Vidhibiti asili vya wadudu waharibifu wa wanyama vilivyo hatarini kutoweka: Kole (Oxpeckers) watoweka katika ukanda wenye ng’ombe, Kusini Magharibi mwa Uganda.

Vidhibiti asili vya wadudu waharibifu wa wanyama vilivyo hatarini kutoweka: Kole (Oxpeckers) watoweka katika ukanda wenye ng’ombe, Kusini Magharibi mwa Uganda.

Na Kajumba Godfrey

John Kayangire ni mfugaji wa ng’ombe huko Rutooma, wilaya ya Kashari Mbarara, Kusini Magharibi mwa Uganda. Kama wafugaji wengine wa ng’ombe, yeye hutazama tu jinsi mifugo yake inavyoendelea kuathiriwa na kupe, “dawa za mifugo sokoni siku hizi ni bandia, haziwezi kufanya chochote katika vimelea vinavyonyonya damu kwa wanyama”.

Akiwa na umri wa miaka 98, Kayangire, ambaye ni afisa wa zamani wa polisi na daktari wa mifugo bado ana nguvu za kimwili na anakumbuka wazi kabisa jinsi walivyokuwa wakipambana na kupe enzi za utoto wake. “Tulizoea kung’oa  kupe kwenye ng’ombe kwa kutumia mikono, tukiwabandika kwenye vijiti na kuwachoma moto. Wakati huo tukiwa watoto tulikula kupe waliochomwa” anasimulia.

“Juhudi zetu zilikuwa zikiongezeka kila wakati na kutoka kwa ndege tunaowaita “Esasi” kwa kilugha. Hawa walikuwa wakitapakaa katika kila eneo la mwili wa ng’ombe, masikioni, kwenye viwele, na mkiani wakichambua na kuokota kupe”, Kayangire anaongeza.

Ndege hawa walikuwa wakifanya hivyo hivyo hata kwa wanyama wengine wa porini kama vile nyati na swala wa porini kwani wanyama hawa wa pori mara nyingi huingiliana na ng’ombe kwani kulikuwa na sehemu ndogo ya kutenganisha maeneo ya malisho wakati huo na maeneo tengefu ya wanyamapori.

“Esasi” wanaojulikana kama Kole (ndege wanaodonoa kupe kwenye wanyama) na kisayansi wanaitwa “Buphagus” walikuwa na ufanisi katika udhibiti wa kupe katika mifugo ya ng’ombe wa kienyeji kabla ya kuletwa mifugo ya kigeni nchini.

Kayangire anaeleza kuwa kuletwa kwa mifugo ya ng’ombe wa kigeni nchini kulikuja na matumizi ya dawa za mifugo kudhibiti kupe ambao wameanza kuwa tatizo kwa ng’ombe hao wapya.

“Serikali ilihamasisha wafugaji kuanzisha majosho ya ng’ombe na kuwagawia dawa za mifugo kulingana na kanda ili kusambaza dawa kwenye mifugo. Magharibi mwa Uganda ambako wilaya ya Mbarara inapatikana, dawa ya kwanza ya mifugo tuliyopokea ni Gamatox kabla ya dawa nyingine kuletwa katika eneo hilo baadaye” anasema.

Tom Kayangire
Tom Kayangire aliyekuwa daktari wa mifugo akionyesha baadhi ya vitabu vya mifugo vilivyotumika kuhamasisha wakulima katika mapambano dhidi ya kupe enzi za ukoloni.

Hili lilisababisha vifo vya kole waliokula kupe walioambukizwa dawa zilizokuwa zikitumika huku wengine wakilazimika kuhama kutoka kwenye ukanda wa ng’ombe hadi katika mbuga za wanyama zilizo karibu kama vile Mbuga ya Kitaifa ya Malkia Elizabeth na Hifadhi ya Kitaifa ya Ziwa Mburo.

“Ndege hawa bado wako porini wakiokotaokota kupe kutoka kwenye nyati na swala wa porini, walitoka kwenye ushoroba wa ng’ombe baada ya wengi wao kufa walipoanza kutumia dawa za mifugo kupambana na kupe” anasimulia Kayangire.

Mamlaka ya Kitaifa ya Dawa (NDA) – ya Uganda iliyopewa mamlaka ya kudhibiti dawa nchini, ikiwa ni pamoja na utengenezaji, uingizaji, usambazaji na utoaji wa leseni inasema dawa zote za mifugo sokoni ni salama kwa wanyama na mazingira.

Abiaz Rwamiwiri, Msemaji wa NDA anasema dawa zinazoruhusiwa sokoni hupimwa vizuri. “Dawa zinapotengenezwa hupitia hatua mbalimbali na kupimwa ili kuhakikisha hazina madhara kwa wanyama, binadamu na mfumo wa ikolojia wakiwemo ndege, nyuki, mazao, nyasi, maji miongoni mwa viumbe vingine vya mfumo wa ikolojia”.

Hata hivyo anahusianisha tishio la dawa za mifugo katika ukanda wa ng’ombe wa magharibi na matumizi mabaya ya dawa hizi kwa wakulima.

“Ni kweli baadhi ya wanyama hawaonekani tena katika ukanda wa ng’ombe wa magharibi, wanyama wanapata upofu huku wakulima na wahudumu wa mashamba wanapata magonjwa ya ajabu. Yote hii ni kutokana na jitihada za wakulima kuondoa kupe” Rwamwiri anafichua.

A tick infested cow that turned blind after the farmer applied a concoction of drugs on it to get rid of the ticks
Tom Kayangire aliyekuwa daktari wa mifugo akionyesha baadhi ya vitabu vya mifugo vilivyotumika kuhamasisha wakulima katika mapambano dhidi ya kupe enzi za ukoloni.

Anaeleza kuwa matatizo yalianza baada ya kuletwa ng’ombe wa kigeni, “ng’ombe aina ya Ankore hawakuathirika sana na kupe lakini hawakuwa na thamani sokoni. Hii ilisababisha kuanzishwa kwa wafrisia ambao hutoa maziwa mengi kwa siku, hukomaa haraka na pia hukupa nyama nyingi ya ng’ombe. Hata hivyo, wanashambuliwa sana na kupe na magonjwa yanayoenezwa na kupe.”

Baada ya muda, kupe hawa walianza kustahimili dawa baada ya kubadilika na kuwaacha wakulima wakiwa njiapanda. “Ng’ombe wao wa kifrisia walianza kufa, wafugaji waliingiwa na hofu na kuanza kutumia dawa za mifugo na mbaya zaidi walianza kuchanganya kwa kutumia mchanganyiko wa dawa za mifugo na wadudu.” Rwamwiri anasimulia.

Bottles of used veterinary drugs found at one of the farms
Chupa za dawa za mifugo zilizotumika zilizopatikana kwenye shamba moja.

Msemaji wa NDA anasema mchanganyiko huu umegeuka kuwa hatari kwa wanyama, wakulima na wafanyakazi mashambani, mfumo wa ikolojia na masoko wanayouzia bidhaa zao. “Wanyama wamekuwa vipofu katika kipindi hiki ambacho wamekuwa wakitumia mchanganyiko huu. Kole sasa wametoweka katika ukanda wa magharibi wa ng’ombe, huku wachavushaji kama nyuki na wengineo pia wako hatarini.”

Jeconious Musingwire – mwanamazingira mstaafu anasema kupe ndio chakula kikuu cha kole. “Kupe wakiwa kwenye miili ya ng’ombe, kole wangeweza kudonoa kupe kwaajili ya chakula”.

Musingwire anaongeza kuwa ndege hao wa kienyeji walikuwa wameongezeka kwa wingi kwenye ukanda wa ng’ombe hadi kuanzishwa zilipoletwa dawa za mifugo za kupambana na kupe katika ng’ombe wa kifrisia. Kole hao walipungukiwa na chakula na wengi waluhamia katika maeneo yaliyotengwa wakitafuta chakula kwenye wanyama walioko katika familia ya ng’ombe kama nyati na swala pori.”

Anabainisha kuwa hata porini ambako ndege hao walikuwa wamekimbilia, wanatishiwa kwani wengi waliuacha ukanda wa ng’ombe wakiwa na mabaki ya dawa za mifugo, “wanaendelea kufa kwenye mapori ya akiba ya mabaki ya dawa za mifugo na pia wanakufa kutokana na upungufu wa upatikanaji wa chakula.”

Katika utafiti wa wataalam wa afya ya wanyama uliochapishwa na tovuti ya ScienceDirect na Maktaba ya Kitaifa ya Dawa, Kituo cha Kitaifa cha habari za bioteknolojia juu ya kupe wa ng’ombe na magonjwa yanayoenezwa na kupe: Marejeo ya hali ya Uganda, nchi inakabiliwa na hasara kubwa ya kila mwaka – ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja ambapo zaidi ya dola bilioni 1.1 za Marekani hutumika katika kukabiliana na  magonjwa yanayoenezwa na kupe.

Rwamwiri anaona ukosefu wa wahudumu wa ugani wa kutosha kama sababu kuu ya kwa nini wakulima wamechukua jukumu la kutibu mifugo yao mikononi mwao.

Abiaz Rwamwiri
Abiaz Rwamwiri – Msemaji wa NDA (mwenye shati la kijani) akiwa shambani na wafanyakazi wengine wa NDA wakimpeleka mkulima njia bora ya kutumia pampu yake ya kunyunyuzia.

Kulingana na taarifa ya wizara ya Kilimo, Sekta ya Wanyama na Uvuvi kwa vyombo vya habari mwaka wa 2019, uwiano wa sasa wa mfanyakazi wa ugani kwa kaya za wakulima ni takriban 1:1,800, ambao bado ni wa juu sana ikilinganishwa na uwiano unaokubalika kimataifa wa 1:500.

“Wakulima wameishia kuchanganya na kuja na dawa hizi hatari kwa mazingira huku wakijaribu kutafuta suluhu na tiba ya afya iliyodolola ya wanyama wao na pia kuwaondoa kupe” Rwamwiri anafafanua. Hii ni kwa sababu idadi ya wafanyakazi wa ugani nchini ni ndogo.

Wakulima wanatamani sana kupata suluhu na hii imesababisha matumizi mabaya ya dawa ambazo zingekuwa salama kwa mifugo. “Imependekezwa kuwa wakulima wabadilishe dawa zao za mifugo shambani angalau kila ya mwaka mmoja. Hata hivyo, kutokana na wakulima wengi kutumbukiza mifugo yao kwenye majosho au kunyunyizia dawa ng’ombe wao kila wiki, wengine hutumia dawa tofauti kila wiki huku wengine wakibadilisha kila mwezi ambapo wakati mwingine hutumia dozi ya juu au wengine kutumia chini ya dozi” anaonelea hivyo.

Bila ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalam wa ugani, kesi za usugu wa dawa kwa kupe zitaendelea kurekodiwa na kuwaacha wakulima wakiumiza kichwa jinsi ya kuokoa chanzo chao cha kujipatia riziki. Wanaishia kutumia dawa hatari za mifugo pamoja na michanganyiko ya dawa za kuulia wadudu.

Jeconious Musingwire ambaye kwa miaka kadhaa alifanya kazi katika shirika la kulinda mazingira la Uganda Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA) anasema ukataji miti uliokithiri katika ukanda wa ng’ombe na uharibifu wa maeneo oevu jirani umechangia pakubwa kutoweka kwa wanyama hao.

Environmentalist Jeconeous Musingwire
Mwanamazingira Jeconeous Musingwire

Ukanda wa ng’ombe ulikuwa na miti mikubwa ambayo ilitumika kuweka viota vyao vya kuzaliana huku wengine wakihamia ukingo wa maeneo oevu. “Uharibifu wa maeneo yao ya kuzaliana umeathiri kuzaliana kwao na kama ilivyo kwa Korongo wa Uganda, nao wako karibu kutoweka”.

Musingwire anawataka wahifadhi wa mazingira kuwaweka kole katika “Orodha Nyekundu”. Kulingana na Umoja wa mataifa wa Uhifadhi wa Mazingira, unasema spishi zilizo kwenye Orodha Nyekundu zipo kwenye hatari ya kutoweka.

Anasema ni wakati mwafaka kuchukuliwa juhudi za pamoja kuwahifadhi ndege hao, “tunahitaji kuwainua kutoka katika kiwango ambacho tumekuwa tukiwaona na kuwaweka chini ya Orodha Nyekundu ili kuwaepusha na kutoweka kabisa kwa kushughulikia masuala yanayosababisha kutoweka kama vile dawa za kisasa za mifugo na mazalia yao”.

Abiaz Rwamwiri – msemaji wa NDA anasisitiza kuwa dawa za mifugo zilizopo sokoni ziko salama zikitunzwa na kutumika vizuri, “dawa zilizopo sokoni zinaweza kupambana na kupe bila kuathiri ikolojia, ikiwa wakulima hawatatumia njia zao za kushughulika na dawa hizi tunazokwenda kupoteza zaidi hasa katika kilimo kwasababu wadudu wachavushaji kama nyuki kuna uwezekano wa kutoweka”.

Waziri wa Mifugo Luteni Kanali (Mst) Bright Rwamirama anasema kwa sasa wanafanyia kazi chanjo mbili za kupe. “Chanjo hizo ziko katika majaribio ya mwisho. Watu wawe na subira tunapojaribu kuhakikisha kuwa chanjo hizo hazina madhara kwa wanyama, binadamu na mazingira”.

Hadithi hii imetolewa kwa ushirikiano na InfoNile kwa usaidizi kutoka kwa IUCN/TRAFFIC na kwa ufadhili wa JRS Biodiversity Foundation na Earth Journalism Network.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts