Curity Adhiambo na Alis Okonji
Mto Kisian hupitia milima ya Kisian hadi kijijini. Mashamba madogo yanaonekana kwa umbali, huku kilimo cha unyunyizi usio rasmi ukistawi ukingoni mwa mto.
Mary Akinyi Ouko, aliyeolewa akiwa na miaka 13 tu, alijiunga na jamii ya Kisian Mashariki ya Kisumu, Kenya, angali mwanamke mdogo; mchanga zaidi. Kwa miongo sita iliopita Ouko na familia yake wameishi kijiji hiki, huku wakipata riziki yao kutoka kwa mto Kisian, pamoja na mamilioni ya Wakenya. Walakini, yeye hajui chanzo chake.
“Kwa kusema kweli, sijui chanzo cha mto huu,” asema Ouko, mzaliwa mtunga hadithi asili, hapo anasisitiza kwamba “Najua unatoka mbali sana, labda Kajomwa- maneo ya Magharibi ya Kenya”, huku akikumbuka tu kumbukumbu zinazofifia.
Hata hivyo, ana uhakika na jambo moja: mto huu ni wa maana sana kwake na jamii ya hapa. Umehudumia bibi zao wakuu, ambao walipitisha manufaa ya mto huo kwao, na sasa wanawapitishia wajukuu wao. Umekuwa kama chemichemi kinachoendelea kutoa maji bila kulegea yanapohitajika. Ni chanzo cha maji ya kunywa kwa jamii na mifugo wao; wanayatumia kupikia, kwa kilimo na ujenzi, miongoni mwa mambo mengine. Mto Kisian unashikilia jamii hii pamoja; ukiteremka kwa siri, kumbukumbu, kifo, furaha, uovu, na mengi zaidi.
Ni kiini cha jamii hii.
Mto na Chanzo chake
Chanzo cha Mto Kisian unaanza kwa Msitu wa Maragoli na kuzungukwa na vyanzo vya maji ya Riat na milima Kodiaga. Unateremka kupitia Wilaya ya Kisumu.
Eneo hilo hupokea mvua mara mbili kwa msimu, mmoja mfupi kutoka Oktoba hadi Disemba na msimu wa mvua mrefu kuanzia Machi hadi Julai. Mvua hutofautiana kwa viwango kutoka 258.0mm hadi 816.0mm kila mwaka. Wakati wa mvua kubwa, sehemu za juu za mto hupata mvua nyingi sana, na husababisha Mto kufurika zaidi, kuvunja kingo zake na kuosha mashamba ya nyanda za chini.
Tabia na Harakati za Mto Kisian
Tabia inaweza maanisha utulivu na amani, pamoja na harakati kidogo au shughuli. Katika fani hii, ninarejelea mwendo wa Mto Kisian kama safari ya amani kabla tu kuingia kijijini.
Milima yenye mawe ya Kisian, kwenye mto unapitia, ni ya kuvutia sana kana kwamba ni ajabu usioaminika. Unapokuwa hapa, unajihisi kama unasafirishwa kwa ulimwengu mwingine ambao mambo yake ni tulivu tupu.
Nimekulia hapa. Safari hii ya kuandika masaibu ya Mto Kisian unanikumbusha utoto wangu wakati rafiki zangu na mimi tungethubutu kuogelea ndani yake. Bila shaka, nilikatazwa kuogelea kwa Mto huu kwa sababu mama alifahamu ningezama, na ni sawa kwa sababu singeweza kuogelea.
Hapo awali, nakumbuka mto huu ulikuwa wenye kina kirefu, na kingo zenye afya pamoja na mimea maji. Nakumbuka nyoka walikuwa wanazaana kando ya mto huu. Tungefua nguo zetu kwa kingo zake, kuoga na kuwaleta mifugo wetu kunywa maji. Kulikuwa na waogeleaji kila wakati wakipiga mbizi kutoka kwa ukingo moja hadi mwingine wenye kina kirefu, huku wapiga kelele, kucheka, na kucheza michezo mingi ndani ya maji. Hizo ndizo kumbukumbu za utoto ambazo ninathamini sana hadi sasa. Mto Kisian ulikuwa pahali pa furaha pwangu wakati wote.
Mto Kisian kwa Usalama wa Chakula
Kijijini Kisian wakulima wanakuza mboga, mahindi, mitama, maharagwe, gramu za kijani, na kunde. Wanatumia maji ya mto Kisian kwa unyunyizi. Mamia ya mashamba yako kwenye kingo za Mto.
Chiro (soko la jamii) limejaa mazao kutoka kwa mashamba na bustani jirani ambazo wakulima, wafanyabiashara, na wanawake huweka bidha zao kila jioni kwa minajili ya kuuza.
“Niliwahi kuwekeza kwenye kilimo wakati ulikuwa wazi nisingeweza kupata kazi haraka baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu. Nilihitaji kutunza familia yangu; kilimo kando ya Mto kilinisaidia kwa kupata maji kwa urahisi kumwagilia matunda na mboga zangu, ambayo ningewauzia wanawake sokoni kwa faida,” Francis Oduor, mkulima wa zamani na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Egerton.
Licha ya usalama wa chakula unaoonekana wa faida za kiuchumi wa Mto Kisian kwa jamii hii, manufaa ya unyunyizi endelevu kwa ardhi na kilimo ni suala linalojitokeza.
Mwaka wa 2015, Sekretarieti (Nile-sec) wa Nile Basin Initiative (NBI) ilifanya Uchambuzi Mkakati wa Rasilimali za Maji kwa nia ya kuendeleza endelevu ya kukidhi mahitaji ya maji yanayozidi kuhitajika kwenye nchi maneo ya mto Nile, ikiwemo Kenya, na kupunguza shida za maji ya sasa na baadaye.
Utafiti huo uligundua kuwa upanuzi na kuimarisha kilimo ni muhimu kwa kuhakikisha usalama wa chakula, uboreshaji maisha, na kupunguza umaskini katika bonde. Uboreshaji wa vifaa vya unyunyizi unazingatiwa kuwa mkakati muhimu kwa kuongeza tija katika kilimo.
Kulingana na ripoti hii, nchi za Uhabeshi, Kenya, Sudan, na Tanzania, eneo chini ya unyunyizi kwa mimea ni ndogo sana likilinganishwa na eneo lililopangiwa unyunyizi kutokana na utofauti kati ya maji yanopatikana na mahitaji yake.
Mto Kisian uko katika eneo lililorodheshwa kati ya Entebbe Nile Basin Initiative (NBI)) kwa msingi wa Juhudi za Pamoja ya Bonde la Nile kwa ripoti yao ya kiufundi kama Pembezoni hadi Wastani inafaa kwa unyunyizi. Ripoti hiyo ilikadiria ufaafu wa ardhi kwa kutathmini udongo na ardhi, mteremko wa topografia, na mali ya udongo kikamilifu na kikemikali.
Shughuli za kibinadamu, zikiwemo ukataji miti na ukulima kando ya Mto Kisian, husababisha kuongezeka kwa joto la maji, umeme majimaji, jumla ya vigae vinavyoelea na kuchanganyika kwa maji na tope, hii ni kulingana na Kituo cha Utafiti wa Uvuvi na Baharini ya Kenya (yaani, Kenya Marine and Fisheries Research Institute -KMFRI).
Mifugo wametumia vibaya maeneo ya kando ya mto na kuongeza amonia na nitriti kutokana na kuongezeka kwa chafu za mifugo kwenye vijito. Shughuli za binadamu kando ya mto kama uchimbaji mchanga, kuoga, kufua nguo na kilimo cha mimea yanayopandwa kwa mistari imeathiri pakubwa makazi na mkondo wa kijito na sifa za kibayolojia.
Kwa miaka mingi, ukingo wa Mto Kisian umekuwa ukikabiliwa na uvunaji mkubwa wa mchanga, na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo wakati wa mvua kubwa au mafuriko. Mto Kisian unafahamika kwa kuvunja kingo zake wakati wa msimu kama huo, lakini maporomoko ya ardhi yanaelekea kusababisha kingo zake kupanuka kwa sababu ya mchanga kuvunwa.
Juhudi za pamoja ya Bonde la Nile inafahamu ya kuwa kutekeleza vipimo vya mwenendo wa mazingira kwa mahitaji yako kwa hatua ya mapema. Sera za kitaifa zinazoshughulikia mwenendo wa mazingira ni za Tanzania na Kenya pekee. Tathmini na ufuatiliaji zaidi kwa hali ya kihaidrolojia na za maji masafi na mifumo ya ikolojia inahitaji mpango endelevu na usimamizi wa kuhifadhi maji . Mwenendo wa mazingira kwa ufupi ni ubora na wingi wa maji masafi kwa kijito au mto kwa muda mrefu.
Nchini Kenya kanuni ya matumizi endelevu husema kwamba, rasilimali za mazingira zitatumika kwa namna ambayo haziathiri ubora na thamani ya rasilimali, au kupunguza uwezo wa kushikilia mifumo ya ikolojia.
Hali Mbaya
China ya daraja la makutano ya Mto Kisian, mita michache kutoka kwa soko la Kisian ni mahali wakazi wengi huja kuteka maji ya kunywa or kupikia. Msichana wa shule pia anaviosha viatu vyake kando ya ukingo.
Mbali na mchanga na miamba, kuvunwa kwa mchanga aina ya klei ni shughuli nyingine ya uharibifu wa uchumi wa mazingira zinazofanyika kwa Mto Kisian. Vyungu vya ajabu na vilivyochongwa vya kupendeza ni baadhi ya vifaa vya ufinyanzi kutoka kwa udongo uliovunwa kwa kingo za Mto Kisian.
“Wanawake wengi wanategemea ufinyanzi kwa kulisha familia zao. Uvunaji wa udongo umekuwa katika jamii zetu kwa miaka mingi! Miaka michache iliyopita, baadhi ya wafinyanzi walizikwa ndani ya machimbo hayo huku wakichonga udongo,” asema Mourine, mkazi hapa.
Wavunaji wa udongo mara nyingi hushawishiwa kuchimba zaidi kwenye kingo za Mto kwani wanaamini huko ndani wanaweza pata udongo uliosafishwa zaidi, laini na bora zaidi. Vichuguu na machimbo waachao nyuma huathiriwa kwa kusombwa na maji na mara nyingi kuanguka.
Watoto wanaotumia barabara hii wanalazimika kuvuka Mto kila siku ili kwenda shule pia wako hatarini kwa sababu daraja iko karibu kuporomoka na barabara za kutembelea zimemomonyoka. Hivi karibuni harakati katika sehemu hizi za Mto Kisian zitakuwa haziwezekani. Licha ya uharibifu unaoonekana, uvunaji wa udongo unaendelea kutokana na ukosefu wa ajira na umaskini.
“Hawa wavuna mchanga sio watu waovu; ni watu tunaowajua; hawana ajira; jinsi gani nyingine wanatakiwa kutunza familia zao,” alihoji mwanamke mmoja ambaye jina lake halikufahamika akiyachota maji karibu na miteremko ya kingo zilizomomonyoka. Maji aliyokuwa anayochota hayakuonekana kuwa safi hata kidogo.

Nashangaa alifikaje pale na atapandaje akirudi.
“Nimezoea,” asema, “lakini inakuwa ngumu zaidi na zaidi kuyapata maji kutoka upande huu wa mto kutokana na miteremko. Wakati wa mvua, hatuwezi hata kukaribia kingo hizi; ni mtego wa kifo” anaeleza.
Vile ninavyofahamu, shughuli kama uvunaji mchanga zinaweza kusababisha matatizo yao; jamii hawajui cha kufanya, wakiwaona wavunaji mchanga wamezidi ujanja wenye mamlaka.
Wakati Mamlaka ya Kitaifa ya Mazingira (NEMA) wanashika doria, lori zinazosomba mchanga wakati wa mchana hubadilisha wakati na kufanya kazi hiyo usiku.
“Tumepoteza mifugo wetu wengi sana kupitia mto huu. Ikiwa ng'ombe atateleza ndani haswa wakati wa mafuriko, haiwezekani kumtoa.Tunaangalia ng'ombe wakifa. Watoto wetu pia wako katika hatari kubwa,” alieleza kabla sijamtazama akirudi akipanda mlima unaoonekana kuwa hatari akielekea nyumbani kwake akiwa ameekeza mtungi wake wa maji kichwani.
Uvunaji wa mchanga unaathiri ubora wa maji aje? Sayansi
Hapo zamani za kale, Mto Kisian ulikuwa chanzo maarufu kwa samaki, anayefahamika sana kwa eneo hilo ni kambare almarufu kama mumi, lakini hii sio hali kwa sasa. Hakuna shughuli za uvuvi tena kwenye Mto huu; wanyama wa majini walikwenda wapi?
“Uvunaji mwingi wa mchanga kwa Mto Kisian umechafua maji na kusababisha hasara kwa mimea na wanyama wa majini waliokuwa wakinawiri ndani ya mto” aeleza Linet Andiego, Mwanasayansi wa Ubora wa Maji na aliyekuwa katika Mamlaka ya Kitaifa ya Mazingira chini ya sehemu ya Ubora wa Maji.
Wakulima kando ya ukingo wa Mto Kisian wanatumia mbolea za kemikali na dawa za kuua wadudu kwenye mimea yao. Kupitia unyunyizi na wakati wa mvua, kemikali hizi hupata njia ya kuingia mtoni kupitia mkondo wa hayo maji, na hivyo kubadilisha hali ya kawaida ya maji (pH). Kupanda au kushuka kwa pH ya mto pia una jukumu kubwa katika maisha ya wanyama na mimea ya majini, ambayo imekuwa sababu ya upotevu wa maji, anaeleza Andiego.
Kiwango cha pH pia huathiri familia wanaotumia maji haya bila kutibiwa, mifugo wanaokunywa, na mimea iliyonyunyiziwa maji yake. Kubadilisha pH ya maji ni hali nzuri kwa magonjwa ya bakteria kwa watu na mifugo. Kemikali na uchafu kwa maji inaweza pia kusababisha kukauka kwa mimea na kusababisha uhaba wa chakula.
Rangi ya maji ya Mto Kisian ni kahawia kwa sababu ya shughuli za kuchimbwa kwa mchanga kutoka mtoni ambayo husababisha uchafuzi wa matope (kipimo cha uwazi wa angalau kioevu) cha maji.
Mchanga una jukumu muhimu katika kudumisha na kusafisha maji. Wakati mchanga unavunwa, hasa kwa kiasi kikubwa kama Mto Kisian, hakuna mchanga wa kutosha kwenye mto ili maji yasafishwe yakawa safi zaidi.
Uvunaji wa mchanga husababisha kupotea kwa mimea kando ya kingo za mto, kulegeza udongo katika eneo hilo, kuifanya ikabiliwe na mmomonyoko wa udongo ambao husababisha maporomoko ya ardhi. Hii inachochea kwa kupungua kwa wingi wa maji na mwelekeo wa maji kwa mto, na kusababisha ugavi wa maji yasiotosha kwa jamii wanaoishi maeneo ya juu ya mto ambao hutegemea sana maji hayo.
Uvunaji wa udongo, zikiwa pamoja na klei na mchanga, husababisha uharibifu mkubwa wa kingo za mto na mfumo wa ikolojia na huzuia ukuaji wa bioanuwai katika eneo hilo. Hivi ndivyo tunavyopoteza aina tofauti za wanyama, samaki, na mimea ambayo hapo awali ilistawi katika ukanda wa mto huo.
Je, Jamii/viongozi wamejaribu kutatua suala hilo?
Mbunge aliyemaliza muda wake wakudumu, Olago Aluoch, alijenga daraja mwaka 2013/2014 ili kusaidia jamii kuvuka mto huo kuhudhuria shughuli zao za kila siku kwa upande mwingine na vilvile watoto wa shule huvukia daraja hiyo wafike shuleni.
Kando ya daraja, shirika la KEMRI(Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya), lilijaribu kusaidia kwa kujenga mfumo mpya wa mifereji ya maji na kuweka mitaro mipya ya maji badala ya iliyojaa mchanga kusaidia kukabiliana na ongezeko la kuporomoka kwa mto, bila mafanikio.
Chini ya Sheria ya Madini, mchanga ni mali ya serikali licha ya eneo la ardhi na umiliki wake. Hii ni kulingana na Katiba ya Kenya kwenye Ibara ya 62(3) inayowezesha serikali ya kitaifa kumiliki madini pahali popote.
Licha ya serikali kumiliki mchanga chini ya Sheria ya Madini, uvunaji wa mchanga nchini Kenya unaonekana kutawaliwa na watapele ambao kila mchimba mchanga wanaendesha shughuli hizo kama wao ndiyo wenyeji.
Katika utafiti wake wa 2021 kuhusu uvunaji wa mchanga nchini Kenya na maendeleo endelevu, Caroline Njoroge anasema kwamba ufikiaji kwa ardhi ya umma kwa urahisi (miti na mwambao wa pwani) umepunguza hali ya hatari na gharama ya chini kwa bidhaa zinazohitajika hivyo kuunda ushindani kwa maeneo yaliyo chini. Hakuna kinachotia motisha kwa wavunaji mchanga au wafanyabiashara au wanaosimamia ili wahifadhi rasilimali. Hatua zozote za kuhifadhi zinakabiliwa na hali tata ya upinzani . Kwa sasa hakuna njia sahihi yakufuatilia asili ya rasilimali za mchanga, hivyo kuacha mwanya wa uchimbaji haramu wa mchanga.
Kuna haja ya kuoanisha muundo wa utawala uliogawanyika ili kuweka msingi dhabiti ambazo zinaweza kusaidia kuokoa mito iliyoko Bonde la Nile inayopitia hatima kama hiyo.
Je, kuwahamasisha wachimbaji mchanga kujiunga na shughuli mbadala ya kujiongezea kipato ni motisha ya kusitisha uchimbaji mchanga kikamilifu?
Mtazamo wenye Matumaini
Kabla Mto Kisian kumwagilia maji Ziwa Victoria, hupitia jamii ndogo iitwayo Rota. Hapa, maji yanapokaribia Ziwa, kuna daraja kuu ambalo limesimama imara kwa miaka mingi.
Kwa wakati huu, kingo za Mto Kisian zimejengwa upya kutumia kuta za mawe na mitaro ya maji ambayo mara nyingi huisaidia kuhimili mafuriko wakati wa mvua kubwa.
Hakuna uvunaji wa mchanga unaoshuhudiwa katika sehemu hizi za Mto. Kuta za mawe zimejengwa chini yake, na daraja imesimama kwa msingi imara inayohakikisha huduma yake inaendelea kwa jamii kwa miaka mingi.
Rota ni jamii ya mfano bora kwa kuongoza katika uhifadhi na urejesho wa Mto Kisian.
James Alai, mwenye umri wa miaka 85, mmoja wa wazee wa jamii ya Kisian, anataka hatua za haraka za kurejesha Mto Kisian.
Anawataka jamii ya Kisian wachukuwe mfano kutoka kwa mikakati ya Jamii ya Rota ili nao pia wahifadhi sehemu yao ya Mto.
Baadhi ya wakazi wa Kisian pia wamewekeza kwa kupanda mianzi kwenye kingo zilizomomonyoka kwa mto. Mianzi husaidia kwa kufufua hali nzuri ya udongo. Matumizi ya mianzi husaidia kwa kudhibiti mmomonyoko wa udongo mbinu ambayo imeonekana ikifanikiwa kote duniani. Mbinu hii ya kutumia sifa za mianzi na uwezo wa kimakanika ni gharama nafuu kwa uimarishaji wa sehemu za mteremko. Mianzi ni rahisi kwa kuzaliana na ukuaji wake wakufunika udongo pia ni wa haraka. Jamii hii ina busara ya kutosha kutambua vile wanaweza punguza mabaya yaliyofanywa kwenye mto huu, upanzi wa mianzi ni njia ambayo ikitekelezwa na wote inaweza saidia kurejesha mfumo wa ikolojia na kustawisha viumbe vyenye uhai kwenye Mto Kisian.
“Mianzi hukua haraka sana na hufunika sehemu pana kwa sababu ya asili yao ya ukuaji, husaidia kulinda na kwa kufunika udongo. Pia husaidia katika kupunguza mmomonyoko wa udongo na kudumisha uwiano wa vijidudu. Halikadhalika husaidia katika usawa wa virutubisho vya udongo na kupunguza kukatika kwa maji,” anasema Andiego.
Mkazi wa Kisian, anapanda miti kadhaa ya mianzi kwenye miteremko mikali ya mto, juhudi inayolengwa kwa kudhibiti mmomonyoko wa udongo.
Safari ya Mto Kisian katika Ziwa Victoria; Mzunguko wa nyumbani
Wakati maji ya Mto Kisian yanasafiri chini ya milima na miamba viungani vya Kisumu, yanajitokeza tena, baada ya kuhimili shughuli za uharibifu wa mazingira zinazoelekezwa ndani yake.
Kwa mkondo wake wa mwisho kuelekea Ziwa Victoria, Mto Kisian unashika kasi tena kama mtoto anayekimbia kwa mama yake, huku akililia msaada. Umeimarika kwa kina na nguvu. Eneo linalolizunguka ni kijani. Shughuli za uvuvi zipo tena. Kando za mto zina afya na pembeni mwa mto zimejazwa maisha; jambo nzuri la kutia moyo, na viumbe vyenye uhai ndio msingi wake.
“Ndiyo, hapa ni kina sana; kama unavyoona, hata tunavua samaki kwa kutumia mashua za mwendo wa kasi; ukizama hapa, hatutakupata kamwe. Inaweza kumeza mtu mzima,” mvuvi kutoka jamii ya Rota anasimulia kwa uchangamfu, huku yeye na wavuvi wengine wakipita kwa kasi baada ya usiku kucha wenye mafanikio wa kuvua samaki.
Ni mtazamo wa kuvutia Mto Kisian hatimaye unapojiunga na Ziwa Victoria, huku kukiwa na pumzi ya raha hewani si kwa jamii pekee wanaoutegemea na watoto ambao wanaishi kuvuka kila siku, lakini pia kwa Mto wenyewe ambao umetoka mbali katika safari iliyojaa changamoto ya mapambano, maumivu, kupuuzwa, furaha, na maisha.
Hatimaye, Mto Kisian umefika nyumbani na kuunganishwa na Ziwa Victoria kwa kumbatio la daima. Mto Kisian unalilia usaidizi wa dharura. Dhidi ya shughuli za kibinadamu. Dhidi ya viongozi fisadi Mto Kisian unaungana na mito mingi katika Bonde la Nile, kulilia urejesho.
Hadithi hii ilitolewa Juni 2022, ilidhaminiwa na InfoNile na Media in Cooperation na Transition (MiCT) kwa ushirikiana na Nile Basin Initiative (NBI) na kwa msaada kutoka kwa Gesellschaft fur Internationale Zusammenarbeit (GIZ) GmbH, iliyoagizwa na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani.