Na Grace Mwakalinga, MBARALI MBEYA
Wananchi wa vijiji vya Madundasi na Iyala vilivyopo kata ya Luhanga wilayani Mbarali mkoani Mbeya nchini Tanzania wamekuwa na changamoto ya uhaba wa vyazo vya maji kwa muda mrefu ambapo wanakwenda kwenye mto ambao upo mbali na makazi yao.
Hata hivyo uwepo wa changamoto ya upatikanaji maji ya uhakika inaweza kuwa kikwazo kwa jamii ya vijiji hivi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ya kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka katika kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona kwa sababu wananchi wengi wanaweza kuwa na maji machache kwa matumizi mengine kama kupikia chakula pamoja na kunywa pekee.
Uchunguzi uliofanywa na Bomba fm radio Mbeya kwa kushirikiana na taasisi za InfoNile na Code for Afrika umebaini kuwa wananchi wa vijiji vya Madundasi na Iyala wamekuwa wakitumia maji ya mito ambayo hutumiwa pia na mifugo hali ambayo husababisha baadhi yao kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Kwa mujibu wa Utafiti uliofanywa na taasisi ya TWAWEZA na UWEZO nchini Tanzania mwaka 2017, umeonesha kuwa zaidi ya nusu ya wananchi (54%) wameripoti kutumia vyanzo vya maji vilivyoboreshwa kupata maji ya kunywa huku kukiwa na utofauti mkubwa kati ya kaya za mjini (74%) na vijijini (46%) kwenye utumiaji wa vyanzo vya maji vilivyoboreshwa.
Wakizungumza na Bomba Fm radio wananchi wa vijiji hivi wamesema katika msimu wa masika walikuwa na unafuu wa kutenga ndoo ya maji kwa ajili ya kunawa lakini shida kubwa huanzia mwezi wa saba hadi wa kumi ambapo hawatakuwa na uhakika maji ya kutosha kutokana na kutokuwa na mito ambayo inatiririsha maji kwa mwaka mzima na hivyo hukauka.
Aidha wamesema kutokana na changamoto hiyo hulazimika kununua maji yanayosafirishwa kutoka vijiji vingine, zaidi ya kilometa 10 ambayo huletwa na vijana ambao wamejiajiri kuendesha pikipiki na kueleza kuwa itakuwa vigumu kutenga maji kwa ajili ya kunawa ili kujikinga na virusi vya Corona.
Nao viongozi wa vijiji hivi wamekiri kuwepo kwa tatizo la uhaba wa maji na kwamba tayari wameshazifikisha changamoto hizo kwenye halmshauri ya wilaya ya Mbarali kwa ajili ya kufanyiwa kazi ambapo mpaka sasa bado hakuna kilichofanyika huku wakiwaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuwasaidia wananchi wao.
Katika kukabiliana na changamoto za maji vijijini, serikali ya Tanzania ilianzisha wakala wa usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira vijijini yaani(Rural Water Supply and Sanitation Agency – RUWASA), ambapo baadhi ya majukumu ya wakala huu ni kusanifu na kusimamia ujenzi wa miradi ya maji vijijini,kufanya utafiti kuhusu maji chini ya ardhi pamoja na kuchimba visima.
Mhandisi Job Mwakasala ni meneja wa usambazaji maji na usafi wa mazingira wilayani Mbarali amesema wanafahamu uwepo wa tatizo la maji katika vijiji hivyo na kwamba hatua zilizowahi kuchukuliwa awali ilikuwa ni kusanifu mradi wa maji wa Luhanga – Mpolo mwaka 2010 ambapo baadae ulisimama kutokana na changamoto za kifedha na kwamba kwa sasa wataanza upya kuutengeneza mradi huo ili kuhakikisha wananchi wa vijiji vya Madundasi na Iyala wanapata maji.
Aidha amewataka wananchi wa vijiji hivi kuuchukulia ugonjwa wa Covid-19 kama dharura au vita hivyo katika kipindi hiki waendelee kutumia mbinu mbadala za kuhakikisha wanapata maji ya kunawa ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona wakati jitihada za kupeleka huduma ya maji zikiendelea.
Pamoja na changamoto hizi za upatikanaji wa maji, idara ya afya wilayani Mbarali kupitia kwa mganga mkuu wa wilaya hiyo Dokta Godfrey Mwakalila amewahimiza wananchi wa vijiji hivi kuendelea kunawa mara kwa mara kwa tiririka na sabuni kwa kupitia vyanzo mbalimbali vya maji wanavyotumia katika maeneo yao na kwamba wanaendelea kutoa elimu juu ya ugonjwa huo.
Aidha mganga mkuu amewaeleza wananchi kuwa hata kama usalama wa maji yanayopatikana katika vyanzo vyao ni mdogo, waendelee kuyatumia kunawa kwani kinachohitajika ni povu ambalo watanawa na sabuni ambalo litaua vimelea vyoyvyote vilivyopo kwenye mikono.Hata hivyo wizara ya maji nchini Tanzania kupitia hotuba ya wizara iliyowasilishwa bungeni na waziri mwenye dhamana Prof. Makame Mbarawa alisema serikali ina lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini unafikia asilimia 85 mwaka 2020 na kwamba katika kufikia lengo hilo Wizara imepanga kutekeleza miradi itakayoongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa haraka na pia kutekeleza miradi kwenye maeneo yenye uhaba mkubwa zaidi wa maji. Pia amesema dira ya Taifa ya Maendeleo inalenga kuboresha huduma za maji vijijini kufikia asilimia 95 ifikapo Mwaka 2025.