ardhini, na hivyo kuchangia moja kwa moja maji ya juu ya ardhi kwenye Ziwa Victoria. Msitu mkubwa zaidi katika utafiti huu, Msitu wa Mabira, ulikuwa na ubora mbaya zaidi wa maji kati ya maeneo yote 17. Hii inatisha, kwani mkondo huu unaelekea moja kwa moja kwenye chanzo cha Mto Nile huko Jinja,” utafiti huo uligundua.

Tishio lingine linaloendelea ni kuendelea kwa matumizi ya plastiki zisizoharibika, ambazo ni kuanzia chupa hadi majani na mifuko ya nailoni. Ingawa wenyeji wanakiri kujua kwamba ni hatari, wengi wanakiri kuzitumia kwa sababu hawana chaguo lingine.

Mifuko ya nailoni inayojulikana kama ‘kavera’ ndiyo inayochangia zaidi uchafuzi wa plastiki nchini Uganda. Serikali mara kadhaa imepiga marufuku matumizi yake lakini utekelezaji umeshindikana. 

goats feeding at Ggaba
Trucks ferry sand from Ggaba landing site after it is delivered by boat. 

Margaret Akankwasa amekuwa akiuza samaki wa kukaanga katika eneo la mwalo wa Ggaba kwa miongo miwili iliyopita. Anaona kuna upungufu wa uvuaji wa samaki ikilinganishwa na wakati alipoanza, hata wakati wa misimu ya kilele cha uvuvi.

“Samaki huwa wengi wakati wa masika, lakini samaki wanaovuliwa hupungua wakati wa kiangazi kutokana na joto. Kunapokuwa na upepo, wavuvi wanahofia usalama wao, hivyo wanaovuliwa pia hupungua,” anaeleza Akankwasa.

Hapo awali bei ya samaki ilikuwa shilingi 2,000, lakini kwa sasa inagharimu kati ya shilingi 8,000 na 10,000. Akankwasa na wachuuzi wenzake wanafahamu vyema uchafuzi wa plastiki unaoathiri ziwa na athari zake. Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Makerere waliwaelimisha kuhusu hatari ya kutupa plastiki ziwani.

Licha ya ujuzi huu, Akankwasa analalamika kuwa jamii inasalia kuwa sugu kukubali mabadiliko. Anaamini kwamba utekelezaji ni muhimu, akipendekeza kwamba ikiwa watu watakabiliwa na matokeo ya kisheria kufuatia kuchafua ziwa, wengine wangezingatia na kuogopa. Kwa miaka mingi, Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA) imeendesha vikao vya elimu kuhusu uhifadhi wa ziwa, ilhali wengi hupuuza ushauri huo, hata maonyo kwamba ulaji wa samaki wanaokula taka za plastiki huenda ukasababisha saratani.

Riziki ya Akankwasa inajikita katika mauzo ya samaki, kutoa mahitaji ya familia yake na kusomesha watoto wake katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Safari yake ilianza kwa kuuza samaki wadogo 15-30 kila siku, lakini sasa anashughulika na angalau kilo 50 za samaki kwa siku.

Ssempa Matovu Ssalongo simulizi yake inafanana na ya Riziki ya Akankwasa. Ameuza samaki wabichi huko Ggaba kwa miongo miwili, akishirikiana na wavuvi moja kwa moja. Miaka mitano iliyopita, walianza kuona kupungua kwa idadi ya samaki. Ssalongo anahusisha hili na vitendo hatari vya uvuvi kama vile uvuvi wa kupita kiasi na kuvuaa samaki ambao hawajakomaa, ambao unaendelea licha ya juhudi za UPDF za kutekeleza katika Ziwa Victoria.

Ssalongo anasisitiza kuwa uchafuzi wa mazingira pia unachangia kupungua kwa idadi ya samaki. Plastiki, ikiwa ni pamoja na chupa na mifuko, hutupwa ziwani, zikichukua maeneo ambayo samaki kwa kawaida huanguliwa, karibu na ufukwe. Maeneo haya yanapokosekana, samaki huacha mchakato wa kuangua, na hivyo kusababisha kupungua kwa idadi yao.

Analaumu ukosefu wa khofu miongoni mwa vijana ambao hupuuza maonyo kuhusu uchafuzi wa plastiki. Pia anaangazia uchimbaji mchanga kama sababu inayoathiri idadi ya samaki. Kwa hiyo, sasa wanatafuta samaki kutoka Ziwa Kyoga na kuwauza katika eneo la Ggaba kwenye Ziwa Victoria.

Ssalongo hakuwahi kutarajia lwamba ipo siku samaki wangesafirishwa kutoka Ziwa Kyoga ili kuendeleza jamii za Ziwa Victoria. Kufungwa kwa Ziwa Kyoga kumeliruhusu kurejea na kupunguza viwango vya uchafuzi wa mazingira na sasa linalisha jamii kwenye mwambao wa Ziwa Victoria. Wawili hao wanasisitiza kuwa utekelezaji ndio njia bora ya kukabiliana na uchafuzi wa plastiki kwenye ziwa.

Mnamo Aprili 2015, baraza la mawaziri liliunda kamati ya wizara inayojumuisha Wizara za Biashara, Maji na Mazingira, Fedha na Kilimo pamoja na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira, Chama cha Wafanyabiashara wa Uganda na Chama cha Wafanyabiashara wa Jiji la Kampala, kushughulikia utekelezaji wa marufuku ya mifuko ya plastiki kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Fedha ya 2009, na kuungwa mkono tena na Rais Yoweri Museveni.

Hata hivyo, tarehe 2 Oktoba 2018, Mkurugenzi Mtendaji wa wakati huo wa NEMA, Tom Okurut aliwaambia wabunge kwenye Kamati ya Maliasili ya Bunge kwamba mamlaka iliagizwa kuendeleza marufuku ya uingizaji, utengenezaji wa ndani, usambazaji na sisi wa kubeba plastiki chini ya microni 30, kana kwamba ilisubiri mwongozo kutoka katika Baraza la Mawaziri kuhusu jinsi ya kushughulikia aina zingine za nyenzo za plastiki ambazo ni zaidi ya maikroni 30.

Akiwa amefika mbele ya kamati hiyo tarehe 3 Oktoba 2018, Waziri wa Biashara wa wakati huo, Amelia Kyambadde, alishauri dhidi ya kupigwa marufuku mara moja kwa ‘kavera’, lakini badala yake kukomeshwa kwa uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki. Alidai kuwa kupiga marufuku mara moja kwa mifuko ya plastiki chini ya maikroni 30 haitoi mkakati wazi kwa NEMA kushughulikia fidia ya wafanyikazi ambao wanaweza kuachishwa kazi kwa sababu ya uamuzi huo.

“Uamuzi wa kupiga marufuku kabisa utengenezaji, uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki uliharakishwa na kulikuwa na mashauriano machache ya wadau,” alisema Kyambadde wakati huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa NEMA, Barirega Akankwasah, anasema kuwa haiwezekani kupima mikroni 30 kwa macho ya nyama, na hivyo kufanya kuwa vigumu kutekeleza sheria. Huku wito huo wa Baraza la Mawaziri ukiungwa mkono na Rais, Barirega anaamini kuwa sheria ya kupiga marufuku matumizi ya plastiki sasa itapitishwa.

“Baraza la Mawaziri liliazimia kupiga marufuku kabisa kavera. Hii ina maana tunarudi Bungeni kutetea hoja, kurekebisha sheria (National Environment Act) na kupiga marufuku kabisa. Wakati huu itapita kwa sababu Rais pia ameongeza sauti yake,” alisema Barirega.

Mnamo Agosti 2021, serikali kupitia Baraza la Mawaziri ilitoa wito upya wa kupiga marufuku kabisa utengenezaji, matumizi na uingizaji wa kavera. Beatrice Anywar, Waziri wa nchi ofisi ya Mazingira, alibaini kuwa wakati huu, hakuna kitakachokwamisha utekelezaji.

Kushindwa kutekeleza zuio hilo kumechangiwa na sababu kadhaa zikiwemo rushwa, siasa, ukosefu wa uhamasishaji wa raia na ukosefu wa njia mbadala zinazofaa. Mpaka sheria kama hizo zitakapowekwa na kuanza kutekelezwa kwa usawa, lakini kwa sasa matumizi ya plastiki yanasalia kuwa tishio kwa ziwa kubwa zaidi la Afrika.

Tarifa hii imezalishwa kwa ushirikiano na InfoNile kwa ufadhili wa JRS Biodiversity Foundation; ripoti ya ziada na Annika McGinnis, Ruth Mwizeere na Primrose Natukunda.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts