Jitihada za uhifadhi zaanza kuzaa matunda Tanzania, wanyamapori wakiongezeka

Jitihada za uhifadhi zaanza kuzaa matunda Tanzania, wanyamapori wakiongezeka

Peter Elias, Tanzania

  • Hifadhi ya Taifa ya Katavi ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa nchini Tanzania yenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,471.
  • Hifadhi hiyo ina wanyama pori zaidi ya 100,000 na zaidi ya aina 450 za ndege.
  • Uwindaji haramu wa wanyamapori ni changamoto kubwa kwa sababu mbuga hiyo haina uzio
  • Kuimarika kwa ufuatiliaji na ushiriki wa jamii katika shughuli za uhifadhi kumesaidia kupunguza usafirishaji wa wanyamapori katika miaka ya hivi karibuni.
  • Licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na wadau, ujangili bado unaendelea

Safari ya kilomita 1,513 kutoka Dar es Salaam inanipeleka hadi Hifadhi ya Taifa ya Katavi- makazi ya maelfu ya wanyama kwenye mkoa wa Katavi uliopo magharibi mwa Tanzania.

Ikiwa ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa nchini Tanzania, Katavi ina ukubwa wa kilomita za mraba 4,471 na moja ya sifa kuu za hifadhi hii ni kuwa   na viboko zaidi ya 5,400 na baadhi ya wanyama wakuu wa tano  yaaani simba Tembo, kifaru, Chui na Mbogo.

Tofauti na mbuga nyingine nyingi, mbuga hii ina historia ya kipekee kutokana na  asili yake na pia ina mkusanyiko wa  mito na maziwa mengi ambayo hutoa maji kusaidia wanyamapori.

Maurus Msuha, Mkurugenzi wa wanyamapori, Wizara ya Mali asili na Utalii aelezea jitihada zilizochangia kuongezeka kwa idadi wa wanyama pori.

Hifadhi hii ina wanyama pori zaidi ya 100,000 wanyama hao ni pamoja na  simba, chui, tembo, viboko, mamba, swala, nyati, twiga na pundamilia. Pia, Katavi ni makazi ya zaidi ya spishi 450 za ndege, wakubwa kwa wadogo

Tanapa
Viboko wakiota jua kwenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi

Hazina hizi zinaifanya kuwa kivutio cha utalii na watu wa ndani na wageni wamekuwa wakitembelea hifadhi hiyo ili kuona wanyama wa aina mbalimbali, hasa viboko wanaoifanya hifadhi hii kuwa ya kipekee.

Francis Konde, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi, anasema wanapokea watalii 3,800 kwa mwaka. Anasema idadi hiyo ilipungua mnamo 2020 kwa sababu ya vizuizi vya Covid-19 lakini iliongezeka tena mnamo 2021.

“Watu wengi wanaotembelea hifadhi hiyo ni Watanzania wakifuatiwa na watu kutoka Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Ubelgiji. Hii ni kwa sababu mbuga hiyo iko karibu na Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),” anasema.

Katavi, sawa na maeneo mengine ya hifadhi, ujangili wa wanyamapori ni changamoto kubwa. Hii ni kwa sababu mbuga hiyo haina uzio; kwa hiyo, mtu yeyote anaweza kuingia na kuua wanyama kwa urahisi ikiwa atabahatika kutoka bila kukamatwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya African Wildlife Foundation (AWF), tembo wengi wanakufa kutokana na ujangili kuliko sababu za asili au migogoro ya kibinadamu.

Viungo vya wanyama hawa vinauzwa kinyume cha sheria kama nyara, dawa za kiasili au vitambaa kwenye soko lenye faida kubwa  – viumbe hawa  sio spishi pekee za wanyamapori wanaouwawa kwa faida ya binadamu.

Paka wakubwa kama simba na duma wanauawa kwa ajili ya mifupa yao; mbwa mwitu wa Kiafrika na wanyama wengine wakubwa wanaokula nyama hufa mikononi mwa wanavijiji wanaohami mifugo yao.

“Mara nyingi tunawakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake. Lakini tunawaomba wananchi waache vitendo hivyo kwani tumejipanga vyema na yeyote atakayeingia kwenye hifadhi kwa vitendo vya uhalifu, atakamatwa na kufikishwa mahakamani,” anasema Bw.Konde.

Konde anafichua kuwa kuwepo kwa soko la meno ya tembo na nyara nyingine katika nchi za Asia kama China na Thailand kunachangia kwa kiasi kikubwa ujangili. Hata hivyo

Hifadhi hiyo imeboresha ufuatiliaji pamoja na ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi, jambo ambalo limesaidia kupunguza usafirishaji wa wanyamapori katika miaka ya hivi karibuni.

Francis Konde, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi,

Anaongeza kuwa wanajenga barabara mpya ili kuongeza ufikiaji wa baadhi ya maeneo ya hifadhi. Pia, anabainisha kuwa wana askari wa ziada wenye magari mengi yatakayowawezesha kuongeza ufanisi katika ulinzi wa wanyamapori.

Hifadhi ina mpango wa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi ifikapo Juni ambapo wananchi wenyewe wataunda vikundi hivyo ambavyo vitasaidia katika ulinzi wa wanyamapori na maliasili nyinginezo. Wako tayari kujitolea kwa sababu wananufaika na hifadhi hiyo inayowapatia maji na imewapatia kituo cha afya na hosteli kwa ajili ya watoto wao.

“Wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi, na tunapata taarifa kutoka kwao kuhusu majangili hao. Hii inaonesha pia wanavutiwa na shughuli za uhifadhi wa maliasili kwa manufaa ya wote,” anasema Konde.

Mkurugenzi wa AWF Didi Wamukoya, anasema juhudi za kupambana na ujangili wa tembo zimezaa matunda kwa sababu mauaji haramu ya tembo kwa ajili ya pembe za ndovu barani Afrika yamekuwa yakipungua tangu mwaka 2011.

Wamukoya anabainisha kuwa idadi ya tembo nchini Tanzania imekuwa ikiongezeka kwa kasi kutoka 43,000 mwaka 2014 hadi 60,000 mwaka 2019, kulingana na Ripoti ya Sensa ya Wanyamapori Tanzania ya 2019.

Tembo Wetu 1
Tembo wa Kiafrika porini, Tanzania

Wamukoya anasema kweli kumekuwa na kupungua kwa nyara nchini Tanzania. Anaongeza kuwa ukamataji unaweza kuwa wa endelevu kutokana na kuimarishwa kwa utekelezaji na kuundwa kwa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kupambana na Ujangili (NTAP) mwaka 2016, ambacho ni jukwaa la mashirika ya kusaidia kukabiliana na uhalifu wa wanyamapori.

“Usafirishaji haramu wa wanyamapori, haswa  pembe za ndovu, unaendeshwa na mitandao ya kimataifa ya usafirishaji haramu wa wanyama pori. Wasimamizi wa sheria wa Tanzania wamebaini makundi ya watu wanaohusika na usafirishaji wanyapori, raia wa Afrika Magharibi na China.

Ni vigumu kutambua na kuzuia makundi yanayofanya biashara haramu kwa sababu wanaweza kubadilika kutoka kusafirisha pembe za ndovu hadi kusafirisha mazamo ya misitu kama vile mbaona silaha huku wakifahamu vyombo vya sheria vinaangalia zaidi aina fulani ya bidhaa.” 

Didi Wamukoya, Mkurugenzi wa AWF

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilianzishwa mwaka 2014 kwa lengo la kufanya doria za kupambana na ujangili ndani na nje ya Mapori ya Akiba na Maeneo ya hifadhi.

Kwa mujibu wa taarifa kwenye tovuti yao, tangu kuanzishwa kwa TAWA hadi Septemba 2016, jumla ya doria 69,278 zilifanyika ndani na nje ya Mapori ya Akiba na Maeneo Tawala na kusababisha kukamatwa kwa majangili 1,563.

Nyara zilizokamatwa ni pamoja na vipande 90 vya pembe za ndovu zenye uzito wa kilogramu 376.33  kilo 29, 529.5 za nyama ya wanyampori wa aina mbalimbali, bunduki 141 na risasi 278.

TAWA ina kitengo cha mbwa kinachosaidia katika ukaguzi wa mazao ya wanyapori kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na bandari ya Dar es salaam.

Jibu kali la kisheria

Bi Wamukoya anabainisha kwamba kupungua kwa ujangili na usafirishaji wa tembo nchini Tanzania kumechangiwa na juhudi zinazofanywa za kutekeleza sheria zilizopo kwa kudhibiti makundi yanayo jihusisha na ujangili huu kama hatua zilizochukuliwa hivi karibuni za kumkamata raia wa China Bi. Yang Fenglan ajulikanaye kwa jina la utani la Malkia wa Tembo akishikiana Bwana Boniphace Malyango kwa jina la utani anajulikana kama Shetani ambao kwa pamoja walikuwa wakiongoza mtandao unaosafirisha pembe za ndovu kuelekea barani Asia.

Pia anatoa shukurani zake kwa ushirikiano wa jumuiya ya kimataifa katika kupiga vita ujangili na usafirishaji bidhaa za wanyama pori kwa kuwa  biashara hii ni ya kimataifa,

Bi Wamukoya anasema mahitaji kwenye nchi zinapokea bidhaa hizi   yanapaswa kushughulikiwa kwa kufanya uhamasishaji na  kupunguza mahitaji na umuhimu wa kuwa na sheria kali. Kwa sasa Tanzania inauchukulia uhalifu huu kama uhujumu uchumi na unabeba adhabu ya kifungu cha miaka thelathini au kifungo cha maisha na faini

“Kwa mujibu wa data zilizokusanywa na WidlifeEye East Africa nchini Tanzania, idadi kubwa ya watu waliopatikana na hatia ya uhalifu wa wanyapori walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.  Pia Baadhi ya hukumu ziliambatana na faini au dhabu zinazolingana na thamani ya wanyapori waliokamatwa; hata hivyo adhabu zilikuwa chache ikilinganishwa waliowekwa kifungoni na hakukuwa na thamani ya kifedha ya adhabu iliyolingana kwa mtu aliyepatikana na hatia”

Mkurugenzi wa wanyamapori  kutoka Wizara ya Mali asili na Utalii bwana Maurus Msuha anasema ongezeko la tembo limechangiwa na mifumo mizuri ya ulinzi kwenye maeneo ya hifadhi. 

Dr Maurus Msuha Director of Wildlife
Maurus Msuha, Mkurugenzi wa wanyamapori, Wizara ya Mali asili na Utalii.

“Operesheni zetu tumeziweka kijeshi. Pia tuna mfumo mwingine unaozihusisha taasisi zingine; kwahiyo tuko vizuri kwenye ulinzi wa wanyamapori” anasema bwana Msuha.

Pembe nyingi za Tembo zilizokamatwa hivi karibuni zina umri wa miaka sita au saba, hali inayoonyesha kuwa ujangili umepungua sana ikilinganishwa na miaka ya kabla ya mwaka 2014 ambapo maelfu ya Tembo waliuwawa kila mwaka.

Msuha anabainisha kuwa haya yote yanafanyika ili kuwalinda faru pia ambao idadi yao inaongeka kabla ya lengo lililowekwa.

“ Tuna mkakati wa miaka mitano wa 2018 hadi 2023, Kwa hiyo, tupo kwenye njia sahihi na mpango wetu ulikuwa ni kuhakikisha idadi ya Faru inaongezeka kwa asilimia tanokwa mwaka lakini tumevuka malengo kadiri tunavoendelea”  alisema bwana Msuha

“Kwa mujibu wa data zilizokusanywa hadi sasa na WildEye East Africa nchini Tanzania, takriban nusu ya kesi zote zinahusisha pembe za ndovu na asilimia 90 ya kesi hizi zilihusisha umiliki haramu wa pembe, nyama tembo na sehemu zingine za wanyama hawa.

Takwimu hizi zilikusanywa katika kufuatilia  washitakiwa waliokamatwa ambao kesi zao zinasubiri hukumu ambapo nusu ya watuhumiwa walikutwa na hatia, kesi kumi zilikuwa bado zinasikilizwa pamoja na watu wengine wakiwa wametiwa nguvuni.”

Ujangili, tatizo linaloendelea

Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali na wadau wengine kukomesha ujangili wa wanyapori, bado tatizo hili linaendelea. Kuna baadhi ya wahalifu wanawatumia wenyeji, walinzi wa wanyapori na hata wafanyabiashara kupata pembe za ndovu kutoka kwenye hifadhi za wanyama pori.

Askari mmoja kutoka hifadhi ya wanyamapori ya Katavi ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za kiusalama anasema wapo askari wenzao wanaowasaidia majangili kuuwa tembona kuuza meno. “ Miongoni mwetu kuna watu wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wanavijiji au wafanyabiashara kuwaua tembo wetu, hili halikubaliki, wanatuangusha katika vita hivi” Anasema mlinzi wa wanyampori katika hifadhi ya Katavi

Naye mkaazi wa kijiji cha Stalike wilayani Mpanda bwana Ibrahim Makusa anasema wanatambua umuhimu wa kulinda hifadhi, lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakishiriki kuua wanyama hawa ili kupata pembe zao.

“ Baadhi ya wanakijiji walikamatwa wakiwa na pembe za ndovu; kesi yao bado inaendele. Wanadhoofisha juhudi zetu za kulinda hifadhi kwa sababu tunafaidika na hifadhi hii; imetujengea shule, imesambaza maji kwenye kijiji chetu “ anasema bwana Makusa.

Bwana Msuha anasema bado kuna soko haramu kwenye nchi za asia kama vile Vietnam, Malaysia na nchi nyingine Mashariki mwa bara la Asia mbako watu wanaamini kuwa na mapambo yaliyo tengenezwa  kutokana na pembe za ndovu ni ishara ya utajiri.

Tembo
Tembo malishoni

Hakimu wa mahakama ya Kisutu iliyoko jijini Dar es Salaam amekuwa akisikiliza kesi kadhaa zinazohusu ujangili na pembe za ndovu ambapo baadhi ya watu wamehukumiwa kwenda jela na wengine kuachiwa huru.

Mnamo mwezi wa machi 2022, wakazi watno wa Katavi na Sumbawanga walifikishwa kwenye mahakama ya Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ikiwa ni pamoja ma kukutwa na vipande vinne vya pembe za ndovu.

Watuhumiwa hao ni Craft Kileo(43), Godfrey Kashuli(42), Richard Kafwa((43), Moses Zakaria (33), na Benjamin Lushina (33) ambao ni wakazi wa Sumbawanga, Nmanyere na Mpanda.

Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam wanawashikilia watu watatu wanaotuhumiwa kukutwa na vipande ishirini na tano vya meno ya tembo kwenye opresheni maalum iliyofanyika maeneo ya Magomeni na Manzase Jijini Dar es Salaam.

Hivi karibuni kamanda wa kanda maalumu ya kipolisi ya Dar es Salaam bwana Jumanne Muliro alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na kikosi maalum kupmbana na ujangili walifanikiwa kuwatia nguvuni watuhumiwa watatu ambao ni mabwana Gabriel Mgana, Haffaman Yona na Felician Cyril wakiwa na vipande 25 vya pembe za ndovu zenye uzito kilogramu 20 kilo uzito ambao ni sawa pembe za tembo 14 waliouwawa.

Mapema mwaka huu Hakimu mkazi wa mahakama ya Kisutu alimhukumu bi Haika Mgao mwenye umri wa 26 kifungo cha miaka 60 jela baada ya kukutwa na hatia kukutwa na vipande vya pembe za ndovu na meno ya kiboko yenye thamani shilimgi za kitanzania millioni 69.5 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mgao mkazi wa kimara jijini Dar es salaam alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi kwenye kesi nambari 69/2018. Moja ya mashataka hayo ni kukutwa na pembe za  ndovu na meno ya kiboko akiwa hana kibali cha mkurugenzi wa wanyama pori.

Usaidizi wa  ukuzaji na utengenezaji wa hadithi hii ulitoka kwa InfoNile, kwa ushirikiano na Oxpeckers Investigative Environmental Journalism, kwa ufadhili wa Earth Journalism Network. Vielelezo vya data na Ruth Mwizeere na Annika McGinnis / InfoNile.

Print Friendly, PDF & Email

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts