Jinsi ambavyo maji yanavyoingia katika guba

Jinsi ambavyo maji yanavyoingia katika guba

Na Nada Arafat

Sehemu kubwa ya kijani kibichi inayoenea hadi upeo wa macho, inashughulikiwa na mashine ya kisasa, ambayo imechukuwa nafasi ya wafanyi kazi. Ardhi hii inamwagiliwa maji kwa kutumia mfumo unaohusisha mashine ya umwagiliaji maji iliyo unganishwa kwa mifereji ambayo hutumika kupitisha maji yanayosukumwa kutumia mojawapo ya vituo vya mabomba kubwa zaidi ulimwenguni. Wahandisi kadhaa wanasimamia shughuli za upanuzi kwa ukuzaji wa mmea wa aina ya alfalfa katika ardhi inayomilikiwa na makampuni ya uwekezaji ya Guba katika mradi wa Toshka.

Hili ni eneo la jangwa la magharibi nchini Misri, ambamo madiliko ya kasi yanafanyika ili kuifanya eneo iliyokuwa jangwa la changarawe  kwa miongo miwili iliyopitia kubadilika na kuwa kijani.

Chanzo cha mabadiliko haya yalitokana na wazo la kuendeleza na kuwekeza katika mradi wa kilimo, lililowasilishwa kama njia ya “kuwanufaisha” watu wa Misri. Hata hivyo, kinyume na lengo hili, mashirika mengi ya nchi za Guba yalinyakuwa sehemu kubwa ya ardhi, kama mojawapo ya mpango wa mataifa yenye utajiri mkubwa wa mafuta, kulinda usalama wao wa chakula, kwa kunyakuwa na kukuza mimea nje ya mipaka yao.

Egypt Image 05

Mandhari yake wakati huu umepelekea nchi za Guba kutambua umuhimu wa kuhifadhi raslimali zao za maji zilizo chache. Mnamo Januari, 2009 Ufalme wa Saudia ulizindua mradi wa Mfalme Abdullah bin Abdulaziz wa kuwekeza ng’ambo, huku ukidokeza mipango ya kuafikia hali ya usalama wake wa chakula, kwa kuwekeza katika nchi zilizo na nafasi bora zaidi kufanikisha ukulima.

Mradi huu ulihusisha usaidizi wa kifedha kwa wawekezaji wa Kisaudia, huku serikali ikidhamini asilimia 60 ya gharama za ujenzi na uzalishaji. Serikali pia iliahidi kujihusisha katika mijadala ya mikataba, baina ya mataifa tofauti ili kurahisisha biashara ya wawekezaji huko ng’ambo bali na kuhakikisha kwamba takriban asilimia 50 ya mazao yao inasafirishwa hadi Ufalme huo.

Mkakati huu wa muda mrefu ulibadilika kufuatia uamuzi wa mara kwa mara kutoka kwa wizara, ukianza na ule wa mwaka wa 2015 wa kupunguza uzalishaji ngano. Maazimio ya miaka 30 ya kukuza na kuzalisha ngano yalididimia hatua kwa hatua katika Ufalme hadi ulipositishwa kabisa mnamo mwaka wa 2008 kutokana na shaka ya upunguaji mkubwa wa raslimali ya maji. Ijapo serikali ya Saudia ilioondoa marafuku ya kilimo cha ngano mwaka jana chini ya masharti maalum, uzalishaji wa lisho la kijani ulipigwa marafuku kabisa kwa vile hutumia maji hadi mara sita zaidi yam mea wa ngano.

Saudia haikuwa peke yake kati ya nchi za Guba zilizo na shida kubwa ya maji. Nchi ya Falme za Kiarabu ilikumbana na kudidimia kwa raslimali ya maji na ikageukia kuagiza takriban asilimia 90 ya chakula chake kutoka nje. Hivyo, nchi hii pia ikaanza kushindiza uwekezaji wa kilimo ng’ambo.

Nchi hizi mbili zinazokumbana na changamoto sawa, zilitangaza kwa pamoja “Mkakati wa Nia” mwaka jana ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijeshi. Hii ni pamoja na kuanzisha mkakati wa pamoja wa usalama wa chakula, ikiwemo mipango ya kunasa uwezekano mkubwa wa uzalishaji wa kilimo na mifugo pamoja na kushirikiana katika miradi ya pamoja.

Kwa miaka michache tu iliyopita, Falme hii iliweza kuthibiti takriban zaidi ya feddan milioni 4.25 ya ardhi zilizoenea katika nchi zaidi ya 60, huku Saudia ikithibiti takriban feddan milioni 4 ulimwenguni.

Baadhi ya watu wametaja pilkapilka hizi za ununuzi na ukodishaji wa maeneo makubwa ya ardhi katika nchi zilizo na uwezo mkubwa wa kilimo kama ukoloni mamboleo, ambao umefanikisha usalama wa chakula katika nchi zinazowekeza huku zikijinufaisha kwa raslimali ambazo haziwezi kutumika tena, ikiwemo maji, nchini ambamo shughuli za kilimo hufanyika.

Wawekezaji kutoka Guba walipata suluhu Misri, nchi ambayo yazidi kufuata sera bepari za ukulima ambazo huzipa kipaumbele uwekezaji wa mashamba makubwa, kilimo cha kisasa cha usafirishaji mazao nje ya nchi kuliko mikakati maalum ya uzalishaji mazao na mbinu asili za ukulima katika bonde na Delta la Nile.

***

“Andamana nami nchini Misri

uone nchi ilivyo badilika, taswira iliyo tofauti

kuliko miaka miwili ama mitatu iliyopita.

Kati ya utawala miwili, si fananishi, ama kufa moyo,

Ama kupiga kelele kwa kicheko.

Ni haki ya watoto wangu kuiona 

Misri, nchi yangu,

Katika millennia,iking’aa upya iwezekanavyo.?

Hivyo ndivyo wimbo wa taifa ulivyochezwa na runinga zote za kitaifa nchini Misri, mwanzoni wa mwaka wa 1997 wakati Rais Hosni Mubarak alizuru Jangwa la Magharibi nchini Misri, kilomita 225 pekee kusini mwa Aswan. Iliyogeuka kuwa picha maarufu zaidi katika utawala wa Mubarak, alionekana kuinua mikono yake kuwapigia saluti wahandisi kuanzisha mradi wa Toshka.

Ujenzi wa mradi huu ulipangwa kuanza mwaka wa 1997 hadi 2017. Maazimio yake yalikuwa kujengwa kwa Delta kusini kwa jangwa la Western Desert,  kuongezwa kwa faddan milioni moja ya mashamba ya kilimo, kubuniwa kwa jamii za viwanda na makao, kubuniwa kwa nafasi 45,000 mpya za kazi kila mwaka ili kutosheleza Wamisri milioni 4-6 ndani ya miaka 10.

Hata hivyo, miaka mingi imepita, na Misri haijanufaika na mradi wa Toshka. Ongezeko kubwa la watu ndani ya bonde la Nile na swala la usalama wa chakula haujatatuliwa. Kwa upande mwingine, mradi huu umenufaisha pakubwa wawekezaji wa kigeni.

Falme za Kiarabu ilikita mizizi katika mradi huu mapema mwaka wa 1997, ilipotoa msaada wa dola milioni 100 kupitia shirika la Abu Dhabi Fund for Development. Pesa hizi zilitumika katika ujenzi na ulainishaji wa mfereji muhimu wa mradi huu. Ukiwa na urefu wa takriban kilomita 51, umeshabadilishwa jina na kuitwa “Sheikh Zayed Canal” jina lake mtawala wa Abu Dhabi.

Mamlaka inayohusika ilitenga sehemu moja kwa kumi ya mgao wa nchi ya Misri wa maji ya mto Nile (fiti bilioni 5.5 mchemraba kutoka kwa fiti bilioni 55.5 mchemraba) wa mradi huu. Kituo cha megawiti 250 kiliundwa kuvuta maji kutoka bonde la Toshka, ambalo limeshikana na Ziwa Nasser na hujazwa na maji yatokanayo na mafuriko, hadi katika mfereji ule wa Sheikh Zayed Canal, unao gawa maji yake katika matawi manne yanayoenea kando kando ya maeneo yatakayo “boreshwa.”

Mnamo mwaka wa 2003, maji yalisukumwa katika mfereji huu kwa mara ya kwanza, hivyo kupelekea mfululizo wa wawekezaji katika eneo la Toshka. Kwa sasa, mradi huu umeenea takriban feddan 405,000, miongoni wake ikiwa feddan 100,000 inayomilikiwa na kampuni ya Al Rajhi International for Investment, iliyo na makao yake nchini Saudia na feddan 100,000 nyingine inayomilikiwa na kampuni ya Al Dahra for Agricultural Development iliyo na makao yake katika Falme za Kiarabu.

Misri pia inamiliki hisa katika mradi huu: feddan 25,000 tayari yako chini ya utawala ule wa National Service Products Organisation nchini Misri, ambalo lilinunua ardhi hii kutoka kampuni ya KADCO (Kingdom Agricultural Development Company) ya Al-Waleed bin Talal, mwaka wa 2017. Feddan 62,000 zaidi iko chini ya kampuni ya South Valley for Development na hivi juzi feddan 92,000 ilitengewa kampuni ya Egyptian Countryside Development Company – kampuni hizi mbili zikiwa zinamilikiwa na makampuni ya kiserikali. Feddan elfu kumi pia ilitengewa wizara ya nyumba kwa ujenzi wa  mji mpya wa Toshka, huku feddan 16,000 ikiwa bado haijatengwa.

Hivyo basi, makampuni haya mawili ya Guba, Al Rajhi na Al Dahra, yanamiliki takriban asilimia 49.4 ya ardhi yote ya mradi huu.

Eygpt image3

Makampuni ya uwekezaji ya Guba yalinyakuwa ardhi huko Toshka kupitia mikataba ya ardhi, iliyopelekea kampuni kumiliki ardhi kwa awamu. Makubaliano ya idadi ya feddan inayokusudiwa kukombolewa hufanyika katika kila awamu na baada ya kukamilika kwa kila awamu, umiliki wa ardhi hupewa kampuni hadi ambapo kampuni hiyo mwishowe hupata umiliki kamilifu.

Mnamo mwaka wa 2014 ripoti ya mamlaka ya Central Auditing Authority ilisema kwamba ardhi iliuzwa kwa LE50 (US$ 3) kwa kila feddan, huku bei la soko likikadiriwa kuwa LE 11,000 (US$ 635) wakati huo. Serikali ya Misri ililipia gharama ya ujenzi wa miundo misingi yote ya mfumo wa mfereji, huku wawekezaji wakigharamia shughuli za kukomboa ardhi kwa menajili ya ukulima na ukamilishaji wa ujenzi wa matawi kutoka mfereji wa umwagiliaji maji, mifumo ya kuondoa maji na vituo vya kusukuma maji katika ardhi walionyakua.

***

Mtandao wa uwekezaji usioeleweka

Mtandao wa shughuli za uwekezaji na nchi za Guba katika ukulima nchini Misri umefungamana, jinsi ambavyo matarajio ya wawekezaji wakibinafsi wa Misri na wale wa nchi za Guba zinavyoungamana na uhusiano mpana wa kisiasa na kiuchumi kati ya Misri na nchi za Guba.

Shirika la Al Rajhi Investment Group lililo na makao yake Saudia, linamilikiwa na familia ya Al Rajhi. Lilianzishwa na Sulaiman al-Rajhi ambaye ni mmoja wa washirika wakuu katika mpangilio wa Mfalme Abdullah wa kuwekeza nchi za kigeni. Ilipenya nchini Misri mnamo mwaka wa 2009.

Kwa sasa, Al Rajhi inamiliki kampuni ya Tabuk Agriculture Development Company, ambayo nayo ni mshirika wa muungano wa Jannat Agricultural Investment Company. Makampuni sita mengine yenye makao yake nchini Saudia, ambayo yanajishughulisha na uwekezaji wa ukulima, yako chini ya upeo wa Jannat, miongoni mwao ikiwa Al Kharif ya umwagiliaji maji pamoja na Al Marai.

Kampuni ya Saudi Jannat Agricultural Investment Company inamiliki takriban asilimia 78 ya hisa katika kampuni ya Rakha for Agricultural Investment ya Misri, ambayo inamiliki shirika la serikali la REGWA, kampuni ya mfumo wa umwagiliaji maji iliyoshutumiwa kwa  visa vya ufisadi na unyakuzi wa ardhi katika kesi kadhaa.

Rakha for Agricultural Investment pia inahusiana na Wafrah for Industry and Development, kampuni iliyo na makao yake nchini Saudia, ambayo inajishughulisha na uzalishaji wa chakula.

Al Dahra ni shirika la nchi ya Falme za Kiarabu inayojihusisha na kilimo, uzalishaji na ugavi wa lisho kwa mamlaka ya Food Security Authority ya nchi ya Falme za Kiarabu. Inamilikiwa pia na Hamdan bin Zayed Al Nahyan ambaye ni jamaa wa kifalme, na muwakilishi wa mtawala wa eneo la magharibi ya nchi ya Abu Dhabi, hivyo kulifanya shirika hili kuhusika pakubwa katika mipango ya serikali ya kutekeleza utaratibu wa usalama wa chakula wa Emirates Strategic Food Security Program.

Kampuni hii ilianza shughuli zake nchini Misri mnamo mwaka wa 2006, na kuanzisha Al Dahra Egypt mwaka wa 2007. Ilishirikiana na serikali za Misri na ya Falme za Kiarabu kupitia ununuzi kampuni ya Misri ya Navigator for Agricultural Investment.

Makampuni haya mawili ya Al Rajhi na Al Dahra yana uhusiano mkubwa na serikali za nchi zao na yanajihusisha pakubwa na mipango ya uwekezaji wa kilimo katika nchi geni iliyoanzishwa na Saudia na Falme za Kiarabu, kama ule mkakati wa “Strategy of Resolve.”

Egypt image4

Tangu uanzilishi wa mpango wa usalama wa chakula wa Gulf Food Security, kampuni ya Falme za Kiarabu ya Al Dahra tayari imeshanyakuwa feddan 400,000 ulimwenguni, ikiwemo feddan 116,000 maeneo ya Toshka, Oweinat, Salheya na Nubaria nchini Misri pekee. Kampuni ya Al Rajhi imejipatia faddan 120,000 nchini Mauritania na inapanga kunyakua feddan 450,000 nchini Sudan, pamoja na feddan 100,000 ambazo imeshanyakuwa eneo la Toshka.

Mawakili kadhaa wamewasilisha kesi dhidi ya makampuni haya yaliyotajwa hapo awali, wakidai kwamba baadhi ya masharti ya mikataba ilienda kinyume na katiba ya Misri na kupelekea kufujwa kwa raslimali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa wakili mmoja aliyeshughulikia mojawapo ya kesi hizi, mashirika makubwa kwa kawaida huendesha shughuli zao chini ya utando uliyopindamana na mafaa, ikiwa ni mbinu ya kujipatia umiliki wa kipekee chini ya singizio ya makampuni kadhaa.

Wakili huyu aliyezungumuza jina lake likiwa limebanwa, anasema kwamba mbinu hii husaidia kuficha kiwango cha ushawishi wao katika soko, kwa sababu hisa hugawiwa makampuni mengi, ambayo hurahisisha kuepuka ulipaji kodi.

Mpangilio huu huhakikisha mashirika yote yanayohusika hunufaika. Kwa mfano, Al Rajhi, kampuni ya Saudia inayokuza mmea wa alfalfa, nafaka inayokuzwa kulisha mifugo, ni mshirika wa Almarai, kampuni inalojijusisha na bidhaa ya maziwa. Kampuni hii pia ni mshirika wa Alkhorayef, ambayo hushughulika na mifumo ya umwagiliaji maji. Makampuni haya yote huendeleza shughuli zao chini ya muungano wa uwekezaji wa kilimo wa Jannat ya Saudia, ambayo huisaidia kuongeza mgao wao wa soko na kukithi mahitaji. Pia, hurahisisha mikataba isiyo ya moja kwa moja, na makampuni mengine kama vile Wafrah, ambayo ni kampuni ya vyakula ya Saudia inayotengeneza nafaka na pasta, na Marina, kampuni ya Misri inayotengeneza vyakula vya mifugo. Mbinu hii ya uwekezaji inanuia kuthibiti ugavi mzima wa mtando wa chakula, kuanza na bidhaa za uzalishaji hadi kufikia uzalishaji mwenyewe pamoja na harakati za uzalishaji, na mwishowe, soko ili kuhakikisha uthibiti kamilifu wa bidhaa ya vyakula.

***

Mikataba iliyo na shaka

Mikataba baina ya serikali ya Misri na wawekezaji wa Guba, haswa katika eneo la Toshka, limejaa ukiukaji sheria, kwa mujibu wa habari zilizochapishwa na vyombo vya habari, pamoja na nakala rasmi za stakabathi zilizokuwa mikononi mwa Mada Masr.

Haya yote yalianza na mkataba kati ya serikali ya Misri na Al-Waleed bin Talal, tajiri mkubwa kutoka Saudia mnamo mwaka wa 1998. Kampuni ya Kingdom Holding Company wakati huo, ilikuwa ya kwanza miongoni ya makampuni ya uwekezaji kutoka Guba iliyonunua ardhi eneo la Toshka, ikipata feddan 100,000 kwa bei ya LE50 (US$3) kwa kila feddan, hivyo, kuifanya bei yote  kwa jumla kufikia milioni LE5 (US$ 289,000), asilimia 20 pekee ya hela hizi ililipwa wakati wa utiaji sahihi kandarasi. Hakuna chochote kilichotajwa katika kandarasi hii kuhusu jinsi pesa zilizobaki zingelipwa, na haijulikani ikiwa pesa zilizobaki zililipwa baadaye. Kandarasi hii ilimuwezesha muwekezaji kukuza zao lolote bila pasi kuhitaji idhini kutoka kwa wizara husika. Pia, ilipatia kampuni haki ya kuagiza mbegu kutoka nje pamoja na aina ya mimea na mifugo bila idhini rasmi. Zaidi ya hayo, vipengee katika kandarasi hii ilipatia muwekezaji ruhusa ya kutolipa kodi.

Baada ya uchunguzi wa kina, kufuatia mapinduzi ya mwaka wa 2011, baadhi ya vipengee katika kandarasii hii ilirekebishwa, na kampuni ya bin Talal ilikubali kuregesha kipande cha ardhi ambacho hakiwakimekombolewa na ambacho kilijumuisha feddan 75,000. Katika mwaka wa 2017, jeshi la Misri lilinunua feddan 25,000 zilizobakia kutoka kwa bin Talal kwa bei ya LEI milioni 1.25.

Hali kadhalika, katika mwaka wa 2011, kituo cha kutetea haki za kiuchumi la Egyptian Center for Social and Economic Rights, liliwasilisha kesi dhidi ya Al Dahra likitaka kubatilishwa kwa kandarasi. Kesi hii ilidai kwamba uuzaji wa feddan 100,000 ya ardhi katika eneo la Toshka ulihusisha ubadhirifu mkubwa wa fedha na kwamba ardhi ya kitaifa iliuzwa kwa bei ya chini mno kuliko makadirio ya bei ya kawaida sokoni, kwa kuwa ardhi iliuzwa kwa LE50 (US$3) kwa kila feddan huku bei ya wastani ilikuwa LE11,000 EGP (US$ 637) kwa kila feddan. Kulingana na ripoti zaidi zilizotolewa na kituo hiki, baraza la Egyptian State Council lilitoa taarifa likipendekeza ubatilishaji wa kandarasi. Hata hivyo, afisi ya kiongozi wa mashtaka haikuendelea na uchunguzi, hivyo kupelekea kesi kusitishwa bila ya uamuzi.

Licha ya kesi hizi, sheria nchini Misri kwa hivi sasa inazuia pingamizi kisheria ya kandarasi iliyofanyika kati ya serikali na wawekezaji, isipokuwa wakati inapohusisha wawekezaji walio na maslahi katika kandarasi. Sheria hii ilipitishwa wakati Rais wa mpito wa zamani Adly Mansour alipoidhinisha marekebisho ya sheria inayohusisha haki za mashtaka mnamo mwaka wa 2014.

Pamoja na ukiukaji wa makubaliano yaliyoko ndani ya kandarasi, ukiukaji huu uhusisha utekelezaji wa wajibu kama ilivyo ndani ya kandarasi, kando na utaratibu kamili wa ukomboaji ardhi.

Kwa mfano, Al Rajhi ilipokea feddan 25,000 kutoka kwa feddan 100,000 waliokubaliana wangekomboa kwa awamu tano. Mapema mwaka wa 2010, kampuni hii iliwasilisha ombi la ukaguzi, huku ikidai kukamilisha utaratibu wa kukomboa feddan 25,000.

Mwaka jana, mamlaka ya General Authority for Agricultural Development Projects iliidhinisha kukabidhiwa kwa feddan 17,000 kwa kampuni hiyo, ili kuanzisha kwa awamu ya pili ya kukomboa ardhi kwa shughuli ya kilimo kwa msingi kwamba kampuni kwa kweli ilishatamatisha awamu ya kwanza, ambayo ilitenga feddan 25,000. Hata hivyo, unchanganuzi kutumia picha za setilaiti ulithibitisha kuwa hivyo sivyo ndivyo, kwa kuwa eneo lote zima lililolimwa mwaka wa 2013 ilikuwa takriban feddan 6,000 na, katika mwaka wa 2019, ilifikia kuwa feddan 10,402.

Egypt image1

Ukiukaji mwingine dhidi ya Al Dahra ulibainishwa na duru za kuaminika ndani ya taasisi ya Centre for Water Research in Abu Simbel, pale picha za setilaiti zilionyesha kwamba kampuni ilitumia feddan zote 18,351 za ardhi kwa ukuzaji wa alfalfa, kinyume na kandarasi, ambayo ilihitaji asilimia 5 pekee ya shamba kutumika kwa ukuzaji wa alfalfa.

Huku Hamdy Abdel Dayem, msemaji rasmi wa wizara ya kilimo, akithibitishia Mada Masr kwamba kandarasi nyingi humuwekea muwekezaji kiwango cha asilimia 5 pekee ya ardhi kwa upanzi wa alfalfa, ili kulinda raslimali ya maji, mbunge Raef Temraz, aliyekuwa naibu wa kamati ya bunge ya ukulima na umwagiliaji maji, alitangaza kwamba upanzi wa alfalfa ulitumia asilimia 25 ya ardhi nzima iliyotumika kwa upanzi eneo la Toshka na lile la la ugavana la New Valley. Temraz alidokeza jinsi ambavyo mmea wa alfalfa husafirishwa hadi nchi za Uarabuni kwa kiasi kikubwa, haswa nchi ya Saudia na Falme za Kiarabu.

***

Ubadhirifu katika ngazi zote

Gamal Seyam, profesa wa uchumi wa kilimo katika Chuo Kikuu cha Cairo, akumbuka jinsi ambavyo Wizara ya Umwagiliaji Maji ilivyosihi chuo kutekeleza utafiti utakaobainisha ufanisi wa mradi wa Toshka, baada ya miaka mbili wa uanzilishi wake, kufuatia manung’uniko ya umma kwamba mradi ulishaanguka.

Seyam aeleza jinsi mazao yenye thamani kuu, kama vile matunda na mboga, kwa kawaida hutoa nafasi bora zaidi ya kiuchumi, katika maazimio ya ukombozi wa ardhi, kwa vile mazao haya yanaweza kuboreshwa hivyo kuzifanya kuwa na thamani kubwa, kubuni nafasi za kazi na kuinua kiwango cha pato la taifa.

Aeleza kwamba aina hii ya uwekezaji wa kigeni, hauletei taifa pato kwa kuwa huwaruhusu wawekezaji kununua maji kwa bei ya chini, kujipatia ardhi kwa bei duni na kusafirisha nyingi ya mazao yao hadi nchi za kigeni. Zaidi ya hayo, mtaji wa mashirika haya huwa na makao yake nje ya Misri. Hivyo basi, hakuna manufaa kamili kwa uchumi wa kitaifa.

Kulingana na Seyam, taifa lapaswa kufanya mikataba na makampuni ya uwekezaji kwa misingi uchanganuzi wa kiuchumi wa muda murefu wala sio kulenga manufaa ya muda mfupi wa kifedha, kwa vile mipango ya aina hii huruhusu mashirika ya nchi za Guba kujitengea maeneo na kuthibiti utawala wa ardhi ya Misri. Seyam ashuku uamuzi wa serikali kuuzia wawekezaji wa kigeni ardhi ya taifa kwa LE50 (US$3) kwa kila feddan, huku bei ya ardhi ya jangwa hivi leo ni LE40,000 (US$2,311) kwa kila feddan. “Hata kama bei hii iliruhusiwa kwa madhumuni ya uwekezaji, itakuwaje wawekezaji wa kigeni kupewa nafasi bora zaidi?” auliza Seyam.

Katika utafiti wa kiuchumi aliotayarisha, Seyam aelezea vile ukubwa wa eneo lote lililotumika na makampuni kwa upanzi lilikuwa takriban feddan 29,000. Kiwango cha maji cha wastani kilichotumika kilikuwa takriban milioni 210 mita za ujazo kwa mwaka. Kama tunaweza kadiria bei sokoni ya mita ya ujazo moja ya maji kuwa LE2 (US$0.12), hii inamaanisha kwamba muwekezaji alinunua maji yenye thamani ya LE420 milioni (US$24.3 milioni) kwa milioni LE20 (US$ 1.2milioni) pekee.

Huu “unyakuzi wa maji” hautendeki tu katika feddan 29,000 zinazohusisha ardhi ambazo kwa sasa zinatumika kwa upanzi, ila tu unyakuzi huu utaenea hadi siku za usoni ambapo makampuni haya mawili yatamiliki feddan 200,000 kati yao. Uchanganuzi wa Seyam unathibitishwa na mmoja wa wanaofanya kazi katika mojawapo ya makampuni haya mawili yanayomilikiwa na wawekezaji wa Guba katika eneo la Toshka, anayenukuu mmoja wa wanaosafirisha bidhaa ndani ya nchi akisema: “Tunanunua maji, na sio alfalfa.”

Kiwango sawa hicho cha maji, cha takriban 210 mita za ujazo, asema Seyam, unatosha kukuza feddan 84,000 ya ngano, hivyo kuongeza kiwango cha zao muhimu nchini Misri kwa takriban tani 62,000. Misri hutumia takriban tani 16,000 ya ngano kwa mwaka, na inaongoza kwa uagizaji ngano kutoka nje duniani. Mwaka jana, nchi hii iliagiza takriban tani milioini 6 ya ngano.

Katika taarifa rasmi kuhusu unyakuzi wa ardhi kwa shughuli za kilimo, wawekezaji husisitiza wasiwasi wao kuhusu kulinda raslimali ya maji kwa uendelevu wa miradi yao kwa siku za usoni kupitia uzalishaji mimea kwa matumizi ya nyumbani. Nchini Misri, serikali imeshinikiza makampuni kukuza ngano kama mojawapo ya zao muhimu ambayo inategemeza watu wa Misri. Hatahivyo, serikali imeshindwa kusimamia makampuni haya ili kuhakikisha yanakuza ngano. Kwa mujibu wa mfanya kazi mmoja katika kampuni moja ya Guba eneo la Toshka, ambaye alitaka jina lake libanwe, kiwango chote cha ngano kilichozalishwa na kampuni hii kilikuwa cha tani 15,000 pekee, ikimaanisha kwamba eneo lilotengwa kwa upanzi wa ngano ilikuwa feddan 6,000 pekee.

Hali kadhalika, katika mwaka wa 2007 Saudia iliamua kupunguza na kupima kiwango cha maji inayotumia kupitia uagizaji wa alfalfa kutoka nje, ambayo hutumika katika lisho. Kwa vile mmea wa alfalfa hutumia kiwango kikubwa zaidi cha maji, (kila feddan ya alfalfa huitaji takriban 8,000 mita za ujazo ya maji kwa upanzi), baraza la mawaziri nchini Saudia lilipitisha uamuzi mwaka wa 2011 ikiishurutisha mashamba ya maziwa kuagiza kiwango cha lisho ambacho kinalingana na kiwango cha bidhaa mashamba haya husafirisha nchi za nje. Katika mwaka wa 2015, baraza hili lilitekeleza marufuku kamilifu ya upanzi wa lisho. Hii inamaanisha kwamba mashamba ya maziwa nchini Saudia yanategemea kikamilifu lisho inayoagizwa kutoka uwekezaji wa kilimo wa nchi za ng’ambo kama vile Misri.

Kwa upande wake, mkakati wa wizara ya kilimo nchini Misri wa mwaka wa 2030 unalenga kuhifadhi maji kupitia ustawishaji wa mfumo wa umwagiliaji maji katika Delta la Nile na kupunguza ukuzaji wa baadhi ya mazao muhimu kama vile mpunga – ambayo ni nguzo ya wakulima nchini Misri wanauona kama mojawapo ya mazao yenye faida kubwa. Chini ya mkakati huu, taifa litahifadhi bilioni 14.5 mita za ujazo za maji kutoka kwa eneo la bonde na Delta la Nile na kiasi kingine cha maji haya kitatumika katika umwagiliaji maji na upanzi wa mazao katika baadhi ya miradi iliyo chini ya serikali, katika ardhi zilizokombolewa. Ki msingi ni kwamba, serikali inayachukuwa maji kutoka kwa wakulima wenyeji na kubadilisha mkondo wake ili kuwanufaisha wawekezaji wa kigeni, kwa madhumuni ya upanzi wa mmea wa alfalfa na kusafirisha bidhaa nje ya nchi, huku ikifyonza raslimali la taifa.

Egypt image2

Ufyonzaji huu wa raslimali ya nchi na makampuni haya, unaendelezwa pia katika nishati. Mbinu za kisasa zinazotumiwa na wawekezaji wa kigeni kwa uzalishaji huitaji kiwango kikubwa cha nishati katika uletaji na ugavi wa maji katika mashamba na kuendesha mifereji ya umwagiliaji maji. Kwa mujibu wa duru ya kuaminika katika mojawapo ya mashamba inayoendeshwa na Al Rajhi, inakadiriwa kwamba kampuni hii hutumia milioni 1.5 saa kilowati kila mwezi, huku Al Dahra ikitumia milioni 2 saa kilowati kwa mwezi. Hii inamaanisha kwamba utumiaji nishati na makampuni haya mawili kwa pamoja ni asilimia 28 ya nishati yote inayohitajika kuendesha laini la kwanza la gari-moshi la chini kwa chini jijini Cairo, ambayo ni saa kilowati milioni 12.5 kwa mwezi.

Licha ya kutanda kwa eneo la ardhi linalomilikiwa na makampuni haya mawili ya Guba, wafanya kazi wote kwa ujumla hawazidi 200, kwa mujibu wa duru ya kuaminika katika kampuni moja. Idadi hii ni ya chini mno, ikilinganishwa na kiwango cha kazi kinachohitajika katika maeneo sawia ya ardhi kama yale ya bonde la ugavana la Nile na lile la Delta. Pia, linatofautiana na mojawapo ya malengo makuu ya mradi wa Toshka, ambao unakusudiwa kubuni nafasi 450,000 za kazi kila mwaka na kuwapa manyumba idadi ya wananchi kati ya milioni 4 hadi 6 kupitia usitawishaji ya makao ya miji katika maeneo hayo.

Nchi ya Misri ni miongoni ya mataifa yaliyolengwa kwa unyakuzi wa ardhi kwa madhumuni ya kuendeleza kilimo na mashirika yanayomilikiwa na nchi za Guba. Hata hivyo, baadhi ya nchi zimeanza kukomesha haina hii ya uwekezaji. Nchi ya Sudan ambayo inaongoza kwa ukodishaji ardhi kwa kilimo cha lisho, hivi karibuni imedinda kukubali uwekezaji zaidi wa kilimo, baada ya baadhi ya wabunge kuonyesha wasiwasi wao kuhusu kupungua kwa raslimali ya maji ya chini kwa chini. Katika mwaka wa 2013, waandamanaji walizua rapsha kukataa ugawaji ardhi kwa wawekezaji wa nchi za Guba, na hasira iliibuka kutokana na kupoteza ardhi kama ilivoangaziwa na maandamano yanayoendelea nchini Sudan.

Sherif Fayad, ambaye ni profesa wa uchumi wa kilimo katika baraza la utafiti la Desert Research Council, aeleza kwamba tatizo la ukombozi wa ardhi jangwani nchini Misri, ni ukosefu wa maono katika taifa ya kunasa uwezo wa eneo hili. Ni muhimu kuwepo kwa uwiano kati ya kinchokuzwa jangwani na kile kinachokuzwa katika bonde na Delta la Nile, ili kuwezesha utumizi kamilifu wa raslimali zilizoko, asema. Ni jambo la hekima kwamba bonde la Nile la zamani kusalia kuwa kitovu cha kuzalishia viwanda enyeji mazao muhimu, kwa vile baadhi ya mazao yanahitaji kushughulikiwa vilivyo (kama pamba), huku mengine yakihitaji ardhi iliyo na rotuba nyingi (kama ngano), ama maji mengi (kama mpunga), asema. Pia, soko ya mazao haya imekaribia mahali ambapo yanazalishwa na kuboreshwa. Inapohusu ardhi ya jangwa, hii inafaa kwa ukuzaji wa matunda ya jamii ya mchungwa miongoni mwa matunda mengine kama vile mizabibu, komamanga na mapera kando na ukuzaji wa mimea yanaonukia ama yale ya kijani ambayo hayahitaji maji mengi, Fayad asema.

Kuna ukosefu wa sera za kitaasisi nchini Misri ambazo hunuia kulinda haki za jamii ama aina yeyote ya ujumuikaji unaohusisha jamii enyeji katika kuamua mazao yatakayopandwa na jinsi ya kuthibiti vilivyo raslimali kutumia njia mwafaka endelevu, asema.

Muwekezaji yeyote yule, huja kwa nia inayolenga kujinufaisha zaidi kutoka kwa mkataba, lakini taifa lazima lifuate malengo yake inapohusisha sekta ya kibinafsi, Fayad asema. Lazima iwe na utaratibu wa kuwashurutisha wawekezaji kuzingatia madai yake. Muwekezaji hutoa fedha, utaalamu na teknologia. Kwa upande wake, taifa hutoa ardhi, maji, nishati, vibarua, umeme na hali bora ya utenda kazi. Raslimali hii yote inamilikiwa na wenyeji.

Huku wawekezaji wakinufaika kutokana na uwekezaji wao kupitia upataji ardhi, hakuna kile kinachoweza chukua nafasi ya maji, ardhi na athari za tabia nchi, Fayad asema.

“Ikiwa hivyo ndivyo itakavyokuwa, kwa nini basi tusikodishe nchi nzima?” auliza, akiongeza kusema kwamba kuwepo kwa maono kamili ya wawekezaji minghairi ya maono kutoka taifa, hupelekea wenyeji kupoteza haki zao.

Makala haya ya unyakuzi wa raslimali ghafi ya Misri, ili kulinda usalama wa chakula wa eneo la Guba, imewezeshwa na usaidizi kutoka kwa InfoNile na Pulitzer Center.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts