Prosper Kwigize na Hadija Jumanne
Licha ya kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maisha ya Waafrika, maarifa asilia, mila, na tamaduni zinafifia taratibu, hasa baada ya kuvurugwa na mifumo rasmi ya kielimu.
Kulingana na ngano za jadi za Kiafrika, katika karne ya kabla ya ujio wa miongozo ya kisayansi na ustaarabu wa kimagharibi, maarifa asilia, mila, na tamaduni zilikuwa na misingi mizuri na imara zilizowezesha vyanzo vya maji na hifadhi za misitu kulindwa na jamii.
Nchini Tanzania, mojawapo ya mikoa ambayo bado inategemea maarifa asilia, mila na desturi hifadhi ya rasilimali za maji ni wilaya ya Karagwe, inayopatikana katika Bonde la mto Kagera.
“Tuna wazee wetu wa kimila, na wana umoja. Wanapokutana na vijana, hutoa maarifa asilia kuhusu uhifadhi wa rasilimali za maji na mazingira. Baadhi ya vyanzo vyetu vya maji vipo leo kwa sababu wazee wetu wamevihifadhi wao”, anasimulia Mwalimu Julieth Binyura, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe.
Viongozi hawa wa kimila wanatoka katika kabila la asili la Nyambo. Dk Godfrey Aligawesa ni mmoja wa viongozi wa jamii ya kabila hili. Anasema kabila lake lina mila na desturi maalum zinazozuia uharibifu wa mazingira, na desturi hizi zinataja adhabu kwa yeyote atakayepatikana akiharibu vyanzo vya maji.
Anaongeza kuwa wanajamii wamepigwa marufuku kulima karibu na vyanzo vya maji, kukata miti, na kufua au kuosha vyombo katika chemchemi za maziwa, au mito.
Kwa mujibu wa wataalamu wa maji na mazingira mkoani Kagera, mabadiliko ya tabianchi yamesababisha mifumo ya mvua isiyo ya kawaida, inayoathiri kilimo katika eneo hilo.
Hii inasababisha maji hayo kuingia maeneo ya vyanzo vya maji, lakini viongozi katika eneo hilo wanaongeza uhamasishaji wa jamii juu ya umuhimu huo na jinsi ya kulinda vyanzo vya maji.
“Sote tunafahamu kuwa kilimo kinahusisha ukataji miti na uondoaji wa uoto wa asili ndani maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji, lakini tunahakikisha kwamba watu wanalima kulingana na mfumo wa usimamizi wa uliopo”, anasisitiza Mwalimu Binyura.
“Nawaomba wananchi tuendelee kutunza vyanzo vya maji kama tunavyoelekezwa na wazee wetu wa kimila, na wataalam kwa sababu tukihifadhi mazingira yetu, tutaendelea kupata maji safi, anaongeza Mwalimu Binyura.
Wakazi wengi wa wilaya ya Karagwe hutumia maji yanayopatikana juu ardhini na yale ya chemichemi kwa wakati mmoja. Wanachota maji kwenye madimbwi, mifereji, mito, maziwa, na pia chemchemi, na visima.
Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mhandisi Simon Ndyamkama Wilaya ya Ngara ambayo pia ni sehemu ya Bonde la mto Kagera anaelezea umuhimu wa kushirikisha jamii kupitia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na viongozi wa kimila, sheria ndogo na sheria za serikali kuu za kulinda na kuokoa rasilimali za maji, ikiwa ni pamoja na vyanzo vya chini ya ardhi.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Andrew Athanasio anakubaliana na Mhandisi Ndyamkama. Anasema ushirikishwaji wa wanajamii, uelewa,mila na tamaduni katika uhifadhi wa misitu zimekuwa muhimu katika upandaji upya wa miti.
“Kijiografia, wilaya yetu ni ya milima, na karibu kila mlima, chini una chanzo cha maji. Sasa tunahifadhi uoto wa asili, na wananchi wetu wameambiwa wahakikishe kwamba wanahifadhi mazingira ili kulinda vyanzo vya maji vilivyopo chini ya ardhi, anaongeza Athanasio.
Mkoa wa Kagera uko chini ya chemichemi ya maji ya Kagera yenye ukubwa wa kilomita za mraba 5,778 inayozunguka hadi sehemu za kusini magharibi mwa Uganda, Burundi, na Rwanda.
Ili Kuzisaidia nchi hizi katika juhudi zao kuelekea matumizi endelevu na usimamizi wa Chemichemi za maji za Kagera, Nile Basin Initiative (NBI), taasisi baina ya serikali, hivi sasa wanatekeleza mradi unaolenga kuimarisha msingi wa uelewa, uwezo, na mikakati ya pamoja ya kitaasisi kwa nchi washirika.
Mradi wa Dola za Kimarekani milioni 5.3, Kuimarisha Usimamizi Shirikishi wa Maji yapatikanayo juu ardhini na Rasilimali za Maji ya Chini ya ardhi katika Chemichemi Zilizochaguliwa, zitajenga na kupanua zaidi uelewa wa rasilimali za maji chini ya ardhi kupitia upembuzi wa kina na tathmini ya tatu ya mifumo ya chemichemi ya maji.
Hii ni pamoja na kusaidia mafanikio ya kitaifa na kuripoti taarifa za maji zinazohusiana na Malengo ya Maendeleo Endelevu na kusaidia ulinzi wa mazingira huku kukiwa na uimarishaji wa shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika bonde hilo.
Kulingana na Dk. Maha Abdelrahim, Meneja Mradi kutoka NBI, vyanzo vingine viwili vya maji, ambavyo ni Chemichemi ya maji ya Mlima Elgon inayozihusisha nchi za Kenya na Uganda na chemichemi ya Gedaref-Adigrat inayozihusisha nchi za Ethiopia na Sudan, pia ni sehemu ya mradi huo.
Mradi huo wa miaka mitano (2020 – 2025) unafadhiliwa na Global Environment Facility (GEF), kupitia Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), na kutekelezwa na NBI.
Makala haya yamewezeshwa na InfoNile kwa ufadhili wa Mpango wa Bonde la Mto Nile.