Ongezeko la migogoro ya binadamu na wanyamapori inayohusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na uvamizi wa ufuo wa ziwa
Na Kevine Omollo
Iddi Omar Yusuf ameketi sebuleni kwake akitafakari jambo. Mvuvi huyo wa zamani na mtengenezaji wa mashua za uvuvi alipoteza uwezo wake wa kuona muongo mmoja uliopita. Akiwa na umri wa miaka 85 sasa, na afya yake ikiwa imezorota, hana tena cha kufanya. Lakini historia ya uvuvi katika Ziwa Victoria bado iko wazi akilini mwake.
Ni baadhi ya kumbukumbu gani unazofurahia kuhusu Ziwa Victoria? mwandishi anauliza.
Anarekebisha kiti chake, anainua nyusi zake, na kuanza; “Nina mazuri na mabaya, lakini ningependa kuanza na haya ya mwisho.”
“Nilimpoteza mwanangu na mjukuu wangu katika ziwa hili. Nilipata riziki yangu yote kutokana na ziwa hili,” anaongeza.
Kimya kifupi kilitanda chumbani, na mke mdogo kati ya wake zake wanne; Saumu Abdallah, akimkumbatia, ili kumfanya akae kwa raha na kujinafasi zaidi.
Nyumba ya Omar iko takriban mita 200 kutoka katika ufukwe wa Ziwa Victoria, ndani ya kijiji cha Usoma, Kisumu Magharibi. Alizaliwa na kukulia hapa. Alianza kuvua samaki akiwa na umri wa miaka 18, na alitumia takriban miaka 57 katika ziwa hilo. Aliacha uvuvi akiwa na umri wa miaka 75, wakati ambao haukuwa na nguvu tena za kutosha kufanya kazi hiyo.
“Tulipoanza kuvua samaki, kulikuwa na samaki wengi wa kutosha. Lakini wakati naacha kuvua, sikuweza hata kusimamia sehemu ya kumi ya kile tulichokuwa tukipata tulipojitosa kwenye shughuli hiyo,” alisema. Madai ya Omar yanathibitishwa na Taasisi ya Utafiti wa Majini na Uvuvi ya Kenya (KEMFRI) mjini Kisumu.
Taasisi hiyo inabainisha kuwa ziwa hilo lina shida, na watu wanaoishi kando ya fukwe ndio waathirika wakubwa wa athari za shida hizo.
KEMFRI ni shirika la serikali chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika, Idara ya serikali inayoshughulikia Uvuvi, Ufugaji wa viumbe bahari na Uchumi wa Bluu. Jukumu lake ni kufanya utafiti katika “uvuvi wa baharini na maji safi, ufugaji wa samaki, masomo ya mazingira na ikolojia, na utafiti wa baharini ikijumuisha uchunguzi wa matumizi ya kemikali na yasio ya kemikali baharini,” ili kutoa takwimu na habari za kisayansi kwa maendeleo endelevu ya Uchumi wa Bluu.
Wakati Omar akiendelea kusimulia kumbukumbu zake za ziwa, tunamrejesha kwenye simulizi ya wanafamilia aliowapoteza kupitia ziwa hilo. Anamkumbuka mjukuu wake, Ramadhan Omar, aliyevamiwa na mamba mwaka 2014 wakati akivua samaki karibu na Usoma Beach. Aliokolewa, na akapona kabisa. Lakini mwaka mmoja baadaye, alishambuliwa na kiboko, ambaye alimuua. Alikuwa na umri wa miaka 22 tu, na aliacha mke na watoto watatu.
Mwaka mmoja baadaye, mtoto wa Mzee Omar, Abubakar Iddi alivamiwa na mamba karibu na ufukwe. Mwili wake ulipatikana huku kiungo kimoja kikiwa hakipo. Alikuwa na umri wa miaka 25 alipokufa, na aliacha mke na watoto wawili.
Nchini Kenya, kifo, majeraha au uharibifu wowote unaofanywa na wanyamapori hulipwa na Shirika la Huduma za Wanyamapori (KWS). Lakini familia ya Mzee Omar bado inasubiri fidia hiyo. Kila mara Omar anapoketi kwenye nyumba yake, akitazamana na ziwa, uchungu wa kufiwa na kizazi chake hurejea tena, na kumkumbusha juu ya ziwa hilo lenye matatizo. “Siku hizi viboko wanalisha kwenye maeneo yetu, na ni hatari sana,” alisema. Na KWS inathibitisha hili.
Kulingana na Christine Boit, Mlinzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Wanyamapori nchini Kenya anayesimamia Kaunti za Kisumu na Siaya, anasema mfumo wa ikolojia ulioharibiwa, unaosababishwa na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabia nchi, ndio unaosababisha kuongezeka kwa visa vya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Hii, anasema, inawalazimu wanyama kama vile viboko kutafuta maeneo mapya ya malisho, ambayo ni maeneo yanayokaliwa na watu walio karibu na mwambao wa ziwa. Nyoka na mamba pia wanasukumwa hadi ufukweni. Anasema visa vya mizozo kati ya binadamu na wanyamapori katika kaunti za Kisumu na Homa Bay vimeongezeka kutoka 10 mwaka wa 2017 hadi 20 mwaka wa 2021, kulingana na ripoti zao za kila siku.
“Ili kukabiliana na hili, tumekuja na mikakati kadhaa, ambayo ni pamoja na kuongeza ushirikiano na jamii kuhusu mahusiano ya binadamu na wanyamapori, kuongeza vituo zaidi vya KWS ili kuongeza kasi ya mwitikio, miongoni mwa mengine,” anasema.
Kulingana na rekodi za KWS, mashambulizi ya mamba yanaongoza kwa asilimia 30, wakifuatiwa na nyani asilimia 26, viboko asilimia 20, na fisi asilimia nane. Nyoka huchangia asilimia tatu ya visa hivyo, huku wengine ni Sokwe (asilimia 6), chui (asilimia 5) na paka tsavo (asilimia 2).
Katika ripoti ya mwisho ya serikali iliyopatikana kuanzia 2015-Februari 2017, kulikuwa na zaidi ya migogoro 4,875 kati ya binadamu na wanyamapori iliyofuatiliwa kote nchini. Hii ilijumuisha vifo 28 na majeruhi 43 kutokana na viboko, na vifo 221 na majeruhi 2,670 kutokana na nyoka. Katika kipndi hicho hicho, serikali pia ililipa jumla ya Kshs 513 milioni (USD $4.3 milioni) katika madai ya fidia kwa kesi kama hizo.
Fidia bado zinachelewa
Maumivu ya Omar hayatofautiani sana na ya Mzee Sylvanus Okello Nundu, ambaye anaishi umbali wa kilomita 80 katika Kaunti jirani ya Homa Bay.
Mnano Januari 13, 2011, mwanawe Nundu mwenye umri wa miaka 13 alikwenda ufukweni mwa ziwa kuchota maji pamoja na marafiki zake. Mamba alitokea wakati wanayaacha maji, na kumkamata mtoto wa Nundu. “yowe zilipotolewa, mamba alitorokea kwenye kina kirefu cha maji akiwa na mvulana huyo,” alisema. Walimtafuta kwa wiki mbili, na hakuna kitu kilichopatikana. Hakuna hata sehemu ya mwili iliyopatikana.
Katika mila ya Wajaluo, kifo kinapotokea, hufanya mazishi kama njia ya kumaliza msiba. Wajaluo ni kabila kubwa zaidi ambalo linamiliki mwambao wa ziwa Viktoria nchini Kenya. Iwapo hakuna hata kipande cha sehemu ya mwili kitakachotolewa, familia ya marehemu huchukua vumbi kutoka eneo la tukio, au vipande vya nguo vilivyoachwa, kwaajili ya mazishi. Ikiwa hakuna chochote kati ya hivyo, kilichopatikana, familia huzika shina la ndizi.
Lakini kwa Mzee Nundu mwenye umri wa miaka 54, hilo halikufanyika. “Mimi na mke wangu ni Wakristo wenye imani na tulichagua kusali badala ya kufuata njia za kitamaduni,” alisema. Wakati Lake Region Bulletin ilipoitembelea familia hiyo, Nundu alikuwa tayari kazini kwake katika Shule ya Sekondari ya Lala iliyoko Arojo, nje kidogo ya mji wa Homa Bay.
Kwa hivyo, ilimbidi kusubiri kwa miaka saba kabla ya kudai fidia yoyote, kipindi kinachotambuliwa na sheria za Kenya ili kuthibitisha kwamba mtu ambaye hajulikani aliko anaweza kutangazwa kuwa amefariki. Wakati wa kukutana na Bulletin ya Kanda ya Ziwa, Nundu alikuwa akisubiri mawasiliano kutoka KWS kuhusu maendeleo ya fidia hiyo.
“Hasara ilikuwa kubwa, na imeathiri familia yangu hadi leo,” alisema Nundu. Anasema watoto wake watatu waliobaki hawaendi tena ziwani, maji au kunywesha wanyama. “Kwangu mimi, sina chaguo. Pamoja na hofu hiyo, sina budi kwenda ziwani,” anasema. “Hata ajali za barabarani zinaua watu kadhaa kila siku, lakini watu bado wanatumia usafiri wa barabarani.”
Migogoro na wanyamapori inayohusishwa na mabadiliko ya tabia nchi na uvamizi
Huko Kisumu Magharibi, Florence Atieno alifiwa na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 17 Januari 24, 2016. Mvulana huyo, Duncan Otieno alikuwa ameenda kuoga ufukweni; mamba alipomrukia. Mayowe kutoka kwa mashuhuda hayakuzaa matunda, na mnyama huyo alifanikiwa kuondoka na mvulana ndani ya maji yenye kina kirefu, na kuacha nguo zake ufukweni.
Lakini, tofauti na tukio la Nundu, Bi Atieno, 55, alifanikiwa kupata baadhi ya sehemu za mwili wa mtoto huyo; na kuzika. Huyu alikuwa kitinda mimba wangu, na unaweza tafakari uchungu wa kumpoteza kitinda mimba,” alisema.
Andrew Rakwaro ni Mwenyekiti wa usimamizi wa Usoma Beach Management. Ameshuhudia maisha ya watu wengi wakipotea ziwani, na pia ameshiriki katika baadhi ya harakati za uokoaji au utafutaji. “Kukuta viboko katika boma zetu na mashamba yetu si habari tena,” anasema.
Rakwaro, 48, alizaliwa na kukulia katika kijiji hiki, na amekuwa mvuvi maisha yake yote. Tulipomtembelea, Bw Rakwaro alitupeleka kwenye ufukwe wa ziwa.
“Unaweza kuuona ule mti pale? Huo ulikuwa ufukwe, lakini maji yameongezeka katika mashamba na nyumba zetu. Sio sisi tunaovamia mfumo ikolojia wa wanyamapori, kama KWS inavyodai,” asema.
Maoni ya Rakwaro yanaungwa mkono na Shirika la anga la Marekani (NASA). Takwimu za Rada za Altimetry (Radar Altimetry Data) zinaonyesha kuwa viwango vya maji vya Ziwa Victoria vilifikia mita 1,137.29 juu ya usawa wa bahari mnamo Mei 19, 2021, kiwango cha juu zaidi kurekodiwa kwa rekodi za takwimu za satelaiti za mwaka 1992.
Kwa Michael Nyaguti, mwanaharakati wa mazingira katika mwambao wa Ziwa Victoria, hakuna mtu anayepaswa kuelekeza lawama juu ya ziwa linalovuja damu. “Ni wazi kwamba makazi na maeneo ya malisho ya wanyamapori hawa yameingiliwa,” anasema.
Lake Region Bulletin lilipompata, Bw Nyaguti alikuwa akijiandaa kwa ajili ya kongamano la mazingira, lakini alijitenga na kutupeleka ufukweni. Tuliposogea karibu na maji, kulikuwa na lundo la mchanga wa kuchimba. “Unaweza kuona hili? Je! hili silo nililokuwa nazungumzia?” alisema.
Anaongeza kuwa, “Chakula kikuu cha Mamba ni nyama. Lakini samaki wanapopungua na makazi yake kuharibiwa, ikiwa ni pamoja na maeneo oevu ambayo huhifadhi baadhi ya wanyama wanaokula, basi hubaki na binadamu kama chakula.”
Nyaguti amekuwa akiongoza vita vikali dhidi ya samaki wadogo na wakubwa; wavuvi wanaotumia nyavu haramu za uvuvi, wakusanyaji kuni wakikata mimea kwenye ufukwe wa ziwa, na wanaume na wanawake wakubwa ambao wamekuwa wakijichukulia ardhi kando ya ufukwe.
Kupitia shirika lake la usimamizi wa mazingira- MAGNAM, Nyaguti amekuwa akitetea uhifadhi, pamoja na utatuzi wa kisheria dhidi ya wanaofanya uhalifu wa mazingira katika ziwa hilo.
Wakati wa mkutano wetu, alikuwa akingojea uamuzi wa kesi mahakamani ambapo alikuwa akitaka kunyang’anywa vipande vya ardhi vinavyodaiwa kunyakuliwa na waliokuwa maofisa wakuu watatu wa serikali.
Mnamo 2013 baada ya kesi yake, Mahakama ya Mazingira na Ardhi huko Kisumu iliamuru uchunguzi ufanyike kuhusu mashamba matatu ya kando ya ziwa yaliyokuwa yakishikiliwa na aliyekuwa gavana wa Kisumu Jack Ranguma, aliyekuwa gavana wa Nairobi Evans Kidero, na aliyekuwa Katibu wa Mazingira Alice Kaudia.
Mnamo mwaka wa 2018, Kaudia na Ranguma walizuiliwa kufanya shughuli zinazoweza kusababisha madhara ya mazingira katika ziwa hilo baada ya kubainika walikuwa wameweka uzio wa viwanja ndani ya hifadhi ya ziwa. Kesi bado inaendelea.
Katika kesi nyingine ya 2020, Nyaguti alishtaki Mamlaka ya Bandari Kisumu na afisa anayesimamia Kituo cha Polisi cha Reli na Bandari, kwa madai kuwa walikuwa wamewaamuru wavuvi kuondoka katika eneo la kutua la Kichinjio BMU ili kuendeleza bandari ya Kisumu bila kuwapa eneo mbadala la uvuvi, au kutangaza kwenye gazeti la serikali eneo oevu. Katika kesi hiyo, mahakama iligundua kuwa washtakiwa walikuwa wamekiuka haki za kiuchumi za wavuvi kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Kenya.
“Nimechukiwa hapa,” Nyaguti anasema, akiongeza kwamba alifukuzwa ofisini kwa njia isiyo ya kawaida kama mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe kufuatia msimamo wake mkali kuhusu uhifadhi wa ziwa.
Mpango wa anga wa kuweka mipaka maeneo yenye bayoanuai
Dk. Christopher Aura ni Mkurugenzi wa Utafiti wa Mifumo ya Maji Safi KEMFRI. Anahusika na utafiti wa maji katika maziwa ikiwa ni pamoja na; Victoria, Turkana, Naivasha na Baringo. “Mbali na kufanya utafiti katika mfumo ikolojia wa majini, tunafanya tathmini ya hali na kufuatilia mifumo ya majini na kuishauri serikali juu ya uhifadhi,” anasema.
Kulingana na KEMFRI, bayoanuai ya Ziwa Victoria imegawanywa katika Flora (mimea), Fauna (wanyama) na Wasio hai (maji, mchanga, kati ya zingine). Dk. Aura anathibitisha kwamba Ziwa Victoria kweli linavuja damu. Kulingana na Dk. Aura, shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabia nchi yanabaki kuwa tishio kubwa kwa mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo.
“Kuna shinikizo la uvuvi, mabadiliko ya ubora wa maji, uhusiano usio na usawa wa wanyama wanaowinda wanyama wengine, na masuala ya utawala ambayo yanapaswa kuangaliwa,” anasema. Anasema changamoto hizi ndizo za kulaumiwa kwa ongezeko la visa vya migogoro ya binadamu na wanyamapori.
Dk Aura anakiri kwamba Ziwa Victoria halina mpango wa anga ambao ungeongoza uvunaji endelevu wa rasilimali zake. Bila hati kama hiyo, watu wanaoingiliana na ziwa hawana ujuzi juu ya hesabu ya wanyama wakubwa kama vile mamba na viboko. Kwa ufahamu mdogo juu ya maeneo yao ya kulisha, na uzazi, wanadamu wanalazimika kugongana nao, na kusababisha mzozo.
“Kwa sasa tunaongoza timu ya washikadau ambao watakuwa wakitekeleza mpango wa anga ili watu waelewe kuhusu bayoanuwai, kupitia uwekaji wa maeneo yenye maeneo motomoto kwa sababu ziwa lina kazi nyingi na halipaswi kuachwa kufanyiwa upasuaji kama pori,” alisema.
Dk. Aura anahisi kuna haja ya kuimarisha utekelezaji wa mifumo ya udhibiti juu ya ulinzi wa ziwa. Pia anabainisha kuwa upangaji wa anga utasaidia katika kutenga maeneo mbalimbali ya ziwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali, hivyo kuleta utulivu na unyonyaji endelevu. Majina hayo yanaweza kujumuisha kuwa na maeneo ya wazi ya uvuvi, maeneo ya kuzaliana samaki, maeneo ya kuzaliana na malisho ya viboko na mamba, maeneo ya usafirishaji, miongoni mwa mengine.
Mnamo mwaka wa 2022, Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Rasilimali za Uvuvi nchini Uganda ilizindua Tovuti ya Uganda Freshwater Biodiversity Portal, tovuti ya takwimu inayofuatilia na kuweka ramani matukio ya viumbe vya maji baridi nchini Uganda, ikiwa ni pamoja na katika Ziwa Victoria.
Sampuli ya maji haikidhi viwango vya maji ya kunywa
Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) ni wakala wa serikali uliopewa jukumu la kuratibu usimamizi wa mazingira nchini Kenya. Tom Togo, Mkurugenzi wa NEMA Kaunti ya Kisumu, anasema Ziwa Victoria linakabiliwa na uchafuzi wa mazingira unaotoka umbali wa kilomita 50.
Kulingana na Bw Togo, uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za kilimo unaongoza kwa kuchafua ziwa kwa asilimia 40, ukifuatiwa na uchafuzi wa taka za nyumbani kwa asilimia 30. “Uwezo wa kusambaza maji taka katika mji wa Kisumu uko chini hadi chini ya asilimia 20. Hii inamaanisha kuwa taka nyingi za vimiminika ambazo hazijadhibitiwa huingia ziwani,” alisema.
Kulingana na Kampuni ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Kisumu (Kisumu Water and Sanitation Company -KIWASCO), taasisi ya serikali inayohusika na kutoa huduma za maji na usafi wa mazingira mjini Kisumu, mji huo kwa sasa una kiwango cha maji taka cha asilimia 18, na maji ya bomba kwa asilimia 83.
Togo alibainisha kuwa mfereji wa maji machafu uliowekwa katika miaka ya 1950 tangu wakati huo umezidiwa na ongezeko la watu mjini, na hauwezi tena kuhudumia ipasavyo. Anasema chombo hicho kimekuwa kikichukua nafasi kubwa katika kukabiliana na wachafuzi wa mazingira, lakini akalaumu udhaifu katika utekelezaji wa sera za uhifadhi kama kiungo dhaifu zaidi katika kulinda ziwa.
Alibainisha kuwa maeneo oevu mengi katika eneo hilo hayajatangazwa kwenye gazeti la serikali kama maeneo ya hifadhi, hivyo kuzuia msako dhidi ya wanaoharibu maeneo hayo. Dunga, Lwang’ni na Kichinjio ni baadhi ya maeneo oevu ambayo hayana ulinzi.
Lakini pamoja na changamoto hizi, taasisi hiyo iliweza kufungua kesi 12 za kisheria dhidi ya waharibifu wa mazingira katika eneo hilo mnamo mwaka 2021. “Saba kati ya kesi hizo zilitolewa, wakati tano bado zinaendelea,” aliongeza Togo. Mwaka huu, kesi nyingine tatu zimewasilishwa mahakamani.
Kulingana na Togo, taka zisizodhibitiwa ambazo huingia kwenye ziwa huharibu mfumo ikolojia, na kufanya maisha kuwa mabaya kwa viumbe vya majini. Madai ya Togo yanathibitishwa na ripoti ya tathmini ya kemia ya maji kwenye mifereji ya maji taka inayotiririka katika Ziwa Victoria kwenye ghuba ya Kisumu iliyofanywa kati ya Julai 4 na 8, 2022, na InfoNile kwa ushirikiano na Mamlaka ya Rasilimali za Maji (WRA).
Mradi huu uliofadhiliwa na InfoNile kwa usaidizi kutoka JRS Biodiversity ulichukua sampuli 24 za maji ili kupima miongoni mwa vigezo vingine; Mahitaji ya Oksijeni ya Kibiokemikali (BOD), Mahitaji ya Kemikali ya Oksijeni (COD), Turbidity, Alkalinity, Mafuta na Grisi, pH, Nitrojeni, Fosforasi, na Metali kama vile Ledi, Zebaki na Kalshiamu.
Tathmini hiyo ilifanywa katika sehemu ya mashariki ya ghuba ya Winam ya Ziwa Victoria ndani ya eneo la Kenya katika Kaunti ya Kisumu. Sampuli zilichukuliwa kando ya Rivers Auji na Kisat na ghuba ya Kisumu.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa Mto Auji na Kisat ndio njia kuu za uchafuzi wa mazingira katika ghuba hiyo. Mito yote miwili inapita katikati ya makazi ya Kisumu, ikiingiliana na shughuli za kibinadamu ambazo huchangia uchafuzi wao.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya shughuli zinazochafua mto huo ni pamoja na dampo zisizo na udongo katika makazi yasiyo rasmi, uchafu wa maji maji kutoka kwenye nyumba za jirani, miundombinu duni ya usafi, maji ya kuoshea magari yanayotiririka moja kwa moja mtoni, na wakati mwingine kutoka kwenye magari yanayotiririka yanaelekea moja kwa moja kwenye mto.
Vyanzo vingine vya uchafuzi wa mazingira ni pamoja na taka zilizooza zinazotiririka kutoka kwenye dampo la Kachok wakati wa msimu wa mvua, utupaji mbovu wa mafuta yaliyotumika kutoka katika gereji za magari ya Jua Kali, utupaji wa mifereji ya maji taka ndani ya mto, na kuziba mifereji ya maji taka inayotiririsha maji taka kwenye mifereji ya dhoruba, ambayo huelekea mtoni wakati wa mvua.
Tathmini ilionyesha kuwa baadhi ya viashiria vilikuwa ndani ya viwango vilivyopendekezwa, ikiwa ni pamoja na pH, Upitishaji wa Umeme, Jumla ya Fosforasi, Chlorophyll, Cadmium na Zebaki.
Hata hivyo, ripoti hiyo ilionyesha kuwa Mahitaji ya Kemikali ya Oksijeni (COD), Jumla ya Coliforms na E-coli, Lead, na Mafuta na viwango vya Grease vilikuwa juu ya viwango vilivyopendekezwa. Jumla ya Nitrojeni, Total suspended solds, Mahitaji ya Oksijeni ya Kibiokemikali, na Thamani za Oksijeni Iliyoyeyushwa pia zilikuwa nje ya viwango vinavyopendekezwa, hasa katika Mto Kisat.
Mahitaji ya Oksijeni ya Kemikali (COD) ni kiasi cha oksijeni kinachohitajika ili kuongeza oksidi ya viumbe hai vilivyomo ndani ya maji. Kadiri thamani ya COD inavyoongezeka, ndivyo uchafuzi wa maji unavyozidi kuwa mbaya.
“Mkondo wa Mto Kisat, Mto Kisat kwenye klabu ya gofu, Mto Kisat chini ya mkondo wa ETP, rasi ya Kisat ETP na Nyalenda humwaga thamani iliyorekodiwa ya COD kati ya 64 – 160 mg/l. Maadili hayazingatii Kiwango cha Utiririshaji wa Effluent Afrika Mashariki cha upeo wa 60 mg/l,” ilibainisha ripoti hiyo.
Coliforms na e-coli ni bakteria wanaopatikana kwenye kinyesi. Jumla ya hesabu za coliform hutoa dalili ya jumla ya hali ya usafi wa usambazaji wa maji. Jumla ya kolifomu ni pamoja na bakteria wanaopatikana kwenye udongo, kwenye maji ambayo yameathiriwa na maji ya juu ya ardhi, na katika taka za binadamu au wanyama. Ikiwa sampuli ya maji ina e-coli, inamaanisha kuwa kuna uwezekano kwamba maji yamechafuliwa na maji taka au samadi.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa sehemu zote za sampuli kando ya Mto Kisat, Mto Auji, Kituo cha kutibu maji taka cha na kituo cha kisasa cha kutibu maji cha Nyalenda vilionyesha majaribio chanya kwa coliforms na makoloni ya e-coli kwa kila 100ml ya Too Numerous to Count (TNTC).
Maji ya kina kirefu katika ghuba hiyo pia yalisajili colonies ya E-coli kwa kila 100ml ya thamani kati ya 28 na 46.
“Viwango hivyo ni dalili ya kutofuata viwango vya maji ya kunywa vya Afrika Mashariki,” ilisoma ripoti hiyo. Tovuti hiyo hiyo ya sampuli ya ziwa ilionyesha na kusajili majaribio chanya kwa jumla ya colonies ya kolifomu kwa kila 100ml ya thamani kati ya 62 na 86.
Kulingana na Bw. Fanuel Onyango, Afisa Udhibiti wa Ubora wa Maji na Uchafuzi katika Mamlaka ya Rasilimali za Maji, Eneo la Bonde la Ziwa Victoria, bakteria hao wawili wanauawa wakati wa matibabu ya taka ya kibiolojia. “Katika hatua ya mwisho ya matibabu ya taka, Usafi (disinfection) unapaswa kufanywa ili kuua bakteria,” alisema.
Hata hivyo, kulingana na Mamlaka ya Rasilimali za Maji, uchafuzi wa kolifomu unaweza kuwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa mitambo ya kisasa ya kutibu maji machafu ili kuua vijidudu vya mwisho.
“Mitambo ya kutibu maji machafu haijajumuishwa na mfumo wa matibabu wa hali ya juu wa kuua vijidudu kabla ya kutiririka kwenye mazingira. Zaidi ya hayo, maji machafu ya majumbani ambayo hayajatibiwa yanayotoka katika makazi yasiyo rasmi ya Obunga na Nyalenda na pia maji yanayotiririka na dhoruba yanayotiririka moja kwa moja kwenye mito na ziwa yanaweza pia kuwa chanzo cha uchafuzi wa coliform,” ripoti hiyo ilibainisha.
Dk Onyango alibainisha kuwa kuwepo kwa bakteria hao kwenye maji ni dalili ya kuwepo kwa bakteria wengine wa pathogenic kama wale wanaosababisha homa ya matumbo (typhoid) na kipindupindu.
Kulingana na ripoti ya Kenya Health Information Systems (KHIS), matukio ya magonjwa yanayoenezwa na maji yakiwemo kipindupindu na salmonella katika kaunti ya Kisumu kwa ujumla yamepungua kutoka 2017-2021, ingawa homa ya ini iliongezeka tena 2020.
Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya sehemu za sampuli pia ziligundua risasi (Lead) katika kiwango kilicho juu ya kiwango kinachopendekezwa.
“Vituo hivi viko karibu na bandari ya reli ya Kisumu ambayo iko karibu na mji na makazi yasiyo rasmi ya Obunga na Nyalenda,” ripoti hiyo ilisema. “Shughuli mbalimbali za “juakali” na taka kutoka maeneo haya, mafuta ya risasi (lead) yanayotumiwa na magari, rangi na utupaji wa taka za viwandani na manispaa huenda vikawa chanzo cha risasi (lead) katika maeneo haya.
Risasi ni sumu kali sana katika mwili wa binadamu. Inaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, kama vile kupoteza uwezo wa kusikia, shinikizo la damu, kuharibika kwa figo, kutofanya kazi kwa mfumo wa kinga, na sumu kwenye viungo vya uzazi. Hasa ni hatari kwa kiumbe kilichoko tumboni, watoto wachanga na watoto wadogo, ambao viungo vyao vinaendelea kukua.
Mabwawa ya oksidi ya Kisat na Nyalenda hayana uwezo wa kudhibiti viwango vya ziada vya metali nzito, ripoti ilihitimisha.
Hakuna zebaki iliyogunduliwa katika sampuli ya 2022 huko Kisumu, ingawa viwango vya zebaki viligunduliwa hapo awali kwenye maji na samaki katika Ghuba ya Winam, Kenya.
Pamoja na afya ya binadamu, uchafuzi wa mazingira pia huathiri viumbe hai vya majini. Katika tathmini, Mafuta (Oil) na Grease pia yalikuwa juu ya viwango vilivyopendekezwa, ambayo inaweza kuingilia kati maisha ya kibaolojia katika uwanda wa maji na kutengeneza filamu zisizovutia.
Dk. Paul S. Orina, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufugaji wa viumbe Maji katika Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi ya Kenya, alitoa maoni kuhusu matokeo ya sampuli ya 2022.
“Viwanda vingi, viwanda na karakana za sekta isiyo rasmi ndio vyanzo vikuu vya utiririshaji wa mafuta na grisi kwenye mfumo ikolojia wa ziwa,” aliandika. Pia alibainisha kuwa uchafuzi wa mazingira unaogunduliwa una athari kubwa kwa viumbe wanaoishi ndani ya maji.
“Viwango vya juu vya uchafuzi wa mazingira kando ya mito kutoka mahali pa kutibu maji ina athari kubwa kwa huduma za mfumo ikolojia wa mto kwa wanyama wadogo na wasio na uti wa mgongo,” aliandika. “Viwango vya uchafuzi wa mazingira huzuia utofauti, wingi na utajiri wa viumbe vya majini. Zaidi ya hayo. kwa hawa avian (ndege) wanaweza kuwa wanaumwa kimyakimya kutokana na ulaji wa viumbe vilivyo na mrundikano wa metali nzito. Hii inaweza kusababisha kupungua kwa ndege wa majini katika miaka ya hivi karibuni.”
Uhai wa majini hutegemea kiwango cha kutosha cha oksijeni iliyoyeyushwa ndani ya maji. Katika sehemu kadhaa za sampuli kando ya Mto Kisat, thamani zilikuwa chini ya viwango vya chini, kumaanisha kuwa viwango vya oksijeni vilikuwa chini sana.
Naitrojeni, ambayo huchochea ukuaji wa mwani(algae) ambao hupunguza oksijeni, pia ilikuwa juu sana katika sehemu mbili za sampuli za Mto Kisat. Naitrojeni inaweza kutoka kwenye mbolea za kilimo, maji machafu, na taka za wanyama.
Ubora wa maji katika Ziwa Victoria umekuwa ni tatizo kwa miaka mingi. Utafiti wa 2020 na sampuli zilizokusanywa mwaka wa 2015 kutoka fukwe mbalimbali za uvuvi katika Ziwa Victoria upande wa Kenya ulihitimisha kuwa vigezo vya ubora wa maji vinatofautiana kwa kiasi kikubwa katika maeneo tofauti ya sampuli katika eneo lililofanyiwa utafiti.
Hata hivyo, sampuli zilizofanywa mwaka 2022 zilionyesha kiwango cha kemikali ambacho “kimekuwa kikiongezeka hatua kwa hatua,” kulingana na ripoti ya Mamlaka ya Rasilimali za Maji (Water Resources Authority report ) iliyoombwa na InfoNile.
Wastani wa thamani za mahitaji ya oksijeni ya kibiokemikali (BoD), jumla ya yabisi iliyoyeyushwa na jumla ya yabisi iliyosimamishwa ilikuwa juu zaidi katika sehemu nyingi za sampuli mwaka wa 2022 kuliko katika maeneo ya karibu ya Kichinjio na Seka mwaka wa 2015, ingawa maeneo yalikuwa tofauti kidogo. Hii inaonyesha uwezekano wa kuzorota kwa uchafuzi wa maji.
“Inaweza kuzingatiwa kuwa ghuba ya Kisumu katika upande wa Ziwa ina sifa ya kemikali za maji ambazo viwango vyake katika maji vinaongezeka polepole huku thamani za baadhi ya kemikali na vichafuzi vya viumbe hai vikizidi viwango vinavyopendekezwa vya Afrika Mashariki vya Utiririshaji wa Maji taka, Usimamizi wa Mazingira na Sheria ya Uratibu ya (2006) na Kanuni za Usimamizi wa Rasilimali za Maji (2007),” ripoti ya Mamlaka ya Rasilimali za Maji inahitimisha.
Ripoti inapendekeza utekelezaji wa hatua za makusudi zinazolenga kupunguza mizigo ya uchafuzi wa mazingira ili kuhakikisha utiririshaji wa maji taka yanayokidhi mahitaji katika rasilimali ya maji.
Pia inatoa wito wa kuimarishwa kwa kanuni za kitaifa na mashirika husika ili kuhakikisha uzingatiaji wa usimamizi wa taka.
Dakt. Orina anakubali hivi: “Kuna uhitaji wa kuimarishwa kwa sera na kanuni zilizopo za miradi yoyote kuhusiana na mazingira badala ya kuwa nazo kwenye makaratasi,”.
Tarifa hii imezalishwa Kwa ushirikiano na InfoNile kwa ufadhili wa JRS Biodiversity Foundation; ripoti ya ziada na Annika McGinnis, Ruth Mwizeere na Primrose Natukunda.