Kwa ufupi
Ukosefu wa vyoo Mkoani Songwe, Wilaya ya Songwe imetajwa kuwa mojawapo ya sababu ambayo ilipelekea kuenea kwa kipindupindu eneo hili, mnamo mwishoni mwa mwaka uliopita hadi mapema mwaka wa 2018.
Raymond Mhaluka, wa kituo cha radio cha Bomba FM alizuru eneo hili kutaka kujua jinsi ambavyo, ukosefu wa vyoo, mazingira yaliyosafi na kutokuzingatia usafi binafsi unavyochangia kuenea kwa maradhi.
Ndani ya kipindi cha miezi tisa kati ya mwezi Septemba 2017 hadi Mei 2018 vimeripotiwa visa vya ugonjwa wa kipindupindu ndani ya kata tisa za wilaya ya hiyo, ambapo wagonjwa 852 waliugua na kutibiwa na vifo vya watu wawili vilitokea. Katika taarifa ya wataalam wa afya imebainishwa kuwa matumizi ya vyoo yasiyo sahihi na ukosefu wa vyoo ni moja ya sababu za mlipuko wa ugonjwa huo katika jamii. Kijiji cha Mbala ndani ya kata ya Mwambani ni miongoni ya maeneo ambayo wakaazi wake walikumbwa na maradhi hayo ya mlipuko. Nimefika kijijini hapa. Kwanza nimewauliza wakaazi hawa kama wanazingatia kuweka maji ya kujisafisha chooni.
“Wengine wanatumia vitambaa, wengine makaratasi, mwingine anatoka hivyo hivyo. Mwingine anaenda tu chooni anajisaidia anatoka hivyo hivyo. Yaani hata tukisema tuzunguke kaya hapa Mbala, hamna kwamba utakuta choo kina maji. Viongozi wenyewe hawana maji wenye vyoo vyao. Wanaingia wanatumia kama tu wananchi wakawaida. Kwa hivyo magonjwa kama kipindupindu yanaingia. Ni jambo la kawaida. Mazingira kwa ufupi hayafai.”
“Kwa kweli upande wa vyoo, tulikuwa tunaenda kiholela. Hamna cha maji, tunaingia tu na kutoka, lakini hatunawi. Ilikuwa ukishaenda choo mara ingine unatumia bunzi, maana utaratibu kamili ulikuwa haupo kwa kweli.”
“Sisi kama wananchi, bado tuna utaratibu ule wa kutoweka maji chooni. Majani yanayotumika hasa zaidi ni mchongoma ambayo ni mjohoro na karatasi hizi za madaftari yaliyotumika, magazeti, na mabunzi, kwa sababu bado hatuna vyoo vya kisasa. Kwa hivyo hapa kijiji nzima waweza hesabu ishirini au thelathini.”
“Hata mazingira yenyewe yanabana kwa sababu mazingira huku vijijini, haufundiswi namna hata ya kutumia maji kwa kuflash, ndio maana anatumia labda akiwa mtoto, kiasi kwamba anaweza akamusaidia kuflash, la sivyo, baada kama mzazi hayuko anazunguka nyuma ya nyumba kujisaidia, kiasi kwamba anaweza chukuwa jiwe au tofali au majani kujichambia. Kiukweli kimazingira, elimu bado iko chini sana.”
Mbali na wakaazi hao kubainisha kuwa wanatumia nyenzo tofauti na maji kujisafisha, bado wanasema hata utaratibu wa mtu kunawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kujisaidia ni jambo ambalo halijazoeleka.
“Hii swala ka kunawa, hapana. Mimi ni mzaliwa wa hapa lakini ninafahamu. Mtu akishatoka tu chooni hajawahi kunawa,”
“Asilimia sabini hatunawi, asilimia thelathini wananawa sababu wenzetu wengine wanatumia vyoo vya kisasa sababu kutokana na uwezo walio nao. Wengine kidogo ambao kidogo uwezo umetubana, tunatumia vyoo vya kienyeji, mara nyingi unakuta hatunawi. Utawekaje maji kwenye choo ambacho ni cha kienyeji?”
Ripoti kadhaa zimewahi kuonyesha kuwa kuna baadhi ya jamii hazina vyoo vya kujisaidia haja zao katika kaya.
“Kwa haja ndogo asilimia nyingi tunajisaidia kwenye kichaka na haja kubwa tunajisaidia kwenya chooni. Huko mashambani sisi huwa tunajisaidia huko shambani. Unaweza tumia mkono, unafukua chini, unajisaidia unafukia. Lakini tulihamasishwa, kila mtu akawa na choo na bafu, sababu ilikuwa tayari ni kauli mbiu kutoka kwa mkuu wa wilaya kwamba asiye kuwa na choo na bafu anatakiwa akamatwe mara moja na achukuliwe hatua za kisheria. Kama sisi wananchi tuliweza tukajitambua kwamba inatakiwa ujenge choo na bafu kwa ajili ya kujiepusha na mambo mbalimbali.”
Wakaazi hawa wamebainisha ukweli kuwa kuna baadhi ya kaya hazikuwa na vyoo, ndio maana walipata kipindupindu.
Makala haya yameletwa kwa hisani ya InfoNile na Code for Africa, ikishirikiana na Bomba FM