Na Lina Mwamachi
Eneo la Rombo, mpakani mwa Kenya na Tanzania, twiga wanalisha wakiwa na woga wa kuwindwa na binadamu. Kulingana na takwimu za African Wildlife Foundation (AFW), zaidi ya twiga ishirini na wanane wameuawa na wawindaji haramu kati ya mwaka 2020 na 2021.
Uwindaji huu unahusishwa pakubwa na mabadiliko ya tabia nchi. Aidha, shirika la African Wildlife Foundation pamoja na wakfu wa Biglife Foundation wamekuwa mstari wa mbele kupigana na uwindaji huo haramu.
Lina Mwamachi anaangazia suluhu rahisi zilizowekwa kukabiliana na uwindaji huo haramu wa twiga.
Amos Chege ni mwanasayansi na mtafiti wa maswala ya wanyama pori na kutathmini idadi ya wanyama pori katika shirika la mazingira African Wildlife Foundation eneo la Tsavo, Mkomanzi. “Mabadiliko ya tabia-nchi ni tatizo kwa wanyama. Hii inahusiana na mito kukauka na ukosefu wa maji ambayo hufanya wanyama pori kutoka kwenye hifadhi na kuelekea kwenye mashamba ya jamii ambako wao huuwawa na kuwindwa na jamii.”
Francis Legei mkuu wa kitengo cha ulinzi katika shirika la wanyama pori la Biglife Foundation anasema uwindaji haramu umeongezeka. “Mwaka wa jana 2021, tulipoteza twiga saba eneo la Rombo. Wengine kumi na wawili walipata majeraha makubwa. Tuliweza kutibu twiga wawili lakini hatukuweza kufaulu kuokoa hao wengine. Tulipofanya utafiti, tulipata majeraha waliyoyapata yalitokana na nyaya ambazo watu hutumia kuwatega kwa njia mbali mbali.”
“Jambo lingine ambalo linachangia uwindaji wa twiga ni ongezeko la idadi ya watu, ” aliongezea.
Aidha, Legei na Amos wanasema janga la Covid-19 limechangia pakubwa uwindaji haramu wa twiga sehemu za Rombo katika mpaka wa Kenya na taifa jirani la Tanzania.
“Msimu huu wa Covid kumekuwa na uwindaji wa twiga kwa sababu watu wanapata na kuuza nyama nyingi ukilinganisha na pundamilia ama swara,” alinena Amos Chege. “Pia ni rahisi kuwinda twiga, kusafirisha nyama yote kwa pikipiki na kupata mapato makubwa ukilinginisha na wanyama wengine.”
Watunzaji mazingira nchini Tanzania na hapa Kenya wameanzisha mikakati ya kutoa hamasa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza na kulinda mazingira na wanyama pori huku ulimwengu ukipambana na mabadilio ya tabia nchi.
Kuongezeka kwa uwindaji wa wanyama pori hasa twiga kunawakosesha usingizi wadau mbalimbali, hasa hali hii inapokosa kudhibitiwa. Anavyoelezea mtafiti Amos Chege.
“Hofu kubwa ni kwamba huenda hawa twiga wakaisha. Wale twiga wanaowindwa mara mingi ni wachanga sana au ni twiga wa kike ambao ni rahisi kuwawinda ukilinganisha na twiga wa kiume ambaye ni mkubwa. Kulingana na utafiti wetu, yale maeneo ambayo huwa na visa vingi vya uwindaji, idadi ya twiga inaendelea kupungua kwa kiasi kikubwa.”
Maendeleo na miradi ya serekali inayotekelezwa katika njia wanyama pori wanazopitia (wildlife corridors) kama vile reli ya kisasa SGR, na makazi ya jamii zimezuia uhuru wa wanyama pori kutembea huru, jambo ambalo limechangia kushamiri kwa visa vya uwindaji haramu.
Kama njia moja ya kupigana na uwindaji haramu, walinda mazingira kutoka Kenya na Tanzania wanalenga kuwahamasisha vijana na kina mama kupitia michezo ya kirafiki na miradi ya kujiendeleza ya kijamii.
Udhalimu huu kwa wanyama pori unatarajiwa kupungua baada ya kubuniwa kwa kitengo kikuu cha ulinzi – Multi Agency Security Hub eneo la Kasigao Kaunti ya Taita Taveta, kilichofadhiliwa na shirika la AWF kikilenga kumaliza uwindaji haramu katika mbuga za wanyama pori; Tsavo Mashariki, Tsavo Magharibi na maeneo ya Rombo, Tanzania.
AWF inasema suluhisho za kukoa twiga wasiangamizwe zaidi ni pamoja na kupanda miti aina ya Acacia kwa wingi ambayo ndio chakula chao, kuhamasisha umma juu ya umuhimu wake, pamoja na kubuni mikakati ya kimaendeleo ya kuinua jamii zinazoishi karibu na mbuga ya wanyama hawa.
Hadithi hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye Sifa FM, Voi Kenya.