Green Horizon, mradi wa usalama wa chakula washughulikia maslahi ya jamii za Jebel Ladu huku ukikuza mazao kutuliza janga la njaa nchini Sudan Kusini

Green Horizon, mradi wa usalama wa chakula washughulikia maslahi ya jamii za Jebel Ladu huku ukikuza mazao kutuliza janga la njaa nchini Sudan Kusini

Zaidi ya hektari milioni 2.5 ya ardhi nchini Sudan Kusini imetwaliwa na wawekezaji haswa wa kimataifa tangu mwaka wa 2006

Na David Mono Danga

Ripoti hii imetayarishwa kwa ushirikiano wa InfoNile na Code for Africa na usaidizi kutoka kwa Pulitzer Center.

SouthSudanForeignInvestments 1

Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani inakumbana na changamoto nyingi, ikiwemo umaskini na njaa. Taifa hili limeshuhudia malumbano yasiyoisha, hali ambayo imetisha lengo lake kuu la kufurahia amani.

Tangu mwaka wa 2013, nchi hii imejizatiti kulisha watu wake, huku baa la njaa likitangazwa kukumba maeneo mengi nchini, haswa sehemu ya Central Equitoria ambako maelfu ya watu walilazimika kuhama kutokana na vita mnamo Julai, 2017.

Ili kukabiliana na upungufu wa chakula nchini, serikali ilitoa kandarasi mnamo Novemba 2015 kwa Green Horizon, kampuni ya Israel ili isaidie kuondoa pengo katika uzalishaji wa chakula.

Green Horizon ni mradi wa serikali unaotekelezwa na Waisraeli ili kukabiliana na umaskini, huku ikiimarisha maishilio kwa kuwaelimisha wakulima na kuzalisha chakula  cha kuuzwa kwa masoko ya ndani na nje ya nchi.

DSC 0303

“Kiini kikubwa cha makubaliano, ilikuwa ni kwa kampuni kumudu tingatinga 1,000 zilizofadhiliwa na Rais Salva Kiir kwa wakulima wa Sudan Kusini,” alisema Dkt. Erneo Balasio Peter, mratibu katika wizara ya kilimo ambaye pia ni msimamizi katika mradi wa Green Horizon.

Usimamizi ulisema kwamba mradi huu ulikabithiwa hektari 500 ya ardhi katika eneo la Jebel Ladu, kilomita 37 iliyoko katika vitongoji vya jiji la Juba.

Green Horizon linamiliki mashamba ya kisasa katika Juba na Jebel Ladu ndani ya majimbo ya Central Equatoria State, Bor Jonglei State, Renk Upper Nile na Torit, Eastern Equatoria State.

matooke

Linamudu pia miradi ya Community Commercial Farming Projects katika miji ya Wau, Gok na Rumbek. Miradi hii huwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kiwango kikubwa, kwa kuwazawadia mbegu zilizoidhinishwa, vifaa, mbolea na mwongozo wa kiufundi, huku wakulima wakitakiwa kuregeshea Green Horizon asilimia fulani baada ya kuuza mazao.

“Punde tu mkulima amevuna mazao yake, sisi humsaidia kuikusanya, kuipeleka sokoni, kisha kuiuza na kugawanya faida,” alisema Yoash Zoha, mkurugenzi mkuu.

Kwa mujibu wa Yoash, tangu mwaka wa 2016 mradi huu tayari umeshazalisha tani 1,000 ya mahindi, tani 200 ya mtama, tani 100 ya njugu, tani 200 ya mpunga, tani 250 ya ndizi na tani 300 ya mboga. Tani 2,500 ya kitunguu bado kiko shambani kikisubiri kuvunwa mwishoni mwezi huu.

Matunda na mboga zilizozalishwa na kampuni hii ni pamoja na tikiti tamu, tikiti maji, tango, kabeji, sukuma wiki, nyanya, papai, pilipili hoho na kali, mbiligani, okra na kitunguu.

Kampuni hii huzalisha sehemu moja kwa kumi ya chakula chote nchini Sudan Kusini, kwa mujibu ya wizara ya kilimo.

Yoash aeleza kusema kwamba, mradi huu bado haujauza zao lolote nje ya nchi, ingawaje wanakusudia kuuza kiwango kidogo cha kitunguu baada ya mavuno mwisho wa mwezi wa Machi.

“Mradi bado hauna faida. Tunatarajia kusawazisha uwekezaji wetu mwaka wa 2019, na kuanza kupata faida mwaka wa 2020,” alisema.

Takwimu za Land Matrix, mpangilio huru wa kufuatilia mikataba ya ardhi, yaonyesha kwamba, tangu mwaka wa 2006 hektari milioni 2.5 ilinyakuliwa Sudan Kusini kupitia mikataba 15, yaliyohusisha haswa wawekezaji wa kigeni. Kuna mikataba mingine 9 yangali yanajadiliwa ambayo yakiidhinishwa, basi yataongezea hektari milioni 1.5 zaidi, takwimu zaonyesha.

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya Oakland Institute iliyo na makao yake nchini Marekani, unyakuzi ardhi ulianza miaka michache kabla kuwadia kwa uhuru mwaka wa 2011. Tayari, zaidi ya hektari milioni tano ilikuwa imeidhinishwa kwa uzalishaji wa mazao nishati, kuendeleza utalii wa kimazingira, kilimo na upanzi wa miti ndani ya miaka minne kabla ya kura ya maoni ya kujipatia uhuru iliyofanyika Januari, 2011, ripoti yadokeza.

Wenyeji kufutwa kazi

Ardhi ya Jebel Labu, iliyoko karibu na Juba, imetumika kwa ukulima kwa miongo mingi. Katika mwaka wa 1978, Gaafar Nimeiri, aliyekuwa Rais wa Sudan, aliweka huru ardhi kama mojawapo ya mashamba ya serikali kwa ukuzaji wa mtama katika iliyekuwa nchi ya Sudan, kulingana na Sultan Angelo Ladu, naibu wa chifu wa eneo la Jebel Labu.

Shamba hili lilimilikiwa kwa muda mfupi na aliyekuwa gavana wa jimbo la Equatoria Region, kabla kuregeshewa jamii.

MD Yoash R 2

Sultan Angelo alisema kwamba, kabla ya wawekezaji walioko kuja sehemu hii, ardhi haikuwa na kazi kwa kuwa serikali ilikuwa imesitisha shughuli za kilimo eneo hili na jamii haikuwa na uwezo wa kuendeleza kilimo cha mashamba makubwa.

Hivi leo, shamba hili la Waisraeli linasimamiwa kwa ushirikiano na shirika moja kutoka Kanada liitwalo Canadian Economic Development Assistance for South Sudan (CEDASS), ambalo hapo awali ndilo lilitayarisha na kulima shamba hili katika mwaka wa 2006 kwa maksudi ya kutekeleza mradi wa kilimo endelevu, kwa idhini ya serikali ya Sudan Kusini kwa ushirikiano na wenyeji. Tangu mwaka wa 2006, CEDASS imetoa elimu ya kiuchumi na kilimo na kubuni nafasi za kazi kwa jamii.

Sultan Jenabio Kenyi Loku, chifu wa kijiji cha Gwerekek, katika kaunti ya Ladu, alisema kuwa Wanakanada walikuwa na uhusiano mwema na wenyeji kwa muda wa miaka minane waliokuwa katika eneo hili.

Ili kubadilisha muelekeo na kuangazia shughuli zinazowiana na maswala ya kibinadamu kama vile elimu, huduma za afya, maslahi ya watoto na afya ya kina mama, CEDASS iliwachana na mradi huu, ila tu ilishirikiana na mradi wa Israel Agricutultural Green Horizon kumudu shamba hili.

Kwa mujibu wa CEDASS, Green Horizon ilifaa zaidi kuwa mshirika mkuu, kwa kuwa lengo lao ni kuleta maendeleo ya kisasa, utengamano na kuzingatia maslahi ya jamii ulimwenguni kote.

Chifu Kenyi alisema kwamba, Green Horizon imeboresha maisha ya jamii eneo hilo, likitoa asilimia kidogo ya mazao kwa kila boma pamoja na kupa jamii huduma za afya katika zahanati ya Green Horizon Clinic.

“Tulifanya kazi vyema pamoja kwa mwaka wa kwanza na wa pili. Walitupa madawa. Walipatia jamii magunia 100 ya mahindi mwaka jana, yaliyogawiwa maboma,” Sultan Kenyi alisema.

Alisema kwamba, kampuni hii ilisajili wenyeji kufanya kazi katika shamba hili. Kulingana na Dkt. Erneo, mradi wa Green Horizon unajiri wafanya kazi 362 pamoja na kati ya vibarua 350 na 1,234 kila mwaka.

Hata hivyo, chifu alisema kwamba kampuni hii iliwafuta kazi wenyeji, miongoni mwao wakiwa wanawake waliokuwa wakiondoa magugu shambani, na badala yake kuwapa kazi watu kutoka Juba.

Sultan Kenyi alisema kwamba jamii haijafurahishwa na usimamizi wa kampuni hiyo. Kwa vile ardhi inamilikiwa na jamii, inafaa kampuni hii kuwafikiria wenyeji kwanza, badala ya kuwapa kazi watu kutoka mbali, alisema.

Onions 1

“Ardhi ni yetu, ndio sababu tunafaa kunufaika na uwekezaji hapa. Kwa hivyo, ni kwa nini tunazuiwa kufanya kazi?” Kenyi alidai.

Yoash Zohar, mkurugenzi mkuu wa Green Horizon, alisema “Hakuna mfanya kazi aliyefutwa kazi kwa njia isiyo faa.”

“GH hufanya kazi kuzingatia kikamilifu kanuni na sheria za kazi za Sudan Kusini…baadhi ya wafanya kazi walifutwa kazi kwa kutepetea katika majumu yao, au kwa utovu wa nidhamu. Sababu kuu ilikuwa ni kutoripoti kazini,” Yoash alisema.

“Ikiwa mfanya kazi yeyote alihisi kuthulumiwa, yeye anaweza kuja kuniona wakati wowote. Nitachunguza kila kisa, inavyohitajika,” aliongeza kusema.

Yoash alikiri ya kwamba, ni bora zaidi kuajiri wenyeji kuliko kuwaajiri watu kutoka kwingineko.

“Uajiri au ufutaji kazi wowote, hutegemea utenda kazi, kujitolea, na nidhamu,” aliambia gazet la Juba Monitor kupitia barua pepe.

Cililia Laku Wani, mwenyekiti wa jamii ya Kaunti ya Ladu, hushauri mradi wa Green Horizon kuajiri wenyeji kwa ushirikiano na serikali ya jimbo la Jubek.

“Baadaye, serikali ndiyo itakayo tuandikia katika kaunti kufuatilia ni watu gani wanaostahili kuajiriwa katika shamba,” alisema.

Wani alisifu serikali kwa kuletea watu wake mradi wa kilimo ijapokuwa alisisitiza kwamba angependa kuona wenyeji wakinufaika.

“Wao ndio wanaostahili kufanya kazi shambani, pamoja na kukabidhiwa vyeo vya usimamizi, kwa sababu shamba huwa halining’inii popote (hewani). Huwa liko katika ardhi ya mwenyewe ambaye anaweza patikana. Wenyeji lazima wanufaike hata kama ni mradi wa kiserikali,” alisema.

Mmoja wa wafanya kazi aliyepoteza ajira yake na ambaye aliomba jina lake kubanwa ili kulinda usalama wake, alisema kwamba mradi wa kilimo ulioendeshwa na Waisraeli ndio ulioleta madiliko makubwa zaidi ya ule uliotekelezwa na shirika la Kanada.

Alisema kuwa usimamizi wa mashamba haya sasa ni mzuri, haswa jinsi ambavyo wasimamizi wanavyohusiana na walioajiriwa. Yoash Zohar, ambaye ni mkurugenzi mkuu, huwa mwepesi kushughulikia jambo lolote punde tu linaenda mrama, alisema.

Hata hivyo, alisema kwamba kuna shida nyingi itokanayo na mabadiliko ya mara kwa mara katika nyadhifa za usimamizi. Hivyo, ilikuwa vigumu kwa wafanya kazi kukabiliana na mpangilio wa kazi unaobadilika kila mara, unaoletwa na msimamizi mpya, alisema.

“Wafanya kazi walilalama kwamba walidhulumiwa. Nilipata kushuhudia matukio haya bali na kuyapitia mimi mwenyewe pia,” kasema aliyekuwa mfanya kazi huku akisisitiza kwamba baadhi ya wafanya kazi walikosa kuajibika katika majukumu yao kutokana na tukio hili.

Alisema kwamba ilikuwa jambo la muhimu kwa Green Horizon kukuza uhusiano mzuri kati yake na jamii ili kuendeleza sekta ya kilimo nchini.

Water melon 2

“Ushauri wangu ni kwamba, usimamizi wa Green Horizon wafaa kukarabati sera zake na kudumisha uhusiano mwema kati yake na jamii,” alisema. “Iwapo Green Horizon itakosea jamii heshima, hawatapiga hatua mbele, na iwapo jamii haitaheshimu sera za Green Horizon, nao hawatafaidika.

“Iwapo wataimarisha uhusiano mwema, basi jamii itatoa ardhi ya kutosha kwa miradi ya Green Horizon kupanua mashamba,” mfanya kazi huyu wa zamani alisema.

Serikali ya mtaa ilikataa kusikia malalamiko rasmi yaliyohusu kufutwa kazi kwa wenyeji wa kijiji cha Gwerekek.

Mheshimiwa Kandido Swaka Ladu, Kamishna wa kaunti ya Ladu alikiri kuwa na ufahamu wa maendeleo ya kilimo yanayoendeshwa na Green Horizon katika eneo laJebel Ladu.

“Kuwepo kwa shamba la kisasa kama lile la Jebel Ladu katika jamii yako, inakupasa kufurahi kwa vile wenyeji hawatahangaika,” Kamishna Ladu alisema.

Alieleza kwamba uwekezaji wa aina hii huboresha bei ya bidhaa sokoni kwa sababu wananchi huwa na uwezo wa kununua mazao kwa bei nafuu.

Kwa vile mradi huu ni wa serikali ya kitaifa, Kamishna Swaka alisema, “utatunufaisha, sio kwa chakula tu, bali kupitia njia zingine katika jamii. Lakini iwapo wenyeji watakuwa hawafanyi kazi, ila shamba hili liko katika jamii yao, basi athari zake zitakuwa mbaya. Ndio tunasema ya kwamba kuwepo kwa uwekezaji wa aina yeyote basi wanaostahili kunufaika kwanza ni jamii enyeji.”

Sheria ile ya South Sudan Land Act ya mwaka wa 2019, yaorodhesha ardhi kuwa ya umma, jamii au ya kibinafsi. Ardhi ya umma inamilikiwa kwa pamoja na watu wote wa Sudan Kusini na kushikiliwa kwa muamana na idara tofauti zinazohusika za serikali. Ardhi ya jamii inashikiliwa na jamii ambazo zinatambulika kwa misingi ya kikabila, makao ama malengo, sheria yasema.

Nayo ardhi ya kibinafsi ni ardhi yeyote ambayo imesajiliwa na mtu yeyote yule chini ya umiliki huru ama umiliki wa kukodisha na/ ama ardhi nyingine yeyote ile ambayo imetangazwa kuwa ya kibinafsi kwa mujibu wa wa sheria, mtawalia. Jebel Ladu yaorodheshwa chini la ardhi ya jamii.

Nakisi ya chakula

Ukadiriaji wa usalama wa chakula uliotekelezwa na wizara ya kilimo katika mwezi wa Septemba mwaka uliopita, ulidokeza kwamba Sudan ilihitaji zaidi ya tani milioni moja ya chakula kulisha kila boma.

Takriban tani milioni 1.2 ya chakula kinahitajika kukithi mahitaji ya milo mitatu kwa siku ya kila mtu nchini Sudan Kusini, alisema Dkt. Loro George Leju, mwelekezi mkuu wa uzalishaji wa ukulima.

Kufuatia hasara iliyotokana na mavuno duni mwaka huu, nchi yahitaji uzalishaji wa zao haswa la nafaka kusitisha njaa inayotarajiwa, Leju aliliambia gazeti la Juba Monitor.

Kwa mujibu wa wizara ya kilimo, Sudan Kusini ilizalisha tani 404,109 pekee ya chakula katika mwaka wa 2018 – kiwango kilicho cha chini zaidi kuliko inavyohitajika kulisha idadi ya watu iliyoko sasa, ambayo takwimu za Umoja wa Mataifa ulikisia kuwa takriban watu milioni 13.2 kufikia mwezi wa Feburuari mwaka huu.

Ukame na vita imechochea shida kubwa ya njaa. Watu wengi kutoka miji inayozalisha chakula ya Yei katika jimbo la Central Equatoria, Yambio katika jimbo la Western Equatoria na Torit ilioyoko jimbo la Eastern Equatoria, walilazimika kuhama kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea.

Kwa mujibu wa sasisho ya Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR) katika mwezi wa Januari, vita hivi vilipelekea kuhama kwa zaidi ya watu milioni 2.2 hadi mataifa jirani na watu milioni 1.97 waliohamia sehemu tofauti ndani ya Sudan Kusini, miongoni mwao wakiwa 193,219 katika maeneo ya UNMISS Protection of Civilian (POC), kambi za wahamiaji wa ndani ya nchi yaani ile ya Internally Displaced People ikiwa chini ya uthibiti wa misheni ya Umoja wa Mataifa.

Ripoti ya Integrated Food Security Phase Classification (IPC) la Shirika la Chakula Ulimwenguni (WFP) ambalo hutabiri kiwango cha ukosefu wa usalama wa chakula katika mwishoni wa mwaka wa 2018 na katika robo ya kwanza mwaka wa 2019, ulionyesha kwamba watu milioni 5.3 wanahitaji msaada wa chakula nchi zima.

Dkt. Leju alisema kwamba shida ya njaa inakumba hususa majimbo ya Eastern na Central Equatoria. Mradi huu wa Green Horizon unalenga kupunguza shida hii, kwa vile mazao ya chakula huuzwa katika masoko ya Juba.

Hata hivyo, mradi huu ungali bado mchanga, Leju alisema. Awamu ya pili ya mradi huu utazalisha mifugo pamoja na bidhaa za maziwa zitakazoboreshwa na kuuzwa nchi za nje ili kuimarisha pato la nchi lisilotegemea uuzaji wa raslimali ya mafuta, Erneo alisema.

Wizara ya Biashara, Viwanda na Maswala ya Jumuia ya Africa Mashariki, ilisema kwamba ukosefu wa usawaziko kibiashara,  inazuia uuzaji wa bidhaa za kilimo zinazozalishwa nchini Sudan Kusini hadi mataifa ya nje.

Stephen Doctor Matatias, mkurugenzi mkuu wa mipango, alisema “inatulazimu kubadilisha bidhaa za kuuzwa nje na bidhaa nyingine ili kusawazisha hali ya biashara.”

“Biashara inayoendelezwa na Sudan Kusini huegemea upande mmoja, ambapo nchi hii huagiza tu bidhaa kwa matumizi yake kutoka nje na huwa inauzia mataifa mengine bidhaa chache mno. Lakini, amani iliyoko sasa itatuwezesha kuzalisha mazao mengi na wawekezaji halisi kama Green Horizon, watakuja nchini,” Matatias alisema.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipunguza uwezo wa nchi kuuza bidhaa nje, Matatias alisema. Lakini alisisitiza kuwa Sudan Kusini iko na uwezo mkubwa wa kuuza mazao yake nje kama vile mahindi, mpunga, mtama, maharagwe, njugu, sandarusi, mbao, asali, kahawa, pamba, samaki, siagi, hibiscus, mifugo na ngozi.

Dkt. Leju aliungama kuwa makampuni ya kigeni kama vile Green Horizon yameboresha uzalishaji chakula na uwezo wa kuuza mazao nje ya nchi.

“Kwa kweli Green Horizon imatupatia muelekeo wa jinsi ya kuongeza uzalishaji wa sio tu mahindi bali pia uzalishaji wa mpunga, mtama na mboga, lakini pia na mazao mengine,” alisema.

Erneo aliunga mkono wazo hili, “Mradi huu umetoa nafasi ya kuboresha hali ya maisha ya wakulima na wafanya kazi wa mradi huu,” alisema.

Matokeo kwa Jamii ya Jebel Ladu

Wenyeji wamegawanyika kuhusu athari za Green Horizon katika eneo hili. Vita Samuel, ambaye ni mkaazi na mkulima katika jamii anasema kwamba kampuni hii imenufaisha jamii kupitia njia tofauti, kama vile utoaji wa vifaa vya ukulima, mbegu na usambazaji wa maji safi ya kunywa kwa watu walio na mahitaji.

“Manufaa makubwa tumeyapata kutoka kwa Green Horizon ni uajiri ya vijana wa Jebel Ladu. Wameleta kazi karibu na wakaazi wa watu wa eneo hili,” Vita alidokeza. “Kunapokuwa na mazishi na sherehe, Green Horizon pia hutoa maji ya kunywa, vitunguu na huduma kama ile ya usafiri hadi mjini. Sio rahisi kupata usafiri hadi mjini kutoka kijiji hiki,” aliongeza kusema.

Catharina Poni, mama wa watoto sita, alisema kuwa Green Horizon hutoa vifaa vya masomo kwa wanafunzi wa shule ya msingi ya Gwerekek ambayo ni shule ya pekee katika eneo hili ambako wajukuu wake hupata masomo. Bibi huyu wa miaka 58 alisema wakati wowote kampuni hii inavuna mazao, jamii hupokea kiwango Fulani cha mavuno haya, kitu ambacho anakitaja kuwa si cha kawaida kwa makampuni mengi kufanya.

Poni alihimiza kampuni hii kuboresha huduma za afya kwa kutoa madawa kwa zahanati ya pekee kijijini, pamoja na kuchimba kisima ili kuwapatia watu maji safi. Alisema kwamba baadhi ya watu hunywa maji moja kwa moja kutoka Mto Nile yaliyo na viini, hivyo kusababisha magonjwa hatari. 

Teknologia mpya ya umuagiliaji maji

Mradi huu unaosimamiwa na Waisraeli umeshabikiwa kwa kuleta teknologia mpya za ukulima nchini Sudan Kusini zenya thamani ya mabilioni ya Pauni za Sudan Kusini (SSP).

“Mfumo wa umuagiliaji maji ambao wameubuni ni mzuri mno,” alisema Leju, muelekezi mkuu anayesimamia uzalishaji wa kilimo.

Kampuni hii ilianzisha mfumo wa umuagiliaji maji wa aina ya pivot ili kunyunyuzia maji mazao katika shamba lenye ukubwa wa hektari 448.8 lililoko katika shamba la Jebel Ladu, nyakati za hali ya hewa isiyoabirika.

“Tayari tumeshaweka pivot sita katika shamba la Jebel Ladu na pivot moja katika shamba la New Land. Uwekezaji huu wote, ikiwemo shughuli za ufyekaji na uandalizi wa shamba kiligharimu takriban SSP bilioni moja,” Mkurugenzi Mkuu, Yoash, alisema.

Kampuni hii hutumia pia umuagiliaji maji wa matone katika shamba kubwa la ndizi pamoja na lile la majaribio la mboga katika shamba la New Land iliyoko eneo la Luri Surre pale Northern Bari Payam jijini Juba. Kiwango cha maji ambacho mfumo huu hutumia ni takriban 200,000 na 50,000 mita za ujazo katika Jebel Ladu na New Land Farm, mtawalia.

Yoash alisema kwamba mita za ujazo milioni 6 ya maji hupita katika Mto Nile kila saa moja.

“Kiwango cha matumizi ya maji kwa mwaka shambani mwetu ni sawa na kiwango kinachopita Mto Nile kila nusu saa… Kile ninachojaribu kusema ni kwamba Nile iko na kiwango kikubwa zaidi cha maji, waweza shughulikia mashamba mengi kama haya kunyunyuzia maji ya Nile, bila ya kukwaruza sehemu ya kiwango cha maji ambacho Sudan Kusini hutumia kutoka Nile,” Yoash alisisitiza.

Alikadiria kwamba, nchi nzima yahitaji takriban hektari 50,000 ya ardhi kwa ukulima wa umuagiliaji maji, kando na kuendeleza kilimo bora ili kujitosheleza.

Mhandisi Robert Peter Zakayo, mkaguzi mkuu katika idara ile ya Directorate of Hydrology and Survey katika Wizara ya Raslimali ya Maji na Umuagiliaji Maji, alisema mifumo ya umuagiliaji maji inayotumiwa na Green Horizon ina ufanisi katika uhifadhi wa maji.

“Mifumo ya umuagiliaji maji kwa matone na ile aina ya pivot yana ufanisi ilinganishwapo na ile ya mifereji wazi, kwa sababu maji yanayosukumwa hutumika kwa kusudio halisi,” alisema.

Uarifu wa ziada na uhariri umetekelezwa na Annika McGinnis

Print Friendly, PDF & Email

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts