Ukame wachangiza ujangili wa Pundamilia wa Grevy Samburu Kaskazini, Kenya

Ukame wachangiza ujangili wa Pundamilia wa Grevy Samburu Kaskazini, Kenya

Lenah Bosibori

  • Pundamilia wa Grevy walio kaskazini mwa Kenya pekee, bado wako hatarini kutoweka, kulingana na Grevy’s Zebra Trust.
  • Uwindaji na ujangili umepunguza idadi yao kwa miaka miingi
  • Matokeo ya sensa ya Great Grevy ya 2016 yalionyesha kwa Kenya ilikua na pundamilia 2,350 wa Grevy, 90% ya ya idadi yao duniani
  • Makadirio ya hivi majuzi yanaonyesha kuwa ni 3,042 pekee walio hai, ikiwakilisha kupungua kwa 80% kwa idadi ya watu ulimwenguni.
  • Ukame ulioanza mwaka 2021 umeongeza umaskini na kusababisha ujangili zaidi.
  • Kati ya 2017 na 2022, washukiwa wengi wanaohusika na uhalifu wa wanyamapori dhidi ya pundamilia walikamatwa na nyama.
  • Uhalifu 14 unaohusisha pundamilia ulifuatiliwa ndani ya muda uliowekwa.

Mnamo mwezi wa Februari, mwaka huu pundamilia wawili  wa grevy moja ya wanyama ambao wapo hatarini kutoweka walikutwa wameuwawa kwenye eneo la Sarima lililopo kwenye hifadhi ya Nyiro  inayopakana na wilaya ya Masarbiti na ziwa Turkana, tukio amabalo lilizua sintofahamu miongoni mwa watunza mazingira Kaskazini mwa Kenya.

Joel Oronyo  anayefanya kazi   kwenye Taasisi ya Pundamilia wa Grevy  ijulikanayo kwa kimombo Grevy’s Zebra Trust Kaskazini mwa Samburu anasimulia kadhia nzima ilivyo kuwa na anasema; “ Tulipata taarifa za kutokea kwa ujangili eneo la Sarima kwenye Hifadhi ya Nyiro na tulichukua hatua haraka na kufika kwenye eneo hilo na kukuta pundamilia wawili wamejeruhiwa, mmoja akijruhia miguu na mwingine kwenye tumbo, hatuwa na la kufanya kwa jinsi walivyo kuwa wameruhiwa.”

Oronyo alikiagiza kikosi kazi chake kutoka huduma za wanyama pori ( Kenya Wildlife Services)  ambao walifika haraka eneo la tukio ili kuokoa maisha ya pundamilia hawa, ambao kutokana na majeraha makubwa waliyoyapata walifariki dunia.

Dida Fayo 1
Dida Fayo, kiongozi wa Northern Rangelands Trust (NRT) huko Samburu Kaskazini, akionyesha picha ya pundamilia aina ya Grevy aliyejeruhiwa huko Sarima Samburu Kaskazini na baadaye kufariki dunia kutokana na majeraha. Picha: Lenah Bosibori

Punda hawa ambao wanapatikana Kaskazini mwa nchi ya Kenya pekee wapo hatarini kutoweka, kwa mujibu wa Taasisi ya Punda wa grevy (Grevy’s Zebra Trust). Punda hawa ni wakipekee; ni warefu wakiwa na michirizi myembamba na upana mkubwa unaowafanya wapendeze.

Mwishoni mwa miaka ya 1970 pundamilia wa grevy wapatao 15000 walikuwa wanazunguka kwenye mapori duniani . Lakini ujangili na uwindaji ulipunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya punda hawa kadiri miaka inavyokwenda na mwaka 2016 sensa ya idadi ya punda hawa ilionyesha kuwa kulikuwa na punda 2,350 nchiuni Kenya ambao ni asilimia 90 ya punda wote duniani. Takwimu hizi zinapatika kwenye taarifa ya uhifadhi ya taasisi ya uhifadhi ya Pundamilia wa grevy (Grey’s Zebra Trust)

Makisio ya hivi karibuni yanaonyesha kuwepo kwa takribani punda 3,042 duniani kote ikionyesha kupungua kwa punda hawa kwa asilimia 80 na mnamo mwaka 2018 nchini Kenya pekee makisio yanaonyesha kuwepo kwa pundamilia hawa  2,812 ikiwa ni ongezeko dogo kwa mujibu wa idadi ya punda hao ya mwaka 2016 na nchi Ethiopia pundamilia hawa wapo 230.

Taasisi ya Pundamilia wa Grevy (Grevy Zebra Trust)

Kutokana na wingi wa majangili ambao wamejidhatiti kwa kumiliki silaha  ikilinganishwa na idadi ya askari wa wanyama pori kutoka taasisi ya huduma za wanyama pori ya Kenya, askari hawa walishindwa kuwafikisha majangili hawa kwenye vyombo sheria mnamo mwezi wa Februari.

Oronyo anasema: “Tulipoanza kuwasaka majangili hawa tuliwakuta wakila nyama, hii ikiwa na maana kwamba tayari walikuwa wameua punda na kwa kuwa tulikuwa wachache ilibidi turudi nyuma ili kuepusha tafrani. Tukio hili halikuwa zuri kwetu kwani tulisikitishwa sana kuona wanyama wanauwawa kwenye maeneo haya ambayo kuyafikia ni vigumu hasa wakati huu wa ukame wakati wanyama wanahama wakitafuta malisho na maji.”

Umaskini unasababisha ujangili

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Punda wa grevy  Julius Leknit anasema ukame ulioanza mwaka 2021 umezidisha umaskini miongoni mwa wakazi na hivyo kupelekea kuwapo na ujangili ambapo wenyeji wanaua punda wa grevy ili kujikimu hususan wakati wa ukame ambao kila moja anatafuta rasilimali muhimu ambazo ni malisho ya mifugo na maji.

Samburu women 1
Athari za ukame zinawalazimu wanawake katika eneo la Samburu Kaskazini kusimama juani wakisubiri Wasamari wema wawape chakula. Picha: Lenah Bosibori
Water shortage 1
Ardhi tambarare inayoonyesha athari za ukame wa muda mrefu katika eneo la hifadhi ya Samburu Kaskazini Nyiro. Picha: Lenah Bosibori

Leknit anasema Taasisi ya Punda wa grevy inashirikiana na jamii kaskazini mwa Kenya katika kuwahifadhi punda hawa ili idadi yao iongezeke.

Taasisi hiyo imeajiri maskauti 29 kutoka jamii mbalimbali zilizopo ili kufuatilia pundamilia hawa na kuongeza muamko kwa kulinda viumbe hai. Pia imeundwa timu ya wanamgambo kumi ambayo kazi yake itakuwa kulinda kiasi cha pundamilia 200 na kuamsha ari ya kuhifadhi na kulinda viumbe hai.

Kuchangamana kwa vijana hawa na jamii iliyopo kumesababisha kuwapo na mtandao mpana wa jamii ambao unasaidia kupeleka ujumbe wa uhifadhi na hivyo kuongezeka kwa shughuli za uhifadhi.

Suala la migogoro kati ya wanyama pori na binadamu limekithiri  kwenye eneo la  Kaskazini mwa Kenya na kusababisha matatizo kwa pundamilia wa grevy ambao ni moja ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka duniani.

Grevy Zebra Trust

Afrika, pundamilia wa grevy ni moja ya wanyama wakubwa walioko kwenye hatari kutoweka na Pundamilia hwa wameorodheshwa na IUCN/SSC kwenye kundi la viumbe ambavyo vipo hatarini kutoweka na pia kuorodheshwa CITES kwenye orodha ya viumbe vinavyotakiwa kulindwa dhidi ya biashara haramu ya viumbe hai. Marufuku ya kuwinda pundamilia hawa imewekwa kisheria nchini Ethiopia na kwa Kenya ni marufuku kuwinda wanyama hawa tangu  1977.

Justus Lesanjore Mratibu Msaidizi wa hifadhi kwenye kaunti ya Samburu anasema, tukio la ujangili lililofanyika mwezi February 1977lilitokana kutoweka kwa mlinzi pekee wa hifadhi hiyo ambaye msaidizi wake alishindwa kuhimili sakata  hilo.

“ Kulikuwa na upungufu kwenye eneo la Sarima, askari wa wanyapori mmoja tu aliyekuwa kwenye eneo la aliondoka bila taarifa akiacha eneo hilo bila ulinzi, hata hivyo tumefanikiwa kuajiri mlinzi mwingine,” anasema bwana Lesanjore

Kwa mujibu wa Mohamed Salat ambaye ni askari wa wanyama pori mwandamizi kwenye kata ya HorrNyiro anasema tukio hilo liliwakera kwa kiasi kikubwa.

“ Tulitamani kuingia uvunguni mwa vitanda wakati tunawaangalia. Majangili tumewapata lakini uwezo wa kuwakamata tulikuwa hatuna kwa sababu walikuwa wengi na kuna wakati tunajikuta katika hali ambayo inatufanya tusiwe na la kufanya,”Anasema Salat

Salat anabainisha kuwa ujangili wa wanyamapori ni wa hapa na pale na hutegemea mazingira fulani.

Adhabu kali kwa wahalifu

“Wakati wa ukame wa 2021, tulikuwa na wanyama watano waliofanyiwa ujangili na jamii ya wenyeji kwa ajili ya nyama yao, lakini safari hii hatuna idadi halisi ambayo imepotea kwa uhalifu huu wa kutisha kutokana na kipindi cha ukame wa muda mrefu ikilinganishwa na 2021 ,” anasema Lesanjore, Mratibu Msaidizi wa wa hifadhi katika Kaunti ya Samburu.

Kati ya 2017 na 2022, washukiwa wengi wanaojihusisha na ujangili wa wanyamapori hususan  pundamilia walikamatwa wakiwa na nyama, kwa mujibu wa data za #WildEye Afrika Mashariki ((Kampuni Utalii wa kupiga picha iliyopo nchini Kenya)  iliyokusanywa na InfoNile kwa ushirikiano na Oxpeckers Investigative Environmental Journalism( Taasisi ya habari za uchunguzi za kimazingira). Matukio 14 ya  Uhalifu  unaohusisha pundamilia ulifuatiliwa ndani ya muda uliowekwa

Marekebisho ya Sheria ya Wanyamapori ya 2013 ambayo yalipitishwa mwaka 2018, ambayo kwa sasa yanafanyiwa mapitio, yanabainisha adhabu mpya kwa uwindaji wa nyama pori. Kama ifuatavyo”Kuwashughulikia (wauzaji, wasambazaji, wanunuaji,wasafirisha na wamiliki wa  mzoga au nyama ya aina yoyote ya wanyamapori”  kifungo chake miaka 3 bila chaguo la kulipa faini.

Ununuzi wa nyama au mayai yoyote ya aina yoyote ya wanyamapori kutozwa faini ya hadi shilingi za Kenya milioni 1 au kifungo cha jela cha miezi 12, au adhabu zote mbili; hata hivyo, Hakimu ana mamlaka ya kujumuisha adhabu zote mbili au moja. Adhabu ni sawa na Sheria ya awali ya Usimamizi wa Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 1976, ambapo mtu aliyepatikana na hatia ya kuwinda mnyama yeyote katika hifadhi ya taifa alitozwa faini ya kuanzia shilingi 5000 za Kenya (karibu dola za Marekani 58) hadi shilingi 20,000 (karibu dola za Marekani 176), na /au kifungo cha kuanzia miezi sita hadi miaka mitatu, ambacho kinaweza kujumuisha adhabu ya viboko.

Kanzidata  iliyofuatiliwa kwenye  tovuti ya WildEye Afrika Mashariki inaonyesha kuwa kati ya 2017 na 2021, hukumu ya juu zaidi iliyotolewa kwa mtu yeyote aliyehusika katika uhalifu dhidi ya pundamilia ilikuwa kifungo cha miaka 11 jela  au faini ya shilingi za Kenya  sh. 2.2 milioni (karibu dola za Marekani 19,396.33). Katika kesi hiyo, mtuhumiwa alipatikana na hatia ya makosa matatu kinyume na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2013. Haya ni pamoja na kuua wanyamapori kinyume cha sheria, kukutwa na nyama ya wanyamapori kinyume cha sheria na kumiliki nyara kinyume cha sheria.

Kinyume chake, hukumu ya chini kabisa iliyotolewa kwa mshukiwa yeyote aliyehusika katika uhalifu wa pundamilia wakati huo huo ilikuwa faini ya shilingi za Kenya . 20,000 (karibu dola 176 za Marekani) au kifungo cha miezi mitano kwa kupatikana na hatia ya kumiliki nyara kinyume cha sheria ya wanyamapori kinyume na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2013.

Hifadhi za kulinda bayoanuwai kaskazini mwa Kenya

Kwa mujibu wa Leknit, Samburu Kaskazini ni mandhari nzuri sana, ikilinganishwa kipekee  na mbuga ya wanyama ya Maasai Mara ambayo ni  mbuga maarufu Duniani inayopatikana kwenye  uwanda wa kusini mashariki mwa Kenya.

Ilianzishwa mwaka wa 2013 na serikali ya kaunti ya Samburu, hifadhi ya Nyiro ni mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi katika kaunti hiyo kubwa, huku maskauti 52 wakilinda bayoanuwai ya jamii hiyo.

“Tulianzisha uhifadhi huu kwa sababu tuligundua kuwa Hifadhi ya Kitaifa ya Samburu ndiyo chanzo pekee cha mapato kwa jamii. Tulitaka jamii kumiliki na kulinda maliasili zao,” anasema Lesanjore.

Mashirika ya Hifadhi ya  majimbo yalitoa  fursa ya kupata kazi, huduma bora kwa maendeleo ya jamii na fursa zaidi za biashara kama vile uanzishwaji wa kampuni ya  Northern Rangelands Trust Trading, ambayo ni kichocheo cha biashara kwa makampuni ya kijamii na ya uhifadhi.

Hata hivyo, ukame umeongeza umaskini hata kwenye maeneo ya hifadhi, hivyo kusababisha kuongezeka kwa ujangili.

“Watu wanaozunguka eneo hili wana njaa; hata kama tukianza kuwalisha hatuwezi kuwadhibiti wote; tuna rasilimali chache, na ndio sababu inayowafanya wanaua pundamilia,” Lesanjore anaongeza.

Tukio la ujangili la Februari lilisababisha mkutano wa mashauriano mnamo Machi 24 huko Samburu,  kujadili jinsi wadau wanavyoweza kushirikiana kupunguza kesi za ujangili.

Mkutano huo uliwaleta pamoja maafisa kutoka Northern Rangelands Trust (NRT), Taasisi ya Pundamilia wa grevy (Grevy’s Zebra Trust), waratibu wa uhifadhi, KWS, Kaunti ya Samburu na walinzi wa jamii ili kuchunguza njia bunifu za kuimarisha ulinzi wa pundamilia wa grevy.

meeting 1
Kudumisha ushiriki wa jamii zinazozunguka kumekuwa muhimu katika kulinda wanyamapori na mandhari ya kaskazini mwa Kenya. Picha: Lenah Bosibori

Northern Rangelands Trust ni shirika la uhifadhi ambalo huleta pamoja hifadhi 43 za jamii katika kaunti 10, nyingi zikiwa kutoka sehemu za kaskazini na pwani ya Kenya.

Kaunti hizo ni Samburu, Isiolo, Marsabit, Laikipia, Meru, Lamu, Pokot Magharibi, Baringo, Tana River na Garissa.

Shirika linatoa msaada wa kiufundi, kusaidizi wa uchangishaji fedha, huduma za ujenzi wa amani, na maendeleo ya hifadhi za jamii, ambazo ziko katika nafasi nzuri zaidi ya kuimarisha maisha ya watu wa eneo hilo na kuhifadhi mazingira asilia.

“NRT ilikuja kusaidia maeneo matano mapya ya hifadhi ambayo yanajumuisha maeneo ya uhifadhi ya Baragoi, Nyiro, Ltungai-Malaso, Ndoto na Kirisia-Nkoteiya yaliyoundwa na serikali ya kaunti ya Samburu,” asema Dida Fayo, kiongozi wa NRT Samburu Kaskazini.

Hifadhi hizo zilianzishwa mwaka wa 2013 na serikali ya kaunti ya Samburu ili kuboresha maisha ya jamii na kuimarisha ulinzi wa mazingira pamoja na mipango ya usalama.

Uhifadhi wa wanyamapori  unafanyika kwenye ardhi inayosimamiwa na mmiliki mmoja mmoja, ushirika wa  wamiliki, au jumuiya kwa madhumuni ya uhifadhi wa wanyamapori na matumizi mengine ya ardhi yanayofanya maisha  bora. Shirik limesaidia jamii kulinda bayoanuwai yao huku wakipokea mapato kutokanakodi ya ardhi na utalii.

“Samburu Kaskazini kwa miongo kadhaa imekuwa ikikabiliana na ujangili, migogoro inayotokana na  rasilimali, migogoro ambayo  imeongezeka   kutokana mabadiliko ya hali ya hewa,” anasema Fayo.

“Kama kuna mzozo kati ya binadamu basi moja kwa moja inatafsiriwa kuwa ni mzozo wa wanyamapori na binadamu. Ikiwa sisi wanadamu hatuna amani kati yetu basi hatuwezi kutarajia tuwe na amani na wanyamapori,” anaongeza Fayo.

Ukame na kuongezeka kwa migogoro ya binadamu na wanyamapori

Wadau wamebaini kuwa ujangili unachagizwa  na ukosefu wa taarifa na ujuzi kuhusu wanyamapori na manufaa ya wanyamarpiri miongoni mwa wanajamii wakati huo, ukame umebainika kuwa chanzo kikuu cha migogoro ya wanyamapori.

Mifugo imeendelea kuhama kutoka katika makazi ya wafugaji kutokana na kupungua kwa maji na chakula, kulikosababishwa na ukame. Hali hiyo imepelekea migogoro miongoni mwa jamii.

-Mtandao unaotoa angalizo kuhusu ukame nchini Kenya (KFEWS),
IMG 5119 2 2
Kijiji kilichokumbwa na ukame huko Samburu. Picha: Lenah Bosibori

Mnamo Septemba 8th, 2021  Rais Uhuru Kenyata alithibitisha kuwa ukame umeathiri sehemu kubwa ya nchi na kutamka rasmi kuwa hilo ni janga. Alisema,maeneo yaliyoathirika zaidi ni Ukanda wa  pwani, Bonde la ufa, Mashariki na Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Ukame uliathiri zaidi mifugo ya nyumbani na wanyamapori. Kutokana na baa la njaa, magonjwa, kuzorota kwa afya za wanyama kumesababisha vifo vya wanyama wafugwao katika maeneo ya kaunti za wafugaji.

Kwa mfano, eneo la Marsabit, asilimia 9 ya mifugo ilikufa kutokana na ukame wa mwaka 2021.

Camel 2 1
Ngamia anayekufa njaa kwa ukame mkali. Wafugaji wamepoteza mifugo yao mingi. Picha: Lenah Bosibori

Akihutubia kamati ya bunge ya fedha, Katib Mkuu wa Bunge, Maliasili na Utalii, Najib Balala, alisema Kenya imepoteza tembo 62 kutokana na ukame katika miezi ya Agosti na Desemba, 2021.

Idadi ya pundamilia kadhalika imeathirika. Kwa mujibu wa WildEye East Africa, mnamo Aprili, 2021, mamlaka zinazosimamia usalama eneo la Kajiado waliwakama watu wawili, David Musyimi na Mwendo Mumba wakiwa na nyama ya pundamilia na dikidiki. Watuhumiwa hao pia walikamatwa na visu viwili na panga vilivyotumika katika ujangili huo na kuachiliwa baada ya kulipa faini ya Ksh 300,000(USD 2596) pamoja na kiwango cha mdhamini..

Kupotea kwa mifugo, kushuka kwa kiwango cha maziwa na kushuka kwa biashara ya mbadilishano wa mbuzi kwa mahidi, miongoni mwa watu wa jamii ya wafugaji ya Kaskazini na mashariki, kumesababisha migogoro katika kaya (IPC Phase 3) na dharura (IPC Phase 4). Licha ya kiasi cha asilimia 11 cha Fedha zilizotolewa kwa ajili ya kupambana na ukame Kenya, mwaka 2021, misaada ya ziada inahitajika ili kusaidia watu wa jamii ya wafugaji wakati huu ambapo kunatarajiwa mvua za muda mrefu kati ya Machi na Mei mwaka huu.

Kwa kuongezea, idadi ya polisi wanaosimamia ulinzi wa wanyamapori na vijana wa skauti, katika maeneo yale ni ndogo na kipindi ambacho ukame hujitokeza, wanyama hujikuta mikononi mwa wakulima na wafugaji pindi wanaposaka maji na chakula.

Hifadhi ya Melako, iliyo Kaskazini mwa Kenya yenye ukubwa wa (546,777ha) ni miongoni mwa hifadhi kubwa zaidi Kenya ukilinganisha na ile ya Laikipia au maarufu kama Ol Ari Nyiro yenye kilometa za square, 365.

KWS inafanya jitihada ya kuchimba visima vya muda kwa ajili ya wanyama kupata maji, kadhalika kambi za KWS  katika maeneo ya Kawap, zinaendelea kutoa elimu ya ushirikishwaji zaidi wa wadau, kutoa kozi fupi za kuwaleta walinzi na kuimarisha doria katika maeneo hayo.

Habari hii ilitayarishwa na ufadhili wa InfoNile, kwa ushirikiano na Oxpeckers Investigative Environmental Journalism, kwa ufadhili wa Earth Journalism Network. Imeripotiwa zaidi na kuhaririwa na Sharon Atieno na Annika McGinnis kutoka InfoNile. Taswira ya data na Sharon Atieno. Uchunguzi huu pia ulichapishwa na TalkAfrica na kwenye Oxpeckers.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts