Waridi: Mto Nile wa samawati unaodhuru maua na jamii za Uhabeshi

Na: Ayele Addis Ambelu

Makala haya yametayarishwa kwa hisani ya InfoNile na Code for Africa pamoja na usaidizi kutoka kwa Pulitzer Center

Abreham Bekele mwenye umri wa miaka 58 kutoka kijiji cha Meshenti, karibu na jiji la Dar, eneo la Amhara nchini Uhabeshi alibakia fukara baada ya shamba alilotegemea pamoja na familia yake ya watu kumi na moja kwa maishilio kunyakuliwa na mwekezaji mnamo mwaka wa 2008 kukuza waridi.

“Tulifurushwa bila ya fidia mwafaka,” akumbuka vyema kwa hasira, na “sasa tunapambana kuishi bila shamba, chakula, maji.”

Kisa kilichomkumba ni kama maisha ya mamilioni ya Wahabeshi waliopoteza mashamba yao kwa wawekezaji, wanaolenga uzalishaji wa maua na mazao ya kilimo ya kusafirishwa nje ya nchi.

Uhabeshi ni nchi ya pili kubwa barani Africa baada ya Kenya katika usafirishaji maua hadi Mashariki ya Kati, Ufaransa, Ujerumani, Canada, Uswidi, Uingereza na Uholanzi miongoni mwa nchi zingine.

Takwimu kutoka kwa shirika la uzalishaji wa mboga na maua zinazouzwa nchi za nje la Uhabeshi (EPHEA) zaonyesha kwamba, Uhabeshi ilijipatia pato la kiasi cha dola za Kimarekani 300 milioni kwa uuzaji wa maua na mazao mengine ya mboga katika mwaka 2017. Na ndani ya mwaka wa fedha uliopita, sekta ya mboga na maua ililetea nchi ya Uhabeshi kiwango cha pesa kisichopungua dola milioni 271 za Kimarekani, kutokana na uuzaji wa maua haswa.

Picture13

Zelalem Berhanie, mkuu wa tume ya mipango ya kitaifa asema kuwa Uhabeshi yalenga “kujipatia dola nusu milioni kutoka sekta ya maua kufikia mwisho wa muhula wa pili ujulikanao kama Growth and Transformaion Plan.” Ukuwaji wa pili wa Growth and Transformation Plan (2015/16-2019/20) GTPII inazingatiwa kuwa hatua muhimu kuafikia ono la Uhabeshi kuwa nchi ya chini ya mapato ya kati kufikia mwaka wa 2025.

Hata hivyo, hali si shwari! Kadiri ambavyo sekta ya maua inavyonawiri nchini Uhabeshi, ndivyo ambavyo watu 3,000 wanavyohamishwa na wawekezaji wanaonyakua ardhi ili kuanzisha mashamba ya maua, kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika la Amhara National Regional State Prevention and Food Security Coordination Office.

Hifadhidata ya Ardhi Matriki, ambayo hukusanya takwimu za unyakuzi wa ardhi kutoka kwa serikali, makampuni na mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari na wananchi, imefuatilia takriban hektari milioni 1.4 ya mashamba yaliyonyakuliwa nchini Uhabeshi katika miongo ya hivi karibuni. Mikataba 120 imeshakamilika nchi nzima, huku mikataba 15 ingali inajadiliwa na ambayo huenda ikaongezea hektari 0.5 milioni itakapokamilika.

Thuluthi mbili ya ardhi iliyonyakuliwa nchini iligawiwa wawekezaji wa kimataifa. Makampuni ya Kihindi ndio yalinyakuwa vipande vikubwa vya ardhi, haswa kwa uzalishaji nishati itokanayo na mimea pamoja na kuendeleza kilimo cha mashamba makubwa, ikiwemo mashamba ya maua. Makampuni kutoka Saudia, Marekani, Italia, Malaysia, Uchina, Austria, Israeli, Uturuki, Canada na Singapore ni wawekezaji wakubwa pia.

Kama vile Abrehem, Hiwote Yazie, aliye na umri wa miaka 27, mkaazi wa kijiji cha Zenezelma karibu na jiji la Dar, eneo la Amhara asimulia kwamba jamii yake imebakia kuwa “wahamiaji katika ardhi ya iliyomilikiwa na mababu zao.”

Anasema kwamba jamii yake haikupoteza ardhi tu, bali ilipoteza pia maji iliyoko mitoni na ziwani. “Maji asili tunayo, ila hatuwezi yanywa. Wawekezaji waliyachukuwa,” aongeza kusema Hiwote.

“Maji asili tunayo, ila hatuwezi yanywa. Wawekezaji waliyachukuwa,” aongeza kusema Hiwote.

Kijiji cha Zenezelma ambamo Hiwote alikuwa anaishi, kiko kilomita tatu kutoka Mto Nile na takriban kilomita 4.7 kutoka Ziwa Tana, chanzo cha Mto wa Blue Nile.

Siku za hivi karibuni nchi ya Uhabeshi ilitoa hektari 6,000 ya ardhi kwa sekta ya maua katika maeneo inayoshirikisha Bahir Dar, upande wa Ziwa Tana na upande wa Mto wa Blue Nile kwa mujibu wa tume ya Amhara Investment Commission.

Wawekezaji 10 wakubwa wa maua nchini Uhabeshi wanapatikana karibu na Ziwa Tana na Mto wa Blue Nile, eneo la hektari 12,000 upande wa Tana na hektari 2,000 zaidi upande wa Mto wa Blue Nile. Hii ni kwa mujibu wa takwimu kutoka shirika la Ethiopian Horticulture Producers and Exporters Association (EHPEA), ambalo linanukuu makampuni, ikiwa pamoja na Giovanni Alfano Farm, Condor Farms PLC, Fontana Horticulture PLC, Pina Flowers PLC, Arini Flowers PLC, Solo Agro Tech PLC, Tal Flowers PLC, na Joy techfresh PLC miongoni ya makampuni mengine.

Ni dhahiri kwamba makampuni haya hayalengi tu ardhi iliyo na rotuba katika eneo hili, ila yanalenga pia maji ya mto na ziwa.

Asrat Tsehay, ambaye ni mkuu wa mamlaka ile ya Ethiopian Blue Nile River Basin Authority asema kuwa wawekezaji wa makampuni ya maua hutumia maji mengi zaidi ikilinganishwa na wenyeji.

“Nchi kavu kaskazini ya Uhabeshi watu wanaishi kwa lita tano ya maji kwa wiki pekee, huku idadi kubwa ya mifugo yao ikiangamia,” ajadili Asrat, “kwa wastani, kila shina la mmea wa waridi (pale) linatumia lita saba la maji kwa wiki.”

Adem Woku, ambaye ni mkuu katika idara ya uhusiano bora ya Amhara National Regional State Water, Irrigation and Energy Development Bureau, ahisi kwamba, uhakika, hii “inafyonza maji ya eneo hili.”

Uzalishaji maua katika eneo hili yahitaji takriban, “vidimbwi vya kuogelea 20,000 vya Olimpiki vilivyojaa maji kila mwaka,” asema Meselech Zelalem, mwanasayansi wa maswala ya maji katika shirika la kitaifa la Amhara National Regional State Water, Irrigation and Energy Development Bureau. Maji haya hufyonzwa kutoka Ziwa Tana na Mto wa Blue Nile.

Dkt. Mesay Abebe, ambaye ni mtaalam na mchanganuzi wa sekta ya maua nchini Uhabeshi, alaumu sekta hii kwa “utumiaji mkubwa wa raslimali asili.”

“Hii” adumisha Dkt. Mesay, “inasababisha uchafuzi wa udongo, maji na hewa kutokana na utumizi usiofaa wa mbolea na kemikali dhidi ya wadudu pamoja na mifumo duni ya taka.”

Picture18

Kwa vile imejaa madini kupita kiasi, asimulia Dkt. Mesay, maji haya machafu huwezesha ukuwaji wa mimea ndani ya mito na maziwa. Utafiti mwingi pamoja na habari zaonyesha kwamba Ziwa Tana linazidi kupungua kutokana na kuingiliwa na gugumaji vamizi.

Kando na hayo, mashamba ya maua yamekosolewa kwa kutumia mbolea na kemikali za wadudu, ambazo zaweza kuingia katika Mto wa Blue Nile na Ziwa Tana jirani, kwa urahisi. Tadele Yeshiwas Tizazu, mtafiti wa kilimo na mazingira asema kemikali kama hizi “hujikita kwa urahisi kwa maji ya chini kwa chini.”

Wakati maua yanapotayarishwa kuuzwa sokoni, husababisha taka, kama vile matawi yaliyo na chembechembe za kemikali. Ikiwa chembechembe hizi haziondolewi ipasavyo, huenda ikaleta madhara ya afya kwa binadamu na mifugo.

Kwa mfano, Shega Belay, ambaye ni mmoja wa wakulima asema kwamba jamii yake haikumbani tu na “kupungua kwa mashamba kwa shughuli za kilimo, ila pia mifugo kuangamia baada ya kumeza kemikali za wadudu.”

“Tunalalamikia maafisa wa manispaa lakini hakuna kilichotendeka. Serikali inanufaika kutokana na ushura ambapo sisi tunadhirika,” alalamika Shega.

Shirika la maua nchini Uhabeshi yaani Ethiopian Horticulture Development Agency (EHDA) ni shirika la kiserikali lilijitolea kuinua sekta hii ambayo inashirikisha maua, matunda na mboga pamoja na ile sekta ya mitishamba.

Alem Weldergerima, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hili anasema kwamba sekta hii ya maua iliendelea kutokana na jitihada za sekta ndogo za kibinafsi ambazo ziliangazia “utumizi wa udongo, maji, ekolojia na ukaribu wake na soko, nafasi ambayo nchi ya Uhabeshi iliwazawadia wapanzi wa maua.”

Solomon Worku, mwanaharakati wa kundi la Nile Water for Nile People Initiative, asema kwamba wawekezaji wa kigeni wengi katika sekta ya maua walinyakua ardhi ili kuendesha ukulima eneo ya chanzo cha Mto wa Blue Nile, hivyo kuwahamisha watu wengi bila ya kuwasaidia kuinua hali yao ya maisha.

“Walinyakuwa vipande vikubwa vya mashamba na raslimali kwa kisingizio cha maendeleo ambayo hatujayaona,” asema Solomon.

Baadhi ya mashamba haya yameshutumiwa kwa kukosa kutumia vipande walivyogawiwa kwa lengo la kusudi lao.

Alem Weldergerima, Mkurugenzi Mkuu wa EHDA anaungama kwamba baadhi ya wawekezaji hawajaitumia kikamilifu mashamba yao.

Anafichua ya kwamba shirika lake limeshatoa ilani ya onyo kwa wapanzi wa maua 25 kuhusu swala hili.

Wahasiriwa wa unyakuzi ardhi wazungumuza

Amelework Yazi, mwenye umri wa miaka 28, ambaye ni mkaazi wa kijiji cha Bezawit jijini Bahir Dar, ashutumu serikali kwa kuwapendelea wawekezaji wa kigeni, na kuwapuuza wenyeji.

“Milango imefungwa kwa vijana wenyeji walio na matumaini, ila yameachwa wazi kwa wageni,” asema Amelework.

Aster Tesema, mwenyekiti wa kundi la wakulima asilia katika kijiji cha Zegeie asema kuwa ingawa wafanyi kazi wengi wa makampuni ya maua katika kijiji chake hufanya kazi kwa bidii, “mapato yao ni duni mno” ambayo “hayawezi kuwategemeza, ilhali wawekezaji wanazalisha mamilioni ya dola kila mwaka.”

Picture8

Wakosoaji wa makampuni ya kigeni ya maua nchini Uhabeshi, mara kwa mara wamesema kwamba huku makampuni haya yanazidi kujitajirisha, wenyeji wa nchi hata hawapigi hatua.

Yordanoes Mandefero mwenye umri wa miaka 33 kutoka kijiji cha Zegie anafanya kazi katika kampuni moja ya kigeni ya maua eneo hilo. Alituomba tusifichue jina la kampuni hilo, akihofia kuftwa kazi na wakubwa wake kwa kuzungumza nasi. Afichua kwamba, pato la Wahabeshi wengi katika kampuni hiyo ni takriban, “Euro 30 kwa mwezi.”

Wawekezaji na manispaa  wajibu shutuma

Sami Banchu, mwakilishi wa shamba la Giovanni Alfano Farm asema, “wao wanashirikiana na wenyeji na kuwasaidia kujenga mashule na hosipitali ili kusisimua maendeleo.”

Vile vile, kupitia majibu yaliyoandika, Mohammed Mohayub wa Yemeni Farm, aliongeza kusema kwamba, “wao wanafanya kila kitu kwa mujibu wa vigezo jinsi inavyopaswa.”

“Kemikali dhidi ya wadudu inatumika sawa na inavyokubalika Ulaya. Sisi tuko na cheti ya usawa wa kibiashara,” asema Mohammed.

Yehenew Belay, mkuu katika afisi ya uwekezaji, jimbo la eneo la Amhara aungama kwamba wengi wa wakulima katika eneo hili wamehamishwa kutokana na uwekezaji wa sekta ya maua kwa miaka 10 iliyopita.

Alaumu tukio hili kwa “sera za serikali” zinazolenga “kuvutia wawekezaji wa kigeni huku wenyeji wakigharimika.”

Utafutaji wa suluhu mwafaka

Tafiti kadhaa, miongoni mwao ile ripoti ya mwaka wa 2008 la kongamano la mazingira, shirika lisilo la kiserikali la kutetea maswala ya kimazingira nchini Uhabeshi, na ripoti ya mwaka wa 2016 ya mtafiti Asnake Demena nchini humo, imeonya kuenea kwa athari za unyakuzi wa ardhi kwa wenyeji waliokuwa wakiishi katika ardhi hio, ambayo ni pamoja na kuhamishwa, kutoweza kutumia raslimali asili inayowakimu kimaisha. Mashamba inayotumika kwa ukulima, misitu ambayo haijaingiliwa na misitu mingine iliharibiwa kutengeneza nafasi ya miradi ya uzalishaji nishati itokanayo na mimea, ambayo imeharibu ekolojia asili, kulingana na ripoti hii.

Dkt. Mesay Abebe, mtaalam na mchanganuzi wa maswala katika sekta ya maua adokeza kwamba serikali ya nchini Uhabeshi yafaa kuchunguza ufurushaji na uhamaji huu na kuhakikisha kuwa wakulima wamepewa makao na kufidiwa kwa njia inayoheshimu haki za wakaazi na kufuata sheria ya nchi.

Aongeza kusema kuwa suluhu ya kudumu ni serikali ya Uhabeshi kushirikiana na shirika la Horticulture Producers and Exporters Association (EHPEA) ili kuzindua kanuni kamilifu zitakazohakikisha utumizi bora wa maji ya mito na maziwa kwa shughuli za ukuzaji maua katika eneo hili.

“Mashamba yote ya maua yafaa kushurutishwa kutumia mfumo wa umwagiliaji maji wa matone ambayo husaidia kuhifadhi raslimali ya maji,” ahitimisha Dkt. Mesay.

Ripoti na uhariri wa ziada umefanywa na Fredrick Mugira

Share the Post:

Related Posts