Patrick Kossima, Unyanja FM Radio
Likiwa na idadi ya watu wapatao 1,802 – miongoni mwao wakiwa wanawake 921 – kijiji cha Lundo kiko umbali wa takribaan kilomita 30 kutoka makao makuu ya Wilaya ya Nyasa. Kijiji hiki kinajumuisha kaya 417.
Shughuli kubwa ya kiuchumi katika kijiji hiki ni kilimo cha mpunga ambacho hufanyika katika bonde la Mto Luika. Kijiji hiki kwa kipindi kirefu kimekuwa kikikabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa mlipuko wa magonjwa ya tumbo, kuhara damu na ugonjwa hatari wa kipindupindu.