Na George Achia
Rose Okeyo mwenye umri wa miaka 38, alikuwa tayari anatatizika kupata maji ya kutosha kwa matumizi yake ya nyumbani katika kipindi cha kutotoka nje kufuatia janga la COVID-19, wakati ruzuku ya maji ilipobomolewa na maporomoko wa ardhi karibu na nyumbani kwake katika kitongoji duni cha Kawangware, mjini Nairobi.
Mvua nyingi iliyonyesha msimu wa kati ya miezi ya Machi na Mei, iliskumilia mbali mabomba ya maji iliyopita katikati mwa msitu ulioko mlima wa Abadares, kaskazini mwa jiji kuu la Kenya.
Punde baadaye, kampuni ya maji ya Nairobi (NCWSC), ilisitisha shughuli za kutibu maji katika kituo kilioko Ng’ethu.
Pamoja na kituo kile cha bwawa la Sasumua, vituo hivi wiwili vya kutibu maji hukidhi mahitaji ya wakaazi wa jiji la Nairobi kwa kiwango cha asilimia 96.6, huku kituo cha Ng’ethu kikitoa asilimia 85 na kile cha Sasumua kikitoa asilimia 11.6.
Maeneo mengi ya jiji la Nairobi, ikiwemo vitongoji duni hata pia maeneo ya matajiri yanatatizika kwa kuwa na kiwango kidogo cha maji au kukosa kabisa maji.
Haya yanajiri huku serikali ikiahimiza watu kukaa manyumbani, kuosha mikono na kuzingatia usafi ili kukabiliana na kuenea kwa COVID-19.
Shirika la Afya Ulimewenguni pamoja na Wizara ya Afya nchini Kenya inashauri watu waoshe mikono yao wakitumia sabuni na maji yanayotiririka kama njia mwafaka ya kupigana dhidi the virusi vya Covid.
Hata hivyo, shughuli ya kutafuta maji katika maeneo ya mapato ya chini inaenda kinyume na ushauri wa kutokaribiana, kwa vile kwa kawaida watu hukusanyika pamoja katika vituo vya kuteka maji, hivyo kuwaweka hatarini ya kuambukizwa na COVID-19.
Baada ya ugavi wa maji kutatizwa mwezi mmoja baadaye jijini, ukosefu mkubwa wa maji unaokumba jiji la Nairobi unatarajiwa kuendelea.
“Tutakabiliana na ukosefu wa maji ama janga la virusi vya Corona? Tutaishi vipi bila maji, huku tukihimizwa tuoeshe mikono yetu,” aliuliza Rose Okeyo, mama wa watoto wanne.
Na katika eneo la majiji jirani la Ngong lililomo Jimbo la Kajiado, hali ni ile ile. Jimbo hili lina.
Jimbo hili hugawa maji kwa hali isiyothabiti katika eneo hili. Ugavi huu shakiki, imewaacha wakaazi kutafuta njia mbadala ya kupata maji.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa NCWSC, Mhandisi Nahashon Muguna, maeneo yanayopata maji kutoka kwa kituo cha kutibu maji cha Sasumua, watendelea kukumbana na ukosefu wa maji kwa muda wa wiki tatu zaidi.
Alikanusha madai yanayoshutumu magenge kwa kubadilisha mkondo wa maji kutoka kampuni hii, ili kuuzia wakaazi hivyo kusababisha ukosefu “bandia” wa maji jijini Nairobi.
“Haiwezekani kubadilisha mkondo wa maji kutoka mabomba yetu, kwa vile ugavi wa maji jijini ni mshikamano wa mtandao, hivyo basi sio rahisi kuutatiza,” alisema.
Hata hivyo, wenzi wanaoishi katika eneo la Ngong, wanasimulia hadithi tofauti.
Daniel Mutinda na Dorcus Mutinda, walifahamu kuweko kwa njia mbadala wa kuipatia jamii yao maji, pasi na kuwalipa wauzaji maji pesa zaidi au kwa kuiteka kutoka katika kidimbwi.
Wenzi hawa walipata mkopo mdogo kupitia mpango wakifedha wa WaterCredit uliozinduliwa na shirika la kimataifa lisilo la kiserikali lijulikanalo kama Water.org, hivyo kuwawezesha kununua tanaki la kuhifadhi maji. Sasa, wanao uwezo wa kuteka na kuhifadhi maji wakati wa msimu wa mvua na kuyatumia kwa muda murefu baada ya msimu huu kupita.
“Tanaki hili hupatia jamii yangu maji yaliyoboreshwa. Hii imeisaidia jamii yangu kuboresha hali ya usafi kwa kuosha mikono yetu wakati huu wa janga,” asema Daniel.
Aligharamia suluhu kwa shida ya maji kwa bei nafuu ambayo jamii yake ilikumbana nayo. Kwa shilingi 2,000 ($18.80) pesa za Kenya, kila mwezi, Daniel alinunulia jamii yake matanaki mawili ya kuhifadhi maji ya mvua.
Atalipa mkopo huu kikamilifu kwa chini ya miezi 36.
Kama vile Daniel, Patricia Kahumbu anayo sababu ya kutabasamu. Kwa bidii yake, mama huyu wa watoto watatu, mwenye umri wa miaka 53 alimudu shamba ndogo alimokuza mazao kama vile mahindi, maharage, kitunguu, mtama na njugu.
Wakati ule mama huyu haishughulikii shamba lake na kuwalisha mifugo, Patricia hutumia wakati wake kama karani katika kikundi cha kujitegemea katika eneo lake. Kikundi hiki kinachowajumuisha majirani wake kijijini, hutoa nafasi mwafaka wa usaidizi wa kifedha kwa wanachama wake.
Wanachama hawa, hukusanya fedha kwa pamoja na huzihifadhi katika hazina, ambazo huzitumia kama dhamana itakapohitajika.
Katika mkutano wa hivi juzi, kikundi hiki kilitaja upatikanaji wa maji kama changamoto kubwa mabomani mwao. Walibaini kuwa, muda mwingi unaotumika kutafuta maji huathiri shughuli zingine za kila siku kando na kuwa mzigo mkubwa wakati msimu wa ukame unaporejea.
Yeye binafsi, Kihumbu alitumia masaa kadhaa kwenda na kurudi kutoka kwa chanzo cha maji ili kuipatia jamii yake maji.
Kupitia Benki ya Equity, Kihumbu pamoja na wanachama wenzake walifahamu kuwa, wangenufaika na mkopo nafuu ili kujipatia suluhisho muafaka wa tatizo la maji. Kikundi hiki kilikata kauli kwamba hii ndio suluhisho kwa mahitaji yao ya maji, hivyo kupelekea kwao kuchukuwa mkopo. Kiwango cha mkopo wake Kihumbu kilikuwa shilingi 25,000 ($250).
“Pesa hizi ziliniwezesha kununua matanaki matatu. Sasa hivi, niko na maji yakutosha kwa mifugo yangu na kukuza mboga pamoja na ya matumizi yangu ya nyumbani,” alisema.
Ukosefu wa maji nchini Kenya
Maji na usafi zimetambulika kama nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu, na katika uzingatiaji wa haki za binadamu kando na kuwa raslimali muhimu katika maisha ya binadamu.
Lengo Endelevu la 6 linanuia kuwezesha upatikanaji wa maji na usafi kwa kila mtu kufikia mwaka wa 2030.
Hata hivyo, watu wengi ulimwenguni bado hawana njia ya kujipatia maji masafi na salama na usafi wa kimazingira wakati huu wa janga la COVID-19.
Takriban watu bilioni 2.4 ulimwenguni, hawatumii hali safi za kimazingira zilizoboreshwa, na watu milioni 663 ambao hawana njia ya kupata maji masafi, kulingana na Shirika la Afya Duniani.
Nchi ya Kenya bado ni nchi iliyo na ukosefu mkubwa wa maji, huku ikiwa na kiwango cha chini cha ujazo wa maji asili.
Ripoti ya maji na usafi iliyotolewa kwa pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) mwaka wa 2019, ilionyesha kwamba asilimia 59 pekee ya Wakenya wanao uwezo wa kupata huduma za kimsingi za maji na asilimia 29 pekee wakiwa na uwezo wa kupata huduma za hali ya usafi.
Hii inahatarisha afya ya watu haswa watoto ambao hawawezi kujipatia huduma hizi muhimu kutokana na pingamizi za kifedha.
Ukosefu wa maji nchini Kenya ni tatizo la tangu jadi.
Kulingana na Water Project, shirika ambalo hutoa maji kwa jamii katika Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Africa, ukosefu wa maji nchini Kenya imekuwa changamoto kwa miongo mingi.
“Raslimali asili ya maji nchini Kenya haitoi maji kwa maeneo kadhaa ya nchi kwa usawa. Hivyo, watu wengi wanasalia bila maji,” shirika hili lasema.
Mabadiliko ya tabia nchi yanadhuru raslimali ya maji nchini kwa kuathiri mzunguko wa maji, hivyo kubadilisha kiwango, ugavi, muda na ubora wa maji yanayopatikana. Wakati huo huo, wanaotumia maji, ikiwemo jamii, wanyama na viwanda, mwishowe huathirika: shughuli na matendo yao hutegemea maji moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Kote nchini Kenya, baada ya miongo mingi ya maendeleo ya kuboresha vyanzo vya maji, upatikanaji wa maji katika taifa zima umepungua – kutoka takriban asilimia 75 ya manyumba yaliyokuwa yanapata maji ya kunywa kutoka vyanzo vya maji vilivyoboreshwa mwaka wa 2015 hadi kufikia asilimia 65 mwaka wa 2019, kulingana na twakimu za kitaifa.
Mradi wa Water Project ulidokeza kuwa, ukuwaji wa kasi wa majiji imesindikiza wakaaji maskini wa majiji kuishi katika vitongoji duni, ambamo maji salama au hali ya usafi haipatikani, huku msongamano mkubwa wa watu ukizorotesha hali ya afya ambayo tayari ni hatari.
Asilimia ya manyumba katika miji yanayotumia maji salama ya kunywa yaliyothibitiwa vyema, ilishuka kutoka mwaka wa 2000 hadi 2017, huku watu wengi – haswa walio maskini zaidi – wakitegemea maji yanayouzwa na wachuuzi, ama yale yanayopatikana juu ya ardhi pia vijito na maziwa – hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mpango wa Pamoja wa Kufuatilia Hali ya Usafi na Ugavi wa Maji.
Basi, hii inatoa nafasi ya kuenea kwa COVID-19 miongoni mwa wakaazi.
Kufikia tarehe 15 mwezi wa Juni, Kenya tayari ilikuwa imethibitisha visa 3,727 katika taifa nzima, huku watu 1,286 wakipona na watu 104 wakiaga.
Visa vya hapo mwanzo viliripotiwa jijini Nairobi na maeneo ya pwani kama vile jimbo la Mombasa katika mwezi wa Machi. Majimbo haya mawili yanaongoza kwa visa vya ugonjwa huu vikiwa na visa vilivyothibitishwa 1,691 na 1,097 mtawalia.
Patrick Alubbe, mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la maji la Kenya (KWAHO), alidumisha kwamba ukosefu wa maji nchini umesababishwa na mgao wa maji unaotokana na ongezeko la watu.
“Takriban asilimia 40 ya idadi ya watu majijini huishi katika maeneo ya mapato ya chini. Hivyo, kutoa huduma kwa maeneo haya itabakia kuwa changamoto kubwa kwa sekta ya maji kwa miongo mingi ijayo, ikizingatiwa kiwango cha ongezeko kubwa la idadi ya watu,” Alubbe alisema.
Katika jimbo la Kajiado, asilimia 66 ya manyumba yalikuwa na uwezo ya kujipatia maji yatokanayo na vyanzo vya maji vilivyoboreshwa katika mwaka wa 2019, ikiwemo maji ya mfereji, visima na maji ya chupa. Hata hivyo, asilimia 23 ya watu bado inategemea maji kutoka kwa wachuuzi na asilimia 9 inategemea bidhaa hii kutoka maji yasiyo salama, yapatikanayo juu ya ardhi ndani ya mito na vijito.
Alubbe alidokeza kuwa, ukosefu wa maji salama na iliyo ya bei nafuu huenda ikahujumu jitihada za kupambana na kuenea kwa janga la COVID-19, kwa vile kile kitendo cha uoshaji mikono kutumia sabuni kimetambulika kuwa katika mstari wa mbele dhidi ya COVID-19.
Ndani ya miaka minne iliyopita, asilimia 31 pekee ya manyumba katika jimbo la kajiado, yalikuwa na sehemu iliyotengwa ya kuosha mikono, hii ikiwa ni kiwango cha juu kidogo, ikilinganishwa na asilimia 21 ya kiwango cha wastani cha kitaifa wakati ule, kufuatia utafiti wa bajeti nchini Kenya uliofanyika miaka ya 2015-2016. Nayo idadi ya chini ya nusu – asilimia 44 – ya manyumba jijini Nairobi, ndiyo yaliyokuwa na sehemu maalum iliyotengwa kwa mathumuni ya uoshaji mikono.
Alielezea kwamba, magonjwa kama vile uendeshaji, yanayosababishwa na maji yasiyo salama na hali duni ya usafi; idadi kubwa ya watu inayotokana na uhamiaji majijini; na ugavi usio wa sawa wa maji na vituo vya usafi ni miongoni mwa changamoto za kimsingi za maji na hali ya usafi zinakumba jamii ambazo ziko hatarini.
“Hatua za dharura zinazochukuliwa mapema pamoja na uratibu miongoni mwa washika dau wote katika siku za hivi nyuma, zimesaidia kuthibidi magonjwa yanayoambukiza ndani maeneo yanayokumbana na changamoto ya maji,” alieleza.
Changamoto hizi zinahatarisha jamii ambazo hazina uwezo wa kujipatia maji salama na hali bora ya usafi, muhimu katika kukabiliana na kuenea kwa COVID-19.
WaterCredit: Utoaji wa mikopo midogo nafuu ili kusuluhisha tatizo la maji na kuboresha usafi
Ili kukabiliana na changamoto hizi, washika dau tofauti katika sekta za ugavi wa maji na usafi wa kimazingira, wanabuni ili kuboresha uwezo wa kupata maji na hali ya usafi kwa walio na mahitaji ya dharura.
Mojawapo ya washika dau hawa ni shirika la Water.org. Kupitia njia inayokubalika na mashirika za kifedha za nchi za Kenya, Uganda na Ethiopia, mpango wa WaterCredit unaoendeshwa na Water.org, unazivunjilia mbali pingamizi za kifedha zinazokumba jamaa kama ya Daniel Mutinda, ili kuzipa uwezo wa kifedha utakaowawezesha kupata suluhisho ya maji na hali ya usafi wa kimazingira, kwa walio maskini.
Kulingana na Anthony Githinji, mkurugenzi mkuu wa mipango katika shirika la Water.org, mojawapo ya pingamizi kuu dhidi ya upatikanaji wa maji salama, na hali bora ya usafi wa kimazingira, ni kutokuwa na uwezo wa kifedha.
“Tulibuni mpango wa WaterCredit ili kushughulikia pingamizi hii, moja kwa moja,” Githinji alisema. WaterCredit inasaidia kuleta mikopo midogo kwa wale wanaoihitaji kwa madhumuni ya kufanya hali ya kuwepo kwa maji manyumbani na kutoa suluhisho la vyoo kuwa hali halisi.
Kwa mfano, Daniel, mkaazi wa Ngong, alinufaika na mkopo mdogo kutoka kwa Benki ya Equity kupitia mpango huu iliyomuwezesha kununua tanaki la kuhifadhi maji.
Kulingana na mradi na mahitaji ya anayenufaika na mpango huu, kiwango cha mkopo nchini Kenya ni Ksh. 40,000 ($376) kwa kadiri, ambao utatumika katika ujenzi wa mifereji ya maji kwa gharama ya Ksh. 10,000 ($94), na uchimbaji kisima kwa gharama ya kitita cha hadi shilingi milioni moja ($9,410).
Water.org limekuwa likishirikiana na mashirika madogo ya kifedha pamoja na mabenki kwa muda wa miaka 15 kustawisha na kutoa bidhaa za mikopo kwa jamii maskini nchini Kenya, Uganda na Ethiopia.
Water.org limekusanya pesa kutoka wadau wakifedha kwa ufadhili wa WSS kwa kitita cha hadi shilingi bilioni 26 (dola milioni 244) nchini Kenya.
Kufikia sasa, mpango huu umewezesha Wakenya milioni 3.9 vijijini na walioko kando ya majiji katika majimbo yote 47, kupitia jukwaa la washirika wa mradi huu katika kufanikisha kupatikana kwa maji yaliyo salama, pamoja na kuboresha vituo vya usafi wa kimazingira katika jitihada za kukomesha kusambaa kwa COVID-19, na kuhakikisha kuzingatiwa kwa maslahi ya watu walioko katika maeneo ambayo hutatizika kupata maji masafi. Kando na hayo, mikopo hii imewezesha walionufaika kustawisha biashara zao ndogo na shughuli za ukulima hivyo basi kuimarisha maishilio yao.
Maji na vituo vya usafi wa kimazingira katika kielelezo cha mradi huu, kinahusisha mahitaji ya kawaida kama vile vyoo ambavyo vinaweza kuwa vile vya shimo au vya kisasa, matangi ya maji machafu na mifumo ya maji taka. Uwekezaji katika maji inahusisha ujenzi wa mifereji, utekaji maji kutoka mapaa, visima vya juu ya ardhi pamoja na visima vya kawaida.
“Katika shirika hili la Water.org tunatilia maanani suluhisho za kifedha zinazosindikizwa na muelekeo wa soko ili kuzibadilisha maisha pia na kumaliza janga la ukosefu wa maji,” Githinji alisema.
Hii yaonyesha kwamba, uwezekano upo wa suluhisho za kifedha kubadilisha mandhari ya maji na usafi wa kimazingira kote Barani Afrika, ikiwa wadau wengi katika sekta ya kibinafsi watajitwika jukumu hili, kulingina na kundi la mpango huu.
Kulingana na Githinji, hivi leo zaidi ya watu milioni 3.9 nchini Kenya sasa waweza kufungua mifereji na pia kutumia vyoo kwa njia salama, kwa sababu mikopo midogo nafuu imewawezesha jamii zisizo na uwezo mkubwa, kujipatia maji yaliyo salama na kuimarisha usafi wa kimazingira manyumbani mwao ambazo zimekuwa muhimu mno wakati huu wa janga la COVID-19.
Hata hivyo, mpango huu umekumbwa na changamoto pia.
Mojawapo ya changamoto wa mpango huu, ilikuwa kwamba washirika wa kifedha walikosa ujuzi wa kiufundi katika maswala ya maji na usafi wa kimazingira, kuwawezesha kutekeleza vilivyo mpango huu, Githinji alisema.
Aliongeza kuwa “baadhi ya washirika wa kifedha hawakuwa makini kutekeleza mradi, haswa ilipogusia usafi wa kimazingira, kwa vile swala hili halikuonekana kuwa ni bidhaa ya mkopo itakayo fua dafu.”
Aliwahimiza wadau wanaohusika na maji na usafi wa kimazingira, ikiwemo sekta ya kibinafsi, kuchunguza na kutumia baadhi ya suluhisho vumbuzi dhidi ya changamoto zinazokumba raslimali ya maji na kuwasaidia wale wasio na uwezo wa kupata maji, kujipatia bidhaa hii.
Makala haya yametayarishwa kwa ushirikiano wa InfoNile na hisani ya Code for Africa, ufadhili wa Pulitzer Center pamoja na National Geographic. Uandishi na uhariri wa ziada umafanywa na Annika McGinnis na Fredrick Mugira.