Sharon Atieno na Mary Mwendwa
Ni alasiri katika Kaunti ya Siaya nchini Kenya. Jua limewaka na hali ya anga ni unyevu. Pamoja na hayo, kuna shughuli nyingi zinazofanyika kando ya ufukwe wa Usenge katika Kaunti ndogo ya Bondo.
Mashua chache zimeegeshwa ufukweni huku baadhi ya abiria wakipanga mizigo yao kuabiri mashua na kuvuka hadi visiwa vya upande mwingine wa ufuo vikijumuisha baadhi ya visiwa vya nchi jirani ya Uganda.
Mazulia makubwa ya Rastrineobola argentea, kwa kawaida hujulikana kama Omena wameanikwa vizuri karibu na ufuo huku wanawake wakishughulika kuwatandaza kutumia fagio kavu ili wakauke tayari kwa soko. Ni moja kati ya aina nyingi za samaki katika eneo hili.
Mbele ya ufukwe ni Kitengo cha Usimamizi wa Ufuo wa Usenge ambacho kinapakana na Ofisi ya Uvuvi upande wa kulia. Karibu na hizo ofisi kuna vipozaji vikubwa ambavyo madalali wanapima uzito wa samaki aina ya sangara wakubwa wa Nile na ngege (tilapia) tayari kwa masoko kama Nairobi na mengineyo huku vijana wa kiume wakiwakata samaki aina ya Sangara wa Nile (Nile perch) kwa minajili ya vibofu ambavyo hutumika kama nyuzi za kushona kwenye vyumba vya upasuaji.
Ufuo wa Usenge ni miongoni mwa fuo 21 chini ya wodi za Yimbo Magharibi na Mashariki zinazosimamiwa na Maurice Oyola, Msimamizi wa uvuvi katika wodi hizo mbili.
Kulingana na yeye, matumizi ya wavu wenye uzi moja umeenea kote. Kwa mwezi moja wanaweza kutaifisha hadi nyavu 2,000 haramu. Oyola anaamini kwamba wavuvi wanapenda nyavu hizo kwa sababu ni nafuu zikilinganishwa na nyavu zinazohitajika. Hii ni licha ya nyavu kuingia nchini kupitia mipaka ya vinyweleo kwani hazitengenezwi humu nchini.
“Huu wavu ni hatari sana, kwani umetengenezwa kwa sandarusi, hauozi na pia huvua samaki wachanga sana. Sio endelevu wala urafiki wa mazingira,” anafichua, na kuongeza kuwa nyavu hizi hata zinaporaruka kutoka kwa wavu kuu huendelea na uvuvi ghusi miaka kadhaa baadaye.
Kuhusu mbinu za uvuvi haramu, Oyola asema kwa mwezi, wanaweza kukamata wastani wa wavuvi watano katika tendo hilo. Anaeleza kuwa idadi hii inaeza kuwa juu, lakini mara nyingi wavuvi wakiwaona, wanachana mbuga huku wakiacha zana zao za uvuvi nyuma.
Zana za uvuvi mara nyingi huchukuliwa na kuharibiwa kupitia amri ya mahakama huku wavuvi hao wakikamatwa na kutozwa faini baada ya kufikishwa mahakamani.
Joseph Omondi, Katibu Mkuu wa Ufuo wa Usenge alidhibitisha kuwa nyavu haramu za uvuvi ni kama vile zenye uzi moja na nyavu zenye matundu madogo ni suala kuu miongoni mwa wavuvi katika ufuo huo. Alidokeza kwamba licha ya wavuvi kushtakiwa na nyavu kutaifishwa, bado wao huzinunua tena.
Wavu wenye uzi moja, anasema unaweza gharimu shilingi 1300 (takriban dola za marekani 13) kipande kimoja lakini bado mvuvi anahitaji angalau vipande 10 huku wavu uliyopendekezwa unagharimu karibu shilingi 4,000 (kama USD 40) kwa rundo lakini mvuvi anahitaji mashada saba kwa mfano, katika uvuvi wa omena.
Mbali na kuwa nafuu, Omondi aongeza: “Nyavu za uzi moja hushika samaki wengi weneye ukubwa tofauti mara moja. Wakati uko ndani ya maji, samaki hawawezi kuuona kwa urahisi na hujinasa kwenye wavu.”
Anadokeza ya kuwa matumizi ya sumu kwa samaki ilikuwa jambo la kawaida miaka michache iliyopita. Mbinu hii ilitumika na wavuvi walaghai waliotaka pesa za haraka. Mara tu sumu ingemwagwa kwenye ziwa ingenyima samaki oksijeni kwa maji na matokeo yake, samaki wangekufa na kisha kuelea juu ya maji. Lakini kesi kama hizo hazipo tena, Omondi anasema.
Kilomita chache kutoka ufuo wa Usenge ni kisiwa cha Mageta, Kusafari kwa mashua hadi kisiwa hicho ni takriban dakika 45. Kisiwa hicho kina fukwe zipatazo saba. Tulitembelea ufukwe wa Maganga, ambayo uko karibu na mpaka wa Uganda. Hapa, wavuvi hufanya kazi katika maji ya Kenya na Uganda.
Jairus Iganga, mwenyekiti wa Maganga BMU, anasimamia wavuvi wasiopungua 600. Hapa sheria za uvuvi hutofautiana kidogo na za Uganda na wanapaswa kuzingatia sheria za pande zote mbili. Anailaumu serikali kwa kutowasaidia kutatua migogoro ya mipaka uvuvi unaohusiana Mamlaka ya Uganda.
“Ufukwe huu uko karibu na maji ya Uganda. Uganda ina kanuni kali na zisizo za haki jambo ambalo huwafanya wavuvi wetu kukamatwa mara kwa mara,” anasema.
“Kwa mfano, sajili maalum ya mashua ambayo ni kama leseni ya Mkenya aliye Uganda inaweza kugharimu shilingi milioni 2 (kama USD 20,000) huku raia wa Uganda atalipa shilingi 30,000 (kama USD 300). Tunashirikiana kwa maji haya kwa sababu tunapakana kwa karibu. Jambo jingine ni matumizi ya taa zinazotumia miale ya jua kuvua dagaa ambao wamekubalika Kenya lakini sio Uganda.”
Huu ni mkanganyiko ukizingatia kuwa serikali ya Kenya inasema taa za nanga (zinapendekezwa nchini Uganda) ambazo huvuja mafuta kwa maji ambayo husababisha vifo vya samaki huku serikali ya Uganda ikisema mwanga wa taa za sola huakisi ndani kabisa ya maji hivyo kuathiri hata samaki wanaozaliana.
Licha ya haya, Iganga adokeza kuwa kwa kila siku hawawezi kukosa kesi inayohusu mbinu za uvuvi haramu. Hata hivyo, wavuvi wanafanya shughuli hizi haramu kwa kujificha hivyo basi sio rahisi sana kuwakamata.
Kulingana na Ripoti ya Uchunguzi wa Tathmini ya Catch 2018 kwa Ziwa Victoria matumizi ya zana haramu za uvuvi bado yamekithiri katika Ziwa Victoria (nyavu ndefu za ufukwe, mashua ya nyavu, nyavu zenye matundu madogo na nyavu zenye uzi moja).
Ripoti ya Kituo cha Utafiti wa Viumbe Majini na Uvuvi (KMFRI) inadokeza kwamba, zana zinaendelea kuundwa upya ili kuongeza ufanisi wao (kuongezeka kwa paneli za wima / ndogo za nyavu, matumizi ya laini ndefu ya ndoano ndogo chini ya 10, na kuongeza nyavu za wima/nyavu ndogo kwa paneli, kuongeza kwa idadi ya saizi ya ndoano ndefu, na kupunguza nyavu zenye saizi ya matundu mandogo. Matumizi ya nyavu zenye matundu madogo zimeenea sana hasa ndani ya Ghuba ya Nyanza (wastani wa ndoano wakati wa utafiti huu ilikuwa 11).
Hata hivyo, hili si tatizo la Wakenya pekee lakini changamoto inavuka mipaka na kuathiri ukanda wote wa Afrika Mashariki.
Mnamo 2022, gazeti la kila siku la nchini Uganda liliripoti kuhukumiwa kwa wavuvi 40 wa Kenya, Wanyarwanda 12 na Waganda sita waliopatikana kinyume cha sheria ikiwa ni pamoja na kutumia nyavu zilizopigwa marufuku kama vile vyandaia vya mbu upande wa Uganda wa Ziwa Victoria.
Kulingana na Mpango wa III wa Usimamizi wa Uvuvi wa Ziwa Victoria (2016-2020) kwa mujibu wa Sekretarieti la Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria (LVFO), changamoto kubwa sana ya uvuvi kwenye ziwa hili ni; uvuvi uharamu, usioripotiwa, na usiodhibitiwa ukishirikshwa na matumizi ya zana haramu.
Utafiti wa Regional frame survey (2014) ulionyesha kuwa kati ya 2012 na 2014 karibu zana haramu zote ziliongezeka: ufuo/mashua ya nyavu ziliongezeka kwa 30.3%; nyavu za uzi moja na 28.5%; tupa nyavu kwa 6.5%, na mitego/vikapu kwa 16.4%. Zana hizi huathiri hasa samaki wachanga kwa sababu uvuvi huu hufanywa maeneo ya kuzaliana/vitalu.
Ripoti ya KMFRI 2018 inatahadharisha kwamba kuenea kwa matumizi ya zana haramu kwa ziwa zinazidi kuhatarisha kwa kufilisisha uvuvi, na upungufu mkubwa wa samaki na hivyo, ukisubiri kupotea kwa mapato ya wanaotegemea samaki kwa Jamii za Bonde la Ziwa Victoria.
Kulingana na Dk. Kevin Obiero, Mwanasayansi wa Utafiti na Mkurugenzi wa Kituo, KMFRI cha Sangoro, uvuvi haramu unahusisha kutumia zana za uvuvi zilizopigwa marufuku na serikali na mbinu ambazo matokeo yake ni uvuvi usio endelevu.
Anasema: “Zana haramu za uvuvi huathiri uvuvi wa ziwa katika ngazi mbili; kupitia uvuvi zisizo endelevu na uharibifu wa rasilimali.”
“Kwa mfano, nyavu ndefu za ufukwe huwanasa samaki wakubwa na wachanga. Wakubwa hupunguzwa kutoka kwa mkusanyiko wa samaki na kuzuia kuingizwa wapya katika uvuvi huku wadogo wakiwa hawawezi kukomaa. Samaki wakubwa pia hukamatwa wanapokuja ufukweni kuzaliana.”
Zaidi ya hayo, Dk. Obiero adokeza, zana zisizofaa pia huathiri makazi muhimu ambamo kuzaliana hutokea. Ngege haswa, huathiriwa zaidi wanapotengeneza kiota chao chini, na nyavu zikivutwa zinasumbua maeneo yao ya kuzaliana. Anatahadharisha kuwa kuna haja ya kudhibiti zana hizi ili kuhifadhi mfumo wa ikolojia.
Dk. Mark Olokotum, Afisa Utafiti- Baolojia ya Samaki & Mwanasayansi wa Tathmini ya Hisa, Taasisi ya Kitaifa kwa Utafiti wa Rasilimali za Uvuvi (NaFIRRI) asema zana haramu zinavua samaki wadogo ambao hawajazalisha kwa kiwango kinachohitajika.
Olokotum adokeza kwamba wavuvi wanaotumia zana haramu na hizo mbinu mara nyingi hulenga maeneo ya ufukweni yenye vina vifupi ambavyo vimependwa na samaki kama maeneo ya kuzaliana na kitalu. Hivyo huharibu maeneo au hukamata samaki wanaozalisha.
Kwa dagaa, zana haramu ni nyavu ndogo chini ya 8mm, na paneli nyingi sana zinazotumika ni paneli zaidi ya nane. Hizi huvua samaki wachanga hasa wadogo wa samaki wengine sanasana sangara wa Nile na ngege, anasema.
Anaongeza kuwa kwa sangara wa Nile, zana haramu pia huathiri ukubwa, wingi na ubora wa kibofu cha kuogelea.
Juhudi za serikali
James Otuo, 36, mmiliki wa boti na mvuvi katika kisiwa cha Maganga ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka kumi anakubali kwamba juhudi za serikali nchini Kenya zimepunguza kesi za zana haramu.
“Shughuli za pamoja zikiongozwa na ofisi ya uvuvi na za BMU zimepunguza viwango vya zana haramu za uvuvi. Iwapo kunazo kesi hizi, zipo kwa ni chache” anasema.
Hisia kama hizo zinashirikishwa na wavuvi tuliwahoji akiwemo Pascal Otieno, 36, ambaye anaonelea kwamba hapo awali matumizi ya zana haramu zingeathiri kukamatwa kwa samaki lakini sasa kesi zimepungua na wanavuna kutokana na utekelezaji wa kanuni za uvuvi.
Dk.Obiero anadokeza kwamba ingawa BMU wamepewa jukumu la kusaidia na kutekeleza kanuni za uvuvi na wamefanya juhudi fulani kudhibiti uvunjaji sheria, wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fedha za kutosha na vifaa vya kusimamia majukumu yao kwa ufanisi. Hii inazuia udhibiti kamili ya uvuvi haramu katika maeneo yao ya mamlaka.
Hadithi hii ilizalishwa kwa ushirikiano wa InfoNile kwa ufadhili wa JRS Biodiversity Foundation.