Na Javier Silas Omagor
Mamia ya watu wanapambana na upungufu mkubwa wa maji safi na salama katika vijiji vya Bunambutye ambavyo ni makazi mapya ya wahanga wa maporomoko ya maji, huku kwa upande mwingine wakipambana na janga la Corona.
Kaya takribani 140 zilizoathirika katika Awamu ya II zilihamishiwa kutoka Bududa na kupelekwa makazi ya Bunambutye wilaya ya Bulambuli.
Kama serikali zingine duniani, Uganda imewataka wananchi kujitahidi kuosha mikono vizuri kama sehemu ya juhudi za kujikinga na virusi hatari vya Corona.
Serikali nyingi za mtaa nchini Uganda ikiwa ni pamoja nay a Bulambuli (ambayo ina wahanga wa maporomoko ya Mlima Elgon) pia inajitahidi kuhakikisha kwamba inawahamasisha wakazi wa eneo hilo kunawa mikono
Lakini hili ni swala ambalo ni kama haliwezekani kwa Wakazi wa Awamu ya II wa Bunumbutye ambao wapo katika mahitaji makubwa na imewabidi hata kutegemea chemchem na mabwawa ya maji ya karibu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
“Hatuna visima wala mabomba ya maji chanzo pekee cha maji cha karibu ni mito midogo midogo na mabwawa. Vyanzo vingine vinahitaji kutembea umbali wa si chini ya kilometa 2 mbali na kuomba maji kwa wahanga wengine wa Awamu ya I walioletwa hapa,” alisema Tom Wabuna, mmoja wa wakazi wa kambi ya wahanga.
Kila nyumba ikiwa imekaa ndani ya hekari moja ya ardhi na kila familia ikiwa na uwezo wa kufanya kilimo katika ardhi waliyopewa na serikali, wahanga wa maporomoko wanasema baada ya kuwa wamemaliza shughuli zao za shamba huwa wamechoka sana na kukosa nguvu za kwenda kutafuta maji katika makazi ya wahanga wa Awamu ya I.
Tofauti na Awamu ya II, kila kaya katika makazi ya Awamu ya II ina eneo maalum la kuchotea maji karibu na nyumbani kwao.
Sarah Nekesa, anasema kwasababu ya changamoto za kiuchumi zitokanazo na Corona, baadhi ya wakaazi wa Awamu ya I wamelazimika kuanza kuwatoza malipo ya kuchota maji.
Nekesa anakiri kwamba kutokana na uhaba wa maji safi na salama, familia zao zinashindwa kuosha mikono yao ipasavyo kujikinga na maradhi ya Corona.
“Kabla ya katazo la kutembea kutokana na Corona, wengi wetu tuliweza kutoka soko moja kwenda lingine tukiuza bidhaa zetu ikiwa ni pamoja na kuku na mayai, mifugo na zingenezo ili kujipatia kipato.” alisema Nekesa.
Lakini sasa kwasababu hawawezi kutoka kwenye makazi yao, wahanga wa maporomoko ya ardhi wanasema kwasasa wana shida ya pesa na msongo wa mawazo.
Grace Nabutuwa ambaye alipoteza watoto wake wote 9 katika maporomoko ya ardhi huko Bududa anasema kwa sasa wanahofia maisha yao kwasababu si maji pekee waliyo na shida nayo, lakini chakula na uwezekano wa kunawa mikono yao ni tatizo kubwa pia.
“Ugonjwa huu ukifika katika kambi yetu utatuua wote kwasababu hatuna kinga yoyote ile,” alisema Nabutuwa katika mahojiano
Moses Wambede, baba wa watoto 4 aliyepoteza watoto wawili na mkewe katika maporomoko ya ardhi anasema wamebaki masikini kiasi cha kukosa hata uwezo wa kununua sabuni ya kunawa mikono, vitakasa mikono na barakoa kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona katika kambi yao.
Hata kama Rais amekuwa akiwahamasisha Waganda kuzingatia unawaji mikono na sabuni kama njia moja wapo rahisi na isiyo ya gharama ya kujikinga na Corona, wakazi wa kambi ya Bunambutye wanasema hawawezi kumudu hilo pia
Peter Pex Paak, Mkuu wa Wilaya Mkazi wa Bulambuli, akizungumza katika mahojiano maalum amekubali kwamba ukosekanaji wa maji unakuwa tatizo kubwa katika kambi hiyo, hasa kwa wakazi wa Awamu ya II.
“Ni kweli, kama mtu binafsi, nawahurumia watu waishio eneo hilo hasa watoto na wanawake ambao ndio wanapata adha kubwa zaidi,” alisema Mkuu wa Mkoa Paak
Paak alielezea kwamba muda si mrefu ofisi yake itaikumbusha ofisi ya Waziri Mkuu, wizara husika na taasisi zingine kuchukua hatua za haraka kwa namna bora iwezekanavyo kuwasaidia waathirika wa uhaba wa maji.
Kwasasa, Paak aliwatia moyo wakati wa Awamu ya II kuchota maji kutoka kwa majirani zao wa Awamu ya I kutoka vyambo mbalimbali walivyonavyo.
Hata kama vyanzo hivyo vya maji vimekuwa vikitumika kwa miaka mingi, ongezeko la idadi ya watu lililopelekea kuharibika kwa mazingira ndani ya eneo la Elgon limeviharibu vyanzo hivi vya maji
Mikondo na mito ya maji vimebeba maji machafu hata kama ndio vyanzo pekee vya maji vinavyotegemewa na jamii hizi.
Kama hiyo haitoshi, katika jamii za jirani kama vile Tajar, kitongoji cha Kolir ndani ya wilaya ya Bukedea, ukosefu wa maji safi na salama ni wa hali ya juu.
Wanajamii wa eneo hilo, hasa wanawake na watoto walionekana na mwandishi huyu wakichota maji katika mikondo ambayo haikuwa mizuri kwa matumizi ya binadamu.
“Hichi ndicho chanzo pekee tulichonacho na tunahitaji kupika, kuosha vyombo/ kufua na zaidi ya yote kufuata ushauri wa Rais wa kunawa mikono.” Julia Asekenya, alisema mkazi wa hapo
Wakati wa mahojiano haya, kama ilivyo kwa wakazi wengine, Asekenya alikuwa anachota maji kutoka Mto Sirono ambao upo katikati ya wilaya za Bulambuli na Bukedea
Pius Okello, Okello mwingine na mkazi mwingine wa Tajar anasema jamii yake ya watu zaidi ya 600 inategemea kisima kimoja ambacho nyakati zingine kinatoa maji ya rangi ya ugolo yakiwa na minyoo.
“Nadhani watoto ndio mara zote huwa waathirika wakubwa wa maji haya machafu kwasababu hawachui tahadhari kabla ya kunywa maji haya,” anaelezea Okello
Jamii hii imetegemea maji kutoka kisima hicho kimoja kwa zaidi ya miongo 3 lakini kuongezeka kwa idadi ya watu na mabadiliko ya hali ya hewa yamefanya kisima hicho kisiwe cha kutegemewa tena.
Vijiji hivi ni ishara kwamba upatikanaji wa maji safi kwa jamii za vijijni nchini Uganda bado ni tatizo kubwa japokuwa chini ya Mpango wa II Taifa wa Maendeleo (National Development Plan II (NDP II)) serikali ya Uganda imeahidi kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijijini kutoka 65% mwaka 2012/13 hadi 79% kufikia mwaka 2019/20.
Kwa mujibu wa Ms. Rose Nakabungo Kamishna Msaidizi wa Kikosi cha Kuzuia na Kudhibiti Majanga katika Ofisi ya Waziri Mkuu, msuala yahusuyo usafi katika kambi yanasikitisha lakini yanapangwa kutatuliwa haraka iwezekanavyo.
“Ndio maana vyombo vya habari ni vya muhimu sana, sisi hatuwezi kuwepo kila mahali lakini vyombo vya habari vipo na mara zote hutuletea taarifa kama hizi. Tutaongeza juhudi katika kuhakikisha kwamba jamii za wahanga wa Awamu ya II wanatatuliwa shida yao ya maji haraka iwezekanavyo,” Nakabungo told the New Vision.
Historia
Ikumbukwe kwamba March 2010, maporomoko ya ardhi ya kijiji cha Nametsi, Wilaya ya Bududa, ambayo yalikuwa makubwa kuwahi kutokea nchini Uganda, yalipelekea vifo vya takribani watu 100, zaidi ya watu 300 kupotea na wengine 85 makazi yao kuharibiwa kijijini hapo Nametsi.
Baadae maporomoko ya mwaka 2018 yalisababisha vifo vya takribani watu 60, huku watu wengine 400 wakipotea na mali zao za bilioni za shilingi kuharibiwa na udongo. Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda lilikisia kwamba kutokana na maporomoko hayo watu takribani 12,000 waliathirika maeneo ya Bukalasi na Buwali mjini Bududa.
Mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha mvua zisizo za kawaida hivi karibuni ambazo zinasababisha maporomoko haya, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Uganda.
Maporomoko mengi ya ardhi yanatokea sehemu za maporomoko ambapo maji hujaa. Miteremko ya masharikikaskazini ndio ambayo hukumbwa na maporomoko mengi ya ardhi ambayo hufuatana na uelekeo wa mvua.
Jitihada za Kijamii
Jamii hii ya Awamu ya II ya kambi ya Bunambutye haikai tu ikisubiria msaada kutoka serikalini na washirika wa maendeleo; wahanga hawa wana maporomoko ya ardhi wanajaribu kujitatulia matatizo yao
Watu wazima na watoto katika kambi ya wahanga wanavumbua mbinu za kutatua changamoto zote zinazowakabili, za muda mfupi na muda mrefu
Kwamfano, kikundi cha watoto 110 waishio katika kambi hiyo wamezindua kampeni waliyoipa jina la ‘sahau ya nyuma kwa kupanda mti’.
Kampeni hii iliyoanzishwa na kusimamiwa na vijana wadogo waliopo kambini hapo, inatarajiwa kuchochea ari ya utunzaji wa mazingira kwa vizazi vijavyo vya wale walioathirika na maporomoko ya arhdi ya Mlima Elgon.
Walipoulizwa kwanini waliamua kuanza kupanda miti katika umri mdogo kiasi hicho, James Wakholi, kiongozi kijana wa harakati za utunzaji mazingira hapo kambi ya Bunambutye alisema ilikuwa ni hatua muhimu kuwasaidia kuepuka mauwaji makubwa ya janga la asili ambayo tayari yameuwa ndugu zao.
“Wengi wetu tumepoteza wazazi, marafiki, waalimu na ndugu na njia bora zaidi kwetu kusahau hayo ni kwa kuzuia yasitokee tena.” Alisema Wakholi huku akimuonyesha mwandishi wetu miti ambayo tayari wamekwisha panda tayari.
Vijana hao wadogo wanapnda miti katika eneo la heka moja lililotolewa kwa kila familia na serikali katika kambi hiyo lakini pia ndani na kuzunguka nyumba za wazazi wao.
“Changamoto yetu sisi ni ardhi; kama tungekuwa na ardhi ya kutoshaa hapa, tungeweza kupanda miti mingi zaidi yah ii,” anasema Ever Namataka mwenye umri wa miaka 13.
Vijana hao wa kambi ya Bunambutye tayari wamepanda miti takribani 200 ya aina mbalimbali katika eneo lao kuepuka historia ya kusikitisha ya maisha yao ya nyuma.
Changamoto nyingine ambayo vijana hawa waliizungumzia ni ile ile ya ukosefu wa maji ya kutosha ambayo ni ya muhimu katika kupanda miti yao.
Akisisitiza swala hili, Namataka alisema; “Miti inanyauka na kufa kwasababu vijana wenzetu wote wanaoishi katika kambi ya Awamu ya II hawana maji ya kutosha.”
Wasemavyo Mamlaka
Idara ya Misitu ya Wilaya iliyotoa miti hiyo kwa vijana hao inasema inatarajia kupitia mradi huu wa utaongeza eneo la msitu kutoka takribani 40.6% hadi angalau 55.9% ndani ya miaka 10 ijayo
Wizara ya Maji na Mazingira, ambayo ni taasisi inayoongoza katika upatikanaji wa huduma bora za maji na mazingira salama, imefurahishwa na jitihada hii.
Beatrice Anywar, Waziri wa Mazingira amepongeza jitihada za watoto hawa kutoka katika kambi ya Bunambutye.
“Kwa mazingira waliyonayo, wamefanya kazi kubwa sana. Kama waziri na mwanaharakati wa mazingira pia mimi mwenyewe, nafurahi kuona kwamba watoto hawa wanafanya mambo makubwa hasa kwasababu wao wenyewe wamekuwa wahanga wa shughuli mbaya za kibinadamu ambazo zilipelekea uharibifu wa mazingira Bududa,” alisema Anywar
Kwa mujibu wa Anywar, kuwa na wanaharakati wa mazingira watoto katika maeneo ya vijijini nchini kote Uganda na Afrika kwa ujumla kutasaidia sana katika jitihada za uhifadhi.
Kama ilivyo kwa waziri Anywar, Mkuu wa Wilaya wa Bulambuli Paak pia amefurahishwa na jitihada za watoto hawa za utunzaji wa mazingira katika kambi ya maporomoko ya ardhi akisema kwamba baadhi ya majirani wa maeneo hayo wameanza kuiga mfano kutoka kwa watoto hao”
Waziri wa mazingira anasema mara nyingi, maeneo yenye misitu ya kutosha huwa na maji safi na salama kwa wingi.
Aliahidi pia kuhimiza upelekwaji wa maji katika kambi ya wahanga wa Awamu ya II.
Katika hatua nyingine, kwasababu ya ukosekanaji wa maji safi na salama ya kunawa mikono, baadhi ya wazazi wameamua kuuza pombe ya kienyeji ijulikanayo kama waragi, ambayo baadae wanaitumia kama kitakasa mikono (sanitizer)
“Baadhi yetu tulipanda mihogo ambayo kwasasa tunaitumia kutengeneza pombe ya kienyeji,” alisema Zachariah Matubondo, ambaye mke wake wa kwanza na watoto 5 wote walikufa katika maporomoko ya ardhi ya mwaka 2018 ya wilaya ya Bududa.
“Tatizo la waragi hii ni kwamba watoto wanaiba na kunywa,” Matubondo alimwambia mwandishi wa habari hii
Patience Baganzi, Kamanda wa Wilaya ya Bulambuli aliona kwamba matumizi ya waragi kama vitakasa mikono katika jamiii imechangia ongezeko la unyanyasaji wa majumbani na kuvunjwa kwa haki za watoto kwasababu watu wamekuwa wakinywa kwa kiwango cha kupitiliza wakati wote wa siku.
Wilaya ya Bulambuli imepokea kesi 20 za watoto waliodharirishwa na ukatili wa majumbani ndani ya mwezi Aprili, ongezeko la asilimia 80 kutoka kesi za siku za nyuma za kawaida kitu ambacho Polisi wanalihusisha na utengenezwaji na unywaji wa waragi wa kupindukia katika mapamba dhidi ya Corona katika eneo hilo
Habari hii ya InfoNile ilidhaminiwa na Code for Africa ikipata fedha kutoka Pulitzer Centre na National Geographic Society.