Kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika, Wizara ya Maji na Mazingira ya Uganda iliwekeza kiasi cha shilingi za Uganda 27 bilioni (Dola 70,000 za kimarekani) kuokoa mradi huu ambao ulianzishwa kwa nguvu za wananchi ili uweze kuhudumia ekari 1,670 kutoka ekari 160 zilizokuwa zinahudumiwa hapo awali. Ukarabati ulikuwa unalenga kuwasaidia zaidi ya wakulima 10,000 wapate maji.
“Tulirudi hatua mbili nyuma” anasema Bwana Ingala, mkulima na pia ni katibu wa uzalishaji kwenye kaunti ndogo ya Agoro. “Tulisikitishwa sana na kazi iliyofanyika kwa sababu mifereji kwenye mradi huu ilikuwa na kina kirefu sana hivyo kusababisha maji yote kuishia kwenye mfereji badala ya kutiririka kwenye bustani zetu” anaongea bwana Ingala
Hali hii imesababisha uhaba wa chakula unaotokana na uzalishaji mdogo wa mazao kwenye kaya nyingi huko Agoro, jumuiya ambayo ilionekana kama kapu la chakula kwa maeneo ya kaskazini, huku nchi jirani ya Sudan Kusini ikifaidika kwa chakula pia.
Mnamo mwezi Agosti mwaka jana, serikali iliamua kuipa kandarasi kampuni nyingine ijulikanayo kama la Gets Technical Services Limited ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza kwenye mradi huo kufuatia manung’uniko kutoka kwa wakulima na viongozi wa eneo hilo.
Awamu ya pili ya ukarabati uliotazamiwa kukamilika mwezi wa machi mwaka huu bado haujakamilika, ucheleweshaji unao wapa wasiwasi wakulima ambao tayari wamekwisha athirika na hali mbaya ya hali ya hewa.
Wakulima wengi wameamua kuhamishia mashamba yao kwenye vilima vya Langiya huku baadhi yao wakiacha mpunga kwenye nyanda za chini mpunga ambao ulikuwa ndio tegemeo kuu kwenye ukanda huu na kujikita kwenye mazao yanayo komaa haraka kama vile mahindi, maharagwe, biringanya na kabichi mazao ambayo yanahitaji kiasi kidogo cha maji.
Hata hivyo mchele una bei nzuri kwenye masoko ya kaskazini ya Uganda ikilimganishwa na mahindi na maharagwe. Mchele unauzwa dola 1.5 ya marekani ilikilinga nishwa na mahindi na maharagwe yanaouzwa doa a marekani 0.5 kwa kilo. Kwa mujibu wa msimamizi wa umwagiliaji wa Agoro bwana Thomas Opoka, serikali inataka kukipa kipa umbele kilimo cha mpunga kwa ajili matumizi ya ndani na kuuza nje ya nchi.
Mabadiliko ya tabia nchi, yabadili ukulima wa umwagiliaji bondeni mwa Mto Nile
Wakati athari za mabadiliko ya tabia nchi zikionekana duniani kote, changamoto ya kulima mazao ya chakula kwa wakulima wadogo wadogo ambao wanategemea sana mvua, hususan kwenye nchi zinazoendelea kama Uganda zinazidi kuwa kubwa kutokana na mavuno yasiyo ya uhakika. Kubadilika kwa mifumo ya mvua na hali ya joto kali ikichangiwa na shughuli za kibinamu kama vile uchafuzi wa mazingira na ukataji miti kunawafanya wakulima kugeukia vijito vilivyo karibu kumwagilia mimea yao.
NchiniUganda, utafiti uliofanywa na mpango kabambe wa kitaifa wa umwagiliaji uliofanywa mwaka 2011 na taarifa yake kutolewa na Shirika la Bonde la Mto Nile ulikadiria kuwa hekta za ardhi itakayotumika kwa umwagiliaji zingeongezeka kwa kwa hekta 33,750 ifikapo mwaka 2036. Taifa hili la Afrika mashariki linamiliki hekta 515,000 za ardhi inayoweza kumwagiliwa inayojumuisha hekta 243,500 zilizopo kwenye maeneo oevu na hekta 272,000 zilizopo kwenye miinuko. Kutokana na hekta 9,120 zilizokuwa zikimwagiliwa mnamo mwaka 1989, hesabu iliyofanywa na mpango wa bonde la mto Nile (NBI) inaonyesha kuna ongezeko la hekta 14,717 kufikia mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 37 kwa mwaka.
Hata hivyo idadi ya watu inazidi kuongezeka kwenye bonde hili na wakulima wanalazimika kupanua mashamba yao ili kukidhi mahitaji ikiwamo nishati.
Mahitaji ya jumla ya maji yanayotumika kwa umwagiliaji ni takriban mita za ujazo bilioni 85 na uwezo wa wa mto ni kutoa mita za ujazo 82.2. Hali hii inaonyesha kuna kila sababu ya nchi zinazolizunguka bonde hili kushirikiana kutatua tatizo. La sivyo, kutakuwa na mahitaji makubwa ya maji kuliko yaliyopo.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Nile Basin Initiative, juu ya thamani ya kiuchumi ya maji unaonyesha kwamba nchi zinapaswa kujikita kutafiti mahitaji ya maji kwa kila zao, thamani ya ardhi na nguvu kazi na mavuno kwa kila zao ili kubaini ni zao gani linapaswa kuzalishwa na nchi ipi ili kupata ufanisi katika kutumia rasilimali maji hii.
Kwenye utafiti huo NBI ilipendekeza kwamba Uganda, Misri na Ethiopia walime mazao ya mizizi kama vile viazi vitamu na mihogo ili wasambaze kwenye maeneo mengine ya bonde la Mto Nile kwa kuwa maji wanayotumia thamani yake ni ndogo.
Mabadiliko ya hali ya hewa yamefanya hali kuwa ngumu zaidi. Kwa mfano, Uganda inashikilia nafasi ya 10 duniani katika nchi zilizo athirika na mabadiliko ya hali ya hewa na ni ya 35 dunia nzima katika utayari wa kukablliana na athari zake. Licha ya Uganda kujaliwa kuwa na eneo kubwa lenye uwezo mkubwa kwa umwagiliaji (asilimia 15 ya ardhi yote ya maziwa makuu) vyanzo hivi vya maji havijatumiwa kikamilifu na wakulima na bado wanatatizika katika kupata maji kwa ajili ya mashamba yao.
Ili kutatua tatizo hili mnamo mwaka 2017, Uganda ilibuni sera ya taifa ya umwagiliaji lengo lake kuu likiwa ni kufikia lengo la kumwagilia ekari za ziada 1,500,000 ikiwa ni asilimia 50 ya eneo lote lenye uwezo wa kumwagiliwa hadi kufikia mwaka 2040. Mpango huu unalenga kuhakikisha uwepo wa maji ya uhakika kwa ajili ya umwagiliaji na kuboresha uzalishaji wa mazao na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi.
“Tunahitaji kuchukua hatua haraka ili kuhakikisha kuwa miradi ya umwagiliaji inamalizika haraka kwa sababu mabadiliko ya hali ya hewa yana waathiri wakulima wengi ambao wanategemea mvua” anasema bwana Lamwo Kamishna Mkazi mstaafu wa wilaya ambae alikuwa ni mmoja katika kundi lilosimamia mradi wa umwagiliaji wa Agoro.
Ili kuhakikisha kunakuwa na usambazaji bora wa maji, awamu ya pili ya ukarabati wa mradi wa Agoro utabadilika kutoka mfumo wa kusambaza maji kwa mifereji na kutumia mabomba ya plastiki yajulikanayo kitaalamu kama Glass Fiber Reiforcement Plastic yenye vichwa vya kunyunyiza ili kudhibiti mtiririko wa maji. Mbinu hii ina faida zake kwa mujibu wa bwana Thomas Opoka msimamizi wa skimu ya umwagiliaji ya Agoro ambaye anasema itawasaidia wakulima kuongeza maji na kudhibiti upotevu na pia kuhakikisha kutokuingiliana kwenye mashamba wakati wa umwagiliaji.
Asilimia 24 tu ya kazi ndiyo iliyofanyika
Kwa sasa ni asilimia 24 tu ya kazi yote imefanyika kwenye skimu ya maji ya Agoro, kwa mujibu wa Bwana Opoka huku akibainisha kuwa hali hii inawasikitisha sana wakulima na viongozi wa wilaya ya Lamwo. Baadhi yao wana mkataba wa ujenzi huo kusitishwa iwapo mradi huo hautakamilika kwa haraka . Hata hivyo Meneja wa uzalishaji wa maji kwenye wizara ya mazingira bwana Eric Ocan ameomba mkandarasi apewe muda zaidi kwani vifaa vinavyotumika kwenye mradi huu nyeti vinahitaji kufanyiwa kazi kwa uangalifu.
“Ukarabati upo kwenye hatua mbalimbali na kazi inaendelea vizuri na tuna matumaini makubwa na kazi inayoendelea. Tatizo ni kwamba mfumo huu wa umwagiliaji ni wa kipekee na nyenzo zinazotumiwa hapa ni nyepesi na ni rahisi kuharibika iwapo uangalifu hautakuwepo hivyo ni hatari kufanya kazi kwa haraka.” Anaendelea kusema bwana Ocan.
Lakini wakati wakulima wakisubiri mpango huo kufunguliwa rasmi, baadhi ya wakulima wanaendelea na shughuli za kilimo kwenye kingo za mito licha ya kazi zinaendela kwenye skimu hiyo. Wakulima wamerejea kwenye njia zisizo rasmi za umwagiliaji ambazo walitumia awali zinazohusisha kufunga mkondo mkuu wa maji kwa kutumia magunia ya mchanga ili kuyaelekeza maji kwenye mashamba yao kupitia kwenye mifereji ambayo wamechimba. Shughuli hii inawagharimu sana wakulima kwani kuna wakati malori makubwa yaliyopo kwenye mradi hukanyaga mazao ya wakulima hawa.
Wakulima hawa pia hutumia viutilifu na mbolea kwenye udongo ili kukuza mimea yao, lakini wataalamu wa mazingira wana wasiwasi kwamba kemikali zilizopo kwenye viutilifu na mbolea hizo zinaweza kufua mto wakati huu ambao tiba ya uchafuzi huo hakuna.
Bwana Decimon Anywar, mwanasayansi wa mazingira anasema mbolea inayoambatana na madini ya phosphorus ambayo ni muhimu katika ukuaji wa mmea na nitrogen ambayo pia ni muhimu kwenye ukuaji na uzalishaji kwenye mmea yakiingia kwenye mto wakati ikinyesha inaweza kupelekea kuota kwa mwani. Mwani huu ukifa juu ya maji virutubisho vilivyopo kwenye mbolea vinasababisha kuwepo kwa bakteria ambao wanasababisha mwani kuoza kwa njia ya chemikali na mchakato wa kibailojia na matokeo yake sumu inazalishwa, sumu ambayo baadae inaingiza sumu kwenye maji ya kunywa yanayo sababisha magonjwa kwa wanyama na mimea.
“Mwani uliokufa unazuia mwanga na hewa ya oksijen kuingia kwenye maji vitiu ambavyo ni muhimu kwa mimea inayopatikana ndani ya maji” anasema bwana Anywar. “Na jambo lingine ni kwamba mwani huu ukifa bakteria wanajaribu kuziharibu chembechembe za mwani ili kupata hewa ya oksijen kitendo ambacho kinaleta ushindani wa kupata hewa hiyo kati ya bakteria hao na viumbe waishio kwenye maji” anaongeza bwana Anywar.
Wizara ya Maji na Mazingira inasema mradi ukikamilika mradi wa kusafisha maji utakuwa ni sehemu ya mradi huu.
Kwa sasa wanamazingira kama Bwana Anywar wanawashauri wakazi kutumia njia za gharama nafuu kama vile kulima mazao yao mita 50 kutoka kwenye kingo za mto ili kuepusha kemikali kuingia kwenye mto kirahisi na pia kutumia mbolea za asili kama vile pilipili nyekundu, majivu badala ya viutilifu vya kisasa .
Bwana Anywar anasema hatua nyingine ya dharura itakuwa ni kupanda miti kwenye kingo za mito ili kudhibiti maji yanayomwagika nje mito.
Miti yahitajika kuimarisha mabadiliko ya hali ya hewa
Mtafiti wa hali ya hewa anayeishi kaskazini mwa Uganda bwana Michael Tebere anasema upandaji miti usiishie kwenye kingo za mto tu bali zoezi hilo liendelee hadi kwenye makazi ya watu kwani itasaidia kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi na kuyaboresha pia.
Hata hivyo ukataji miti bado unabaki kuwa tatizo nchini Uganda, hususan eneo la kaskazini, ambalo ndilo kitovu kikubwa cha biashara ya kuzalisha makaa ambayo yanasafirishwa hadi nchi jirani kama vile Sudani Kusini na Kenya. Kwa kipindi cha miaka 25 Uganda imekuwa ikipoteza ekari 301,500 za misitu kila mwaka kutokana na ukataji miti mikubwa kwa ajili ya mbao na makaa.
Ukataji miti kwa kiwango kikubwa huvuruga mifumo ya mvua, wakati wakulima bado wakitegemea mvua kwa ajili ya mazao yao. Kwenye bonde la mto Nile uhaba wa maji unaanza kuwa changamoto ya kutisha kutokana na ongezeko la watu na mabadiliko ya tabia nchi. Hata hivyo, utafiti uliofanywa na taasisi ya bonde la mto Nile (Nile Basin Initiative) unapendekeza kwamba uvunaji wa maji ya mvua ambao utatumia teknolojia nafuu katika uvunaji na uhifadhi kwa matumizi ya siku ambazo maji yatakuwa haba. Mbinu zingine zilizoainishwa ni pamoja na kutumia maji yaliyopo chini ta ardhi na juu ya ardhi , kuchakata na kutumia upya maji yaliyotumika, kufanya umwagiliaji utakaokidhi mahitaji wakati wa uhaba wa maji, kuimarisha kilimo cha kutegemea mvua, kuboresha ufanisi wa matumizi ya maji, mifumo ya upandaji miti.
Kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji, wakazi wa Agoro wamejikita kwenye ulimaji wa mazao yanayohimli ukame kama vile mahindi, kabichi, na karanga mazao ambayo yanakomaa kwa muda mfupi na yanahimili ukame na hayahitaji maji mengi kwenye ukuaji wake.
“Tunalima mazao haya kwa sababu tunavuna mapema na yanatusaidia kujikimu” anasema Apoko Evelyn mama mwenye watoto watatu. Anaongeza kwa kusema “Hiyo ndo njia pekee itakayotuwezesha kupata chakula kuuza cha ziada na kuwapeleka watoto wetu shuleni”.
Baadhi ya wakulima wameanza kukata miti iliyopo kwenye kingo za mto kwa ajili ya uchomaji makaa na kusababisha kina cha maji kupungua kwa kuwa miti hii ni vizuizi vya maji kumwagika nje ya mto na pia kinasababisha taka na mchanga kuingia kwenye kina cha mto.
Bwana Apoko ambaye ni msimamizi wa skimu ya maji ya Agoro anasema, “Nilipokuwa kijana mdogo kulikuwa na misitu mingi hapa ambayo ilikuwa mikubwa na haipitiki. Lakini sasa misitu yote imekatwa na mvua inapungua na wakati wote kuna joto utadhani tupo jangwani”.
Bwana Opoka anasema kina cha maji kinazidi kupungua wakati wa kiangazi na kufanya kazi ya kuyafikia maji yaliyopo kwa wakulima kuwa ngumu. Tangi la akiba lililopo kwenye mradi lina uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 214,000 za maji yanayotumika wakati wa uhaba wa maji. Kwa sasa inachukua muda mrefu kulijaza tangi hili ikilinganishwa hapo zamani.
Kwa sasa mkandarasi anafanya kazi saa ishirini na nne ili akamilishe mradi huu. Inabidi wakulima wawe na subira kidogo kabla hawajaanza kufaidi matunda ya mradi huu. Wakati huo huo, Wizara ya Maji na Mazingira ya Uganda inawataka wakulima kuwa watulivu, ikibainisha ya kwamba ni vigumu kutoa ahadi ya ni lini mradi huu utakamilika.
Hata hivyo wakulima kama bibi Joyce Ayaa mwenye umri wa miaka 62 hawana furaha kwani mafuriko yanaathiri bustani yake wakati mvua inaponyesha. Hata hivyo, mkulima huyu analima kilimo cha kisasa kwa kuhuwisha upandaji wa mazao, mbinu ambayo inasaidia ardhi kuwa na rutuba ya kutosha. Mkulima huyu analima mazao kama soya na miti ambayo husaidia kuzuia upotevu wa maji.
“ Mambo ni magumu hapa na kilimo ndio tegemeo letu na wasiwasi wangu ni kwamba iwapo mafuriko yataharibu bustani yangu na je! Tutasubiri mpaka lini? Anasema Bibi Joyce Ayaa.
Hadithi hii ilitolewa Juni 2022, ilidhaminiwa InfoNile na Media in Cooperation and Transition (MiCT) kwa ushirikiano na Nile Basin Initiative (NBI) na kwa usaidizi kutoka Deutche Gesellschaft fur Internationale Zusammenarbeit (GIZ) GmbH, iliyoagizwa na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani.