Pesa kwanza, afya baadaye

Pesa kwanza, afya baadaye

NA FELIX MWAKYEMBE, CHUNYA

PESA, ndicho kitu pekee chenye thamani kwa wachimbaji wadogo katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, afya sio kipaumbele chao.

Wachimbaji hao wadogo wa dhahabu hawaliangalii suala afya zao kuwa ni jukumu lao wenyewe, bali wamemuachia Mungu, kwao ndiye anayewasaidia kuepukana na magonjwa ya milipuko.

“Mungu anatusaidia, magonjwa ya milipuko hakuna, ila typhoid ndio nyingi,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoani wa Mbeya (MBEREMA), Tawi la Matundasi, Paul Maganga.

Changamoto za maji na huduma za vyoo ni za kawaida kwao lakini hawazipi umuhimu wowote, wanachoangalia wao ni dhahabu inayowapa pesa. Wataifuata popote pale watakaposikia ipo, wao husema imetema.

Mbeya
One of the many gold ore crusher plants scattered in Chunya District, they are busy throughout the day but their operators do not have enough latrines that could prevent cholera outbreaks. Photo by Felix Mwakyembe

Vyoo sio kipaumbele kwa wachimbaji:
Hali ya vyoo kwa jamii za wachimbaji wadogo wa dhahabu wilayani humo ni mbaya, ambapo inakadiriwa kuwa watu wenye kutumia vyoo katika Kitongoji cha Itumbi, kwa mfano, haizidi asilimia 30.

“Tatizo la vyoo ni tabia zaidi na sio pesa, na hutegemea uelewa wa mtu,” alisema Afisa Madini Wilaya ya Chunya, Athuman Fariko.

Hata hivyo Athumani, anauelezea mfumo wa maisha ya wachimbaji wadogo ya kuhamahama, kuwa unachangia uwepo wa makazi ya muda na ujenzi holela.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mdogo Makongorosi, Linus Mwaitega, Kitongoji cha Itumbi kina wakazi wapatao 4,000 wakati Kata ya Matundasi kilimo kitongoji hicho ina wakazi takribani 12,000.

“Ni itadi kubwa sana, sema sheria ya mamlaka za miji haina vijiji, Itumbi inatosha kuwa kata,” alisema Mwaitega.

Sheria inaelekeza kitongoji ni kuanzia kaya 50, ambapo kwa kiwango cha kaya moja kuwa na watu watano hadi sita, ina maana kwamba watu kuanzia 250 wanaweza kuanzisha kitongoji.

Kwa kutumia hesabu ya kaya moja kuwa na watu watano hadi sita, basi Kitongoji cha Itumbi kitakuwa na kaya kati ya 670 hadi 800.

Mbali ya makazi yao kukosa vyoo, hata kwenye kambi zao, wanakoendesha shughuli za uchimbaji dhahabu, hawatumii vyoo, kila mtu anatafuta namna yake ya kutupa uchafu wake.

“Choo sio sehemu ya ujenzi, sio kipaumbele chao, watu hujisaidia popote, hasa vichakani,” alisema Mganga Mkuu Wilaya ya Chunya, Dr. Stanford Mwakatage.

Kukosekana kwa huduma za vyoo kwa sehemu kubwa ya jamii za wachimbaji wadogo wilayani humo inachangiwa zaidi na mfumo wa makazi yao, ni holela, hakuna mpangilio wa nyumba (squatter).

Kiafya, inaelezwa kuwa ujenzi holela wa nyumba, usiofuata utaratibu (squatter) haufuati taratibu za kiafya, na unapoibuka ugonjwa wa mlipuko sio rahisi kuudhibiti au kuzuia.

“Ukiwa na poor waste disposal, water contamination ni lazima,” alisema Dr Mwakatage katika mahojiano yaliyofanyika ofisini kwake katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.

Katika moja ya kambi ya wachimbaji wadogo iliyopo kitongoji cha Matondo, kinaonekana choo kimoja cha shimo kilichozungushiwa karatasi, kinahudumia wawekezaji wawili, kila mmoja akiwa na mitambo yake.

Hata hivyo, ilibainika kutotumika, walipohojiwa kuhusu eneo la kujisaidia, vijana wafanyao kazi kwenye kambi hiyo pamoja na mamalishe, walisema wanapohitaji huduma hiyo hurudi nyumbani kwao kutokana na kukosa choo.

“Hatuna choo hapa, nikibanwa hukumbilia nyumbani,” alisema mmoja wa watoto wa mwenye mitambo ya kusaga mawe ya dhahabu ambaye hata hivyo hakupenda kujitambulisha.

household facilities

Maji, mgodi mwingine wa dhahabu:
Suala zima la afya kwa wachimbaji hao wadogo wa dhahabu wilayani Chunya lina changamoto, hususani vyoo na maji. Katika makazi yao na kwenye kambi, jamii za wachimbaji wadogo hutumia maji yasiyo safi wala salama.

Chanzo kikuu cha maji kwa jamii hizo ni madimbwi, maji yaliyomo kwenye mashimo yaliotelekezwa wakati wakitafuta dhahabu. ni maji yaliyojikusanya kutokana na mvua, na wakati wa kiangazi hukauka.

Chanzo kingine ni vijito vya msimu, ambapo wakati wa kiangazi hatiririshi maji lakini wenyeji hufukua na kukuta maji chini ambayo huyatumia kwa shughuli zao za nyumbani, ikiwemo kupikia, kufulia na kunywa.

Vipo visima virefu vya watu binafsi, hata hivyo ni vichache sana na wamiliki wa visima hivyo huuza maji.

Dr. Mwakatage anayaelezea maji hayo kutokuwa safi wala salama na kwamba walitakiwa wawe wanayahifadhi kwenye matenki na uweka dawa, hapo ndipo yangekuwa salama.

“Tunatumia maji ya kwenye mashimo yaliyochimbwa wakakosa dhahabu, nayatumia nyumbani na huku kwenye biashara zangu,” alisema mamalishe kutoka Kitongoji cha Matondo, Rehema Fanuel na kuongeza,

“Hatuyachemshi, tunakunywa hivyo hivyo.”

Biashara ya maji katika jamii za wachimbaji wadogo ni mgodi mwingine, wenye kufanya biashara hiyo hutengeneza pesa ya kutosha. Mapato kutokana na biashara hiyo hutegemea uwezo wa muuzaji wa kubeba.

Wengi hutumia baiskeli kubeba vyombo vya maji, maarufu kwa jina la dumu, hawa hubeba 50 hadi 100 kwa siku. Wapo wachache wanaotumia maguta ambayo huwawezesha kubeba dumu 250 hadi 300 kwa siku.

Hesabu ya haraka, kama alivyoelezea mmoja wa wauzaji maji, Joseph James, hujipatia kati ya shilingi 25,000 na 50,000 kwa siku, ikitegemea uwezo wake wa kubeba dumu za maji.
Kutokana na kukosekana kwa maji ya bomba na visima virefu, maji ni biashara kubwa ambapo chombo cha ujazo wa lita ishirini huuzwa shilingi 500, pamoja na maji hayo kutokuwa salama.

“Biashara ya maji ndiyo inayoendesha maisha yangu, familia ipo Dar es Salaam, naihudumia kutokana na biashara hii,” alisema mfanyabishara ya maji katika Kitongoji cha Itumbi, Joseph James.

Joseph, baba wa watoto wanne, anasema maji wanayouza huyachota kutoka kwenye madimbwi, mashimo yaliyotelekezwa na wachimbaji wa dhahabu yenye kina cha mita tatu hadi sita, wanayaamini kuwa ni salama kuwa ni salama kwa kuyaangalia tu.

Kupata Takwimu za wagonjwa ni ngumu:
Pamoja na changamoto za kiafya zinazowakabili jumuiya za wachimbaji wadogo wilayani Chunya, hakuna takwimu za athari zitokanazo na ukosefu wa vyoo na maji.

Kukosekana kwa takwimu za wagonjwa kunachangiwa na kutokuwepo kwa huduma za vituo vya afya. Mathalani katika Kitongoji cha Itumbi chenye watu 4,000 hakuna hakuna zahanati, hivyo wakazi wake kufuata huduma za afya makao ya kata, Matundasi, kilometa 16 kutoka kijijini hapo.

Mbali ya Matundasi, wengine hufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya, mjini Chunya, takribani kilometa 25 kwa njia ya mkato inayopita porini au kilometa 32 kwa njia ya barabara inayopita magari.

“ukusanyaji takwimu kwenye jamii za wachimbaji wadogo ni ngumu, hakuna huduma za hospitali,” alisema Dr Mwakatage.

Dr. Mwakatage anayataja magonjwa yanayosumbua jamii za wachimbaji kuwa ni pamoja na kuharisha, kipindupindu na ugonjwa wa ngozi unaotokana na matummizi ya sumu ya zebaki.

Pamoja na wenyeji kudai kutokuwepo mlipuko wa magonjwa kwenye makazi yao, taarifa za afya wilayani humo zinabainishakuwa mwaka jana, (2017) kulitokea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Kijiji cha Shoga, kilichopo kwenye Kata ya Sangambi, mlipuko uliohusishwa zaidi na huduma mbovu za afya na matumizi ya maji yasiyo salama.

Watu zaidi ya 150 waliugua ugonjwa huo, na kati yao watatu walifariki.

Serikali yachukua hatua:

Serikali wilayani Chunya hivi sasa inachukua hatua mbali mbali kukabiliana na changamoto za afya kwenyejamii za wachimbaji wadogo wilayani humo. Miongoni mwa hatua hizo nipamoja na ujenzi wa zahanati, kikiwemo Kitongoji cha Itumbi.

“Tumeanza ujenzi wa zahanati pale Itumbi, itasaidia kukusanya takwimu za wagonjwa na kutoa ushauri,” alisema Dr Mwakatage.

Upo pia mradi mkubwa wa maji unaoendelea kujengwa, na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongorosi, mradi huo utahudumia hadi Kitongoji cha Itumbi.

“Sheria kila mtu awe na choo bora, program imeanzia Itumbi,” alisema Mkurugenzi Mwaitega.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa taasisi ya InfoNile na Code for Africa.

Like this article?

Share on Facebook
Share on Twitter
Share on Linkedin
Share on Pinterest
Share on Telegram
Share on WhatsApp

Leave a comment

Related Posts