Ipatikane suluhu ya kudumu uchafuzi wa mazingira Mto Mara

Ipatikane suluhu ya kudumu uchafuzi wa mazingira Mto Mara

Na Mugini Jacob,  Marycelina Masha  

Jua linaanza kuzama katika Kijiji cha Marasibora, wilayani Tarime mkoani Mara, baadhi ya wachungaji wanaonekana wakiswaga ng’ombe kuelekea nyumbani tayari kwa wanawake na watoto kuanza shughuli ya kukamua maziwa. 

Hata hivyo, hali ni tofauti nyumbani kwa Hosea Bwire. Yeye na majirani zake watatu wameungana kwa namna tofauti kwa kwenda mbali na nyumbani kwao kutafuta malisho na maji katika meneo yenye ustawi na hivyo kujikuta wakikaa huko siku kadhaa, wakati mwingine miezi kulingana na majira ya mwaka. 

“Wakati wa kiangazi malisho huwa adimu, kwa hiyo huwa tunapeleka mifugo karibu na mto na tunaiacha huko mpaka msimu wa mvua utakapoanza,” anasema Bwire mwenye ng’ombe 50. 

Cows Mara River 1 1
Wafugaji wanachunga mifugo yao katika maeneo oevu ya Mto Mara

Wakati malishoni hujenga makazi ya muda kwa kutumia miti na nyasi ili kujikinga na jua na pia moto huwaka muda wote nje ya nyumba ili kujilinda na wanyama wakali. 

Hata hivyo, Bwire na wenzake hawafahamu kuwa kitendo wanachofanya kinaweza kuwa kimechangia uharibifu wa mazingira na uchafuzi katika Mto Mara ambapo hivi karibuni ilishuhudiwa maji yake yakichafuka, samaki wakifa na maji kutoa harufu mbaya iliyosababisha sintofahamu mapema mwaka huu. 

Katika tukio hilo lililotokea Machi mwaka huu, iligundulika kuwa maji machafu na harufu mbaya ilitokana na mrundikano wa kinyesi cha wanyama hasa ng’ombe ambao wamekuwa wakichungwa pembeni mwa mto huo. 

Wanakijiji waeleza hali halisi

Maji katika Mto Mara yanatiririka kutoka msitu wa Mau uliopo nchini Kenya ukipita katika hifadhi ya Wanyama ya Masai Mara na Mbuga ya wanyama ya Serengeti na kumimina maji yake katika Ziwa Victoria nchini Tanzania. 

Final Mara River Map Graphic 1

Mbali na kuwa muhimili muhimu katika kuhifadhi wanyamapori kati ya Serengeti na Mara, mto huu ni tegemeo la wakazi wapatao milioni 1.1 katika nchi zote mbili za Kenya na Tanzania. 

Mto Mara unaochukua eneo la takribani kilomita za mraba 13,504, ikiwa asilimia 65 ipo nchini Kenya na asilimia 35 nchini Tanzania. 

Machi mwaka huu, vyombo vya habari vilipambwa na habari kuhusu uchafuzi wa mazingira katika Mto Mara ambao ulibadili rangi ya maji ya mto huo kuwa meusi, kupatikana kwa samaki waliokufa na harufu mbaya ambayo ilisika katika baadhi ya vijiji vinavyopakana na mto huo. 

Baadhi ya vijiji vilivyokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na   Marasibora ,Kirumi, Kwibuse na Ryamisanga, vyote vya  wilaya za Rorya na Butiama, mkoani Mara. 

“Wanawake wameacha kwenda kuchota maji mtoni. Sasa hivi tunachimba visima vifupi pia tumeacha kununua samaki,” anasema Nyamwicho Wambura (58) mkazi wa kijiji cha Marasibora. “Samaki ndio chakula cha uhakika kwetu lakini baada ya uchafuzi wa mazingira imekuwa adimu kuwakuta sokoni. 

Ni vigumu kuwashawishi watu kuwa maji ni salama baada ya hiki tulichokishuhudia hivi karibuni. Kila mtu anajali afya yake.” anaongeza  huku akisisitiza mamlaka zichukue hatua ili kulikabili tatizo hilo. 

Yohana Osunga, anayejishughulisha na ufugaji amesema suluhu ya kukabiliana na changamoto iliyojitokeza ni kujengwa kwa bwawa kwa kuwa sasa ni vigumu tena kwa wananchi kuyaamini maji ya Mto Mara. 

IMG 20220526 161000 603 1
Yusufu Akuti mfugaji katika kijiji cha Marasibora Mkoani Mara akionyesha sehemu ya kinamasi kilichochafuliwa katika maeneo oevu ya Mara.

“Maji bado ni meusi na yananuka. Tunahofu kuhusu afya zetu na mifugo. Ni vigumu kutushawishi tofauti kutokana na kile tulichokishuhudia. Hiyo itakuwa ni sawa na kutuambia maisha yetu yamefikia tamati, anasema Osunga. 

Uchafuzi ulichangiwa na kinyesi cha ng’ombe, mikojo, takataka na magugu vamizi


Baada ya kupata taarifa kutoka katika vyombo vya habari, serikali ilitoa uamuzi wa kuwazuia wananchi kutumia maji ya Mto Mara na kusimamisha shughuli zote za binadamu ikiwamo uvuvi wa samaki. Mamlaka ya maji ya mkoa huo iliagizwa kutafuta njia mbadala za kuwapatia maji wakazi wa vijiji hivyo kwaajili ya matumizi ya nyumbani.  

Zuio hilo la muda mfupi liliwekwa baada ya tume ya wataalamu 11 iliyoundwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mazingira, Selemani Jafo. 

Ripoti hiyo iliyoandaliwa chini ya uenyekiti wa Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Samweli Manyele iliyobatizwa jina la Report on the Investigation of Mara River Pollution, ilichapishwa Machi 22, mwaka huu ikiwahakikishia wananchi kuwa Maji ya Mto Mara ni salama kwa matumizi lakini ikitoa angalizo kuwa ni lazima yatibiwe kwanza. 

Uharibifu ulidumu kwa muda mfupi baada ya mvua kuusafisha mto huo, hata hivyo ripoti ilisema harufu mbaya na rangi ya maji ingeendelea kubaki kwa mfupi na kwamba haiwezi kuleta madhara kwa binadamu. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya serikali, uchafuzi wa maji katika mto huo uliosababisha samaki kufa ulitokana na mvua kubeba matope, mimea iliyokufa, tani za kinyesi cha ng’ombe, mikojo na takataka. 

“Magugu vamizi yanayoota ndani ya maji, hyacinth na papyrus ambayo huzaliana kwa haraka, yalisababisha upungufu wa hewa ya oksijeni ndani ya maji na hivyo kusababisha samaki kufa,” alisema Profesa Manyele wakati akiwasilisha ripoti hiyo. 

Ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa shughuli za binadamu kando kando ya mto ikiwamo malisho ya mifugo na kilimo vimechangia kuongezeka kwa takataka na vinyesi.

 Uchunguzi huo ulibaini kuwa takribani ng’ombe 300,000 wanatumia eneo la mto huo kama sehemu ya malisho huku wastani wa kilomita za mraba 423 zikitumika kwa shughuli za kilimo. 

Cows grazing at the shore of Mara River 1 1
Ng’ombe wakichungwa pembezoni mwa Mto Mara

Ripoti hiyo ilipendekeza serikali kulitangaza eneo lenye unyevu kando ya Mto Mara kuwa hifadhi ya Taifa ili kuulinda mto huo. 

Kuhusu magugu vamizi na ikiwamo papyrus, hyacinth na typha, ripoti hiyo iliiagiza serikali kutafuta namna ya kukabiliana nayo ili kupunguza kasi ya kuzaliana katika mto huo. 

Hata hivyo, wafugaji wanadai ni haki yao ya msingi kuchunga popote pale katika kipindi cha ukame isipokuwa katika mashamba ya watu tu.

 “Kuwa na mifugo ni sehemu kubwa ya shughuli zetu za kiuchumi. Pia, ni utamaduni wetu kuwa na mifugo mingi. Sisi tumerithi kwa wazazi wetu na ni wajibu wetu kuhakikisha watoto wetu wanarithi mifugo, “ anasema Yusufu Akuti mkazi wa Marasibora. 

Alikataa wazo la kubadili shughuli za kiuchumi au kupunguza idadi ya mifugo aliyonayo akisema sifa ya mfugaji ni kuwa na mifugo mingi. 

“Ng’ombe ni kila kitu kwetu. Huwa tunajisemea kama huna ng’ombe maana yake huna maisha. Tunawatumia kulima mashamba, wanatupa nyama, maziwa na mbolea,” anasema Akuti ambaye ni baba wa watoto 10. 

Kuhusu ufugaji wa bandani, Akuti anasema hawezi kufanya hivyo; “Siwezi kufuga ng’ombe bandani. Halafu ifahamike sio kwamba tunafuga kwaajili ya kipato tu, huu kwetu sisi ni utamaduni na ni lazima uenziwe.” anasema Akuti (64) huku akipiga miluzi kama ishara ya kuwaswaga ng’ombe wake kuelekea kutafuta malisho.   

Soma pia; North Mara Goldmine goes Green

Wanavijiji, wadau waizungumzia ripoti

Pamoja na Serikali kuwahakikisha wananchi kuhusu usalama wa maji ya Mto Mara, bado wameendea kuwa na hofu wakihoji ripoti hiyo. 

Kwa mujibu wa Majura Maingu ambaye ni mwenyekiti wa Taasisi ya Lake Victoria Farmers and Fishermen Organisation (VIFAFIO), anakiri kuwa na uhaba wa malisho kwa wanyama hasa wakati wa kiangazi na kwamba wamekuwa wakisafiri umbali mrefu na mifugo kusaka malisho. Amesema wakati mwingine husafiri mpaka mkoa wa jirani wa Simiyu kutafuta malisho katika vijiji vya Kembwi na Surubu vilivyopo kaskazini mwa Mto Mara. 

Hata hivyo, anasema nadharia ya kuwa kinyesi cha wanyama kimechangia kuchafua maji ya mto huo ina walakini. 

“Serikali inachukua muda mrefu kuweka wazi ukweli. Inabidi tuambiwe ukweli kwanini maji ya mto huu hayafai. Ni kweli maji hayafai kwa matumizi kwa sababu ukiweka mkono unawasha sana,” anasema Maingu huku akisisitiza kuwa wingi wa mifugo sio hoja. Anasema ni kweli zamani kulikuwa na wafugaji wachache lakini walikuwa na mifugo mingi,

“Zamani mfugaji mmoja alikuwa na ng’ombe 1,000 wakati sasa hivi mtu mmoja unaweza kuta ana ng’ombe 50 tu. Sasa nitaaminije kuwa kinyesi cha ng’ombe kinachafua mto sasa na sio miaka 40 iliyopita?”  

Majura Maingu, mwenyekiti wa Taasisi ya Lake Victoria Farmers and Fishermen Organisation(VIFAFIO),

Ziproza Charles, Mwenyekiti wa umoja wa  North Mara Water Users Association, naye anawatetea wafugaji akisema kizungumkuti kuhusu maji ya Mto Mara bado hakijateguliwa. 

“Hatukubaliani na wataalamu na ripoti yao kwasababu tuna historia ndefu na eneo hili. Ninakumbuka miaka yote eneo lenye unyevu katika Mto Mara limekuwa eneo la malisho ya maelfu ya mifugo miaka nenda rudi,” anasema Charles akiitaka serikali kuja na jibu la kueleweka.

Mara River wetlands during the pollution 1
Ardhioevu ya Mto Mara wakati wa uchafuzi wa mazingira

Hata hivyo, pamoja na madai ya wanavijiji, imeelezwa kuwa malisho kando ya Mto Mara yameongezeka miaka ya hivi karibuni na kusababisha uharibifu wa mazingira. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya  Vulnerability Profile Mara Wetlands ya Mei 2019, idadi ya ng’ombe inaongezeka kwa asilimia 9 kwa mwaka kutoka milioni moja na kufikia milioni 1.1 kila mwaka kuanzia 2003. 

Sio wananchi pekee walioipinga ripoti hiyo, Bunge la Tanzania pia limeikataa likisema sababu zilizotolewa haziendani na uhalisia na kuomba iundwe tume nyingine ya uchunguzi.  

Sera ya Tanzania ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira

Mwaka 2015 ripoti ya Management of Environmental Flows in the Nile River Basin: Practices and Experiences, the Nile Basin Initiative (NBI) iliitaja Tanzania kuwa moja ya wanachama wa Nile Basin wenye sheria na sera za kutunza mazingira.  

Uwepo wa sera ya maji ( National Water Policy of 2002) ni kielelezo tosha kuwa serikali inashiriki kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji na mazingira.  

Kwa kuangazia ubora na athari katika Mto Mara, ripoti ya NBI ikinukuu ripoti nyingine ya mwaka 2007,  Global Water for Sustainability (GLOWS 2007), iliyoeleza kuwa ongezeko la uhitaji wa maji umechangia uharibifu wa mazingira. 

Ripoti hiyo imesema ongezeko la watu, kilimo, ukataji misitu, kilimo cha umwagiliaji na maji yasiyo tibiwa ni miongoni mwa matatizo yanayowakabili wakazi wa ukanda wa Nile Basin. 

Inaongeza kuwa sera zinaweza kuwa njia madhubuti ya kukabiliana na matatizo hayo lakini inahitajika zaidi uwepo wa vyombo vinavyoratibu shughuli hizo. 

‘’Sera zinaeleza kinagaubaga haki na wajibu, nchi zote zinapaswa kutekeleza kwa vitendo maelekezo hayo ili kuwa na tija,” inasema sehemu ya ripoti hiyo. Pia inapendekeza kufanyika mara kwa mara kwa marekebisho ya sera hizo ili kuendana na mahitaji ya wakati husika. 

Kuhusu uchafuzi wa mazingira katika Mto Mara, unahitajika ufuatiliaji wa karibu ili maji yatumike ipasavyo kwa kufuata sheria na kanuni zinavyoelekeza. 

Akizungumzia repoti ya NBI, Donald Kasongi ambaye ni Katibu Mkuu wa Nile Basin Discourse Forum, amesema inapaswa kuwa na uangalizi wa karibu wa maji na vyanzo vyake kila siku ukiongozwa na sheria na sera.

“Sera ya maji ya Tanzania ina umri wa miaka ishirini sasa. Siamini kama inakidhi mahitaji yetu ya uratibu wa masuala ya maji kwa sasa,” anasema. 

“Kwa mfano ongezeko la mifugo katika malisho lililojitokeza Mto Mara, wadau na wananchi wanacho cha kujifunza. Uratibu wa programu za maji katika Mto Mara na bonde la Mto Nile unapaswa kuangaliwa upya na njia stahiki zichukuliwe,” anasema Kasongi.  

Makala hii ilitolewa Juni 2022, ilifadhiliwa na InfoNile, Media in Cooperation and Transition (MiCT) kwa ushirikiano wa Nile Basin Initiative (NBI) inayowezeshwa na  Deutche Gesellschaft fur Internationale Zusammenarbeit (GIZ) GmbH, chini ya Umoja wa Ulaya (European Union) na Federal German Government.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts