Vita dhidi ya vifaa haramu vya uvuvi, vyazaa matunda Ziwani Victoria

Ripoti hii imefanikishwa kutokana na ruzuku iliyodhaminiwa na InfoNile pamoja na Code for Africa. Ilichapishwa kwanza na Star TV.

Operesheni ya kuzuia uvuvi haramu inayoendelea katika ziwa victoria imemkamata mvuvi mkubwa, Joseph Kando Mkama maarufu kama Njiwa pori akiwa ameficha zana za uvuvi haramu zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja nukta moja.

Katika kijiji cha Nyamatongo Wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza, ndipo ilipo moja ya kambi za mvuvi huyu mkubwa, Joseph Kando Mkama.

Licha ya serikali kuwataka wavuvi wote kuzisalimisha zana haramu walizo nazo katika awamu ya kwanza iliyomalizika mwezi Machi, alikaidi na kuamua kuzichimbia shambani pamoja na kwenye nyumba inayoendelea kujengwa.

“Katika hali ya kawaida, eneo lilipo na mazao yalivyo, ilikuwa vigumu sana kuzigundua,” kaeleza, Wenceslaus Ruhasile, Kamanda wa Operesheni Sengerema na Buchosa. Alishukuru intelijensia iliyopeanwa kwa timu yake, na ambayo ilipelekea kunasa zana hizo.

Operesheni hii imeibua nyavu mpya katika matumizi ya uvuvi  Ziwa Victoria ikiashiria  kukithiri kwa vitendo vya uvuvi haramu.

“Kwa mtazamo, na kwa mtengenezo wake, inaonekana kwamba inaweza kuwa ni haribifu zaidi,” Ruhasile aliongezea kusema.

Alieleza kwamba, nyavu hii ina kina ya macho mia nne lakini kwa urefu ina macho mia sita. Baadhi ya nyavu zilipatikana kwa mlima ambako mtuhumia alikuwa amezificha.

Mtuhumiwa huyo wa uvuvi haramu amekiri kuendesha uvuvi huo huku akiwa anatambua kabisa anatenda makosa.

“Nimevua hizi nyavu siku nyingi,” kasema Kando, mtuhumiwa wa uvuvi haramu. Alikariri kwamba hakuna mvuvi ambaye yuko salama, huku akiomba msamaha.

Ruhasile alieleza kwamba maafisa wa serikali, walibaini sehemu tano ambako nyavu zilikuwa zimefukiwa. Pamoja na nyavu, pia waliweza kungundua ingini ishirini na nne.

Pamoja na kuwa zana hizi haramu zitateketezwa kwa mujibu wa sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003, lakini mtuhumiwa pia anapigwa faini kutokana na kuhujumu uchumi.

“Ya jumla ya milioni mia mbili na arobaini, ambazo zinahitajika zilipwe ndani ya masaa ishirini na nne,” alieleza Magese Bulai, Mkurugenzi Mkuu wa uvuvi.

Kwa mujibu  mkurugenzi mkuu wa Uvuvi, operesheni hii haitamwacha salama mvuvi yeyote anayekaidi sheria ya uvuvi.

Hii ni awamu ya pili ya operesheni sangara isiyojulikana ukomo wake ikilenga kukomesha uvuvi haramu ambao umeharibu rasilimali kwa muda mrefu.

Share the Post:

Related Posts