Ukosefu wa maji safi bonde la mto Nile na madhara ya mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo

Ukosefu wa maji safi bonde la mto Nile na madhara ya mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo

Prosper Kwigize, Tanzania

Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera nchini Tanzania ni eneo lililo bahatika kuwa na vyanzo vingi vya maji. Vyanzo hivyo ni pamoja na mto Kagera na mto Ruvubuhu.

Hata hivyo wakazi wake wanakabiliwa na uhaba wa maji kwa shughuli za kilimo na matumizi ya nyumbani licha ya kuwapo kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Mpango wa Bonde la mto Nile wa kusaidia mradi wa usambazaji wa maji kama sehemu ya fidia kwa wakazi waliojitolea kuacha ardhi yao kwa ajili ya mradi wa kufua umeme kwenye maporomoko ya mto Kagera.

Ungana naye Prosper Kwigize anapotufahamisha mengi kuhusu athari za mradi wa umeme wa maporomoko ya majiya mito ya Ruvubhu na Rusumo katika eneo ya mipaka ya nchi tatu za Rwanda, Burundi na Tanzania.

Bonde la mto Kagera linaiunganisha Ruvubhu na Akagera kwenye eneo la Rusumo na kumwaga maji kwenye ziwa Victoria, ziwa ambalo ndio chanzo cha mto Nile. Bonde hili lina wakazi milioni kumi na nne kutoka nchi za Tanzania, Burundi, Rwanda na kwa uchache Uganda, wakazi hawa wapo hatarini kukumbwa na mlipuko wa magonjwa  kwa kukosa maji safi na salama.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) kwa sasa ni asilimia 68 tu ya wakazi Ngara wanaopata maji safi kwa takwimu za mwaka 2021.

Ashura Mohamed mkazi wa Ngara anasema kuna mgao wa maji usio wa kawaida ambapo kuna kaya zinapata maji mara mbili kwa wiki wakati maeneo mengine hayapati maji kabisa na Ankara za maji wanazoletwa ni kubwa iwe maji yanapatikana au hayapatikani

Anasema tatizo la usambazaji duni wa maji limesabisha wakazi wa Ngara kutegemea watu binafsi wanao wanauza lita 20 za maji kwa shilingi za kitanzania kati ya mia mbili na mia tano sawa na dola za kimarekani 0.09 na 0.22.

Milolongo mirefu  ya watu wanaohitaji maji kutoka visima vya watu binafsi  huzusha sintofahamu na magomvi ya mara kwa mara kati ya wachuuzi na watu wengine na pia ni chanzo kikubwa cha mafarakano ndani ya familia pale ambapo wanawake wachukua muda mrefu kutafuta maji hali ambayo inawafanya wanaume wengi kutofurahishwa na jambo hili kwani wanaona wanawake hawawajibiki na masuala mengine ya kifamilia.

Baraka Sengiyumva, mmoja wa wachuuzi wa maji
IMG 20211126 120110 839 1 1
Baraka Sengiyumva – Mchuuzi wa Maji Mjini Ngara akitembeza mtaani kwa mkokoteni, kwa siku huuza hadi lita 600 hadi 1000

Kwa mujibu wa Mamlaka ya maji safi na na usafii wa mazingira, RUWASA, kiasi cha maji kinachopatikana kwenye mfumo wa kusambaza maji wilayani Ngara ni mita za ujazo 61,949 wakati mahitaji halisi ni lita 225,000. Taarifa ya mwaka 2017/2018 ya wilaya inaonyesha takwimu hizo.

Mhandisi Simon Ndyamukama ambaye ni meneja wa mamlaka ya maji anabainisha kuwa asilimia 30 ya maji yanayopatikana wilayani Ngara ni kwenye visima vilivyochimbwa , huku asilimia 48 yanatokana na maji ya bomba.

Wakazi wengi wa wilaya za Ngara na Karagwe kwenye mabonde ya  mito ya Ruvubu na Kagera wanategemea maji yanayotokana visima vilivyochimbwa kienyeji kwa matumizi yao ya kila siku.

Kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo baadhi ya watu wanachanganya maji haya na kemikali katika jitihada za kuondoa matope, zoezi ambalo si salama kwa mujibu wa taratibu za usafi wa maji.

Mhandisi Ndyamukama  alieleza idhaa ya Kiswahili ya sauti Ujerumani DW kwamba vyanzo vya maji vimeathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na  shughuli za kibinadamu.

Kwa mujibu wa mhandisi Ndyamukama upatikanaji wa majibu safi unaongezeka. Kutoka mwaka 2019 mpaka 2021 upatikanaji wa maji safi na salama uliongezeka kwa asilimia 68 na unatazamiwa kuongezeka hadi asilimia 78 mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 2022.

Mhandisi Ndamukama anasema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Serikali imeweza kuwasambazia maji wakazi wapatao 246,257 kati 358,975 wilayani Ngara, lengo likiwa ni kuwafikishia huduma asilimia 85 ya wakazi ifikapo mwaka 2025.

Lakini mpango mkakati wa Halamashauri ya Wilaya ya Ngara wa 2016/2017 na 2020/2021 ulionyesha kuwa Ngara ina safari ndefu kuhakikisha wanachi wanapata maji safi na salama.

“Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka yetu imeweka vipaumbele mbalimbali vikiwa na lengo la kuhakikisha huduma ya maji inainufaisha jamii na tuna uhakika idadi ya kaya zinazopata maji kwa asilia 85 kufikia mwishoni mwa mwaka 2022. Wakati huo huo kwa kushirikiana na wabia  wa maendeleo na wadau wengineo kama vile Benki ya Dunia na NELSAP kuendeleza vyanzo vya maji yatapewa umuhimu wa pekee.” Anasema Mhandisi Ndyamukama.

Makutano ya mto Akagera Kagera na Ruvubhu katika eneoo la Rusumo wilayani Ngara mpakani mwa Tanzania na Rwanda 1
Makutano ya Mto Akagera (Kagera) na Ruvubhu Wilayani Ngara, Mpakani mwa Tanzania na Rwanda

Mkakati wa Benki ya Dunia na NELSAP kutoa maji safi

Matumaini ya wakazi wa Rusumo ya kuona mradi wa Benki ya Dunia ulioanzishwa mwaka 2017  pamoja na ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Maporomoko ya Rusumo kuwa suluhisho la changamoto za maji wilayani humo ni madogo.

Mradi wa kufua umeme wa maporomoko ya Rusumo uliozinduliwa na program NELSAP unatazamiwa kuzinufaisha nchi tatu jirani ambazo ni Rwanda, Tanzania na Burundi kwenye mpaka wao wa pamoja wa Rusumo.

Inakadiriwa kuwa Megawati 80 za umeme zitazalishwa kwenye mto Kagera kwenye maporomoko ya Rusumo ambapo ujenzi wake ulianza tangu mwaka 2017 na mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi wa tano mwaka 2022 huku fidia kwa wakazi wa eneo hilo na shughuli zingine za maendeleo zikiwa zimeshaanza kutekelezwa wakati mradi ukiwa kwenye utekelezaji.

Ili kuendeleza mradi huu Tanzania ilipata jumla ya dola za kimarekani milioni 5, kwa mujibu wa afisa mawasiliano wa mradi wa kufua umeme wa Rusumo Bi. Louis-Andree Ndayizeye. Mpango wa maendeleo wa eneo hili (LADP) ulilenga kuchechemua shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kujenga miundo mbinu mbalimbali iliyolenga kuboresha maisha ya wakazi wa Rusumo na sehemu ya mpango huu ni shilingi za kitanzania bilioni 2.7 sawa na dola za kimarekani milioni 1.2 zilizokabidhiwa mpango wa mradi wa bonde la mto Nile na Benki ya Dunia ili kuboresha hali ya upartikanaji maji kwa wakazi wa wilaya ya Ngara.

Wilaya hii ilitakiwa kujenga chanzo cha maji na miundo mbinu yake kwa ajili ya wakazi wapatao 12,925 wa kata ya Rusumo na maeneo jirani. Mpango huu ulitazamia kutatatua changamoto za upatikanaji maji kwa wakazi hawa ambao wanategemea maji ya mito ya Kagera na Ruvubhu. Hata hivyo mradi huu umekwama kutokana na changamoto za kimkataba kati wafadhili, mkandarasi na serikali ya Tanzania.

Kwa mujibu wa kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Ngara Bwana Enock Ntakisigaye shughuli mbalimbali za utekelezaji wa mradi zimekwishaanza ikiwa ni pamoja na upembuzi yakinifu na kutayarisha eneo ambapo mitambo na pampu za maji zitafungwa ingawa mradi umesimama kutokana mivutano ya kimkataba na taratibu za kisheria kati ya wakandarasi kampuni ya ECIA, Abemulo Contactors na Halmashauri ya wilaya ya Ngara na changamoto hii inatatuliwa ili mradi uweze kuendelea. 

Ucheleweshaji wa aina hii unawafanya wakazi wa eneo hili kutoridhika na hali hiyo jambo ambalo linaweza kutishia usalama na mafanikio ya mradi mzima wa kufua umeme.

Rusumo water Project signboard 1
Bango la mradi wa Maji wa Rusumo
rusumo falls
Maporomoko ya maji ya Rusumo kwenye mto Kagera kwenye bonde la mto Nile mpakani mwa Tanzania na Rwanda

Uchafuzi, nyumba zilizoanguka: Madhara ya mradi wa kuzalisha maji wa Rusumo

Wakazi wa kata ya Rusumo kwenye bonde la mto Kagera wanasema tatizo la upatikanaji wa maji safi linazidshwa na ujenzi wa bwawa la kufua umeme.

Wakazi wengi wa Kagera Tanzania, Kirehe Rwanda na Muyinga Bururundi sehemu ambazo mradi huu unatekelezwa wanasema matumaini yao ya kufaidika na mradi huu bado hayafikiwa.

Wanasema hakuna uhusiano mzuri kati ya kampuni zinazotekeleza ujenzi wa mradi wa Rusumo, jamii na wadau wengine jambo ambalo limepelekea kupungua kwa ulinzi wa mazingira ya mto ambao ndio unalisha mradi mzima hivyo kutishia uzalishaji umeme. Maji taka kutoka karakana ya mradi wa kufua umeme Rusumo yanamwagika kwenye mito na kusababisha uchafuzi kwenye mito wanasema wakazi hawa.

Mtaalaamu wa afya mazingira Scarion Ruhula ambae anafanya kazi na Shirika la Huduma za walemavu kwenye mikoa ya Kagera na Kigoma anasema hakuna athari za moja kwa moja iwapo karakana au makazi ya watu yatajengwa kati ya mita 50 na mita 100 kutoka chanzo cha maji hata hivyo ilibainika kuwa mradi wa Rusumo umejengwa ndani eneo hili na  na mifumo ya uwagaji maji taka inaingia ndfani ya  mto.

Kinacho hitajika ni kuhakikisha kwamba maji yanayotoka kwenye makazi ya watu au karakana hayaingii mtoni anasema” bwana Ruhula na kuitaka Serikali kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mradi ili kudhibiti uwezekano wa mlipuko wa maradhi yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.

Kuhusu shutuma kwamba maji taka yanamwagikaa kwenye mto, mkurugenzi wa baraza la usimamizi wa  Mazingira Tanzania (NEMC) Bwana Samwel Gwamaka anasema ofisi yake haina taarifa rasmi kuhusu suala hili kutoka kwa wananchi na ofisi yake itapeleka mkaguzi kutoka eneo la ziwa Victoria kufanya ukaguzi na hatua zaidi zichukuliwe.

NEMC wafanya ukaguzi na kubaini mapungufu kisheria

Mnamo tarehe 1 machi 2002 NEMC ilifuatilia suala hili kwa kuwatuma wakaguzi kutoka ziwa Victoria na Bonde la Mto Kagera kufanya ukaguzi kwenye mradi wa umeme wa Rusumo kufuatia malalamimiko ya uchafuzi wa mazingira.

Ukaguzi ulionyesha kwamba wakandarasi walikiuka taratibu za kimazingira kwa kukosa namna bora ya kudhibiti takataka  kwenye karakana zao. Maji machafu, vyuma, na mabaki ya mafuta yalipatikana yakielea kutoka kwenye eneo la ujenzi hadi kwenye mto Kagera. 

Kutokana na ukiukwaji huu wa taratibu, Mkaguzi kutoka NEMC Bwana Benjamin Dotto alitoa onyo kali kwa uongozi wa mradi na kwamba hatua zitachukuliwa dhidi NELSAP iwapo watashindwa kurekebisha muundo wao wa udhibiti wa taka. Hakutaka kusema adhabu ambayo wameitoa ingawa taarifa kutoka ndani ya Halmashauri ya wilaya Ngara zinasema shilingi milioni 20 ni kiasi ambacho kimewekwa kwa makosa kama hayo.

Mnamo mwaka 2021, kaya 40 zilijikuta zikiwa kwenye tishio la kukumbwa na mafuriko wakati baadhi ya nyumba zao zikiharibiwa kutokana na milipuko inayotokana na kuvunjwa kwa miamba. Milipuko hii ilisababishwa na ujenzi wa  mifereji kutoka kwenye mradi inayopita chini ya ardhi ambayo ilipelekea kutokea kwa tetemeko lililosababisha kubomoka kwa vyoo na kusababisha maji taka kuingia mtoni. 

Kwenye mahojiano maalum mkurugenzi mtendaji wa NEMC bwana Samwel Gwamaka alithibitisha kuwapo kwa athari za kimazingira zinazotokana na mradi wa umeme wa Rusumo

Kwa mujibu wa NEMC mradi wowote unaohusisha mazingira unapaswa kufanyiwa tathmnini ya mazingira ili kuainisha athari za kimazingira zinaweza kusababishwa na mradi. Hata hivyo Bw. Gwamaka anasema changamoto ya sasa inatokana na mabadiliko ya kimazingira ambayo hapo awali hayakuonekana wakati wa tathmini ya awali iliyofanyika miaka kumi iliyopita.

Tathmini ya mazingira iliyofanywa na kampuni ya SNC Lavalin International chini mradi wa NELSAP inasema ujenzi huu ulitazamiwa kusababisha mafuriko kwenye eneo la hekta 17000 na kubadili kina cha maji kwenye eneo la hekta 1700. Hata hivyo tahadhari ya kutosha hakuchukuliwa wakati wa kujenga kizuizi cha maji na kupelekea kuwapo kwa mafuriko kwenye makazi ya watu.

“Hakukuwa na tahadhari yoyote kwa jamii ambayo ingewawezesha kujitayarisha na mafuriko yaliyotokea na hakuna vizuizi vilivyowekwa kuzuia maji kutoka mtoni kufurika kwenye mashamba na makazi ya watu” kwa mujibu wa Bwana Ntiba Alfred Bilaba mwenyekiti wa kamati ya wanuifaika wa mradi wa umeme wa Rusumo.

Malalamiko mengine yalitoka kwenye kaya ambazo hazikulipwa kwa ilikuhama kutokana na uharibifu uliotokana na zoezi la kupasua miamba na ni nyumba 40 tu ndizo zilizofanyiwa ukaguzi kati ya nyingi zilizopo. Hata hivyo NELSAP haijawafidia wale wote waliopatwa na kadhia hii ya uharibifu. Tuhuma hizi zilitolewa na wakazi wa Rusumo na kuthibitishwa na mkuu wa wilaya ya Ngara.

Serikali ya Tanzania ilikiri kuwapo na changamoto na kuwahakikisha kwamba serikali inafanyia kazi suala hili kwa kushirikiana na wakandarasi ili kuhakikisha masharti ya mkataba yanazingatia fidia zilizowekwa. 

Mkuu wa Wilaya ya Ngara kwa niaba ya serikali ya mkoa wa Kagera aliahidi kuhakikisha mgongano wa kimaslahi kati kati ya wananchi na mradi wa umeme wa Rusumo unatatuliwa huku akizitaka pande zote kufuata taratibu zilizohainishwa kwenye makubaliano kati ya NELSAP na srikali ya kijiji katika kutekeleza mradi wa kufua umeme wa Rusumo kwa maslahi ya umma na kuhakikisha tathmini ya mazingira inapewa kipaumbele.

Kufuatia malalamiko haya NELSAP ilithibisha kwamba  mambo yote  yatatatuliwa kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa na nchi zote tatu kwenye mahojiano maaalum 

Afisa wa mawasiliano wa NELSAP Louis Andree Ndayizeye alisema NELSAP kwenye mradi wa Rusumo imekarabati miundombinu ambayo iliathirika kutokana na shughuli za kulipua miamba na sasa mradi unajitayarisha kukarabati miundo mbinu mingine iliyoathirwa ikiwa ni pamoja na nyumba na vyoo.

Hata hivyo uchunguzi uliofanyika kati ya machi 10 n 12 mwaka 2022 katika kata ya Rusumo wilayani Ngara umebaini kuwa NELSAP inaendelea kufanya tathmini ya uharibifu huo huku ikiwa kwenye shinikizo kutoka Serikali ya Tanzania kupitia kwa mkuu wa wilaya na Baraza la Mazingira NEMC ambalo lilifanya ukaguzi na kubaini athari za uharibifu wa mazingira kwenye eneo la mradi wa umeme

Kwa mujibu wa mradi wa kimataifa wa kuzalisha umeme wa maji na ripoti ya tathmini ya Benki ya maendeleo Afrika athari zinahusiana ujenzi wa mradi huu zilitazamiwa kudumu angalau kwa miaka miwili. Athari hizi ni pamoja na vumbi, kelele, mmonyoko wa udongo, kupungua kwa ubora wa maji uchafuzi wa udongo unaotokana na usimamizi mbaya wa utoaji taka na kumwagika kwa kemikali za ukaa (Hydrocarbons) kwa bahati mbaya na pia usumbufu kwa wanyamapori. 

IMG 1451 1
Vifaa vya ujenzi wa mradi wa maji Rusumo kwa ufadhili wa Benk ya dunia ambao umekwama tangu mwaka 2017, na mkandarasi hayupo eneo la ujenzi
RUSUMO WATER PROJECT SITE 1
Eeneo la ujenzii wa mradi wa maji Rusumo uliotelekezwa na mkandarasi tangu mwaka 2017, ujenzi umesimama na eneo limezingira na vichak

Athari zilizotokana na mradi huo ni pamoja na kupoteza makazi, miundo mbinu ya biashara, kupoteza ajira na ardhi ya kilimo na ardhi oevu.

Idadi ya watu waliofidiwa ni pamoja na kaya 67 kutoka wilaya ya Kirehe nchini Rwanda na kaya 103 kutoka wilaya ya Ngara nchini Tanzania.

Kwa mijibu wa Bi Louis Ndayizeye, ulipaji wa fidia kwa jamii zilizoathirika na uwepo wa mradi huo ulihitimishwa kabla mradi haujaanza mwaka 2015. Mradi wa NELSAP Rusumo sasa upo kwenye mchakato wa kuwalipa fidia wamiliki wa maeneo yaliyoharibiwa na mafuriko ya maji.

Wanufaika 10 waliohojiwa walikiri kutolewa kwa fidia, hata hivyo walisema walilipwa fidia ndogo  kutokana na kucheleweshwa malipo kwani tathmini ya makazi ilifanyika mwaka 2015 na malipo yalifanyika 2017 wakati thamani ya nyumba ikiwa imeongezeka na kuwafanya kutafuta vyanzo vingine vya mapato kuongezea malipo hayo ya NELSAP.

Jamii ya Rusumo pia ilisema uhamishaji wa watu kutoka vyanzo vya maji haukufanyika kwa familia zote zilizopimiwa maeneo. Mwenyekiti wa kamati ya wahanga wa mradi huo Bwana Ntiba Bilaba aliilalamikia NELSAP kwa kutozingatia makubaliano yaliyosainiwa na kusababisha kutokea kwa malalamiko mengi kutoka kwa wanajamii wakilalammikia Mpango wa Bonde la mto Nile, wafadhili na serikali ya Tanzania.

Ahadi kwa watu walioathiriwa na mradi 

Kwa mujibu wa makubaliano ya kikanda, NELSAP ilitakiwa kutoa dola za kimarekani 383,832 ikiwa ni fidia kwa ajili ya watu wapatao 200 ambao maeneo yao yyamechuliwa na mradi wa umeme. Hata hivyo Bwana Dionis Albogast mweka hazina wa Programu ya  kusaidia wahanga wa mradi anasema kiwango kilichotolewa kwa wanufaika kwa kipindi cha 2017 hadi 2021 ni dola za kimarekani 293,240 zikibakia dola 90,592 ambazo hazijatolewa suala linalosababisha malalamiko.

Jamii ya watu Bonde la mto Kagera ilikuwa inategemea kuboresha hali ya maisha yao kupitia program ya hiyo (LRP) iliyopo chini ya mradi. Hata hivyo wakazi wanasifu program kama hiyo ya nchini Rwanda  ambayo inawahudumia waathirika moja kwa mija badala ya kupitisha msaada huo kwa wabia wa mradi.

Hata hivyo mratibu wa fedha za miradi inayofadhiliwa kwenye halmashauri ya wilaya Ngara bwana Didymus Sebastian anasema fedha za miradi yote inayofadhiliwa na NELSAP kwa ajili ya jamii imekuwa ikitumika moja kwa kuwafadhili wanufaika na kinachotofautisha kati ya Tanzania, Rwanda na Burundi ni mikakati ya utekelezaji tu. 

Bwana Didymus alisema taasisi za kiraia na zile za umma ikiwa ni pamoja shirika la misaada ya kiraia REDESO na TCRS yalikuwa yamehusishwa kujenga uwezo kwa vikundi vilivyoundwa ili kutekeleza miradi ya kiuchumi.

rusumo woman
Agnes Mutashobya mkazi wa kata ya Rusumo akichota maji kwenye kisima cha mtaa huo

Madhara ya kimazingira kwa wazawa

Pamoja na uchafuzi mazingira unaotokana na mradi wenyewe, maafisa wa serikali mkoani Kagera wametambua changamoto zinazoletwa na shughuli za kibinamu kwenye bonde ambazo zinaathiri ziwa na uwezekano wa kufanikiwa kwa mradi wa kufua umeme

Enock Ntakisigaye, kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara anasema kumekuwa na kuzembea kwenye usimamizi na kuzingatia sheria za mazingira na matumizi sahihi ya maji kwa baadhi ya watu kwenye bonde la mto Nile hususan kwenye mito ya Kagera na Ruvubhu.

Bwana Ntakisigaye ana ainisha kuwa kuna sheria inawataka wananchi kufanya shughuli zao mita umbali 60 kutoka chanzo cha maji pamoja mito, mabwawa na maziwa ili kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji.

Sheria ya mazingira namba 2 ya mwaka 2004, Sheria ya usimamizi wa vyanzo vya maji namba 11 ya mwaka 2019 na Sheria namba 5 ya mwaka 2019 ya maji safi na na usafi wa mazingira inasema ni ni kosa kwa mtu yeyote kuharibu vyanzo vya maji au kutumia maji bila kibali. Sheria hizi pia zinaeleza umuhimu wa jamii kupata maji safi na salama. 

Pamoja na kuwepo kwa sheria hizi, jamii bado inaazisha shughuli za kilimo na makazi kwenye bonde la mto Kagera na hii iinaathiri shughuli za uhifadhi. mwandishi wetu alishuhudia mashamba na makazi mapya kwenye eneo linalounganisha Mito ya Kagera na Ruvubhu ambapo mmiliki hakuwa tayari kufanya mahojiano akidai eneo hilo anamiliki kisheria na serikali inatambua na ameruhusiwa kuanzisha miradi yake.

RUSUMO KILIMO NA MAKAZI BONDENI
Moja ya mashamba mapya yaliyokodishwa katika bonde la Mto Kagera katika kijiji cha Rusumo, wilayani Ngara

Wakazi wa Rusumo walisema kumekuwa na upungufu wa samaki kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu katika mto huo na ongezeko la watu wanaotumia njio haramu za uvivu. Pia walihisi ujenzi wa mradi wa umeme wa maji umeathiro upatikanaji wa samki. Manilakiza John ambaye ni mvuvi alikua akihangaika kutafuta samaki mtoni.

fisherman

Hata hivyo, Mpango wa Bonde la Mto Nile unasema mfumo wa mradi hauna athari kwa bayoanuwai.

“Mradi ni Uendeshaji wa Mto (ROR0; mpango huu ulichaguliwa ili kupunguza atahari kwa jamii na mafuriko kwenye maeneo ya mabwawa. Kwa hivyo, mradi huo hauna athari kwa bioanuwai. Hili si bwawa, kwa hivyo hakuna kemikali zinazotupwa mtoni,” alieleza afisa wa mawasiliano wa NELSAP Louis Ndayizeye.

Uzalishaji wa Umeme wa Maji katika mto Kagera

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia upatikanaji wa umeme ulikuwa ni asilimia 10 kwa Burundi asilimia 16 kwa Rwanda na Tanzania ikiwa na asilimia 18.

Kwa kutumia maji ya mto Kagera, mradi wa kufua umeme wa Rusumo utazalisha megawati 80 za ziada kwenye gridi za umeme ya mataifa Tanzania, Burundi na Rwanda umeme ambao inasemekana utakuwa ni endelevu na wa bei nafuu. Kila nchi itapata megawati za ziada 26.6. 

Kwa mujibu wa msimamizi wa mpango wa Bonde la Nile watu 1,146,000 kwenye nchi hizi tatu watanufaika na mega wati hizi za ziada na kutakuwa na ongezeko la umeme la asilimia 5.4 kwa wakazi 520000 wa Burundi, asilimiia 4 kwa wakazi 467000 wa Rwanda na asilimia 0.34 kwa wakazi 159000 wa Tanzania.

RUSUMO 1
Kizuizi cha kisasa cha maji kwa mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Rusumo.

Kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme kwa kutumia maporomoko ya maji kutasaidia kupanuka kwa shughuli za kiuchumi kwa sekta binafsi na shughuli za kilimo, lakini iwapo mazingira hayatalindwa mradi hauwezi kudumu.

Shughuli za kibinamu kwenye vyanzo vya maji katika nchi za Afrika mashariki, hususan mto Kagera, mto Ruaha, bwawa la Mtera lililopo mto Kilombero, Bwawa la nyumba ya Mungu na mengine zisipodhibitiwa zitasababisha uhaba wa maji na uwepo wake. Hivi sasa Tanzania inashuhudia kupungua kwa maji na kuharibika kwa vinu vya kufulia umeme kunakopelekea kuwapo kwa mgao wa umeme. 

Maeneo yote yanayotegemea umeme wa maji ikiwa ni pamoja na jiji la Dar es salaam, sehemu za kati, kusini na kaskazini mwa Tanzania bado zinapitia kwenye kadhia ya mgao wa umeme.

Kuna hofu kubwa kwamba kama uhifadhi wa mito miwili inayotoa maji kwenye mradi wa kufua umeme hautazingatiwa mradi huu hautadumu. Kuwapo kwa kiwango kikubwa cha maji kwenye mito ya Ruvubhu na Kagera ndiko kulikopelekea ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme ambao utazisaidia nchi za Brundi, Rwanda na Tanzania kupata umeme wa uhakika 

RUSUMO AK 2
Ramani ya bonde la Rusumo inapokutana mito miwili inaathiri ujenzi wa kituo cha kufua umeme kwa nchi tatu.

Habari hii imechapishwa kwa usaidizi wa InfoNile na ufadhili kutoka IHE-Delft Water pamoja na Development Partnership Programme. Uhariri na taswira za data imefanywa na Annika McGinnis.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts