Kidimbwi Chaokoa Mto Mara Kutokana na Uchafuzi Unaosababishwa na Uchimbaji Thahabu

Kidimbwi Chaokoa Mto Mara Kutokana na Uchafuzi Unaosababishwa na Uchimbaji Thahabu

Na Jacob Mugini

Barabara inayoelekea Murito yapitia mashamba madogomadogo na yale makubwa ya kilimo, lakini yafika hapa Tarime, eneo la Mara, kaskazini mwa Tanzania.

Miaka miwili iliyopita, kabla ya kidimbwi kinachotumika kusafisha thahabu kujengwa katika kijiji hiki, Murito ilikuwa kama vijiji vinginevyo kaskazini Tanzania.

Lakini sasa, jamii hii kakamavu, ambamo Bi Eliza Mogesi, mkulima mdogo na mama wa watoto watatu anamoishi, amesifika Tanzania nzima kwa kuruhusu kidimbwi kinachosafisha thahabu kujengwa shambani mwake. Kidimbwi hiki kinaokoa Mto Mara kutokana na uchafuzi unaosababishwa na madini ya zebaki inayozalishw na wachimba migodi wadogo, kando kando ya mto huu, ndani ya Wilaya ya Tarime.

Kabla ya kidimbwi hiki kujengwa, wachimba migodi wadogo walisafisha madini ya thahabu kwenye mito midogo inayotiririka kwenye Mto Mara.

“Twawataka wachimba migodi hawa wadogo wanaoendelea kusafisha madini ya thahabu kusitisha shughuli hii kuanzia sasa, kwa vile zebaki inahatarisha afya,” asema Mogesi.

“Mto Mara ni chanzo cha maji yetu na tunataka mto usiwe na uchafuzi.”

Bonde la Mto Mara lasaidia watu zaidi ya zaidi ya milioni moja na lakhi moja kujikimu kimaisha katika nchi za Kenya na Tanzania. Baadhi ya watu wanaoishi Tanzania wanahatarika kutokana na sumu inayosababishwa na madini ya zebaki.

Kulingana na wauguzi, madini ya zebaki yanadhuru mfumo mkuu wa neva, mfumo wa homoni, mafigo na viungo vingine vingi muhimu ndani ya mwili wa mwanadamu. Na wanawake wajawazito ambao wamekumbana na madini ya zebaki, waweza kujifungua watoto walio na kasoro kubwa za kuzaliwa.

Kwa miaka mingi, uchafuzi unaotokana na uchimbaji wa madini ya thahabu imekuwa mojawapo ya changamoto ya kimazingira inayokumba Mto Mara inayoshirikisha nchi mbili jirani: Tanzania na Kenya.

Bonde hili lina historia ndefu ya uchimbaji madini ya thahabu, kuanzia ugunduzi wake na wakoloni wa Kijerumani, karibu na Ziwa Victoria mnamo mwaka wa 1894, na kufunguliwa kwa mgodi wa kwanza wa thahabu mnamo mwaka wa 1909.

Kuelekea mwisho wa miaka ya 1990, kampuni geni za madini zilijitokeza na kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye uchunguzu wa thahabu. Migodi mikubwa mingi ilianzishwa, ikijumuisha ile ya North Mara Gold Mine: mojawapo ya migodi mitatu inayoendeshwa kaskazini-magharibi mwa Tanzania na Acacia Mining, kampuni iliyo na makao yake jijini London.

Ukataji miti, kilimo cha unyunyuzi maji na ukuzaji mifugo pamoja na matendo mengine ya binadamu imepelekea kuhatarisha kuwepo kwa mto ambao chanzo chake ni msitu wa Mau, upande wa Kenya.

Mto huu unapita katikati mwa hifadhi ya wanyama pori ya Masai Mara Game Reserve nchini Kenya na ile ya Serengeti National Park nchini Tanzania, kabla kuyamwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

Kando na kustawisha pato la watu wanoishi ndani ya bonde la mto, ulinzi wa mto ni muhimu kwa ukuwaji wa sekta za uhifadhi na utalii katika nchi hizi mbili.

 

SULUHISHO LA UCHAFUZI: KIDIMBWI CHA KUSAFISHA THAHABU

 

Safari ndefu ya kuokoa Mto Mara kutokana na uchafuzi unaosababishwa na wachimbaji madini wadogo, ilianza miaka miwili iliyopita, baada ya kidimbwi cha usafishaji thahabu kilipotengenezwa kijijini Murito, Wilaya ya Tarime nchini Tanzania, eneo la Mara.

Wachimbaji madini wadogo kadhaa waliokuwa wakisafisha thahabu kwenye vijito vinavyotiririka kwa Mto Mara walihamishwa hadi kidimbwi hiki, ambacho kilibuniwa kwa madhumuni ya kulinda Mto Mara kutokana na uchafuzi wa madini ya zebaki.

Hasa, kidimbwi kimelenga kulinda mto kutokana na uharibifu zaidi unaosababishwa na wachimbaji madini wadogo wa shirika la Kwinya Mining Cooperative Society.

Ilitengenezwa kwa hisani ya shirika la World Wildlife Fund for Nature (WWF), mojawapo ya mashirika makuu ya uhifadhi.

“Kidimbwi kimesaidia kudhibiti uchafuzi unaotokana na madini ya zebaki; maji hayatiririki kwenye vyanzo kama ilivyokuwa miaka 15 imepita,” alisema Robert Marwa, mwenyekiti wa shirika la Kwinya Mining Cooperative Group.

Kwa sasa, kikundi hiki kinawahusisha wachimbaji 36 wa madini, tisa miongoni mwao ni wanawake ambao wanategemea uchimabaji huu kwa pato lao la kimsingi, kijiji cha Murito, Wadi ya Kemambo.

Kando na kuzuia madini ya zebaki kuingia kwenye vyanzo vya maji, kidimbwi hiki cha kusafishia thahabu kimewapa wachimbaji madini wadogo mazingira safi kuendeleza shughuli zao.

“Mambo sasa yamebadilika na kuboreka katika sehemu hii yetu, sasa miti na nyasi zanawiri kando ya vyanzo vya maji, kama unavyoona, kufuatia kuahamishwa kwa wachimba madini hadi kwenye kidimbwi cha kusafishia thahabu,” asisitiza Marwa aliyeridhishwa dhahiri.

“Tunahifadhi mazingira ambayo imepelekea hali ya utenda kazi pia kuwa ya kuvutia.”

Hata hivyo, kulingana na Marwa, bado kunao wachimba madini wadogo wanaoendeleza shughuli zao kando kando ya mto na anawataka wahamie palipo kidimbwi.

Maafisa wa serikali ya Tanzania katika wadi ya Kemambo wamekuwa wakiendeleza kampeni za kuwaelimisha wanavijiji kuhusu madini ya zebaki na athari zake kwa mazingira na maji na jinsi ambavyo watu hawafahi kuchimbua thahabu karibu na vyanzo vya maji.

“Baadhi ya wachimbaji madini wadogo tayari wameshaondoka kwenye vyanzo vya maji, lakini wengine wameamua kutumia maboma yao,” aeleza wazi Paulo Maisori, Afisa Mtendaji Wadi ya Kemambo, akisisitiza zaidi kwamba, “hii ni hatari mno, lakini tutaendelea kuwapa elimu kuhusu ya athari ya madini ya zebaki.”

Maisori akumbatia chaguo hili la kidimbwi cha kuhifadhi madini ya zebaki na anawashawishi washirika pamoja na serikali kusaidia mpangilio huu.

“Kidimbwi cha kuhifadhi zebaki ni mfano mzuri unaohitaji kuigwa na vijiji vingine vilivyo na wachimbaji madini wadogo wanoendesha shughuli zao kando kando mwa mto,” asema Maisori.

Joseph Ntora Patrice, Afisa Mtendaji Kijiji cha Murito asema kuwa serikali yaunga mkono juhudi za WWF kuzuia uchafuzi wa Mto Mara.

“Kando na uchafuzi, madini ya zebaki ni sumu. Ndio sababu tunashirikiana na washika dau wengine wa kimazingira kama vile WWF kuchukua hatua,” asema Ntora.

Tayari, kidimbwi kimeshaanza kuonyesha ufanisi mkubwa, kwa mujibu wa Kanuni Kanuni, Afisa wa Mradi wa WWF kitengo cha maji safi yaani Mara River Fresh Water Programme.

“Idadi kubwa ya wachimba madini wadogo wameshaanza kutengeneza vidimbwi vyao binafsi, baada ya kuiga mfano wa kidimbwi kile cha kikundi cha Kwinya tulichokiunda. Ufanisi umekuwa mkubwa,” alisema Kanuni.

 

UHIFADHI WA SERENGETI

 

Kutengenzwa kwa kidimbwi, aendelea kueleza, ni mojawapo tu ya mipangilio inayoungwa mkono na WWF, kwa madhumuni ya kulinda Mto Mara kutokana na uchafuzi unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za binadamu.

WWF imekuwa ikishirikiana na serikali ya Tanzania, jamii na washirika wengine walioko kando mwa bonde la Mto Mara ili kufanikisha miradi inayolenga  kuimarisha kiwango na ubora wa maji pamoja na kuhifadhi aina zote za mazingira ndani ya Serengeti.

“Tulihitaji kidimbwi kiwe mfano wa kupunguza uchafuzi wa Mto Mara, hivyo basi tunaridhika na matokeo mema tunayoyaona,” kasema Kanuni.

“Baadhi ya wanavijiji wamechukua hatua moja zaidi, kwa kuunda vidimbwi vya samaki vyenye ukubwa sawa. Sasa wanakuza samaki na hii ni njia mbadala ya kuwapa pato zaidi.”

Hata hivyo, maafisa wa WWF walisema kuwa uamuzi wa baadhi ya wachimbua madini wadogo ya kuendeleza shughuli ya kuchimbua thahabu mabomani mwao, inafaa kupigwa marafuku.

“Baadhi ya wachimbua madini wadogo ambao wameondoka kutoka maeneo ya vyanzo vya maji sasa wanatekeleza shughuli hiyo mabomani mwao. Hii ni hatari kwa afya yao na haifai kuendelea,” asisitiza Kanunu.

Akizungumza alipokuwa akipokeza na kuzindua kidimbwi, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Tarime, Apoo Castro Tindwa aliagiza wachimbua madini wadogo wote wanaoishi kando ya mto, wasitishe shughuli ya kusafisha madini ya dhahabu maeneo ambayo yanachangia uchafuzi wa mto, na wahamie zilipo vidimbwi salama zisizo hatarisha afya.

Wachimba madini wa shirika la Kwinya Mining and Cooperative Society walitaja ukosefu wa maji wakati wa kiangazi kama kikwazo, kufuatia kuhama kwao hadi sehemu iliko kidimbwi cha kuhifadhi zebaki.

“Twahitaji mtambo wa kuvuta maji kutoka Mto Mara, hasa wakatai wa kiangazi. Hii ndio shida inayotukumba,” alieleza wazi Chacha Mtari, mhasibu wa kikundi cha Kwinya.

 

UELIMISHAJI WA WACHIMBA MADINI WADOGO

 

Takriban wachimba madini wadogo 4,000 wanaedesha shughuli zao kando mwa bonde la Mto Mara, kwa mujibu wa Martha Mahule, Afisa Msimamizi wa Mazingira, Baraza la Wilaya ya Tarime.

Vijiji hivi vinajumuisha Murito, Matongo, Nyakunguru, Karende, Nyabichune na Mosege.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikiwaelimisha wachimba madini kutoka vijiji hivi kuhusu athari zitokanazo na zebaki pamoja na umuhimu wa kusafisha madini ya thahabu sehemu iliyo mbali na vyanzo vya maji.

“Sisi huwaeleza wanavijiji kutumia vifaa maalum wakati wanatumia zebaki na kuwahimizia kukaa mbali na vyanzo vya maji,” alinena Mahule.

Hata hivyo, anakerwa na jinsi ambavyo baadhi ya wachimba madini, hasa wale wakiume, wanavyosita kuondoka kutoka maeneo ya vyanzo ya maji.

Mahule anaamini kuwa juhudi za pamoja zinazohusisha washika dau muhimu zahitajika kusitisha uchafuzi wa maeneo ya mazingira ambayo ni sehemu anzilishi ya mikono ya Mto Mara.

“Wachimba madini wadogo kijijini Murito walikuwa wasumbufu hapo awali, lakini wamehamia eneo la kidimbwi hifadhi, kwa usaidizi wa WWF. Changamoto sasa imebaki kuwa kijiji kile cha Matongo,” aeleza.

Anataka shughuli za kuandaa thahabu kufanyika sehemu maalum zilizotengwa, na kupendekeza adhabu kwa wachimba madini wanaokaidi amri.

“Haifai kuandaa thahabu mabomani; tulipiga marafuku shughuli hiyo na kutoa onyo kwa maandishi. Ni hatari sana, lakini baadhi ya watu wameamua kutosikiza maombi yetu. Pengine itabidi tuandamane na polisi,” asema Mahule.

Alifafanua kuwa wanavijiji walielemishwa jinsi ya kutumia mbinu salama za kuandaa madini ya thahabu badala ya kutumia zebaki, ambayo inahatarisha afya.

Alisisitiza umuhimu wa kutenga maeneo maalum ya wachimba madini wadogo, baadala ya kuwaruhusu kuendesha shughuli hizo sehemu zozote zile.

Wakati huo huo, ripoti zaonyesha kwamba kilimo cha umwagiliaji maji, ukati miti na matendo mengine ya binadamu imepelekea mto kujaa mchanga.

“Mto kujaa mchanga ni changamoto nyingine inayokumba Mto Mara, inayosababishwa na matendo ya binadamu zisizozingatia mazingira ndani ya bonde la mto,” alisema Mahule.

Anapendekeza mikakati kuwekwa kabla ya hali kuzoroteka zaidi.

 

HIFADHI KUENDELEZA UHAMAJI MAARUFU WA KONGONI KILA MWAKA

 

Katika juhudi za kutekeleza uhamasishaji wa uhifadhi wa bonde la Mto Mara, Tanzania na Kenya zinaadhimisha Siku ya Mara kila mwaka.

Awamu ya kumi la baraza kuu la mawaziri wanaowakilisha nchi zilizoko ndani ya bonde la Ziwa Victoria yaani The 10th Sectorial Council of Ministers for Lake Victoria Basin, lilifanyika Kigali, mji mkuu wa Rwanda, Mei 2012. Baraza hili lilitoa kauli na kutangaza kwamba kila Septemba 15 kuwa Siku ya Mara, kuambatana na uhamaji maarufu wa kongoni kila mwaka kutoka Serengeti National Park nchini Tanzania na Masai Mara Game Reserve nchini Kenya.

Nchi hizi mbili zahisi kuwa uhifadhi wa Mto Mara kuwa muhimu kwa uendelezaji wa uhamaji wa kongoni, wanaovuka mto kila mwaka.

Uhamaji huu maarufu huwavutia maelfu ya watalii kutoka sehemu tofauti za ulimwengu, hivyo kuziletea nchi hizi mbili hela muhimu za kigeni.

Siku kuu ya Mto Mara huadhimishwa kwa mzunguko, ikizingatia mada tofauti inayolenga kukuza uhifadhi endelevu wa bonde la mto wa kizazi cha sasa na kijacho.

Makala haya yamewezeshwa kwa hisani ya InfoNile na Code for Africa. Uhariri ni kwa mujibu wa Fredrick Mugira, Annika McGinnis na Code for Africa.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts