Gugumaji Yatishia Hali ya Baadaye Ya Samaki na Jamii za Kivuvi Kando mwa Ziwa Victoria

Gugumaji Yatishia Hali ya Baadaye Ya Samaki na Jamii za Kivuvi Kando mwa Ziwa Victoria

Na Mary Mwendwa

George Onyango ni mvuvi pale Ufukoni Dunga ndani ya Ziwa Victoria, kaunti ya Kisumu mashariki mwa Nairobi, jiji kuu la Kenya.

Amekuwa akivua samaki kwa miaka kumi na tano sasa. Akiwa na umri wa miaka 56, na jamii ya watoto saba, imekuwa vigumu kwake kujipatia tija tosha inayotokana na mauzo ya samaki, kinyume na hapo awali.

“Mapato yangu yalikuwa juu, kutokana na samaki. Nilipata hadi dola 200 kwa siku, kwa vile samaki walikuwa wengi. Mambo yamebadilika siku hizi. Sina uhakika kama nitawapata samaki ziwani. Idadi ya samaki imekuwa ikipungua siku za hivi karibuni hata kututia wasiwasi sisi kama wavuvi; pato letu litakatizwa,” alalamika Onyango.

Gugumaji, mmea vamizi unaoelea Ziwani Victoria ndio chanzo cha masahibu yake.

Kwa mujibu wa hati ya kitaarifa, Ziwa Victoria ndilo ziwa kubwa zaidi Afrika likiwa hifadhi kuu ya Mto Nile, ukubwa wake ukiwa 251,000km mraba, na ambalo linajumuisha kichwa cha bonde la Mto Nile unaoshirikisha mataifa tano za Afrika Mashariki. Ukweli wa mambo waonyesha kwamba Tanzania inakalia sehemu kubwa la bonde hili ikiwa ni 44%, ikifuatiwa na Kenya 22%, Uganda 16%, Rwanda 11% na Burundi 7%, huku upwa wake ukishirikisha mataifa matatu pekee, Tanzania ikichukuwa sehemu kubwa ya 51%, Uganda 43% na Kenya 6%.

Ziwa hili ni muhimu kwa watu wanaoishi karibu nalo kwa shughuli za kilimo, maji ya matumizi ya kinyumbani, umememaji, uvuvi na utalii. Lakini mambo yamebadilika pakubwa.

“Uvuvi imekuwa ajira yangu ya kipekee. Niliiridhi kutoka kwa baba yangu aliyekuwa mvuvi mashuhuri miaka mingi imepita. Wakati huo, samaki walikuwa wengi mno na gugumaji halikuwepo,” aeleza Onyango, akisisitiza jinsi ambavyo mambo yamebadilika.

Kunazo nyakati Onyango huambulia patupu baada ya shughuli ya uvuvi. Lakini miaka michache ya hapo nyuma, kabla ya gugumaji kuvamia sehemu hii ya ziwa, tukio hili halingewezekana.

Gugumaji limetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuharibika kwa mazingira ya ziwa. Sababu nyingine ni uchafuzi, mabadiliko ya kitabia nchi na mitindo ya uvuvi zisizo endelevu.

“Gugumaji linatumaliza polepole. Kuna wakati linatoweka halafu linarudi kwa kishindo. Mashua haiwezi kupita katikati mwake,” alalama Onyango.

Onyango anamiliki mashua tano anazotumia kuvua aina ya samaki ya tilapia na sangara, na pia huzikodisha mashua hizo.

Michael Odunga ni mmiliki wa mashua vile vile. Yeye ni mvuvi anayetambulika eneo hili. Anashuhudia jinsi ambavyo shughuli ya uvuvi imebadilika na kuwa gumu, ikilinganishwa na siku za ujana wake.

“Niliwacha shule nikiwa darasa la nane kwa vile nilijua kwamba uvuvi ulikuwa na faida na lingeniletea pato zuri,” asema.

Aeleza kwamba, alipoanza uvuvi miaka kumi imepita, samaki walikuwa wakutosha ziwani.

“Ningewavua na kuwauza samaki na kupata pesa za kutosha hata kuhifadhi zingine za matumizi ya baadaye,” asema Odunga.

“Sasa hata siwezi kuhifadhi chochote. Kunazo siku sipati lolote ziwani kando na omena,” aongeza kusema.

Hadhi ya ziwa hili ambalo ni la pili kwa ukubwa miongoni mwa maziwa ya maji matamu duniani, sasa laelekea ukingoni, huku Odunga akiamini kuwa, “ikiwa hatua za tharura za kiserikali hazitachukuliwa, basi hatuna budi ila kuliaga kwa kheri.”

Kwa mfano, unapokaribia Kisumu, ni vigumu kueleza ni wapi ardhi inamalizikia na ni wapi ziwa linapoanzia. Unachotazama ni sehemu kubwa ya mamia ya hektari ya mmea wa kijani.

Shughuli katika bandari ya Kisumu zasimama kwa ghafla mara kwa mara kwa vile bandari hili limezibwa gugumaji hili la kijani. Meli na aina mbali mbali ya mashua kubwa ambazo ziliendesha shughuli ndani ya Ziwa Victoria, zaonekana kukwama.

Mtazamo huu, huwapatii matumaini wavuvi kama Odunga, waliotumainia mazingara haya.

Casianes Olilo, mtafiti katika taasisi ya Kenya Marine and Fisheries Research Institute (KMFRI), asema “kuongezeka kwa idadi ya watu, umaskini, ukosefu wa lishe bora, ukosefu na upungufu wa chakula, na njaa imepelekea utumiaji kupindukia wa raslimali ya samaki [na] kuhatarisha bayoanuai ya Ziwa Victoria.”

Pia anadokeza kuwa, uvamizi wa viumbe geni kama vile sangara, tilapia aina ya Nile, na gugumaji imebadilisha pakubwa huduma ya kimazingira ziwani, ikiwemo mtanda wa chakula.

Olilo adokeza kwa wasiwasi kuwa, gugumaji imeletea ziwa athari kubwa mno.

“Maisha ya samaki (mayai, zalio, kambe na samaki komavu) huathiriwa wakati upepo mkali wa kusini mashariki unaposukuma visiwa hivi vya gugumaji hadi katikati mwa ziwa.

“Gugumaji huathiri maisha ya samaki na kueneza magonjwa ya samaki katika ile hali ya upungufu wa oksijeni. Samaki pia hugwaruzwa pamoja na hali duni ya maji; gugumaji huwezesha kuenea kwa magonjwa ziwani,” asimulia Olilo.

Asema pia, hatari zingine ni pamoja na uchafuzi, zana duni za uvuvi, uvuvi kinyume na sheria na upungufu wa chakula miongoni mwa sababu nyingine, zimechangia pakubwa kudidimia kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria.

 

UONDOAJI WA MAGUGU

Wanasayansi wa KMFRI wamependekeza njia za kibayologia, kikemikali na kifisikia, ili kuondoa gugumaji na kurejesha ziwa katika hali yake.

Kwa mfano, utumiaji wa bungo kuthibiti ueneaji wa gugumaji imekuwa nguzo muhimu ya utafiti tangu kero la gugumaji lilipoanza kuonekana Ziwani Victoria mwanzo wa miaka ya tisaini.

“Utumiaji wa bungo ni salama na hauna mathara. Bungo hula shina la gugu, hivyo kukatiza muelekeo wa maji hadi katika tawi na virutubishi vitokanavyo na usanidi-nuru kufikia mzizi kutoka kwa tawi,” adhibitisha Olilo.

Sera ya vinamasi nchini Kenya yatambua kwamba vinamasi vinahatarika kutokana na viumbe geni na vamizi.

Sera hii inabainisha kwamba vinamasi vingi, ikijumuisha Ziwa Victoria, katika siku za nyuma, vimeathirika kutokana na kuingizwa kwa viumbe geni na vamizi kama vile gugumaji ambavyo vimebadilisha hali ya kimazingira na kudunisha huduma zinazopeanwa na vinamisi; mfano mzuri ni uvuvi.

 

Ripoti hii ya Mary Mwendwa kuhusu Gugumaji Ndani ya Ziwa Victoria imefanyika kwa hisani ya InfoNile na Code for Africa.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts